Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

ACT Wazalendo yapinga kutenguliwa kwa Mpina kuwania urais Tanzania

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea kwa mshtuko na fadhaa barua ya Tume ya Uchaguzi kuwa mgombea wake wa urais asifike ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri

  2. Uhamishaji wa wakaazi katika mji wa Gaza hauepukiki - jeshi la Israel

    Jeshi la Israel limewaambia Wapalestina kwamba uhamishaji wa wakaazi katika mji wa Gaza "hakuepukiki", huku majeshi yake yakijiandaa kuuteka.

    Katika ujumbe kwenye mtandao X siku ya Jumatano, msemaji wa Kiarabu wa jeshi la Israel Avichay Adraee alisema familia zinazohamia kusini "zitapokea msaada mkubwa zaidi wa kibinadamu".

    Vifaru vya Israel vilisonga hadi eneo jipya la mji wa Gaza usiku kucha, na kuwalazimu wakazi zaidi kutoroka makazi yao, walioshuhudia walisema.

    Maelfu tayari wamehama kwa sababu ya hatua za hivi karibuni za Israel - haswa katika maeneo mengine ya jiji, ambapo takriban Wapalestina milioni bado wanaishi.

    Wito huo wa kuhama unawadia huku Rais wa Marekani Donald Trump akitarajiwa kuongoza mkutano kuhusu maono ya baada ya vita vya Gaza katika Ikulu ya White House.

    Soma zaidi:

  3. Mwanasiasa wa upinzani apatikana na hatia ya matamshi ya chuki Afrika Kusini

    Mwanasiasa mashuhuri wa Afrika Kusini, Julius Malema amepatikana na hatia kwa matamshi ya chuki na mahakama ya nchi hiyo, kufuatia maneno aliyoyatoa kwenye mkutano wa kisiasa.

    Aina ya siasa ya Bw Malema mara nyingi husababisha utata. Mwanasiasa huyo, 44, ni mwanzilishi na kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) ambacho ni maarufu kwa vijana wa Afrika Kusini.

    Mwanasiasa wa upinzaji Julius Malema mara nyingi matamshi yake humuweka matatani - na mahakama ilitoa uamuzi kuwa maneno yake ya mwaka 2022 - "yalionyesha nia ya kuchochea utekelezaji wa maovu."

    Baada ya tukio hilo lililohusisha mzungu anayedaiwa kumshambulia mwanachama wa chama chake, Bw Malema aliwaambia wafuasi "Hamupaswi kuogopa kuua. Mapinduzi wakati fulani, yanataka kuwe na mauaji,"

    Maneno ya Bw Malema yalisababisha mashtaka mawili dhidi yake-mmoja na Tume ya Binadamu na nyingine na mtu ambaye alisema alitishiwa maisha -kufuatia maneno ya Malema.

    Ilikuwa sehemu za video za Bw Malema ambazo Rais wa Marekani, Donald Trump alitumia kumkabili mwenzake Cyril Ramaphosa mnamo mwezi Mei -ingawa Ramaphosa alikanusha kuwa na uhusiano wowote na serikali.

    Bwana Malema amekosoa uamuzi huo, akielezea hukumu hiyo kuwa na dosari - na kuwa maoni yake yalichukuliwa vibaya.

    Soma zaidi:

  4. Ripoti yaonyesha mvutano kati ya jeshi la Mali na mamluki wa Wagner

    Operesheni za kibinafsi za Urusi nchini Mali zimesababisha chuki ndani ya jeshi la taifa hilo la Afrika Magharibi na serikali ya kijeshi, na kupelekea mapungufu ya usalama na kushindwa kupata makubaliano yoyote ya madini, ripoti mpya imebaini.

    Kundi la Wagner lilianza kufanya kazi nchini Mali baada ya jeshi, ambalo lilichukua madaraka katika mapinduzi mawili mnamo 2020 na 2021, kuondoa vikosi vya Ufaransa na Umoja wa Mataifa ambavyo vilikuwa vimehusika katika kupigana na waasi wa Kiisilamu kwa muongo mmoja.

    Kundi la Wagner lilitangaza kuondoka kwake mnamo mwezi Juni, lakini Corps Africa, kikosi kinachodhibitiwa na Urusi, kilisema kitaendelea kuwepo.

    Vikundi vya kutetea haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch lenya makao yake New York, mara kwa mara yamekuwa yakishutumu kundi la Wagner lenye kupigana pamoja na jeshi la Mali, kwa kutekeleza vitendo vya dhuluma na unyanyasaji dhidi ya raia.

    Ripoti hiyo kwa kuzingatia mahojiano na maafisa kutoka kwa jeshi la Mali, shirika la ujasusi, wizara za fedha na madini, na kuchapishwa Jumatano, shirika lenye kufanya uchunguzi - liligundua kuwa Wagner pia imesababisha matatizo kwa jeshi na serikali ilioajiriwa kuunga mkono.

    Kulingana na ripoti hiyo, wanajeshi wa Mali huchukia mamluki wa Urusi ambao "hupendelewa kwa huduma zingine", kama vile kuhamishwa kwa ajili ya matibabu jambo ambalo huwa si rahisi kwa wengine kutokana na uhaba wa mafuta.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi na Wagner haikujibu mara moja maombi ya kutoa maoni yake.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Lil Nas X asema yuko sawa baada ya "siku nne za kutisha"

    Lil Nas X amesema yuko sawa baada ya "siku nne zilizopita za kutisha" tangu alipokamatwa huko Los Angeles.

    Mshindi huyo wa Grammy, anayejulikana kwa wimbo wake wa kufoka wa Old Town Road, alikamatwa siku ya Alhamisi baada ya maafisa wa polisi kusema kuwa aliwashambulia baada ya kumpata akitembea barabarani akiwa uchi. Alipelekwa hospitali kwa matibabu kukiwa na uwezekano wa kutumia madawa kupita kiasi.

    Siku ya Jumatatu, rapper huyo mwenye umri wa miaka 26 alikana kosa la kumjeruhi afisa wa polisi na kukataa kukamatwa. Baadaye aliachiliwa baada ya kulipa dhamana ya $75,000 (£56,000).

    Akiweka ujumbe kwenye Instagram siku ya Jumanne, aliwahakikishia mashabiki akisema: "Msichana wenu atakuwa sawa..." Aliongeza: "zilikuwa siku nne za kutisha zilizopita."

    Soma zaidi:

  6. Aliyekuwa naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua kuwa debeni 2027

    Aliyekuwa naibu wa Rais nchini Kenya Rigathi Gachagua amesema kwamba atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

    Akizungumza kwenye runinga ya Citizen Jumanne usiku, Gachagua alisema amedhamiria kuwa kwenye debe, na kuongeza kuwa ana sifa na ujasiri wa kupata uugwaji mkono wa kutosha.

    "Mimi ni mgombea wa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Nina sifa na nina uugwaji mkono. Natafuta uungwaji mkono zaidi na nitakuwa kwenye debe kama mgombea wa rais," alisema.

    Akijitetea kwa kwasababu ya pingamizi za kisheria zinazomkabili, Gachagua alisema katiba inatoa fursa kwa kila Mkenya kugombea wadhifa wa kuchaguliwa mradi tu machaguo ya kisheria hayajakamilika.

    "Katiba inakuhakikishia haki ya kugombea wadhifa wa kuchaguliwa hata kama umehukumiwa, ikiwa haujamaliza machaguo yanayopatikana kisheria. Mahakama ya Juu Zaidi haijatoa uamuzi kuhusu kuondolewa kwangu madarakani," Gachagua alisema kwenye runinga ya Citizen.

    Soma zaidi:

  7. Mashambulizi mapya yameripotiwa ndani ya Urusi

    Video iliyoonekana na kuthibitishwa na timu ya BBC inaonyesha athari ya shambulio la ndege isiyo na rubani katika jiji la Urusi la Rostov-on-Don.

    Video iliyoshirikishwa kwenye programu ya kutuma ujumbe ya Telegram inaonyesha jengo likiwaka moto baada ya ndege isiyo na rubani kuanguka na kuwaka moto.

    Katika mji wa kusini wa Urusi wa Rostov-on-Don, karibu 200km (maili 125) kutoka eneo la vita la Ukraine, picha kadhaa zinaonyesha jengo likiwaka moto.

    Mchambuzi mwandamizi wa mkoa Yuriy Slyusar, aliweka ujumbe kwenye telegraph, akidai ndege zisizo na rubani 10 zilidunguliwa usiku kucha.

    Vyombo vya habari vya ndani vinasema jengo lililoharibiwa lilikuwa kwenye Njia ya Khalturinsky na picha na video ambayo imethibitishwa na BBC inaonyesha jengo linalowaka moto kwenye kona ya Mtaa wa Moskovskaya.

    Video nyingine, iliyorekodiwa kutoka kwenye roshani ya mita 350 (futi 1,100) kuelekea mashariki, inaonyesha tukio lile lile.

    Wakati huo huo, Urusi imefanya mashambulizi kwa kutumia ndege 95 zisizo na rubani aina ya Shahed na nyinginezo za aina mbalimbali usiku kucha, Jeshi la Wanahewa la Ukraine liliripoti.

    Kulingana na data ya awali, ndege zisizo na rubani 74 za Urusi za Shahed na nyinginezo zilidunguliwa au kuharibiwa na ulinzi wa anga kaskazini, kusini na mashariki mwa nchi, Jeshi la Anga lilisema.

    Athari iliyosababishwa na ndege hizo ilirekodiwa katika maeneo tisa.

    Soma zaidi:

  8. Msafara wa Mpina wazuiwa getini INEC, aenguliwa rasmi

    Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea kwa mshtuko na fadhaa barua ya Tume ya Uchaguzi kuwa mgombea wake wa urais asifike ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi.

    Imesema maamuzi hayo si tu ni aibu bali yanaibua maswali mengi kuhusu uadilifu, umakini, uweledi na uhuru wa Tume iliyopewa dhamana ya kusimamia Katiba, sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza usimamizi wa uchaguzi Tanzania.

    ''Ni hatari kwa Tume na Demokrasia yetu ikiwa uamuzi huu wa kumtaka mgombea asirudishe fomu utabaki bila ya kufutwa na Tume yenyewe, kuendelea na uamuzi huu kutaongeza imaniiliyopo kwa umma kuwa Tume hii si huru na kuwa haiwezi kutenda haki'' ilieleza sehemu ya taarifa ya ACT.

    ACT imeiomba Tume iepuke mtego wa kuifanya itekeleze majukumu yake kinyume na mipaka ya kisheria na katiba.

    Tume ya uchaguzi ilipokea nakala ya barua kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa akitengua uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho.

    Awali Msajili wa Vyama vya Siasa alitangaza kuwa uteuzi wa Mpina kupitia chama chake hicho kipya, haujakidhi matakwa ya kikanuni, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

    Kwa mujibu wa malalamiko ya Monalisa aliyoyawasilisha kwa Msajili, mgombea huyo alikiuka sheria ya chama cha ACT Wazalendo kwa kutokuwa mwanachama wa chama hicho siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.

    Monalisa anasema mwisho w akuchukua fomu za uteuzi ulikuwa mei 25, 2025, kabla ya Mpina kuwa mwanachama hivyo mgombea huyo alikuwa nje ya muda kimchakato wa kikanuni za kiuchaguzi.

    "Mpina alipata uanachama wa ACT - Wazalendo Agosti 5, 2025, siku moja kabla ya kutangazwa kwenye Mkutano mkuu wa chama hicho wa Agosti 6, 2025, kinyume na kanuni zetu zinavyotaka", hakukuwa na ushahidi wa kikao chochote cha chama kilichorekebisha ratiba rasmi ya kuchukua na kurejesha fomu', ilisema sehemu ya taarifa ya Monalisa kuhusu uamuzi wa Msajili.

    Katika uamuzi uliotolewa Agosti 26, 2025 Msajili alibainisha kuwa Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama, akisema kuwa alijiunga ACT-Wazalendo nje ya muda uliopangwa na hivyo hakustahili kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.

    Wakati huo huo, vyombo vya habari Tanzania, ikiwemo Mwananchi imeripoti msafara wa Mpina kuzuiwa getini wakati ukiingia kurejesha fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais wa Tanzania.

    Msafara huo ulifika saa sita mchana na kukutana na maafisa ulinzi wa Jeshi la Polisi waliowazuia kuingia kwenye ofisi za tume.

    Unaweza kusoma;

  9. Ushuru wa 50% wa Trump kwa India waanza huku Modi akihimiza kujitegemea

    Ushuru wa juu wa 50% wa Donald Trump kwa India umeanza, wiki chache baada ya rais wa Marekani kutoa amri ya serikali ya kuweka adhabu ya ziada ya 25% kwa India kutokana na ununuaji wake wa mafuta na silaha za Urusi.

    Hii inafanya India, mojawapo ya washirika wenye nguvu wa Marekani katika Indo-Pasifiki ni miongoni mwa nchi zilizopigwa kwa ushuru wa juu zaidi duniani.

    Hili linaweza kuleta pigo kwa mauzo ya nje na ukuaji katika uchumi wa tano kwa ukubwa duniani, ikizingatiwa kwamba Marekani ilikuwa, hadi hivi karibuni, mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa India.

    Mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitoa ahadi ya kupunguza ushuru ili kupunguza athari zao za kiuchumi.

    Pia amehimiza kujitegemea nyumbani. Alisema kuwa zawadi ya Diwali katika mfumo wa "bonanza kubwa la ushuru" ilikuwa njiani kwa mwananchi wa kawaida na mamilioni ya biashara ndogo ndogo zinazoongoza uchumi wa tatu kwa ukubwa barani Asia.

    Akihutubia umati wa watazamaji mjini Delhi wakati wa sherehe za Siku ya Uhuru, Modi pia aliwataka wamiliki wa maduka madogo na wafanyabiashara kuweka mbao za "Swadeshi" au "Made in India" nje ya maduka yao.

    "Tunapaswa kujitegemea, sio kwa kukata tamaa, lakini kwa kiburi," alisema. "Ubinafsi wa kiuchumi unaongezeka duniani kote na hatupaswi kukaa na kulia juu ya shida zetu, lazima tuinuke juu na tusiwaruhusu wengine kutushikilia katika makucha yao."Alisema Modi.

  10. Korea Kusini yapiga marufuku simu janja shuleni kote nchini

    Korea Kusini imepitisha muswada wa kupiga marufuku matumizi ya simu za mkononi na vifaa janja wakati wa masomo darasani na kuwa nchi ya hivi karibuni zaidi kuzuia matumizi ya simu miongoni mwa watoto na vijana.

    Sheria, ambayo itaanza kutumika kuanzia mwaka ujao wa masomo mnamo Machi 2026, ni matokeo ya juhudi za pande mbili za kuzuia uraibu wa simu janja, kwani utafiti zaidi unaangazia madhara yake.

    Wabunge, wazazi na walimu wamesema kuwa matumizi ya simu janja yanaathiri utendaji wa wanafunzi kitaaluma na kuwaondolea muda ambao wangetumia kusoma.

    Marufuku hiyo ina wakosoaji wake, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, ambao wanahoji jinsi itakavyofanya kazi, athari zake pana na ikiwa inashughulikia sababu kuu ya uraibu.

    Muswada huo ulipitishwa kwa kishindo Jumatano mchana, kwa kura 115 za ndio kati ya wanachama 163 waliohudhuria.

    Shule nyingi za Korea Kusini tayari zimetekeleza aina fulani ya marufuku ya simu hizo.

    Na wao si wa kwanza kufanya hivyo. Baadhi ya nchi kama vile Finland na Ufaransa zimepiga marufuku simu kwa kiwango kidogo, zikitumia kizuizi hicho kwa shule za watoto wadogo pekee.

    Nyingine kama Italia, Uholanzi na China zimezuia matumizi ya simu katika shule zote.

    Lakini Korea Kusini ni miongoni mwa wachache wanaoweka marufuku hiyo kisheria. Watoto siku hizi "hawaonekani kuweka simu zao chini," anasema Choi Eun-young, mama wa mtoto wa miaka 14 huko Seoul.

    Hatahivyo, si watoto tu. Takriban robo ya watu milioni 51 nchini wanategemea sana simu zao, kulingana na utafiti wa serikali wa 2024.

    Lakini takwimu hiyo inaongezeka zaidi ya maradufu hadi 43% kwa wale walio na umri wa kati ya 10 na 19. Na imekuwa ikiongezeka kwa miaka.

    Zaidi ya theluthi moja ya vijana pia wanasema wanatatizika kudhibiti muda wanaotumia kuvinjari video kwenye mitandao ya kijamii.

    Unaweza kusoma;

  11. Trump kuongoza mkutano kuhusu hali ya Gaza siku moja baada ya vita kumalizika

    Rais wa Marekani Donald Trump ataongoza mazungumzo kuhusu Gaza katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff, akiongeza kuwa Washington inatarajia azimio la vita vya Israel huko Gaza ifikapo mwisho wa mwaka.

    Trump alikuwa ameahidi kumalizika kwa haraka kwa vita huko Gaza wakati wa kampeni yake ya uchaguzi wa 2024, lakini baada ya kuchukua madaraka mnamo Januari, lengo hilo linaonekana kutoweza kufikiwa.

    Mkutano huu mpana, unaoongozwa na Trump, unaenda sambamba na mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na mwenzake wa Israel, Gideon Sa'ar, mjini Washington siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

    Alipoulizwa katika mahojiano na Fox News kama kulikuwa na mpango wa awamu ya baada ya vita huko Gaza, Witkoff alisema, "Ndiyo, tuna mkutano katika Ikulu ya White House (Jumatano) ambao utaongozwa na rais, na kuna mpango wa kina ambao tunatayarisha kuhusu siku inayofuata."

    Alipoulizwa, "Je, Israeli inapaswa kuchukua hatua yoyote tofauti kumaliza vita na kuwarudisha mateka nyumbani?" Witkoff alijibu, "Tunaamini tutasuluhisha hili kwa njia moja au nyingine, bila shaka kabla ya mwisho wa mwaka huu."

    Witkov alithibitisha kuwa Israel iko tayari kuendelea na mazungumzo na Hamas. Pia alieleza kuwa vuguvugu hilo limeonesha nia yake ya kufikia suluhu.

    Unaweza kusoma;

  12. UN yataka haki itendeke kutokana na mashambulizi ya Israel dhidi ya hospitali ya Gaza

    Umoja wa Mataifa umesema "kuna haja ya kupatikana kwa haki" kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya hospitali ya Gaza na kusababisha vifo vya takribani watu 20, huku uchunguzi wa awali wa jeshi la Israel ukisema kuwa mashambulizi hayo yalilenga "kamera iliyokuwa iliyowekwa na Hamas".

    Lawama kuhusu shambulio hilo, ambalo waathiriwa wake ni pamoja na waandishi wa habari watano na wafanyakazi wanne wa afya, zimekuwa zikiongezeka, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akikielezea kuwa "haiwezi kutetewa kabisa".

    Baadaye Jumanne Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitoa matokeao ya uchunguzi wake wa awali, ambao ulibaini "dosari" kadhaa kwa uchunguzi zaidi.

    Hatua hiyo ilikuja wakati Waisraeli wakizindua siku ya maandamano ya nchi nzima kuitaka serikali yao kukubali makubaliano ya kuwaachilia mateka.

    Unaweza kusoma;

  13. Urusi kujenga kituo cha nyuklia cha aina yake Niger

    Urusi imeahidi kujenga kituo cha umeme wa nyuklia nchini Niger, taifa lenye utajiri wa urani lakini linaloagiza umeme wake mwingi.

    Ingawa huenda mpango huo usitekelezwe, ni hatua inayoongeza ushawishi wa Moscow barani Afrika wakati Niger ikizidisha mgongano na Ufaransa, aliyekuwa mtawala wa kikoloni.

    Mwezi Juni, serikali ya kijeshi ya Niger ilitaifisha mgodi wa urani uliokuwa chini ya kampuni ya Kifaransa Orano, hatua iliyofungua mlango kwa Urusi kujitokeza kama mshirika mpya.

    Kampuni ya serikali ya Urusi, Rosatom, tayari imesaini makubaliano ya kushirikiana katika uzalishaji wa nishati na matumizi ya kitabibu pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani.

    Iwapo mradi huu utatekelezwa, utakuwa wa kwanza wa aina yake Afrika Magharibi.

    Wakati Ufaransa ilichukua urani ya Niger kwa miongo kadhaa kuendesha mitambo yake ya nyuklia, taifa hilo la Afrika lilibaki likitegemea makaa na umeme wa kuagiza kutoka Nigeria.

    Waziri wa Nishati wa Urusi Sergei Tsivilev alisema mjini Niamey Julai 28 kuwa lengo la Moscow si uchimbaji pekee wa urani, bali kujenga mfumo mzima wa nishati ya atomiki kwa matumizi ya amani nchini Niger.

    Unaweza kusoma;

  14. Urusi yaingia mkoa wa Dnipropetrovsk, Ukraine yathibitisha

    Jeshi la Ukraine limekiri kuwa majeshi ya Urusi yamevuka na kuingia katika mkoa wa viwanda wa Dnipropetrovsk, mashariki mwa nchi hiyo, na kujaribu kujikita katika eneo hilo.

    Afisa wa kundi la kijeshi la Dnipro, Viktor Trehubov, ameiambia BBC kuwa huu ndio mashambulizi ya kwanza ya kiwango kikubwa katika mkoa huo, ingawa alisisitiza kuwa jeshi la Ukraine limefanikiwa kusimamisha kasi ya adui.

    Tangu mapema kiangazi, Urusi imekuwa ikidai mara kwa mara kuwa majeshi yake yameingia Dnipropetrovsk kupitia Donetsk, ambapo mapigano makali yamekuwa yakiendelea.

    Mwezi Juni, viongozi wa Urusi walitangaza kuanza kwa operesheni katika eneo hilo, lakini ripoti za hivi karibuni kutoka Ukraine zinaonesha kuwa wapiganaji wa Urusi wamepenya kidogo tu katika mpaka wa mkoa huo.

    Mkoa wa Dnipropetrovsk, ambao kabla ya vita ulikuwa na wakazi zaidi ya milioni tatu, ni kituo kikubwa cha pili cha viwanda nchini Ukraine baada ya Donbas (inayojumuisha Donetsk na Luhansk).

    Ingawa Urusi haijatangaza rasmi kudai Dnipropetrovsk kama ilivyofanya kwa baadhi ya mikoa ya mashariki, imekuwa ikishambulia miji yake mikuu ikiwemo mji wa Dnipro.

    Hali hii inakuja wakati Marekani ikiendelea kuongoza juhudi za kidiplomasia kumaliza vita, licha ya mazungumzo kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin yaliyofanyika Alaska kutoonesha mafanikio makubwa.

    Ripoti zinaeleza kuwa Putin alimweleza Trump yuko tayari kusitisha vita endapo Ukraine itakubali kukabidhi maeneo ya Donetsk yanayodhibitiwa na Kyiv, ingawa wananchi wengi wa Ukraine wanaamini Urusi ina ajenda pana zaidi.

    Unaweza kusoma;

  15. Wagombea urais, ubunge, udiwani Tanzania kujulikana leo

    Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajiwa leo, Jumatano Agosti 27, 2025, kufanya zoezi la uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wagombea wa Ubunge na Udiwani kote nchini.

    Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi na masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi huo utaanza saa 1:30 asubuhi na kukamilika saa 10:00 jioni.

    Zoezi la uteuzi wa wagombea wa urais litafanyika katika ofisi za INEC, Njedengwa jijini Dodoma, wakati wagombea wa ubunge watawasilisha fomu kwa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo na wagombea udiwani kwa wasimamizi wasaidizi katika ngazi ya kata.

    Mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi, INEC imesema majina ya wagombea wote yatabandikwa kwenye mbao za matangazo katika maeneo husika kwa ajili ya ukaguzi wa umma.

    Tume imewataka vyama vya siasa na wagombea kuhakikisha wanazingatia muda uliopangwa na maelekezo waliyopatiwa, ili kuepuka changamoto katika zoezi hilo muhimu.

    Unaweza kusoma;

  16. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo