Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yaripotiwa kukwama

Mazungumzo kati ya Israel na Hamas nchini Qatar kuhusu mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka yamekwama

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Lesotho yatangaza hali ya janga huku kukiwa na mashaka ya ushuru wa Marekani

    Lesotho imetangaza hali ya janga la kitaifa kutokana na "kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira kwa vijana na watu kupoteza kazi" huku kukiwa na mashaka kutokana na ushuru wa Marekani.

    Lesotho ilikumbwa na ushuru wa juu kuliko nchi nyingine yoyote wa 50% kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Aprili, ingawa ushuru huo umesitishwa kwa sasa.

    Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nthomeng Majara amesema hali ya janga itaanza kutumika hadi tarehe 30 Juni 2027.

    Ukosefu wa ajira nchini Lesotho umefikia 30% lakini kwa vijana kiwango hicho ni karibu 50%, kulingana na takwimu rasmi.

    Tamko hilo, kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Majanga, inaruhusu serikali "kuchukua hatua zote muhimu ili... kupunguza madhara ya maafa" miongoni mwa mengine.

    Maafisa nchini Lesotho - nchi yenye zaidi ya watu milioni mbili - wanasema hatua hiyo itaruhusu serikali kuelekeza fedha haraka kwenye programu zinazolenga kuwafanya vijana kufanya kazi na kusaidia uchumi kuimarika.

    Idara kadhaa tayari zimetangaza hatua za awali, ikiwa ni pamoja na kufuta ada ya usajili wa biashara kwa waanzishaji wadogo wa biashara na wa kati.

    Uchumi wa nchi hiyo unaotegemea nguo ulikuwa unakabiliwa na ukosefu wa ajira uliokithiri, hasa miongoni mwa vijana, hata kabla ya Trump kupunguza misaada na kuweka vikwazo vya kibiashara vya ushuru, kulingana na ripoti ya AFP.

    Lesotho ilikuwa ni mojawapo ya wanufaika wakubwa wa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika na Marekani (Agoa), ambayo inatoa fursa nzuri ya kibiashara kwa baadhi ya nchi ili kukuza uchumi wao.

    Kulingana na serikali ya Marekani, nchi hizo mbili zilifanya biashara ya bidhaa zenye thamani ya dola milioni 240 (£187m) mwaka 2024, nyingi ya bidhaa hizo zikiwa ni mauzo ya nje kutoka Lesotho kwenda Marekani, hasa nguo.

    Ingawa ushuru wa asilimia 50 ulisitishwa, mauzo ya nje ya Lesotho kwenda Marekani bado yanakabiliwa na ushuru wa 10%, kama nchi nyinginezo.

    Serikali ya Lesotho imeonya kuwa inaweza kupoteza hadi ajira 40,000 ikiwa Agoa haitarudishwa hadi mwishoni mwa mwezi Septemba, kulingana na AFP.

    Waziri wa Biashara wa Lesotho Mokhethi Shelile aliiambia tovuti ya habari ya biashara ya Afrika Kusini, Moneyweb mwezi uliopita kwamba wanunuzi kutoka Marekani "hawafanyi manunuzi kwa sababu hawaelewi kitakachotokea."

    Nchi hiyo pia iliathirika pakubwa na kusitishwa kwa programu za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) duniani kote. Lesotho ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), uliozinduliwa mwaka 2003.

    Wakosoaji wanasema mgogoro huu ulikuwa unatarajiwa, kwani hadi mwezi Machi, Lesotho ilikuwa katika hali ya janga ya miezi minane kutokana na uhaba mkubwa wa chakula.

    Wakati huo, Waziri Mkuu Sam Matekane alisema karibu raia 700,000 walikuwa wanakabiliwa na njaa kali, iliyosababishwa na ukame wa muda mrefu.

    Unaweza kusoma;

  2. Waziri wa zamani wa sheria wa DRC afikishwa mahakamani

    Waziri wa zamani wa sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Constant Mutamba, amefikishwa mbele ya Mahakama ya Cassation leo.

    Bw Mutamba, ambaye ana umri wa miaka 37 na ambaye ni mtumishi mdogo zaidi wa serikali, anadaiwa kujaribu kutumia vibaya takriban dola milioni 20.

    Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama fedha hizo zilihamishwa kinyume cha sheria kwa mkandarasi wa ujenzi wa gereza bila kufuata taratibu.

    Bw.Mutamba amekanusha mashtaka hayo akitaja kuwa yamechochewa kisiasa.

    Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 23 ili kuwapa mawakili wake muda wa kukagua majalada ya kesi, kama walivyoomba.

    Bw.Mutamba alijiuzulu wiki tatu zilizopita ili kujibu mashtaka baada ya bunge kuondoa kinga yake na kuidhinisha kushtakiwa kwake.

    Katika kipindi chake cha takribani mwaka mmoja kama waziri wa sheria, alikabiliana na uhalifu, akiwahukumu watu zaidi ya mia moja kuuawa, alitoa madonge nono dhidi ya waandishi wa habari na viongozi wa waasi, na kushinikiza kukamatwa kwa mali za Rais wa zamani Joseph Kabila kabla ya tuhuma hizi za ubadhirifu kuibuka.

  3. Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yaripotiwa kukwama licha ya mkutano wa pili wa Netanyahu na Trump

    Mazungumzo kati ya Israel na Hamas nchini Qatar kuhusu mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka yamekwama baada ya siku tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, afisa wa Palestina ameiambia BBC.

    Afisa huyo alisema mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na jinsi misaada itakavyosambazwa wakati wa usitishaji mapigano na uondoaji wa wanajeshi wa Israel.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anazuru Marekani na matumaini ya kufikiwa makubaliano yameongezwa kwani alikuwa na mkutano wa pili ambao haukutarajiwa na Rais Donald Trump siku ya Jumanne.

    Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff pia alisema kwamba alikuwa na matumaini ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 60 mwishoni mwa wiki hii.

    Mtazamo wa mikutano kati ya Trump na Netanyahu umetoa hisia kwamba kasi kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza inaongezeka.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatano asubuhi, waziri mkuu wa Israel alisema mkutano wao wa hivi karibuni "ulilenga juhudi za kuwaachilia mateka wetu". "Hatulegei, hata kwa muda, na hili linawezekana kutokana na shinikizo la kijeshi la askari wetu mashujaa."

    Aliongeza: "Tumedhamiria kufikia malengo yetu yote: Kuachiliwa kwa mateka wetu wote walio hai na waliokufa, na kuondolewa kwa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas, na hivyo kuhakikisha kwamba Gaza haitakuwa tena tishio kwa Israel."

    Unaweza kusoma;

  4. Ukraine yakabiliwa na mashambulizi makali zaidi baada ya Trump kumkosoa Putin

    Rais Volodymyr Zelensky amesema Ukraine imekumbwa na shambulizi kubwa zaidi kuwahi kutokea la anga kutoka Urusi, ndege zisizo na rubani 728 na makombora 13 ya baharini au ya balistiki yalipiga miji kote nchini humo.

    Zelensky alilaani shambulio na kuongeza: "Inakuja kwa wakati ambapo juhudi nyingi zimefanywa ili kufikia amani, kuanzisha usitishaji wa mapigano, na bado ni Urusi pekee inaendelea kuyapinga yote."

    Shambulio hilo la usiku lilikuja baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa Marekani itatuma silaha zaidi huko Kyiv, kubatilisha usitishwaji wa wiki iliyopita ambao vyombo vya habari vya Marekani vilisema Trump hakufahamu.

    Siku ya Jumanne, kiongozi huyo wa Marekani alionesha kusikitishwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

    "Tunapata upuuzi mwingi wa kutupwa na Putin, ikiwa unataka kujua ukweli," Trump aliwaambia waandishi wa habari. "Yeye ni mzuri sana kwetu wakati wote, lakini inageuka kuwa haina maana."

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Moscow ilikuwa "tulivu sana kuhusu hili. Njia ya Trump ya kuzungumza kwa ujumla ni kali sana, misemo anayotumia." Viongozi hao wawili wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara lakini hadi sasa imeshindwa kutafsiri katika hatua zinazoonekana kuelekea usitishaji vita nchini Ukraine - jambo ambalo Trump aliwahi kusema kuwa ataweza kulifanikisha kwa siku moja.

    Unaweza kusoma;

  5. Familia zaingiwa wasiwasi kuhusu usalama wa Wahindi waliotekwa nyara nchini Mali

    Wiki moja baada ya Wahindi watatu kutekwa nyara nchini Mali, familia zao zinasema bado hazina taarifa kuhusu waliko na zina wasiwasi kuhusu usalama wao.

    Wizara ya mambo ya nje ya India ilisema watu hao, ambao walifanya kazi katika kiwanda cha saruji nchini Mali, "walichukuliwa kwa nguvu" na kundi la "washambuliaji wenye silaha" Jumanne iliyopita.

    Serikali ya Mali bado haijasema lolote, lakini utekaji nyara ulifanyika siku ambayo kundi lenye uhusiano na al-Qaeda - Jama'at Nusrat al-Islam wal Muslimin (JNIM), lilidai kuwa limefanya mashambulizi kadhaa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

    Kulingana na takwimu za serikali, Wahindi takribani 400 wanaishi Mali, nchi ambayo India imekuwa na uhusiano wa kibiashara nayo tangu miaka ya 1990.

    Tukio la wiki iliyopita linakuja baada ya raia watano wa India kutekwa nyara nchini Niger, mwezi wa Aprili wakati wa shambulio la watu wenye silaha ambao pia waliwauwa wanajeshi kumi na wawili, shirika la habari la Reuters liliripoti.

    Hakuna taarifa kuhusu mahali walipo. Niger, Mali na Burkina Faso wanapambana na uasi wenye uhusiano na al-Qaeda na Islamic State (IS) ulioanza kaskazini mwa Mali mwaka 2012 na tangu wakati huo kuenea katika nchi jirani.

    Mali ni taifa la nane kwa ukubwa katika bara la Afrika na lipo katika eneo la Sahel barani Afrika, ambalo Ripoti ya Kimataifa ya Ugaidi (GTI) ilieleza kuwa "kitovu cha ugaidi duniani" mapema mwaka huu.

    Kanda hiyo inachangia "zaidi ya nusu ya vifo vyote vinavyohusiana na ugaidi", kulingana na GTI. Katika taarifa yake siku moja baada ya utekaji nyara huo, wizara ya mambo ya nje ya India iliwataka raia wanaoishi Mali "kuchukua tahadhari kubwa, kuwa macho na kuwa na mawasiliano ya karibu na ubalozi wa India katika [mji mkuu wa Mali] Bamako".

    Wanaume hao walichukuliwa kutoka kwa Kiwanda cha Saruji cha Almasi, kinachoendeshwa na kampuni ya India-biashara ya Prasaditya Group, katika jiji la Kayes. Kampuni na kiwanda hazijatoa taarifa yoyote hadi sasa.

    Unaweza kusoma;

  6. Yemen kumnyonga muuguzi wa Kihindi anayedaiwa kumnyonga mshirika wake wa zamani

    Muuguzi wa India anasubiri kunyongwa tarehe 16 Julai katika nchi ya Yemen iliyokumbwa na vita, wanaharakati wanaojitahidi kumuokoa wameiambia BBC.

    Nimisha Priya alihukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanamume wa eneo hilo - mshirika wake wa zamani wa kibiashara Talal Abdo Mahdi - ambaye mwili wake uliokatwakatwa uligunduliwa kwenye tanki la maji mnamo 2017.

    Njia pekee ya kumuokoa muuguzi huyo ni kama familia ya Mahdi itamsamehe. Ndugu na wafuasi wake wametoa $1m (£735,000) kama diyah, au pesa ya damu, ili kulipwa kwa familia ya Mahdi.

    "Bado tunasubiri msamaha wao au matakwa mengine," mjumbe wa shirika linalomtetea aliambia BBC.

    "Tarehe ya kunyongwa imewasilishwa na mkurugenzi mkuu wa mashtaka kwa mamlaka ya jela. Bado tunajaribu kumwokoa. Lakini hatimaye familia inabidi ikubali kumsamehe," Babu John, mwanaharakati wa masuala ya kijamii na mjumbe wa shirika la linalomuokoa alisema.

    Afisa katika wizara ya mambo ya nje ya India aliambia BBC kwamba bado wanajaribu kuthibitisha maelezo hayo.

    Nimisha Priya alikuwa ameondoka katika jimbo la kusini mwa India la Kerala kwenda Yemen mwaka 2008 kufanya kazi kama muuguzi.

    Alikamatwa mwaka wa 2017 baada ya mwili wa Mahdi kugunduliwa.

    Msichana huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa sasa amefungwa katika jela kuu ya Sanaa katika mji mkuu wa Yemen.

    Alishtakiwa kwa kumuua Mahdi kwa kumpa "kiwango cha juu cha dawa za kumtuliza" na kudaiwa kuukatakata mwili wake.

    Hata hivyo, Nimisha alikanusha madai hayo.

    Mahakamani, wakili wake alidai kwamba Mahdi alimtesa kimwili, akampokonya pesa zake zote, akamnyang'anya pasipoti yake ya kusafiria na hata kumtishia kwa bunduki.

    Muuguzi huyo alisema alijaribu kumpa dawa ya ganzi Mahdi ili tu kuchukua pasipoti yake kutoka kwake, lakini dozi iliongezeka kwa bahati mbaya.

    Mnamo 2020, mahakama ya eneo hilo ilimhukumu kifo. Familia yake ilipinga uamuzi huo katika Mahakama ya Juu ya Yemen, lakini rufaa yao ilikataliwa mwaka wa 2023.

    Mapema mwezi Januari, Mahdi al-Mashat, rais wa Baraza Kuu la Wahouthi, aliidhinisha kunyongwa kwake.

    Mfumo wa mahakama wa Kiislamu wa Yemen, unaojulikana kama Sharia, unampa matumaini ya mwisho - kupata msamaha kutoka kwa familia ya mwathirika kwa kulipa pesa za damu kwao.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Instagram yashutumu kimakosa baadhi ya watumiaji ikidai wamekiuka sheria za unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto

    Watumiaji wa Instagram wameiambia BBC kuhusu "mfadhaiko mkubwa" juu ya kufungiwa akaunti zao baada ya kushutumiwa kimakosa na jukwaa hilo kwa kukiuka sheria zake za unyanyasaji wa kingono kwa watoto.

    BBC imewasiliana na watu watatu ambao waliambiwa na kampuni yao kubwa ya Meta kwamba akaunti zao zilikuwa zimefungwa kabisa, lakini wakazirejesha muda mfupi baadaye, baada ya kuangaziwa na waandishi wa habari.

    "Nimepoteza usingizi kwa saa kadhaa, nikijihisi kutengwa. Haikuwa hali rahisi, bila kusahau mashtaka kama hayo dhidi yangu," mmoja wa wanaume aliambia BBC News.

    Meta ilikataa kutoa maoni.

    BBC News imewasiliana na zaidi ya watu 100 wanaodai kupigwa marufuku kimakosa na Meta.

    Baadhi wanazungumzia kuhusu upotevu wa mapato baada ya kufungiwa akaunti zao za kibiashara, huku wengine wakiangazia uchungu wa kutoweza tena kufikia picha na kumbukumbu za miaka mingi.

    Wengi wanataja athari waliopata ya afya ya akili.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Kiongozi wa zamani wa Bangladesh aliidhinisha msako mkali, sauti iliyovuja yaonyesha

    Msako mkali dhidi ya maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi nchini Bangladesh mwaka jana uliidhinishwa na waziri mkuu wa wakati huo Sheikh Hasina, kulingana na sauti ya moja ya simu zake zilizothibitishwa na BBC Eye.

    Katika sauti hiyo, ambayo ilivujishwa mtandaoni mnamo mwezi Machi, Hasina anasema aliidhinisha vikosi vyake vya usalama "kutumia silaha hatari" dhidi ya waandamanaji na kwamba "popote watakapowapata, watafyatua risasi".

    Waendesha mashtaka nchini Bangladesh wanapanga kutumia rekodi hiyo kama ushahidi muhimu dhidi ya Hasina, ambaye anashitakiwa bila kuwepo katika mahakama maalum ya uhalifu dhidi ya binadamu.

    Hadi watu 1,400 walikufa katika machafuko ya majira ya joto yaliyopita, kulingana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa.

    Hasina, ambaye alikimbilia India, na chama chake wanakanusha mashtaka yote dhidi yake.

    Msemaji wa chama chake cha Awami League alikanusha sauti hiyo kuonyesha "nia yoyote iliyo kinyume cha sheria".

    Soma zaidi:

  9. Trump na Netanyahu wakutana kwa mara ya pili kuzungumzia usitishaji wa mapigano Gaza

    Rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamekutana kwa mara ya pili mjini Washington kujadili juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ukanda wa Gaza.

    Mkutano huo unafanyika baada ya mjumbe wa Trump Mashariki ya Kati Steve Witkoff kusema Israel na Hamas walikuwa na suala moja ambalo bado hawajakubaliana katika mpango wa kusitisha mapigano wa siku 60.

    Netanyahu alifika Ikulu ya Marekani muda mfupi baada ya 17:00 EST (21:00 GMT) Jumanne kwa mkutano huo, ambao haukuwa wazi kwa waandishi wa habari.

    Mkutano wa viongozi hao wawili ulidumu karibu masaa mawili.

    Kabla ya majadiliano kuanza tena Jumanne, chanzo cha Wapalestina kinachofahamu mazungumzo hayo kiliiambia BBC kuwa hawajapiga hatua yoyote.

    Duru ya hivi punde ya mazungumzo kati ya Hamas na Israel ilianza Jumapili.

    Vita vinavyoendelea Gaza vilianza tarehe 7 Oktoba 2023 wakati Hamas iliposhambulia Israel, na kuua watu 1,200 na kuchukua mateka 251, kulingana na takwimu za Israel.

    Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yameua takriban 57,500 huko Gaza kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Gari la Jota lilikuwa likiendeshwa kwa kasi ya juu sana kabla ya ajali, polisi imesema

    Ushahidi wote kufikia sasa unaonyesha kuwa mchezaji soka wa Ureno Diogo Jota alikuwa anaendesha gari lake alipopata ajali kwenye barabara kuu ya Uhispania, na kuna uwezekano alikuwa akiendesha kwa kasi ya juu sana, polisi wanasema.

    Mchezaji huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 28 alifariki dunia pamoja na kaka yake André Silva, 25, wakati gari lao aina ya Lamborghini kushukiwa kupasuka tairi kaskazini-magharibi mwa mkoa wa Zamora mapema Alhamisi iliyopita.

    Kikosi cha polisi nchini Uhispania kilisema wakati huo gari hilo kuna uwezekano mkubwa lilipita gari jingine katika barabara ya A52 karibu na Palacios de Sanabria lilipoacha barabara na kuwaka moto.

    "Kila kitu kinaashiria uwezekano wa mwendo kasi wa juu sana kupita kiwango kinachokubalika katika [barabara kuu]," walisema polisi wa trafiki wa eneo la Zamora.

    Polisi walisema wamechunguza alama zilizoachwa na tairi moja ya Lamborghini na kwamba "uchunguzi wote uliofanywa hadi sasa unaonyesha kuwa dereva wa gari lililopata ajali alikuwa Diogo Jota".

    Ripoti ya wataalam inatayarishwa kwa ajili ya mahakama juu ya ajali hiyo, na uchunguzi wao unaeleweka umefanywa kuwa mgumu zaidi na ukubwa wa moto ambao uliharibu kabisa gari.

    Soma zaidi:

  11. ICC yatoa vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa Taliban kwa kuwatesa wanawake na wasichana

    Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) imetoa hati za kukamatwa kwa viongozi wawili wakuu wa kundi la Taliban, ikiwatuhumu kuwatesa wanawake na wasichana nchini Afghanistan.

    Mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague ilisema kuna "sababu za kutosha" kuamini kuwa Kiongozi Mkuu Haibatullah Akhundzada na jaji mkuu Abdul Hakim Haqqani walifanya uhalifu dhidi ya binadamu kwa jinsi walivyowatendea wanawake na wasichana tangu kutwaa mamlaka mwaka 2021.

    Katika kipindi chao, wameweka mfululizo wa vikwazo, ikiwa ni pamoja na wasichana zaidi ya 12 kutopata elimu, na kuwazuia wanawake kufanya kazi nyingi.

    Ikijibu, Taliban ilisema haitambui ICC, ikiita hati hiyo "kitendo cha wazi cha uadui" na "matusi kwa wenye imani ya dini ya Kiislamu kote ulimwenguni".

    Pia kumekuwa na vikwazo juu ya umbali gani mwanamke anaweza kusafiri bila kuwa na mwanaume anayemsindikiza, na amri inayowakataza kupaza sauti zao hadharani.

    Katika taarifa yake, ICC ilisema kwamba "wakati Taliban wameweka sheria fulani na marufuku kwa watu kwa ujumla, wamewalenga wasichana na wanawake kwa sababu ya jinsi zao, na kuwanyima haki na uhuru wa kimsingi".

    Umoja wa Mataifa hapo awali ulitaja vikwazo hivyo kuwa ni sawa na "ubaguzi wa kijinsia".

    Serikali ya Taliban imesema inaheshimu haki za wanawake kwa mujibu wa tafsiri yao ya utamaduni wa Afghanistan na sheria za Kiislamu.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Viwanja vya ndege vya Marekani vyaondoa hitaji la wasafiri kuvua viatu wakati wa ukaguzi wa usalama

    Viwanja vya ndege vya Marekani havitahitaji tena abiria kuvua viatu vyao wakati wa ukaguzi wa usalama unaoendeshwa na Utawala wa Usalama wa Usafiri (TSA) - ukiondoa sera hiyo isiyopendwa na watu baada ya miongo miwili.

    Katibu wa Usalama wa Ndani Kristi Noem alisema mabadiliko hayo yalianza kutumika mara moja kwa viwanja vya ndege kote Marekani, ingawa mchakato wa ukaguzi wa usalama wa "viwango kadhaa" utasalia.

    Abiria lazima bado watoe mikanda na makoti na watoe tarakilishi zao na vinywaji kutoka kwenye mikoba, lakini sheria hizo pia zinapitiwa upya, Noem alisema.

    Sharti la abiria wa ndege kuvua viatu ili kufanyiwa ukaguzi lilianza kutekelezwa nchi nzima tangu 2006 baada ya Muingereza kuficha bomu katika kiatu chake kimoja akiwa kwenye safari ya ndege ya kuelekea Miami.

    Noem aliambia mkutano wa wanahabari Jumanne: "Teknolojia yetu ya usalama imebadilika sana. TSA imebadilika.

    "Tuna mfumo mpana, unaojumuisha serikali nzima katika suala la usalama na mazingira ambayo watu wanatazamia na kupitia wanapoingia kwenye uwanja wa ndege ambao umeboreshwa."

    Katibu wa usalama wa ndani aliongeza: "Ni muhimu kutafuta njia za kuwaweka watu salama, lakini pia kurekebisha na kufanya mchakato huo kuwa wa kufurahisha zaidi kwa kila mtu."

    Soma zaidi:

  13. Tiba ya kwanza ya malaria kwa watoto yaidhinishwa kutumika

    Tiba ya kwanza ya malaria inayofaa kwa watoto wachanga na wadogo imeidhinishwa.

    Inatarajiwa kuanza kutumika katika nchi za Afrika ndani ya wiki kadhaa.

    Hadi kufikia sasa hakuna dawa za malaria zilizoidhinishwa hasa kwa watoto.

    Badala yake wamekuwa wakitibiwa kwa matoleo yaliyotengenezwa kwa ajili ya watoto wakubwa jambo ambalo linaleta hatari ya kuzidisha dozi.

    Vifo nusu milioni mnamo 2023

    Mnamo mwaka 2023 - mwaka ambao takwimu za hivi karibuni zinapatikana - ugonjwa wa malaria ulihusishwa na karibu vifo 597,000.

    Takriban vifo vyote vilitokea barani Afrika, na karibu robo tatu yao walikuwa watoto chini ya miaka mitano.

    Matibabu ya malaria kwa watoto yapo lakini hadi sasa, hakukuwa na matibabu mahsusi kwa watoto wachanga zaidi na wadogo, ambao wana uzito wa chini ya 4.5kg au karibu 10lb.

    Badala yake wametibiwa kwa dawa zilizotengenezwa kwa ajili ya watoto wakubwa.

    Lakini hiyo ni hatari, kwani dozi kwa watoto hawa wakubwa huenda isiwe salama kwa Watoto wadogo, ambao uwezo wa ini bado unaendelea kukua na ambao miili yao huchakata dawa kwa njia tofauti.

    Wataalamu wanasema hii imesababisha kile kinachoelezwa kuwa "pengo la kimatibabu".

    Sasa dawa mpya, iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Novartis, imeidhinishwa na mamlaka ya Uswizi na kuna uwezekano wa kusambazwa katika mikoa na nchi zilizo na viwango vya juu vya malaria ndani ya wiki kadhaa.

    Novartis inapanga kuitambulisha kwa misingi isiyo ya faida.

    Soma zaidi:

  14. Marekani yapunguza muda wa viza za wasio wahamiaji wa Nigeria hadi miezi mitatu, kuingia ikiwa mara moja tu

    Marekani imetangaza mabadiliko makubwa katika sera yake ya viza za wasio wahamiaji wa Nigeria, ikipunguza muda na kuweka masharti ni mara ngapi Wanigeria wanaweza kuingia nchini humo.

    Kuanzia Julai 8, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema kuwa karibu viza zote kwa wasio wahamiaji wala wanadiplomasia zinazotolewa kwa raia wa Nigeria sasa wataruhisiwa kuingia nchini humo mara moja tu, muda halali ukiwa miezi mitatu pekee.

    Hatua hii ni sehemu ya marekebisho ya kimataifa ya ushirikiano, tofauti kabisa na masharti ya viza ya awali, ambayo mara kwa mara iliruhusu kuingia mara nyingi zaidi ya miaka miwili.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema sera za viza zitasalia "kuwa chini ya upitiaji upya unaoendelea" na zinaweza kubadilika kulingana na kukua kwa masuala ya kidiplomasia, usalama, na viwango vya uhamiaji.

    Katika taarifa, serikali ya Marekani ilisema inafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya Nigeria kuhakikisha nchi hiyo inakidhi viwango muhimu vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na:

    • Kutoa hati salama za kusafiri
    • Kusimamia suala la kupitisha muda wa viza, na
    • Kushirikisha data za kiusalama au uhalifu kwa usalama wa umma.

    Watalii wa Nigeria, wanafunzi na wasafiri wa kibiashara wanatarajiwa kuwa miongoni mwa wataoathirika zaidi.

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 09/07/2025