Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump aitaka Iran ijisalimishe bila masharti, Putin azungumza na rais wa Iran

Trump ametoa wito huo wakati vita kati ya Marekani ikishirikiana na Israel dhidi Iran vinaingia wiki ya pili huku mashambulizi ya kijeshi yakiripotiwa kote Mashariki ya Kati.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Ghana yataka uchunguzi wa UN baada ya wanajeshi wake kujeruhiwa Lebanon

    Ghana imewasilisha rasmi malalamiko kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, baada ya shambulio kusini mwa Lebanon kuwajeruhi wanajeshi wake wawili wa kulinda amani.

    Waziri wa Mambo ya nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema serikali inadai uchunguzi kamili, wa haraka, usio na upendeleo na wa wazi kuhusu tukio hilo.

    Amesema shambulio hilo linakiuka sheria za kimataifa na linaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

    Wanajeshi hao wa Ghana wako nchini Lebanon kama sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinachoitwa United Nations Interim Force in Lebanon (UNIFIL), ambacho kimepelekwa kufuatilia mpaka kati ya Israel na Lebanon.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Ghana, makao makuu ya kikosi cha Ghana kusini mwa Lebanon yalilengwa na makombora Ijumaa jioni.

    Hadi sasa haijulikani ni nani aliyetekelezwa shambulio hilo.

    Serikali ya Ghana imelilaani vikali tukio hilo na pia imesisitiza kuwa wale wote waliohusika lazima watambuliwe na kuwajibishwa.

    Tukio hili linatokea wakati mvutano unaongezeka sana kwenye mpaka wa Israel na Lebanon. Mapigano yameongezeka kati ya jeshi la Israel na kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

    Hezbollah imeanza kushambulia kaskazini mwa Israel kwa roketi na ndege zisizo na rubani karibu kila siku, ingawa Israel inasema mashambulizi hayo yanazuiwa na mifumo yake ya ulinzi wa anga.

    Wakati huo huo, Israel imetoa amri ya kuwataka watu kuhama katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon, umbali wa takribani kilomita 27 ndani ya nchi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Iran haitashambulia mataifa jirani, asema rais wa Iran

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ametangaza ujumbe wa video kwenye televisheni ya taifa ya Iran akisema: “Naona ni muhimu kuomba msamaha kwa nchi jirani ambazo zilishambuliwa.”

    Amesisitiza pia kwamba Iran haina nia ya kuvamia nchi Jirani na kutaka mataifa y a ukanda huo kuhakikisha amani na utulivu.

    Pezeshkian aliongeza kuwa amri imetolewa kwa majeshi ya Iran:

    “Kuanzia sasa, msishambulie nchi jirani isipokuwa kama Iran itashambuliwa kwanza.”

    Aidha alionya kwamba: “Wale wanaofikiria kutumia fursa ya wakati huu kushambulia Iran hawapaswi kuwa vibaraka wa ubeberu.”

    Mwisho, rais huyo alisema kuwa kuunga mkono Israel au Marekani haitafsiri heshima na uhuru.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Watu 10 wafariki kwa mafuriko Nairobi

    Watu 10 wamethibitishwa kufariki jijini Nairobi kufuatia mafuriko makubwa yaliyokumba jiji hilo siku ya Ijumaa.

    Kamanda wa Polisi jijini Nairobi George Seda alisema watu nane walisombwa na maji ya mafuriko yanayoongezeka kwa kasi, huku wengine wakifariki wakiwa ndani ya magari yaliyobebwa na mkondo wa maji.

    Seda aliongeza kuwa waathiriwa wengine wawili walifariki katika matukio tofauti ya umeme wakati wa mafuriko katika sehemu tofauti za kaunti.

    Aidha ameongeza kuwa, takriban magari 71 yalikwama jijini Nairobi baada ya barabara kuu kutopitika kutokana na mafuriko makubwa.

    Kamanda Seda alionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa vibaya na mafuriko.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Tumetekeleza mashambulizi zaidi ya 3,000 nchini Iran: Marekani

    Kamati ya usalama ya Marekani, ambayo inaongoza shughuli za kijeshi za nchi hiyo, inasema imetekeleza mashambulizi zaidi ya 3,000 nchini Iran.

    Meli zipatazo 43 pia zimeshambuliwa au kuharibiwa kama sehemu ya Operesheni Epic Fury, ilitangaza katika chapisho lake katika X.

    Mashambulizi hayo yanapewa kipaumbele kulingana na "maeneo ambayo yanasababisha uwezekano wa kuwa na tishio" kwa lengo la "kubomoa vifaa vya usalama vya utawala wa Iran".

    Uchambuzi wa BBC wa picha na video za setilaiti umeonyesha kuwa shule za Iran, hospitali na mengine muhimu ni miongoni mwa maeneo ya raia ambayo yameathiriwa na mashambulizi ya Marekani na Israeli.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Qatar yafungua anga kuruhusu safari chache za ndege

    Qatar imetangaza kuanza tena kwa safari chache za ndege kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza wiki moja iliyopita.

    Mamlaka ya usafiri wa anga ya nchi hiyo ilisema kuwa anga ya Qatar itafunguliwa kwa sehemu ili kuruhusu tu safari za uokoaji na ndege muhimu za mizigo.

    Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamad umefafanua kuwa safari nyingine katika siku zijazo zitategemea tathmini inayoendelea ya hali ya usalama.

    Maafisa wa Qatar walisema mapema wiki hii kuwa jeshi lilifanikiwa kuzuia jaribio la mashambulizi ya Iran dhidi ya uwanja huo wa ndege.

    Wizara ya ulinzi iliripoti kuwa Qatar ilidungua ndege tisa zisizo na rubani siku ya Ijumaa.

    Moja ya hizo ilianguka katika eneo lisilo na watu bila kusababisha majeruhi.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mashuhuda waripoti milipuko katika uwanja mkubwa wa ndege Tehran

    Kumeshuhudiwa shambulio kubwa katika moja ya viwanja vikuu vya ndege vya kibiashara mjini Tehran.

    Ndege inayowaka moto pamoja na moshi mkubwa unaonekana katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, ambao ni uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi nchini Iran na kitovu kikuu cha safari za ndani.

    Hali hiyo inaonekana katika video zilizochapishwa na mashuhuda kwenye mitandao ya kijamii.

    Picha za satelaiti zilizopigwa Ijumaa zinaonyesha kuwa kulikuwa na ndege kadhaa katika uwanja huo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia vinaripoti kuwa baadhi ya sehemu za uwanja wa ndege zimelengwa katika shambulio hilo.

    Tukio hili linakuja baada ya jeshi la Israel kusema kuwa linaanzisha “wimbi jipya la mashambulizi makubwa” nchini Iran.

    Hapo awali lililenga uwanja huo tarehe 4 Machi, likisema mashambulizi yake yalibomoa mifumo ya ulinzi na ilikuwa tishio kwa Jeshi la anga la Israel, ikiwemo sehemu ya kutengeneza helikopta katika uwanja huo.

    Bado haijafahamika ni sehemu gani hasa za uwanja wa ndege zimepigwa katika shambulio jipya, lakini mashuhuda wanasema mashambulizi ya usiku huu yamekuwa makali zaidi.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Trump aitaka Iran ijisalimishe bila masharti, Putin azungumza na rais wa Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Iran kujisalimisha bila masharti huku mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel yakiendelea. Trump amesema baada ya Iran kuchagua uongozi mpya unaokubalika na Washington, Marekani na washirika wake wataisaidia nchi hiyo kuimarisha uchumi wake.

    Kauli hiyo imekuja wakati vita vinaingia wiki ya pili tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei katika mashambulizi ya hivi karibuni. Hata hivyo bado haijulikani nani ataIongoza Iran baada ya tukio hilo.

    Ikulu ya Marekani imesema operesheni za kijeshi zinaweza kudumu kati ya wiki nne hadi sita, huku lengo likiwa kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran.

    Wakati huo huo, rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa simu na rais wa Iran Masoud Pezeshkian, akitoa pole kwa vifo vilivyotokea katika mashambulizi hayo.

    Urusi imesisitiza kuwa mapigano yanapaswa kusitishwa mara moja na kutafutwa suluhisho la kidiplomasia. Iran nayo imeishukuru Urusi kwa kuendelea kuiunga mkono.

    Wakati huo huo, mapigano yameongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kundi la Hezbollah kushambulia Israel, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yakiripotiwa katika nchi kadhaa zenye kambi za kijeshi za Marekani.