Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

"Tutaishi na kufa katika nchi yetu': Wagaza waendelea kurudi nyumbani baada ya Trump kupendekeza kuichukua

Rais wa Marekani amesema anataka nchi yake ichukue" umiliki wa muda mrefu "wa Gaza, na kuibadilisha kuwa" eneo la kitalii la Mashariki ya Kati ".

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Zaidi ya wanawake 100 walibakwa na kuchomwa wakiwa hai katika gereza la Dr Congo - UN inasema

    Zaidi ya wafungwa 100 wa kike walibakwa na kisha kuchomwa moto wakiwa hai wakati wafungwa walipotoroka jela katika mji wa Goma nchini Congo, kulingana na UN.

    Mamia ya wafungwa walitoroka katika gereza la Munzenze Jumatatu iliyopita, baada ya wapiganaji wa kundi la waasi la M23 kuanza kuuteka mji huo.

    Kati ya wanawake 165 na 167 walivamiwa na kunyanyaswa na wafungwa wa kiume walipovunja gereza, hati ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na BBC inasema.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa wengi wa wanawake hao waliuawa baada ya wafungwa hao kuchoma moto gereza hilo.

    BBC haijaweza kuthibitisha ripoti hizo.

    Goma, jiji kubwa lenye zaidi ya watu milioni moja, lilitekwa baada ya kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda kuingia na kuteka eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Jiji hilo lilikumbwa na machafuko, huku miili ikiwa imetapakaa mitaani na makombora yakiripotiwa kuonekana juu ya nyumba za makazi.

    Picha za jela kuvunjwa za wiki iliyopita zilionyesha watu wakitoroka kutoka kwa jengo hilo huku moshi ukiendelea kupaa kwa nyuma.

    Milio ya risasi pia ilisikika.

    Katika video tofauti, watu wanaoaminika kuwa wafungwa waliotoroka, walionekana wakiwa wamewasili katika mitaa ya Goma.

    Zaidi ya watu 2,000 waliuawa wakati waasi wa M23 wakikabiliana na wanajeshi wa Congo na washirika wao, serikali ya DR Congo imesema.

    Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 900 waliuawa na karibu 3,000 kujeruhiwa.

    Haikuwa wazi kwa nini idadi ya vifo vya Umoja wa Mataifa na DR Congo inatofautiana.

  3. Watoto 17 wafariki dunia katika janga la moto kaskazini magharibi mwa Nigeria

    Takriban watoto kumi na saba wanaripotiwa kuuawa kwa moto katika shule kaskazini magharibi mwa Nigeria.

    Moto ulizuka mara moja katika shule ya Kiisilamu katika Jimbo la Zamfara siku ya Jumanne usiku na kuenea haraka katika Shule ya Kiisilamu huko Kauran Namoda.

    Watoto wengi walikuwa tayari wamelala hivyo basi, na kunaswa wakati jengo hilo lilipokuwa limeshika moto.

    Kufikia wakati waokoaji wa dharura walipofika, moto ulikuwa tayari umesababisha majeruhi makubwa.

    Wakazi wa eneo hilo walisema kwamba wanafunzi wengine kadhaa walijeruhiwa na walikimbizwa katika vituo vya afya vya karibu kwa matibabu.

    Mamlaka ya eneo la Zamfara bado haijazungumza juu ya msiba huo.

    Yahaya Mahi aliyeshuhudia tukio hilo aliambia BBC Hausa eneo la shule hiyo lilifanya iwe vigumu kwa wale wanaojaribu kuzima moto.

    "Hata kama wazima moto wangekuja kwa wakati, kufika katika eneo hilo ingekuwa vigumu kutokana na njia finyu inayoelekea kwenye jengo husika," alisema.

    Afisa wa eneo hilo Mannir Haidara alisema shule zingine za Kiislamu zitakaguliwa ili kuhakikisha kuwa sio hatari ya moto.

    ''Tutachukua hatua kuzuia tukio lingine la namna hii, "alisema.

    Baba wa mmoja wa waathiriwa aliiambia BBC Hausa kwamba aliumia lakini imani yake kwa Mungu ilikuwa ikimfariji wakati huu.

  4. Mapigano yaanza tena huko Kivu kusini licha ya azimio la kusitisha mapigano

    Mapigano yameanza tena katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusini mwa Kivu licha ya kusitishwa kwa mapigano na kundi la waasi la M23.

    Ripoti zinasema mapigano kati ya waasi wa M23 na vikosi vya Congo yameongezeka mapema leo huko Nyabibwe, eneo la Kalehe.

    Siku ya Jumatatu, waasi walitangaza kusitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu, wakisema hawakuwa na nia ya kukamata maeneo yoyote baada ya kuteka mji wa Goma.

    Mamlaka ya Congo inasema shambulio la leo la waasi wa M23 katika maeneo ya serikali linawakilisha ukiukaji wa makubaliano yake yenyewe iliyotoa siku mbili zilizopita.

    Baada ya kuushikilia mji wa Goma, M23 ilitaka kuuteka mji wa Bukavu, ambao ndio mkubwa zaidi katika mkoa wa Kivu Kusini.

    Hata hivyo, inasemekana walikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya Congo na Burundi, ambao walitwaa tena vijiji kadhaa vilivyokuwa vimetekwa na waasi huko Kivu Kusini.

    Serikali ya DRC imeanzisha harakati za kusajili raia kujiunga na jeshi ili kuzuia Bukavu na maeneo mengine katika jimbo hilo kuanguka mikononi mwa waasi.

    Soma zaidi:

  5. Trump atuma wafungwa wa kwanza wahamiaji kwenda Guantanamo Bay

    Marekani imetuma kundi la kwanza la wahamiaji huko Guantanamo Bay tangu Rais Donald Trump atangaze mipango ya kupanua kizuizi cha wahamiaji katika gereza hilo, maafisa wanasema.

    Taarifa fupi kutoka kwa Idara ya Usalama wa Nchi ilisema wafungwa hao walikuwa sehemu ya Tren de Aragua - genge lililotokea katika magereza ya Venezuela.

    Wafungwa kumi walisafirishwa kwa ndege kutoka kambi ya Jeshi la Fort Bliss karibu na mpaka wa Texas hadi kituo cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Cuba Jumanne alasiri, mshirika wa BBC wa Marekani CBS News aliripoti, akinukuu maafisa kadhaa wa Marekani.

    Wiki iliyopita, Trump aliamuru kwamba kizuizi kilichopo cha wahamiaji katika kambi hiyo kipanuliwe ili kuhifadhi watu 30,000.

    Alisema hiyo itaongeza uwezo wa Marekani kukamata wahamiaji wasio na vibali maradufu.

    Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Trump za kukabiliana na wahamiaji wasio na vibali nchini Marekani baada ya kurejea ofisini.

    Ameahidi kuwakamatwa wahamiaji haramu wengi zaidi na kuwarejesha nyumbani.

    Katika taarifa fupi ya Jumanne, Katibu wa DHS Kristi Noem alisema: "Rais Donald Trump amekuwa wazi sana: Guantanamo Bay itakuwa na wahamiaji wabaya zaidi. Hiyo inaanza leo."

    Idara hiyo ilichapisha picha kadhaa za wafungwa hao wakiingizwa kwenye ndege hiyo. Maafisa wawili waliiambia CBS kwamba kundi hilo lilichukuliwa kuwa "tishio kubwa".

    Soma zaidi:

  6. Google yaondoa marufuku ya kutumia AI kwa utengenezaji wa silaha

    Kampuni mama ya Google imeondoa marufuku ya akili mnemba (AI) kutumika katika utengenezaji silaha na zana za uchunguzi baada ya kubadilisha kanuni zake za muda mrefu.

    Imeandika upya miongozo yake ya jinsi itakavyotumia AI, na kuacha sehemu ambayo hapo awali iliondoa programu ambazo "zina uwezekano wa kusababisha madhara".

    Ujumbe wake ulioandikwa huko Google ilitetea mabadiliko hayo, ikisema kwamba biashara na serikali za kidemokrasia zinahitajika kufanya kazi pamoja kwenye AI ambayo "inaunga mkono usalama wa taifa".

    Ilisema: "Tunaamini demokrasia inapaswa kuwa kipaumbele katika maendeleo ya AI, ikiongozwa na maadili ya msingi kama uhuru, usawa na kuheshimu haki za binadamu.

    "Na tunaamini kwamba makampuni, serikali na mashirika yanayoshirikisha maadili haya yanapaswa kufanya kazi pamoja ili kuunda AI ambayo inalinda watu, kukuza ukuaji wa kimataifa na kusaidia katika usalama wa taifa," iliongeza.

    Kuna mjadala kati ya wataalam wa AI juu ya jinsi teknolojia mpya yenye nguvu inapaswa kudhibitiwa kwa ujumla, ni kwa kiasi gani faida za kibiashara zinapaswa kuruhusiwa kuamua mwelekeo wake, na jinsi bora ya kujilinda dhidi ya hatari kwa wanadamu kwa ujumla.

    Pia kuna utata kuhusu matumizi ya AI kwenye uwanja wa vita na katika teknolojia za uchunguzi.

    Uhamasishaji juu ya uwezo wa kijeshi wa AI umeongezeka hivi karibuni.

    Mnamo mwezi Januari, mbunge alisema kwamba mzozo huko Ukraine ulikuwa umeonyesha kuwa teknolojia hiyo "inasaidia pakubwa upande wa kijeshi kwenye uwanja wa vita"

    Soma zaidi:

  7. Hamas yalaani tena matamshi ya 'chuki' ya Trump

    Matamshi ya Rais Trump siku ya Jumanne "yataongeza chumvi kwenye kidonda" huko Mashariki ya Kati, Hamas imesema katika taarifa yake mpya kulaani pendekezo la Marekani kutwaa Gaza "kwa maneno makali zaidi".

    "Matamshi kama haya ni ya chuki kwa watu wetu na maadili yetu, na hayatasaidia katika utulivu wa kikanda," kundi hilo linasema.

    "Tunatoa wito kwa utawala wa Marekani na Rais Trump kuachana na matamshi haya ya kutowajibika ambayo yanakinzana na sheria za kimataifa na haki za kimsingi za watu wetu wa Palestina katika ardhi yao," inaongeza.

    Kundi hilo pia linatoa wito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa kufanya mikutano ya dharura kushughulikia "matamshi hayo hatari" na kuchukua "msimamo mkali" unaolinda haki za Wapalestina.

    Siku ya Jumanne, muda mfupi baada ya Trump kuzungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa Habari katika Ikulu ya White House, afisa wa Hamas Sami Abu Zuhri aliliita pendekezo hilo "ujinga" na "upuuzi".

    Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu, walifanya mkutano wa waandishi wa habari ambapo Trump alitoa pendekezo kwamba Marekani “ichukue udhibiti” wa Gaza, na kuwahamisha watu milioni 1.8 wa Gaza kwenda nchi nyingine za Kiarabu.

    Trump aliongeza kuwa baada ya Marekani kuijenga upya Gaza, inaweza kuwa makazi ya “watu wa dunia nzima.”

    Soma zaidi:

  8. Shirika la posta la Marekani lasimamisha usafirishaji mizigo ya China

    Shirika la Posta la Marekani limesema limeacha kupokea mizigo kutoka China bara na Hong Kong kwa muda usiojulikana.

    Huduma ya barua haitaathiriwa na usitishaji huo, ilisema shirika hilo, ambalo lilikataa kutoa sababu ya uamuzi huo.

    Hata hivyo, mnamo Jumanne sheria mpya zilianza kutekelezwa ambazo ziliziba mwanya ulioruhusu vifurushi vidogo vya thamani ya $800 (£ 641) au chini yake kutumwa Marekani bila kulipa ushuru au ada.

    Ilikuwa moja ya hatua zilizotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alitoa agizo la ulipaji ushuru wa ziada wa 10% kwa bidhaa zote zilizoingizwa Marekani kutoka China.

    Soma zaidi:

  9. Ndege ya kijeshi ya Marekani iliyobeba raia wa India waliofukuzwa yatua Punjab

    Ndege ya Marekani iliyowasafirisha raia wa India takriban 100 wanaodaiwa kuingia nchini kinyume cha sheria nchini humo imetua katika jimbo la Punjab.

    Ndege ya kijeshi, ambayo iliondoka Texas Jumanne jioni, sasa iko katika jiji la Amritsar ambapo mamlaka inasema wamechukua hatua kushughulikia waliorejeshwa nyumbani.

    Rais Donald Trump ameipa kipaumbele shughuli ya kuwatimua raia wa kigeni wasio na vibali na kuifanya kuwa sera yake muhimu.

    Marekani inasemekana kuwatambua takriban raia 18,000 wa India ambao inaamini waliingia nchini humo kinyume cha sheria.

    Trump amesema Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alikuwa amemhakikishia kwamba nchi hiyo "itafanya kilicho sawa" kukubali waliofukuzwa Marekani.

    Soma zaidi:

  10. Uganda yawakamata maafisa 9 kwa tuhuma za udukuzi na wizi wa dola milioni 16 Benki Kuu

    Polisi nchini Uganda inawashikilia maafisa tisa wa Wizara ya Fedha kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za kudukua mifumo ya kielektroniki ya benki kuu na kusababisha wizi wa shilingi za Uganda bilioni 62 (sawa na dola za kimarekani milioni 16.87), imesema wizara na polisi.

    Mwezi Novemba mwaka jana, Waziri wa Fedha, Henry Musasizi alithibitisha kwa vyombo vya habari vya ndani kwamba akaunti za benki kuu zilidukuliwa na pesa kuibiwa.

    Polisi na Wizara ya afya wanasema wanaozuiliwa ni pamoja na afisa mkuu wa idara ya hazina ya Wizara hiyo.

    Baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya mhasibu mkuu katika wizara hiyo "waliitwa na kushikiliwa ili kuwezesha uchunguzi," wizara ya fedha ilisema kwenye chapisho kwenye akaunti yake ya X jioni ya Jumanne.

    Wizara haikutoa majina ya waliozuiliwa wala idadi yao. Hata hivyo, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke, aliambia televisheni ya NTV, maafisa tisa wamezuiliwa na kusoma majina yao.

    Gazeti la serikali la New Vision liliripoti kwamba wadukuzi, wakijitambulisha kama "Taka", walidukua mifumo ya IT ya Benki ya Uganda na kuhamisha fedha hizo kinyume cha sheria.

  11. Zaidi ya mayai 100,000 yaibiwa kutoka kwa muuzaji mmoja Marekani

    Wezi katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani wameiba zaidi ya mayai 100,000 - yenye thamani ya dola za kimarekani 40,000 kutoka kwa muuzaji mmoja.

    Polisi wanasema wizi huo ulifanyika nyuma ya lori huko Greencastle, 1 Februari.

    Umetokea wakati ambao bei ya mayai imepanda huku kukiwa na homa ya mafua ya ndege, na kuyafanya mayai kuwa na gharama kubwa.

    Bei za mayai zimepanda zaidi ya 65% katika mwaka uliopita, kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Marekani. Idara ya kilimo ilitabiri gharama ya mayai itaongezeka kwa 20% mwaka 2025.

    Kwa mujibu wa idara hiyo, ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege ulianza mwaka 2022 na umesababisha mlipuko nchini Marekani katika miezi ya hivi karibuni.

    Ugonjwa huo umeripotiwa kwa ndege, mifugo na mamalia kote Marekani, ingawa maambukizi kwa binadamu ni nadra sana.

  12. Marekani yasitisha ufadhili kwa misheni ya usalama ya Haiti

    Zaidi ya dola milioni 13 za ufadhili unaotolewa na Marekani kwa operesheni ya vikosi vya usalama vya kimataifa vinavyopambana na magenge ya Haiti umesitishwa kwa muda wa siku 90, umesema Umoja wa Mataifa (UN).

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuagiza misaada ya nje ya Marekani isitishwe, ihakikiwe ili isukwe kulingana na maslahi ya taifa hilo.

    Magenge hatari yaliyo na silaha zinazodaiwa zimetoka Marekani wapo katika mji mku wa Port-or- Prince wakidhibiti mji na kuvamia maeneo tofauti nchini Haiti.

    Misheni ya usalama ya kimataifa iliyoidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UN, sio operesheni ya UN bali inategemea misaada kutoka mataifa yaliyoendelea.

    Misheni hiyo kufikia sasa haijafanya cha mno kuhakikisha hali ya usalama imerejea katika taifa la Haiti ambalo limekuwa likihangaishwa na magenge hayo.

    Kuna zaidi ya maafisa wa polisi 900 kutoka Kenya, vikosi vya El Salvador, Jamaica, Guatemala na Belize.

    Zaidi ya dola za kimarekani milioni 110 zimewekezwa katika mfuko wa misheni ya UN, kiasi kikubwa kikitoka Canada, kulingana na data za UN.

    "Marekani iliahidi kutoa dola milioni 15 kwa mfuko huo wa kufadhili operesheni hiyo, dola milioni 1.7 zilikuwa tayari zimetolewa, zikisalia dola milioni 13.3 ambazo zimesitishwa,’’ msemaji wa UN Stephane Dujarric amewaambia wanahabari.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Saudi Arabia inasema haitaanzisha uhusiano na Israel bila kuwepo taifa la Palestina

    Siku ya Jumatano Saudi Arabia imesema haitaanzisha uhusiano na Israel bila kuundwa taifa la Palestina - kauli ambayo inakuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema Saudia haidai kuundwa taifa la Palestina.

    Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Saudia imesema Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman amethibitisha msimamo wa ufalme huo.

    Saudi Arabia pia inakataa majaribio yoyote ya kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao, imesema taarifa hiyo, na kuongeza kuwa msimamo wake kwa Wapalestina hauwezi kujadiliwa.

    Marekani imeongoza miezi kadhaa ya diplomasia ili kuifanya Saudi Arabia kurekebisha uhusiano na Israel na kuitambua nchi hiyo, lakini vita vya Gaza vilipoanza Oktoba 2023, Riyadh iliahirisha suala hilo kutokana na mashambulizi ya Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mfanyabiashara mkubwa duniani Aga Khan afariki dunia

    Bilionea na kiongozi wa kiroho Aga Khan amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, limetangaza shirika lake la hisani la Aga Khan Development Network.

    Prince Karim Aga Khan alikuwa imamu wa 49 wa Waislamu wa Ismailia, ambaye nasaba yake inarudi moja kwa moja hadi kwa Mtume Muhammad.

    "Alifariki dunia kwa amani" mjini Lisbon, Ureno, akiwa amezungukwa na familia yake, shirika lake la hisani lilisema katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii.

    Mzaliwa wa Sweden, lakini alikuwa na uraia wa Uingereza na aliishi katika kasri lake Ufaransa.

    Misaada ya Aga Khan iliendesha mamia ya hospitali, miradi ya elimu na kitamaduni, haswa katika nchi zinazoendelea.

    Aliishi maisha ya kifahari, akiwa na kisiwa cha binafsi huko Bahamas, boti kubwa na ndege binafsi.

    Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan ulisema ulitoa "rambirambi zake kwa familia ya Mtukufu na kwa jamii ya Ismailia duniani kote".

    Madhehebu ya Ismailia yana wafuasi wapatao milioni 15 duniani kote, wakiwemo 500,000 nchini Pakistan. Pia kuna idadi kubwa ya watu nchini India, Afghanistan na Afrika.

    Kwa mujibu wa mtandao wa Aga Khan Development Network, vituo vyake vya afya na hospitali vya Afrika Mashariki vilianzia enzi za ukoloni, kikiwemo kituo cha afya kilichoanzishwa mwaka 1929 jijini Dar es Salaam, ambacho kilipanuka na kuwa hospitali mwaka 1964.

    Pia Mombasa na Kisumu, Kenya, vituo kama hivyo baadaye vikawa ni hospitali zinazotoa huduma kamili katika miaka ya 1950. Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi ilifunguliwa mwaka 1958. Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKUH-N) ilianzishwa 2005.

    Aga Khan pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Nation Media Group, kampuni kubwa ya habari, ambayo inajumuisha magazeti kama vile Daily Nation na Sunday Nation kwa upande wa Kenya. Pia katika nchi za Tanzania na Uganda, yapo magazeti ya Nation, Business Daily, The East African, The Monitor, Mwananchi na The Citizen Tz.

    Vilevile Aga Khan ni muwekezaji wa hoteli za Serena, na maeneo ya kitalii na mapumziko, katika nchi za Kenya, Tanzania, Zanzibar, Uganda, Rwanda na DR Congo.

    Ukubwa wa biashara zake umefika katika mabenki, kilimo na chakula, uzalishaji wa umeme, bima ya afya, mawasiliano na elimu kuanzia msingi hadi chuo kikuu katika mataifa kadhaa Afrika.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Takribani watu 10 wameuawa kwa kupigwa risasi katika shule nchini Sweden

    Polisi wanasema takriban watu 10 wameuawa kwa kupigwa risasi katika shule huko Sweden, akiwemo mtu anayeshukiwa kuwa mshambuliaji.

    Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Ulf Kristersson ameeleza shambulio la Jumanne katika shule ya Risbergska huko Orebro, magharibi mwa mji mkuu wa Stockholm, kama "baya zaidi katika historia ya Sweden".

    Polisi walisema wanaamini kuwa mhalifu huyo mwanaume ni miongoni mwa waliofariki. Sababu ya kufanya tukio hilo bado haijajuulikana na polisi wanaamini alishiriki tukio hilo peke yake.

  16. Rais wa Afrika Kusini ampigia simu Musk kutuliza maneno juu ya sheria mpya ya ardhi

    Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amechukua hatua ya kumaliza mzozo kati yake na utawala mpya wa Marekani kuhusu sheria mpya ya ardhi kwa kuzungumza na Elon Musk.

    Musk ni mshauri wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye siku ya Jumapili alitishia kusitisha ufadhili kwa siku zijazo kwa Afrika Kusini kwa madai kuwa inanyakua ardhi na "kuwatendea vibaya watu wa tabaka fulani."

    Bilionea huyo wa teknolojia mzaliwa wa Afrika Kusini alichapisha ukosoaji wake kupitia X, akiuliza kwa nini Ramaphosa ana "sheria za wazi za ubaguzi wa rangi katika umiliki wa ardhi."

    Ofisi ya Ramaphosa imesema katika mazungumzo ya simu ya rais na Musk, “rais alisisitiza maadili ya Afrika Kusini yaliyopo kikatiba ni ya kuheshimu utawala wa sheria, haki, na usawa"

    Mwezi uliopita, Rais Cyril Ramaphosa alitia saini sheria inayoruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia katika sababu fulani.

    Umiliki wa ardhi kwa muda mrefu umekuwa suala la kutatanisha nchini Afrika Kusini huku mashamba mengi ya binafsi yakimilikiwa na watu weupe, miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa ubaguzi wa rangi.

    Kumekuwa na wito wa mara kwa mara kwa serikali kushughulikia mageuzi ya ardhi na kukabiliana na dhuluma za zamani za ubaguzi wa rangi.

    Katika majibu yake ya awali kwa Trump, rais wa Afrika Kusini amesema "serikali yake haijamnyang'anya ardhi yoyote."

    Siku ya Jumapili, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social: "Nitakata ufadhili wote wa siku zijazo kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii ukamilike!"

    Sheria mpya ya Afŕika Kusini inaruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia katika hali ambapo ni "haki na ni sawa kwa maslahi ya umma" kufanya hivyo.

    Hii inajumuisha ikiwa ardhi haitumiki na hakuna nia ya kuiendeleza au haizalishi pesa, au ikiwa inahatarisha usalama wa watu.

    Mwaka 1913, utawala wa kikoloni wa Uingereza ulipitisha sheria iliyozuia haki ya kumiliki ardhi kwa watu weusi ambao ndio wengi nchini humo.

    Sheria hiyo ilifanya sehemu kubwa ya ardhi kuwa chini ya udhibiti wa Wazungu walio wachache na kuondolewa kwa lazima watu weusi katika ardhi zao na kupelekwa katika vitongoji maskini kwa miongo kadhaa hadi mwisho wa ubaguzi wa rangi.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Donald Trump apendekeza Marekani ichukue udhibiti wa Ukanda wa Gaza

    Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu, wamefanya mkutano wa waandishi wa habari ambapo Trump ametoa pendekezo kwamba Marekani “ichukue udhibiti” wa Gaza, na kuwahamisha watu milioni 1.8 wa Gaza kwenda nchi nyingine za Kiarabu.

    Trump amesema baada ya Marekani kuijenga upya Gaza, inaweza kuwa makazi ya “watu wa dunia nzima.”

    Alipoulizwa na wanahabari ni kwa mamlaka gani Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa Gaza, Trump hakujibu moja kwa moja, lakini amesema anaona kuwa kuna ‘’hati miliki ya muda mrefu.’’

    Netanyahu alikubaliana na wazo la Trump na kumuita rais huyo “rafiki mkubwa wa Israel.”

    Vile vile Trump alimkosoa mtangulizi wake Joe Biden akidai aliruhusu maadui wa Israel kuwa na nguvu zaidi katika kipindi chake cha miaka minne madarakani.

    Mapema, kabla ya pendekezo hilo, msemaji wa Hamas alikosoa pendekezo hilo, akisema ni “mpango wa kuleta machafuko” na akasisitiza kwamba watu wa Gaza hawataruhusu mipango hiyo kupita, bali kinachohitajika ni kumaliza vita.

    Benjamin Netanyahu ndiye kiongozi wa kwanza wa kigeni kutembelea Washington wakati wa muhula wa pili Trump katika Ikulu ya White house.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Hujambo na karibu

    Leo ni Jumatano ya Februari 5, 2025, nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja.