Mashambulizi ya Israel hayapaswi 'kupuuzwa' - Kiongozi mkuu wa Iran

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema shambulizi dhidi ya Iran lilifanikisha malengo yake yote.

Muhtasari

  • Wimbi jipya la mauaji ya halaiki nchini Sudan laipa wasiwasi Umoja wa mataifa
  • “Tulisikia sauti kubwa”: Mwandishi wa BBC aeleza jinsi shambulizi lilivyotokea
  • Shambulizi lililotekelezwa dhidi ya Iran lilitimiza malengo yake - Netanyahu
  • Mashambulizi ya Israel hayapaswi kupuuzwa, asema kiongozi mkuu wa Iran
  • Kinachotarajiwa kenye kampeni za mwisho kabla ya Uchaguzi Marekani 2024
  • Muongozo rahisi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Marekani
  • Wakenya wataka mwanaharakati Boniface Mwangi kuachiliwa huru
  • Makumi ya watu wajeruhiwa baada ya lori kugonga kituo cha basi katikati mwa Israel
  • Kenya: Mwanaharakati Boniface Mwangi adaiwa kutekwa nyara
  • Kongamano lililoandaliwa na Papa Mtakatifu lakamilika na ombi la kutaka nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake
  • Chama ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 58, cha ahidi kufanya mabadiliko nchini Botswana
  • Michelle Obama azungumzia uavyaji mimba huku Trump akiungwa mkono na viongozi wa Kiislamu
  • Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yawauwa wanajeshi wanne - Iran

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Wimbi jipya la mauaji ya halaiki nchini Sudan laipa wasiwasi Umoja wa mataifa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mapigano yanayoendelezwa katika jimbo la Gezira nchini Sudan yamewalazimu raia kuhama makazi yao

    Na Farouk Chothia

    BBC News

    Afisa mmoja mkuu wa umoja wa mataifa nchini Sudan amesema kwamba ametiwa wasiwasi mkubwa na ripoti za madhila makubwa ya kihalifu yanayotekelezwa katika jimbo la kati nchini Sudan la Gezira, ikiwemo mauaji ya halaiki ya raia yanayotekelezwa na kikosi maalum cha wanamgambo cha Rapid Support Force RSF.

    Clementine Nkweta-Salami ametoa matamshi yake baada ya kundi la wanaharakati kusema kwamba watu 124 wameuawa na kikosi cha RSF kwenye mashambulizi yaliyotekelezwa kwenye vijiji katika wiki moja iliyopita.

    RSF imekanusha shutuma hizo kwamba inawalenga raia, ikisema kwamba wapiganaji wake wanakabiliana na waasi waliopewa silaha na jeshi la Sudan.

    Mzozo huo ambao umeendelea kwa miezi 18 sasa umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine milioni 11 kuhama makwao.

    Nkweta-Salam , ambaye ni msimamizi wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa mataifa nchini Sudan, amesema kwamba taarifa za awali zimeashiria kwamba RSF ilitekeleza mashambulizi mawili katika maeneo tofauti kwenye jimbo la Gezira kati ya Oktoba 20 na 25, 2024.

    Aidha amesema kwamba hali hiyo ilichangia maafa ya watu wengi na kuwa shambulizi la halaiki, huku wanawake wakibakwa, nazo biashara zikiporwa na wengine kupora mali ya watu kwenye makazi ya kibinafsi na hata kuchoma mashamba ya watu.

    Bi Nkweta - Salam amesema kwamba maovu hayo ya kihalifu ni saw ana kilichoshuhudiwa katika jimbo la Darfur mwaka wa 2023, wakati ambapo RSF ilishutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ambazo zilionekana kupinga kikosi hicho.

    Nkweta Salam, aidha amesema kwamba idadi kamili ya waliofariki haijulikani, lakini taarifa za awali zimeonyesha kwamba wengi waliuawa katika jimbo la Gezira.

  3. “Tulisikia sauti kubwa”: Mwandishi wa BBC aeleza jinsi shambulizi lilivyotokea.

    Na Nawal Al-Maghafi

    Kutoka eneo la kuegesha magari la hospitali kuu ya Sidon, Hammond, tulisikia sauti kubwa, ambayo ilikuwa sauti ya shambulizi la angani lililotokea takriban mita 600 kutoka tulipokuwa katika barabara kuu ya mji huo - Haret Saidah.

    Bila ya kutoa tahadhari ya muda wa watu kuondoka eneo hilo, shambulizi hilo halikutarajiwa kabisa, kwani mashambulizi katika eneo hili la Lebanon hayajashuhudiwa mara kwa mara, la mwisho likiripotiwa Oktoba 15.

    Katika muda wa dakika chache, sauti za ambulensi zilisikika zikija upande tulipokuwa zikiwa zimebeba majeruhi, huku watu Wattana wakithibitishwa kufariki na wengine 11 wakiwa na majeraha.

    Haya yote ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon.

    BBC imepokea taarifa kuwa shambulizi hilo lililenga ghorofa moja ya jumba la makazi ya watu na magari mawili yalikuwa nje ya jumba hilo – hadi sasa eneo hilo halijajulikana.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa ulinzi wa Israel aipa Marekani taarifa ya ripoti kuhusu mashambulizi dhidi ya Iran

    Wakati huo huo, taarifa zaidi kutoka wizara ya ulinzi ya Israel imesema Waziri Yoav Gallant alimuarifu Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kuhusu shambulizi la Israel dhidi ya Iran.

    Haya ni kwa mujibu wa kituo cha habari cha Reuters.

    Waziri wa ulinzi wa Israel alizungumzia tathmini za awali za shambulizi la makombora kwenye viwanda vya kutengezea makombora, utumizi wa makombora ya kutoka ardhini yanayolenga angani na uwezo wa kivita wa Iran hasa katika shambulizi la angani, kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

    “Waziri Gallant pia alizungumiza nafasi muhimu zilizojitokeza kutokana na operesheni inayoendelea na mafanikio yake, katika eneo la kaskazini na kusini mwa Israel,” taarifa hiyo imeeleza kuhusu yanayojiri Lebanon na Gaza.

  4. Shambulizi lililotekelezwa dhidi ya Iran lilitimiza malengo yake - Netanyahu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akizungumza Jumapili Oktoba 27 kuhusu mashambulizi yaliyotekelezwa na jeshi la Israel nchini Iran usiku wa Ijumaa.

    Amesema kwamba shambulizi hilo la Israel, lilikuwa limelenga eneo maalum na lilikuwa lenye nguvu na lilitimiza malengo yake.

    Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant pia amesema kwamba sio malengo yote ya Israel ambayo yatatimizwa kupitia operesheni za kivita, huku akionya kwamba kutakuwa na hatua kali na chungu zitakazohitajika kufanyika ili kuwanasua mateka wanaoendelea kuzuiliwa Gaza, kwa mujibu wa ripoti za shirika la Habari la AFP.

    Pia amezungumzia jinsi operesheni za kijeshi za Israel zimelemaza shughuli za Hamas huko Gaza na Hezbollah huko Lebanon makundi ambayo ni washirika wakubwa wa Iran dhidi ya Israel.

    Majibu kutoka kwa Iran yamesalia kwa kiwango kikubwa kuwa yamezimwa

    Na Sebastian Usher

    Katika sherehe ya kuadhimisha mwaka mmoja wa shambulizi la Oktoba 7 katika kalenda ya Kihibrania inayofuatwa na Wayahudi, Netanyahu alisema kwamba mashambulizi ya anga ndani ya Iran yalilenga maeneo makhususi na yalikuwa yenye nguvu.

    Aliwazungumzia raia wa Iran na kuwaeleza kwamba vita vya Israel haviwahusu wao wala havitawalenga.

    Athari ya shambulizi hilo ingali inaangaliwa kupitia picha za satelaiti zinazoonyesha eneo la Parchin ambalo ni kambi kubwa ya jeshi iliyo karibu na Tehran, iliyolengwa

    Majibu ya Iran yamekuwa madogo – huku kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatolah Ali Khamenei akisema kwamba Tehran ni sharti ijibu kwa kusahihisha alichokitaja kuwa mapungufu ya kimkakati ya Israel.

    Amesema kwamba majibu yoyote yataamuliwa kulingana na kikubwa kinachofaa Iran.

    Hayo yanajiri huku juhudi mpya ya kuanzisha upya mazungumzo ya kusitisha vita na kuachiliwa huru kwa mateka walioko Gaza zinaendelea, huku viongozi wa MOSSAD na CIA wakitarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Qatar – ambaye amekuwa mpatanishi mkubwa.

    Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema kwamba kuwaachilia huru mateka kutahitaji maafikiano machungu.

  5. Mashambulizi ya Israel hayapaswi kupuuzwa, asema kiongozi mkuu wa Iran

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei amesema kwamba mashambulizi ya anga ya Israel ambayo yalilenga Tehran na maeneo mengine siku ya Ijumaa usiku hayapaswi kupuuzwa wala kuonekana kuwa makubwa kuliko yalivyotokea.

    Jeshi la Iran limesema kwamba wanajeshi wanne waliuawa kwenye shambulizi la anga ambalo jeshi la Israel lilisema lililenga maeneo ya kijeshi.

    Khamenei amesema kwamba Israel ilifanya makosa ya kimkakati kuhusu Iran, jambo ambalo Tahran ni sharti ilifanyie kazi, kulingana na afisa aliyenukulina na kituo cha Habari cha kitaifa cha IRNA.

    “Hawaifahamu vizuri Iran, “na” hawajaelewa kwa undani na vyema nguvu, uwezo na juhudi na ari ya taifa la Iran. Ni lazima tuelewe vizuri,” aliongezea.

    Wanane wauawa kwenye shambulizi la Israel, yasema wizara ya afya ya Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Moshi unafuka angani baada ya shambulizi la Israel huko Sidon.

    Tunapokea taarifa kwamba watu wanane wameuawa huku wengine 25 wakijeruhiwa kwenye shambulizi la Israel katika mji wa Lebanon wa Sidon.

    Haya ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon.

    Mwandishi wetu, Nawal Al-Maghafi, alisema hakukuwa na notisi ya kuhama na anasema chanzo kilithibitisha kuwa shambulizi hilo lilitokea kwenye nyumba ya ghorofa moja na pia kulikuwa na magari mawili nje.

    Tunapokea taarifa kwamba watu wanane wameuawa huku wengine 25 wakijeruhiwa kwenye shambulizi la Israel katika mji wa Lebanon wa Sidon.

    Haya ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon.

    Mwandishi wetu, Nawal Al-Maghafi, alisema hakukuwa na notisi ya kuhama na anasema chanzo kilithibitisha kuwa shambulizi hilo lilitokea kwenye nyumba ya ghorofa moja na pia kulikuwa na magari mawili nje.

  6. Kinachotarajiwa kenye kampeni za mwisho kabla ya Uchaguzi Marekani 2024

    .

    Wiki iliyopita imekuwa yenye shughuli nyingi kwa wagombea wawili wakuu kwenye uchaguzi ujao wa Marekani na huku siku ya kupiga kura ikiendelea kukaribia wawili hao hawaonekani kupunguza kasi za kutafuta kura.

    Kwa hivyo, tutarajie nini baada ya hapa katika kinyang’anyiro hicho kigumu chenye mambo mengi yanayochipuka?

    Kamala Harris

    Anajarajiwa kuendeleza kampeni zake huko Philadelphia, katika jimbo la Pennsylvania lenye ushawishi mkubwa wa kuamua mshindi.

    Jimbo hilo lilikuwa muhimu katika uchaguzi wa 2020, kwani ni mojawapo ya majimbo ambapo Joe Biden alipata uungwaji mkono na kukipa chama cha Democratic ushindi.

    Linatazamiwa kama mojawapo ya majimbo saba yenye ushawishi mkubwa katika uamuzi wa mshindi wa urais nchini Marekani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka.

    Donald Trump

    Anaendeleza kampeni zake kwenye jimbo la nyumbani la New York, atakapoandaa mkutano wa kisiasa kwenye ukumbi wa Madison Square Garden.

    Japo New York haitambuliki kama jimbo lenye ushawishi wa kuamua mshindi wa urais, jimbo hilo limekuwa na utamaduni wa kumuunga mkono mgombea wa chama cha Democratic kwa miongo mingi.

    Lakini ukumbi wenye ghorofa kadhaa wa Madison Square Garden unatambulika kwenye kumbukumbu ya historia ya nchi hiyo kuwa mwenyeji wa matukio muhimu ya kitamaduni, kisanaa, na kispoti na kwa sasa inatoa nafasi kubwa kwa Trump kuendeleza sera zake.

    Mshirki wa BBC nchini Marekani CBS News imesema kwamba Trump atafika jukwaani mwendo was saa 11 jioni (sawia na 2100 GMT/ Saa 7 usiku saa za Afrika mashariki.)

    Maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo, wengi wao wakiwa wamekesha nje ya ukumbi huo usiku wa kuamkia Jumapili kwa ajili ya kujipatia nafasi ya kiingilio.

  7. Muongozo rahisi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Marekani

    .

    Hebu turejee nyuma kidogo na kujifahamisha kuhusu masuala muhimu kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani unaotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba.

    Uchaguzi utafanyika lini?

    Jumanne Novemba 5, 2024.

    Ni nani anaweza kupiga kura?

    Raia wa Marekani wenye umri wa miaka 18 na zaidi. Wanapaswa kuwa wamesajiliwa kama wapiga kura (Isipokuwa kwenye jimbo la North Dakota) na vile vile raia wa Marekani wanaoishi nje ya nchi hiyo wanaweza kujisajili kupiga kura kwa njia ya posta.

    Wagombea ni kina nani?

    Makamu wa Rais Kamala Harris anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Democratic, baada ya Rais Joe Biden kujiondoa na kutokuwa na mgombea mwengine aliyejitokeza kwenye chama hicho.

    Rais wa zamani Donald Trump, anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Republican na anajaribu kunyakuwa kiti hicho kwa mara ya pili.

    Mshindi ataamuliwa vipi?

    Kila jimbo nchini Marekani – Kuna Majimbo – Yana idadi ya kura maalum zinazofahamika kama ELECTORAL COLLEGE VOTES, ambazo zinaambatana na idadi ya jumla ya wakaazi wa majimbo hayo. Kukiwa na jumla ya kura 538 maaluma za Electoral college zikiwa zinapiganiwa, Harris au Trump ni sharti washinde angalau kura 270 ili kutangazwa mshindi.

    Wanapigia kura nani haswa?

    Mbali na kura ya Urais itakayopigwa, Raia wa Marekani pia watakuwa wanapiga kura ya kuwachagua baadhi ya wabunge wa bunge la Congress ambalo lina umuhimu mkubwa wa kupitisha sheria.

    Mshindi atatangazwa lini?

    Kwa kawaida usiku wa kura kupigwa, lakini mnamo 2020, ilichukuwa siku kadhaa kuhesabu kura zote.

    Rais Mteule huapishwa rasmi mwezi Januari 2025, kwenye sherehe ya uapisho itakayoandaliwa mjini Washington DC.

    Jimbo lenye ushawishi wa uamuzi wa mshindi wa urais ni lipi, na ni kwa nini yana umuhimu mkubwa?

    Majimbo yenye ushawishi mkubwa na yenye uwezo wa kuamua mshindi wa urais yaani SWING STATES - ambayo pia hutambulika kama majimbo ambapo makabiliano ya kupata uungwaji mkono yatafanyika – ni yale ambayo wagombea wote wawili wana nafasi bora ya kushinda japo uwezo huu hubadilika kutoka kwa chama kimoja hadi kingine, ndio maana yakatajwa kama kuwa katika hali ya kuhamahama kutoka upande mmoja hadi mwingine.

    Upigaji kura kwenye majimbo ya aina hii, na matokeo yake ni hali ngumu ya kutabiri lakini katika muda mchache unaokaribia siku ya kupiga kura, wagombea wa Urais Kamala Harris na Donald Trump wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya kampeni kwenye majimbo hayo.

    Uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huenda ukaamuliwa na matokeo kutoka majimbo yafuatayo: Pennsylvania, Wisconsin, North Carolina, Georgia, Michigan, Arizona na Nevada.

  8. Wakenya wataka mwanaharakati Boniface Mwangi kuachiliwa huru

    .

    Chanzo cha picha, Courtesy Brian Inganga

    Baadhi ya Wakenya wamepaza sauti wakitaka mwanaharakati Boniface Mwangi kuachiliwa huru baada ya kutekwa nyara nyumbani kwake alfajiri ya Jumapili na watu wasiojulikana.

    Mke wake Njeri Mwangi amethibitisha tukio hilo kwenye akaunti yake ya mtandao wa X.

    Kulingana na Njeri, Boniface alichukuliwa nyumbani na watu wasiojulikana mwendo wa saa moja asubuhi Jumapili.

    Taarifa hizo zimezua hasira miongoni mwa Wakenya ambao wameilaumu serikali kwa kuhusika kwenye visa vingi vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini Kenya.

    Katika taarifa inayotazamiwa kuwa inaangazia kutekwa kwa Mwangi, aliyekuwa Rais wa chama cha mawakili nchini Kenya Eric Theuri ametaja hali ya polisi kuweka raia katika hali ya kuogopa na kuwazuia kutotoa maoni yao hadharani.

    “Mapinduzi hubuniwa hivi. Matumizi ya njia zilizokuwa za kikatiba itachangia tu hali ya utawala huria.

    “Visa vya watu kutekwa na matumizi ya polisi kukandamiza haki za watu kuwa na maoni kinzani na serikali kutaleta ukaidi zaidi. Siku moja, uoga utawatoka raia,’ Theuri alisema.

    Mwandishi wa CNN Larry Madowo amezungumzia suala hilo kwa kusema kwamba visa vya utekaji nyara vimeendelea kuwanasa na kuwakandamiza wanaharakati na wapinzani wakuu wa serikali japo serikali imekanusha kuhusika.

    “Mwanaharakati kutoka Kenya ametekwa nyara na watu wasiojulikana.#FreeBonifaceMwangi,” Alisema Larry Madowo kwenye Mtandao wa X.

    Mwandishi mpekuzi John Allan Namu pia amezungumzia suala la ubakaji kwenye mtandao wa X : “ Hili linapaswa kukoma. #FreeBonifaceMwangi”.

    Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamelaani kutekwa kwa Mwangi.

    Social centres working group wameshutumu kitendo hicho pia na kusema:

    “Tunalaani vikali kitendo hicho kilichotekelezwa na maafisa wa serikali. Mwangi ni mwanaharakati wa haki za kibinadamu ambaye hajakosa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, alikuwa amepanga kuhudhuria mbio za Standard Chartered Marathon. Kuzuiliwa kwa Mwangi kinyume na sheria ni jambo la kuhuzunisha na kukiuka uhuru wa kujieleza. #FreeBonifaceMwangi

    Kundi la The Defenders Coalition kwa upande wake limetaja hatua hiyo ya Mwangi kutekwa kama ukiukaji mkubwa wa haki zake za kibinadamu wakiongezea kwamba uchokozi wa aina hiyo hautakubalika.

    Hata hiyo, polisi imetoa taarifa na kusema wanamzuilia katika kituo cha polisi cha Kamukunji jijini Nairobi

  9. Makumi ya watu wajeruhiwa baada ya lori kugonga kituo cha basi katikati mwa Israel

    .

    Chanzo cha picha, Magen David Adom

    Makumi ya watu wameripotiwa kujeruhiwa baada ya lori kugonga kituo cha basi katika kile kinachoshukiwa kuwa shambulio la makusudi katikati mwa Israel.

    Takriban watu wanne wako katika hali mbaya na wengine bado wamenaswa chini ya mabaki ya lori hilo katika eneo la Glilot, kaskazini mwa Tel Aviv.

    Polisi wanasema mazingira ya tukio hilo bado yanachunguzwa, lakini vyombo vya habari vya ndani viliripoti tukio hilo kama linaloshukiwa kuwa shambulio.

    Chaneli za televisheni za Israel zilionyesha polisi wakiwa wamezingira eneo hilo huku wahudumu wa dharura wakiwasaidia majeruhi na helikopta ikiwa inapaa juu yake.

    "Saa 10:08 asubuhi, ripoti ilipokelewa katika Kituo cha Simu za Dharura cha MDA 101 katika Mkoa wa Yarkon kuhusu lori lililokuwa limegonga kituo cha basi huko Ramat Hasharon", Huduma za dharura za Israel zilisema katika taarifa.

  10. Kenya: Mwanaharakati Boniface Mwangi adaiwa kutekwa nyara

    Mwanaharakati mmoja nchini Kenya Boniface Mwangi amechukuliwa na watu wasiojulikana kutoka nyumbani kwake leo Jumapili.

    Mkewe Njeri Mwangi amethibitisha kisa hicho. Matukio ya hivi punde yanafanyika saa 24 baada ya Mwangi kufichua mipango ya kujipenyeza katika mbio za Standard Chartered Marathon, zinazofanyika leo Jumapili, Oktoba 27 akiwa na nia ya kufanya maandamano.

    Mkewe Njeri Mwangi alithibitisha kisa hicho.

    Usalama uliimarishwa katika mbio hizo huku barabara kuu zikifungwa.

    Polisi walifichua kuwa walikuwa tayari kushughulikia aina yoyote ya vitisho kutoka kwa maandamano yaliyopangwa na mengine.

    Polisi waliovalia sare na wengine waliovalia kama raia walitumwa kwenye hafla ya mbio hizo.

    “Tunamfahamu yeye na wafuasi wake. Wao ni wajasiri na wanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa hafla hiyo kwa hivyo hatua ya kupeleka polisi zaidi imechukuliwa,” alisema afisa anayefahamu suala hilo.

    Katika ujumbe wake siku ya Jumamosi jioni, mwanaharakati huyo aliwataka wafuasi wake kujitokeza kwa mbio hizo za marathon wakiwa na mavazi yanayopinga utawala wa Kenya Kwanza.

    Kulingana na Njeri, mwanaharakati huyo alichukuliwa na watu wasiojulikana Jumapili asubuhi mwendo wa saa moja na dakika kumi na tano asubuhi.

  11. Kongamano lililoandaliwa na Papa Mtakatifu lakamilika na ombi la kutaka nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Kongamano la mwezi mzima lililoandaliwa kwenye makao makuu ya Papa Mtakatifu ya Vatican, limekamilika huku walioshiriki wakitoa ombi kwa kanisa katoliki kubuni nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake.

    Ila ombi hilo halijaangazia suala la kuwataka wanawake kuhudumu kama mapadri, jambo ambalo baadhi walitarajia litajadiliwa kwenye vikao hivyo vya mwezi mzima.

    Mkutano huo wa majimbo ya kanisa unaojadili maamuzi juu ya sera kwenye kanisa katoliki almaarufu sinodi lilikuwa awamu ya mwisho wa mchakato ulioanza miaka minne iliyopita kutafuta muelekeo kutokana na maoni ya wakatoliki wanaoshiriki ibada kanisani kote ulimwenguni.

    Na kisha Papa mtakatifu Francis akafungua mkutano wa maaskofu na wakatoliki wenye ujuzi mbali mbali waliotaka kushirkikishwa, wakiwemo wanawake 60 waliokuwa miongoni mwa wajumbe 368 wenye uwezo wa kupiga kura.

    Wanachama wote wa sinodi walipigia kura kila moja ya mapendekezo 151.

    Na japo mapendekezo hayo yalipitishwa kwa kupata uungwaji mkono unaohitajika wa thuluthi moja, kura zilizopigwa kupinga baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa yaliangazia suala la wanawake kuchukuwa nafasi nyingi za uongozi kanisani, katika kanisa ambalo lina viongozi wa kidini wa kiume.

    Wenye kupendekeza nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake kanisani walikuwa na matumaini kwamba Sinodi ingetoa wito kuwa wanawake wahudumu kama wahudumu wa kike wa kanisa au Deacons - viongozi wa kidini wenye uwezo wa kuwabatiza waumini, kusimamia sherehe za harusi au shughuli za maziko bila ya kusimamia ibada tofauti na mapadri.

    Sinodi haikutaja wala kuendeleza suala hilo ila ripoti yake ya mwisho baada ya vikao imesema kwamba ‘hakuna sababu au kizingiti kinachozuia wanawake kutoshikilia nafasi za uongozi kwenye kanisa.’

    Kwa sasa kanisa katoliki inawakubalia wanaume pekee kuwa wahudumu wa kidini yaani deacons – ambao ni viongozi wa kidini waliolishwa kiapo cha kuhudumu katika kanisa wenye uwezo wa kusimamia sherehe za ubatizo, harusi na mazishi bila ya kuongoza ibada kanisani kama wanavyofanya mapadri.

  12. Chama ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 58, cha ahidi kufanya mabadiliko nchini Botswana

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Na Innocent Selatlhwa akiwa Gaborone na Damiana Zane akiwa London

    Chama tawala nchini Botswana – ambacho kimekuwa uongozini kwa takriban miongo sita – kinajaribu tena kutafuta ujanja wa kushinda uchaguzi mkuu wa Jumatano wiki hii kwa kutumia tamko ambalo limehusishwa kwa muda mrefu na makundi ya upinzani.

    Kwenye manifesto yake, chama cha kidemokrasia cha Botswana (BDP) kinataka “mabadiliko.”

    “Tufanye mabadiliko pamoja na tujenge ufanisi kwa wote,” Rais Mokgweetsi Masis – ambaye amekuwa uongozini nchini humo tangu 2018 – ameyaandika kwenye utangulizi wake.

    Ni utambulizi ambao unahitaji mambo kufanyika tofauti – upinzani unasema kwamba chama cha Rais hakina uwezo wa kutimiza hilo.

    Japo wachambuzi wanasema kwamba matokeo ya uchaguzi huo ni magumu kutabiri wakati huu, chama cha BDP kimeshinda viti vingi bungeni mara 11 kwenye uchaguzi mbali mbali tangu taifa hilo kunyakuwa uhuru wake 1966.

    Chama hicho kimewasaidia wagombea kiti cha Urais kuingia madarakani kila mara huku wabunge wanapomchagua kiongozi wa taifa hilo.

    BDP imepongezwa kwa hatua ilizochukuwa kubadilisha maisha na hali ya Uchumi wa raia katika taifa la Botswana ambalo ni masikini, na lenya hali duni ya miundombinu kama barabara chache za lami na kubadili hali ambapo maisha ya raia wa kawaida nchini humo ni ya juu kuliko kwengine kote barani Afrika.

    Mojawapo ya rasilimali ambazo taifa hilo imetumia kuboresha Uchumi wake ni uchimbaji wa madini ya GEMSTONE, taifa hilo likiwa lenye kuchimba viwango vikubwa vya madini hayo kote ulimwenguni.

    Na japo mambo hayako sawa.

    Botswana inakabiliwa na changamoto za kiuchumi – sababu kuu ya tamko la Masisi kufanyike mabadiliko.

    Kati ya watu wanne wenye uwezo wa kufanya kazi nchini humo, zaidi ya mmoja hana ajira, huku idadi kubwa ya kundi hilo likiwa vijana. Haya ni kwa mujibu wa Benki ya dunia.

    Mhadhiri wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Botswana Zibani Maundeni, ameitaja hali hiyo kama, ‘Uchumi wa watu wasiokuwa na ajira.’

    ‘Tunawatoa waliofuzu kwenye chuo kikuu kila mwaka na Uchumi wetu hautoi nafasi za kutosha za ajira kuwafaa wote,’ aliiambia kitengo cha BBC Africa Daily Podcast.

    Aidha, mali iliyomo nchini Botswana haijasambazwa kwa usawa miongoni mwa raia wake milioni 2.3.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Uchaguzi wa Marekani 2024: Michelle Obama azungumzia uavyaji mimba huku Trump akiungwa mkono na viongozi wa Kiislamu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Zikiwa zimesalia siku tisa hadi siku ya kupiga kura, kinyang'anyiro cha kuelekea Ikulu ya Marekani kinaendelea.

    Jana usiku, katika mkutano wa hadhara huko Michigan - jimbo muhimu - Donald Trump alipokea ridhaa ya viongozi wa Kiarabu mwenye asili ya Marekani, ambao alisema wanaweza "kufanya mabadiliko katika uchaguzi".

    Pia huko Michigan, mke wa rais wa zamani Michelle Obama alijitokeza kwa mara ya kwanza kwenye kampeni katika hafla iliyofanyika Kalamazoo na mgombea wa chama cha Democratic na Makamu wa Rais Kamala Harris.

    Katika hotuba yenye hisia kali, Obama aliwataka wapiga kura "kufanya kitu" na kulinda nchi kutokana na "hatari" za Trump, huku pia akionya jinsi utawala wa Trump unaweza kuathiri haki za utoaji mimba.

    Polls show the two locked in a tight race in Michigan, with Harris holding an extremely narrow lead 10 days before the 5 November election.

    Kura za maoni zinaonyesha wawili hao wakiwa kwenye kinyang'anyiro kikali huko Michigan, huku Harris akishikilia uongozi mdogo kabisa siku tisa kabla ya uchaguzi wa Novemba 5.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yawauwa wanajeshi wanne - Iran

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran ya kulipiza kisasi ikiwa ni hatua ya kujibu mashambulizi ya makombora ya Iran yaliyotokea mapema mwezi huu, yamewaua wanajeshi wanne wa Iran, jeshi la Iran lilisema.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema lililenga viwanda vya makombora na maeneo mengine karibu na Tehran na magharibi mwa Iran mapema Jumamosi.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema ina jukumu la kujilinda, lakini ikaongeza kuwa Iran "inatambua wajibu wake kwa amani na usalama wa eneo," taarifa inayoonekana kuwa ya maridhiano.

    Kulipiza kisasi kwa Israel kwa msururu wa makombora 200 ya balestiki yaliyorushwa kuelekea Israel tarehe 1 Oktoba yalitarajiwa kwa wiki kadhaa.

    Iran ilisema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh katika ardhi ya Iran mnamo mwezi Julai.

    Makombora mengi yalidunguliwa na Israel na washirika wake lakini idadi ndogo ilishambulia Israel ya kati na kusini.

    Mamlaka ya Iran ilisema maeneo katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam yalishambuliwa.

    Jeshi lilidai kuwa limefanikiwa kuzuilia mashambulizi hayo, ingawa kulikuwa na "uharibifu mdogo" katika baadhi ya maeneo.

    Kufuatia shambulizi ya Israel, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilionyesha kanda za video zinazoonyesha msongamano wa magari kama kawaida katika miji kadhaa, huku shughuli za shule na michezo zikiripotiwa kufanywa kama ilivyopangwa.

    Jeshi la Israel lilitangaza operesheni ya Jumamosi muda mfupi baada ya kuripotiwa milipuko nchini Iran. Msemaji wa IDF Daniel Hagari alisema jeshi limeonyesha kujitayarisha "kulinda taifa la Israel".

    Pia alionya ikiwa Iran itaanzisha duru mpya ya kuzidisha mashambulizi, basi Israel "italazimika kujibu".

    Soma zaidi:

  15. Ni Jumapili ya tarehe 27/10/2024 tunapokutana katika matangazo ya moja kwa moja. Karibu uandamane nasi hadi tamati.