Israel na Hezbollah zatakiwa kujidhibiti huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu 'janga'
Jeshi la Israel lilisema takriban roketi 150 , makombora na vilipuzi vilirushwa katika eneo lake usiku wa Jumamosi na mapema Jumapili - hasa kutoka ndani ya Lebanon.
Muhtasari
Marekani yaionya Israel dhidi ya kuzidisha mzozo, White House yasema
Kiongozi wa mrengo wa kushoto ashinda uchaguzi wa urais Sri Lanka
Kenya kutuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti
Hezbollah yamzika kamanda aliyeuawa katika shambulio la Israel huku mzozo ukiongezeka
Waziri Mkuu wa Lebanon atoa wito kwa nchi kuchukua msimamo wa wazi juu ya 'mauaji ya kutisha'
Israel na Hezbollah zashambuliana kwenye mpaka wa Lebanon
Trump akataa mjadala wa pili wa TV akisema 'umechelewa sana'
Israel yaamuru kufungwa kwa siku 45 kwa ofisi ya Al Jazeera Ukingo wa Magharibi
Israel yazuia mikusanyiko kaskazini mwa nchi huku ikiendelea kushambulia Hezbollah
Moja kwa moja
Na Yusuf Jumah
Kwaheri na Asante!
Asante sana
kwa kufuatilia matangazo yetu ya moja kwa moja leo hii.Tukutane tena kesho
alfajiri panapo majaaliwa.
Kumbuka
unaweza kuendelea kuzipokea habari zetu kupitia Chaneli yetu ya WhatsApp ya BBC
News Swahili kwa kubofya hapa
Israel na Hezbollah zatakiwa kujidhibiti huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu 'janga'
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Naibu kiongozi wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem akiongoza maombi ya mazishi ya kamanda mkuu aliyeuawa katika shambulizi la Israel.
Israel na Hezbollah zote zimetishia kuongeza
mashambulizi yao ya mpakani siku ya
Jumapili, huku kukiwa na wito wa kimataifa wa kuzitaka kujiepusha na vita.
Jeshi la Israel lilisema takriban roketi 150 , makombora
na vilipuzi vilirushwa katika eneo lake
usiku wa Jumamosi na mapema Jumapili - hasa kutoka ndani ya Lebanon.
Baadhi yalifikia zaidi ya mashambulizi ya awali, na kupeleka maelfu ya Waisraeli
kwenye makazi ya kujikinga dhidi ya mabomu na kuharibu nyumba karibu na mji wa
Haifa.
Israel ilianzisha mashambulizi yake dhidi ya malengo kusini mwa Lebanon, ambayo ilisema iliharibu
maelfu ya mifumo ya kurusha roketi za
Hezbollah.
Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema
Israel itachukua "hatua yoyote muhimu kurejesha usalama" na
kuwarudisha watu salama kwenye makazi yao kwenye mpaka wa Israel na Lebanon.
Alisema Israel imetoa "msururu wa mapigo kwa
Hezbollah ambayo haijawahi kufikiria". Lakini naibu kiongozi wa kundi hilo
Naim Qassem alitangaza: "Vitisho havitatuzuia... Tuko tayari kukabiliana
na uwezekano wote wa kijeshi".
Akizungumza katika mazishi ya Ibrahim Aqil, kamanda wa
ngazi za juu wa Hezbollah aliyeuawa katika shambulio la Ijumaa la Israel katika
mji mkuu wa Lebanon, Beirut, alisema: "Tumeingia katika awamu mpya, yaani mapambano
ya wazi" na Israel.
Lebanon imesema jumla ya watu 45 wakiwemo watoto
waliuawa katika shambulio la Beirut.
Hezbollah ni shirika lenye ushawishi mkubwa kisiasa la
Waislamu wa madhehebu ya Shia ambalo linadhibiti jeshi lenye nguvu zaidi nchini
Lebanon. Mapigano kati ya kundi hilo na Israel yaliongezeka tarehe 8 Oktoba
2023 - siku moja baada ya mashambulizi dhidi ya Israel na wapiganaji wa kundi
la Hamas kutoka Gaza - wakati Hezbollah ilipofyatua risasi kwenye maeneo ya
Israel.
Mapigano ya hivi punde ya mpakani yamezua wasiwasi mpya wa kimataifa.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliiambia CNN
kuwa anahofia "uwezekano wa mapigano huko Lebanon kuwa Gaza nyingine".
Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon,
Jeanine Hennis-Plasschaert, alichapisha kwenye X kwamba Mashariki ya Kati iko
ukingoni mwa "janga linalonukia".
"Haiwezi kuelezewa vya kutosha: HAKUNA suluhu la
kijeshi ambalo litafanya kila upande kuwa salama," alichapisha Jumapili.
Ikulu ya White House ilisema kuongezeka kwa mzozo wa kijeshi hakukuwa na "maslahi bora"
ya Israeli. EU ilisema ina wasiwasi mkubwa, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa
Uingereza David Lammy akitoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa
mapigano".
Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kilisema kwamba
makombora mengi waliyokumbana nayo yalinaswa usiku wa kuamkia Jumamosi,
yakiwemo mawili yaliyokuwa yamerushwa kutoka Iraq.
Kundi la Islamic Resistance in Iraq, linaloungwa mkono
na Iran, limesema kuwa limerusha makombora dhidi ya Israel.
Eneo la Israel Kaskazini limesalia katika hali ya tahadhari,
huku shule zikifungwa na hospitali zikiwahamisha wagonjwa chini ya ardhi. Watu
huko wameambiwa wazuie mikusanyiko ya nje hadi chini ya watu 10.
Marekani yaionya Israel dhidi ya kuzidisha mzozo, White House yasema
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Marekani imeiambia Israel kwamba inaamini kwamba kuongezeka kwa mzozo wa kijeshi kwenye mpaka wa Lebanon kutakuwa kinyume na maslahi yake, kwa mujibu wa msemaji wa usalama wa kitaifa wa White House John Kirby.
Akizungumza na kipindi cha "This Weeki" cha ABC Jumapili asubuhi, Kirby alisema kuwa hali ya hivi majuzi katika mapigano inatumika "kusisitiza kwetu jinsi ilivyo muhimu kujaribu kutafuta suluhisho la kidiplomasia."
"Labda hakuna mtu anayeelewa jinsi itakavyokuwa vigumu," alisema. "Lakini hiyo haimaanishi kuwa tutaiacha."
Kirby aliongeza kuwa anawaambia maafisa wa Israel kuwa "hawaamini kwamba kuongezeka kwa mzozo huu wa kijeshi ni kwa manufaa yao" na kwamba haitasaidia IDF kufikia lengo lake la kuwarejesha Waisraeli katika makazi yao kaskazini mwa nchi.
Katika mahojiano tofauti na Fox siku ya Jumapili, Kirby alisema kuwa diplomasia ni "njia bora ya kurejesha familia huko".
Kiongozi wa mrengo wa kushoto ashinda uchaguzi wa urais Sri Lanka
Chanzo cha picha, EPA
Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Anura Kumara Dissanayake ameshinda uchaguzi wa urais nchini Sri Lanka baada ya duru ya pili ya kihistoria ya kuhesabu kura.
Hakuna mgombea aliyepata zaidi ya 50% ya kura zote katika duru ya kwanza, ambapo Dissanayake alipata 42.31% huku mpinzani wake wa karibu, kiongozi wa upinzani Sajith Premadasa, akipata 32.76%.
Lakini Dissanayake, ambaye aliwaahidi wapiga kura utawala bora na hatua kali za kupambana na ufisadi, aliibuka mshindi baada ya hesabu ya pili, ambayo ilijumlisha wapiga kura wa chaguo la pili na la tatu.
Uchaguzi huo wa Jumamosi ulikuwa wa kwanza kufanyika tangu maandamano makubwa yaliomuondoa madarakani kiongozi wa nchi hiyo, Gotabaya Rajapaksa, mwaka 2022 baada ya Sri Lanka kukumbwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi.
Dissanayake, 55, aliwaambia raia wa Sri Lanka "ushindi huu ni wetu sote", katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Mara tu matokeo yalipotangazwa, Tume ya Uchaguzi ilisema alikuwa ameshinda jumla ya kura 5,740,179 dhidi ya 4,530,902 za Premadasa.
Ili kufufua uchumi, Dissanayake ameahidi kuendeleza sekta ya viwanda, kilimo na TEHAMA. Pia amejitolea kuendeleza mpango uliofikiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuikomboa Sri Lanka kutoka katika mzozo wa kiuchumi huku akipunguza athari za hatua zake za kubana matumizi kwa watu maskini zaidi nchini humo.
Hadi kura ya wikendi hii, chaguzi zote nane za urais nchini Sri Lanka tangu 1982 zimeshuhudia mshindi akiibuka wakati wa duru ya kwanza ya kuhesabu kura. Kura hii imetajwa kuwa mojawapo ya kura zenye ushindani mkali zaidi katika historia ya nchi.
Raia wa Sri Lanka milioni kumi na saba walistahili kupiga kura siku ya Jumamosi na tume ya uchaguzi nchini humo ilisema ulikuwa wa amani zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Dissanayake aliwaahidi wapiga kura hatua kali za kukabiliana na ufisadi na utawala bora - jumbe ambazo ziliwavutia sana wapiga kura ambao wamekuwa wakipigia kelele mabadiliko ya kimfumo tangu mgogoro huo.
Kenya kutuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti
Chanzo cha picha, WILLIAM RUTO/X
Kenya imeahidi kutuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti katika wiki zijazo kusaidia kupambana na magenge yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince na maeneo ya karibu.
Hii itafikisha kikosi cha Kenya, kilichotumwa kwa kasi tangu Juni kusaidia jeshi la polisi la taifa la Haiti kufikia 1,000.
Akiwa ziarani nchini humo, Rais wa Kenya William Ruto pia alisema anaunga mkono kugeuza ujumbe wa sasa wa usalama unaoongozwa na Kenya kuwa operesheni kamili ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.
Mataifa machache mengine kwa pamoja yameahidi takriban wanajeshi 1,900 zaidi.
Ghasia nchini Haiti bado zinaendelea na mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa magenge yanalenga maeneo mapya, na kusababisha watu wengine kuhama makazi yao.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana mwishoni mwa mwezi huu ili kuamua iwapo litarejesha mamlaka ya sasa ya Kenya kwa muda wa miezi 12 zaidi, na hivyo kufungua njia kwa ujumbe kamili wa Umoja wa Mataifa mwaka 2025.
Hii itasababisha kuongezeka kwa fedha na rasilimali kwa ajili ya operesheni hiyo, ambayo imetatizwa na ukosefu wa vifaa.
Akihutubia maafisa wa polisi wa Kenya katika kituo chao cha Port-au-Prince, Rais Ruto alipongeza kikosi hicho kwa ufanisi wao katika kipindi cha miezi michache iliyopita.
"Kuna watu wengi ambao walifikiri Haiti ilikuwa misheni ambayo haiwezekani, lakini leo wamebadili mawazo yao kwa sababu ya hatua mlizopiga."
Alisema watafanikiwa dhidi ya magenge hayo na akaahidi kujaribu kuwatafutia vifaa bora.
Karibu maafisa 400 wa Kenya waliokuwa uwanjani walikuwa wakishika doria "wakishirikiana bega kwa bega na vikosi vya Haiti kulinda watu na kurejesha usalama", Ruto alisema.
"Kundi letu linalofuata, maafisa 600 wa ziada, wanaendelea na mafunzo . Tutakuwa tayari kwa misheni katika muda wa wiki chache na tunatarajia usaidizi unaohitajika ili kuwawezesha kutumwa,” aliongeza.
Lakini kumekuwa na ukosoaji fulani nchini Haiti kwa kukosekana kwa hatua madhubuti dhidi ya magenge hayo.
Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa huko hivi punde amesema ujumbe huo haukuwa na vifaa vya kutosha na unahitaji helikopta, pamoja na miwani ya kuona usiku na ndege zisizo na rubani.
"Misheni ya Kimataifa ya Msaada wa Usalama (MSS), iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Oktoba 2023, hadi sasa imetuma chini ya robo ya kikosi chake kilichopangwa," William O'Neil alisema Ijumaa .
Licha ya kuwekewa vikwazo vya kimataifa, silaha na risasi ziliendelea kuingizwa nchini kisiri na kuruhusu magenge kupanua udhibiti wao katika maeneo mapya, alisema.
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa ametembelea eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo, ambapo alisema polisi hawana uwezo wa vifaa kukabiliana na magenge hayo.
Alimnukuu polisi mmoja huko Jérémie akisema: “Hali hiyo inapakana na mambo yasiyowezekana. Tunapaswa kujifunza kutembea juu ya maji."
Unyanyasaji wa kijinsia ulikuwa umeongezeka sana na zaidi ya watu 700,000 sasa wameyahama makazi yao, Bw O'Neil alisema.
"Uchungu huu wa kudumu lazima ukome'
Alisema suluhu tayari zipo, lakini juhudi zilipaswa "kuongezwa mara moja".
"Ni muhimu kuyazima magenge kwa kuupa Ujumbe wa MSS njia za kusaidia operesheni za Polisi wa Kitaifa wa Haiti, na pia kutekeleza hatua zingine zinazotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na sheria ya vikwazo vya silaha."
Hezbollah yamzika kamanda aliyeuawa katika shambulio la Israel huku mzozo ukiongezeka
Tunakuletea sasa taarifa kutoka kwa mazishi ya kamanda mkuu wa Hezbollah, Ibrahim Aqil. Aliuawa katika shambulizi la Israel kwenye viunga vya kusini mwa Beirut siku ya Ijumaa.
Shambulio hilo liliashiria kuongezeka kwa awamu ya sasa ya mzozo wa Israel-Hezbollah, ulioanza tarehe 8 Oktoba. Hivi ndivyo wiki hii imekuwa:
Siku ya Jumanne, watu 12 waliuawa na maelfu kujeruhiwa baada ya 'pagers' zinazotumiwa na Hezbollah kulipuka nchini Lebanon.
Siku ya Jumatano, simu za upepo zinazotumiwa na Hezbollah pia zililipuka, na kuua watu 27 na mamia kujeruhiwa.
Hezbollah iliilaumu Israel kwa mashambulizi hayo. Wakati Israeli ilikataa kutoa maoni, inachukuliwa kuwa inawajibika
Siku ya Ijumaa, Israel ilisema ilifanya mashambulizi ya anga katika kitongoji cha Dahieh, ngome ya Hezbollah kusini mwa Beirut.
Hezbollah ilisema Aqil aliuawa katika shambulio hilo. IDF inasema iliua watu kadhaa wakuu ndani ya kundi hilo
Wizara ya afya ya Lebanon ilisema watu 45, wakiwemo watoto watatu, waliuawa katika shambulio hilo - karibu na mahali ambapo mazishi ya leo yamefanyika.
Maandalizi makini yalifanywa kwa ajili ya mazishi ya kamanda wa jeshi la Hezbollah Ibrahim Aqil, huku safu za viti vya plastiki zikiwa zimewekwa mbele ya zulia jekundu.
Sherehe hiyo imefanyika katika kitongoji cha kusini cha Dahiyeh huko Beirut, ngome ya Hezbollah.
Maulamaa wa KiShia waliketi i katika safu ya mbele. Wanaume wengi wamekuja kuomboleza, wamevaa nguo nyeusi, na mikanda ya njano ya Hezbollah shingoni mwao.
Kumpoteza Aqil ni pigo kubwa kwa kundi hilo lenye silaha, baada ya mfululizo wa mashambulizi ya kufedhehesha ya Israel na kulipua vifaa vyao vya mawasiliano vya 'pagers' na simu za upepo.
Naibu katibu mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem alikuwa miongoni mwa waliohudhuria na aliketi mstari wa mbele.
Maulamaa wengi wa Kishia waliovalia vilemba vyeupe pia walijitokeza
Israel iko tayari kuchukua 'hatua yoyote' inayohitajika dhidi ya Hezbollah
Chanzo cha picha, SERIKALI YA ISRAEL
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema Israel itachukua "hatua zozote zile zinazohitajika kurejesha usalama" na kuwarudisha watu salama kwenye makazi yao kwenye mpaka wa Israel na Lebanon.
Akizungumzia mzozo unaozidi kuongezeka na Hezbollah katika taarifa ya video kwenye X, Netanyahu alisema kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lilishambulia Israel "bila kuchochewa kabisa" tangu tarehe 8 Oktoba, na kuwalazimisha Waisrael 60,000 kuondoka makwao mpakani.
"Katika miezi iliyofuata, hawajakoma hata siku moja kutushambulia," aliendelea.
"Hakuna nchi inayoweza kukubali kurushiwa roketi kwa miji yake. Hatuwezi kukubali pia."
Balozi wa Iran atuma ujumbe wa kwanza tangu mlipuko wa 'pager'
Mojtaba Amani, balozi wa Iran nchini Lebanon, anasema "anaendelea vyema" baada ya kujeruhiwa wakati wa wimbi la kwanza la milipuko ya vifaavya mawasiliano vya 'pager' Jumanne iliyopita huko Beirut.
Katika chapisho kwenye X, anawashukuru madaktari wa Lebanon na Iran kwa kutibu majeraha yake. Haijabainika ikiwa yeye binafsi alichapisha ujumbe huo lakini haya ni mawasiliano yake ya kwanza tangu mlipuko huo.
Ripoti nyingi zilidokeza kuwa huenda alipoteza jicho na kupata majeraha mabaya wakati'pager' aliyokuwa amebeba ilipolipuka
Ripoti hizi zilikanushwa na ubalozi wa Iran mjini Beirut, ambao ulikiri kwamba aliumia mkono ambao utahitaji matibabu ya muda mrefu. Pia walisema anatarajiwa kuweza kuona tena.
Video mbili fupi fupi zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii Jumanne iliyopita zilimuonyesha Amani akishuka kwenye gari huku uso wake ukiwa umefunikwa na kitambaa cheupe kilichokuwa na damu, huku mkono wake mmoja ukiwa na majeraha.
Maswali yameibuka kuhusu kwa nini balozi wa Iran alikuwa akitumia 'pager' ambayo ilikuwa imeingizwa nchini kwa ajili ya kutumiwa na wanachama wa Hezbollah.
Lebanon inasema watu watatu waliuawa katika mashambulizi ya Israeli
Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu watatu wameuawa katika mashambulizi ya Israel katika miji mitatu tofauti.
Kwingineko , Hezbollah ilitangaza Jumapili kwamba wapiganaji wake wawili wameaga dunia. Haijabainika ikiwa wapiganaji hao wawili wamejumuishwa katika idadi ya vifoiliyotangazwa na wizara ya afya ya Lebanon.
Hospitali ya Haifa inahamisha wagonjwa hadi kwenye maegesho ya chini ya ardhi
Chanzo cha picha, Hospitali ya Rambam
Hospitali ya Rambam katika mji wa Haifa, kaskazini mwa Israel, inawahamisha wagonjwa kwenye kituo salama cha kuegesha magari chini ya ardhi hadi itakapotangazwa tena baada ya makombora ya Hezbollah kufika mjini humo .
Video na picha iliyotolewa na hospitali hiyo inaonyesha wafanyikazi wakiwabeba wagonjwa kwenye vitanda vya hospitali kupitia maegesho ya magari.
Hospitali zote kaskazini mwa Israeli sasa zinafanya kazi ndani ya maeneo salama yaliyotengwa, wizara ya afya ilisema.
Ikiwa unajiunga tu na matangazo yetu ya moja kwa moja, haya ndiyo yamejiri katika saa za hivi karibuni:
Mapigano kati ya Israel na Hezbollah yalizidi usiku kucha, huku pande zote mbili zikifanya mashambulizi makubwa katika mpaka wa Lebanon.
Hezbollah ilirusha makombora 150 ndani ya Israel, huku jeshi la Israel likisema kuwa mengi kati ya hayo yalizuiliwa.
Baadhi ya majengo ya makazi katika mji wa kaskazini wa Haifa yaligongwa na kuwasha moto na kusababisha baadhi ya majeruhi
Mashambulio ya Hezbollah yalifika kusini zaidi nchini Israel kuliko yoyote tangu mzozo wa sasa kati ya Israel na Hezbollah kuanza tarehe 8 Oktoba 2023.
Israel ilifanya mashambulizi ya anga kwenye maeneo ya kusini mwa Lebanon na kusema kuwa imeharibu maelfu ya mifumo ya kurusha roketi za Hezbollah.
Kundi la Islamic Resistance in Iraq limesema limejiunga na shambulio hilo la usiku mmoja , na kurusha ndege zisizo na rubani na makombora hadi Israel kutoka Iraq.
Afisa wa Umoja wa Mataifa ameonya eneo hilo "liko kwenye ukingo wa janga linalokaribia" , wakati hofu ya kuzuka kwa vita ikiongezeka
Wanamgambo wa Iraq wamethibitisha kujiunga na mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel
Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la Islamic Resistance in Iraq (IRI) linasema lilijiunga na shambulio la usiku la Hezbollah, kurusha ndege zisizo na rubani na makombora huko Israel kutoka Iraq.
Katika msururu wa taarifa, wanamgambo hao wenye makao yake nchini Iraq walidai kuwa wameanzisha mashambulizi mawili tofauti katika maeneo ambayo hayajabainishwa nchini Israel, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia "walengwa kaskazini mwa Israel alfajiri kwa kutumia makombora ya kusafiri ya Al-Arqab".
Taarifa zaidi Jumapili asubuhi ilidai kundi hilo lilishambulia "lengo muhimu" huko Israeli kwa kutumia ndege zisizo na rubani, kulingana na wataalamu wa lugha ya Kiarabu wa BBC Monitoring
Hapo awali msemaji wa IDF aliwaambia waandishi wa habari kuwa kulikuwa na majaribio mawili ya kuipiga Israel usiku kucha kutoka Iraq.
Katika taarifa zaidi kwa umma, IDF ilisema kwamba makombora yaliyorushwa kutoka nchi isiyojulikana kuelekea mashariki yalikuwa yamenaswa na hakuna uharibifu wowote au majeruhi.
Roketi za Hezbollah hufika hadi kusini mwa Haifa
Moshi ulionekana ukipaa juu ya mji wa kaskazini mwa Israel wa Haifa kufuatia wimbi la mashambulizi yaliyofanywa kutoka Lebanon siku ya Jumapili asubuhi.
Baadhi ya majengo ya makazi yamechomwa moto na wakaazi kujeruhiwa. Vikosi vya uokoaji vilifika eneo la tukio kuwatibu majeruhi, huku vikosi vya usalama vya Israel vikizingira eneo hilo.
Mji huo uko kusini zaidi kuliko mashambulizi ya awali ya roketi ya Hezbollah yameweza kufika.
Israel yafunga shule na kutoa onyo la usalama kwa hospitali
Israel imeamuru shule zote kaskazini mwa nchi hiyo kufungwa hadi Jumatatu jioni .
Mikusanyiko pia ilizuiwa katika maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi na sehemu za Milima ya Golan inayokaliwa na Israel, huku watu wasiozidi 10 wakiruhusiwa kukusanyika nje na watu 100 ndani ya nyumba.
Fukwe pia zitafungwa kwa umma.
Wizara ya afya ya Israel pia inasema hospitali za kaskazini mwa Israel zimeagizwa kufanya kazi katika maeneo salama pekee.
Hospitali ya Rambam katika mji wa Haifa imehamisha shughuli za kuegesha magari chini ya ardhi.
Takriban watu 51 wamefariki katika mlipuko wa mgodi wa makaa ya mawe nchini Iran
Chanzo cha picha, APTN
Mlipuko uliosababishwa na uvujaji wa gesi kwenye mgodi wa makaa ya mawe mashariki mwa Iran umeua takriban watu 51, vyombo vya habari vya serikali vilisema Jumapili.
Zaidi ya wengine 20 walijeruhiwa baada ya mlipuko huo katika jimbo la Khorasan Kusini.
Inaripotiwa kusababishwa na mlipuko wa gesi ya methane katika vitalu viwili vya mgodi huko Tabas, kilomita 540 (maili 335) kusini mashariki mwa mji mkuu Tehran.
Mlipuko huo ulitokea saa 21:00 kwa saa za ndani (17:30 GMT) siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya serikali vilisema.
Gavana wa Khorasan Kusini Javad Ghenaatzadeh alisema kulikuwa na wafanyikazi 69 kwenye vitalu wakati wa mlipuko huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, alisema: "Kulikuwa na mlipuko na kwa bahati mbaya watu 69 walikuwa wakifanya kazi katika vitalu vya B na C vya mgodi wa Madanjoo.
"Katika kitalu C kulikuwa na watu 22 na katika kitalu B kulikuwa na watu 47."
Bado haijafahamika ni watu wangapi ambao bado wako hai na wamenaswa ndani ya mgodi.
Vyombo vya habari vya serikali sasa vimerekebisha idadi yake ya awali ya vifo 30.
"Idadi ya wafanyikazi waliokufa iliongezeka hadi 51 na idadi ya waliojeruhiwa iliongezeka hadi 20," shirika rasmi la habari la IRNA liliripoti.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alitoa rambirambi kwa familia za wawlioathiriwa.
"Nilizungumza na mawaziri na tutafanya kila tuwezalo kufuatilia," Pezeshkian alisema katika ujumbe wa televisheni.
Waziri Mkuu wa Lebanon atoa wito kwa nchi kuchukua msimamo wa wazi juu ya 'mauaji ya kutisha'
Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Waziri Mkuu wa Lebanon ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kuchukua msimamo wa wazi" juu ya kile anachoita "mauaji haya ya kutisha" katika taarifa iliyochapishwa leo .
Waziri Mkuu Najib Mikati anasema alikuwa na nia ya kusafiri kwenda New York kushiriki katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lakini aliamua kutosafiri baada ya matukio ya wiki hii.
"Ninasisitiza kwamba hakuna kipaumbele kwa sasa ambacho ni cha juu zaidi kuliko kukomesha mauaji yanayofanywa na adui - Israel na aina mbalimbali za vita wanavyoendesha," ilisema taarifa hiyo.
"Pia natoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na ulimwengu kuchukua msimamowa wazi kuhusu mauaji haya ya kutisha."
Mikati pia anatoa wito wa "kupitishwa kwa sheria za kimataifa ili kupunguza njia za kiteknolojia za kiraia kutoka kwa malengo ya kijeshi na vita" kutokana na mashambulizi ya vifaa vya mawasiliano nchini mwake.
Mashariki ya Kati ipo 'kwenye ukingo wa janga linalokaribia'
Jeanine Hennis, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Lebanon, ametoa onyo kwa Israel na Hezbollah baada ya mapigano ya jana usiku.
Alisema: "Kwa kuwa eneo liko ukingoni mwa janga linalokaribia, haliwezi kuelezewa vya kutosha: HAKUNA suluhu la kijeshi ambalo litafanya kila upande kuwa salama."
Israel na Hezbollah zashambuliana kwenye mpaka wa Lebanon
Chanzo cha picha, Reuters
Iwapo ndio unajiunga na matangazo ya moja kwa moja ya leo, haya ndio tunayojua kufikia sasa kuhusu mapigano ya usiku kucha
Msururu wa maroketi yalirushwa kaskazini mwa Israel kutoka Lebanon usiku kucha, na kutua ndani zaidi ya Israeli kuliko mashambulizi ya awali.
Hezbollah inasema ililenga maeneo ya viwanda na kijeshi, na makumi ya nyumba ziliripotiwa kuharibiwa
IDF inasema roketi nyingi zilinaswa na mifumo ya ulinzi wa anga
Picha zilionekana kuonyesha moto katika eneo la makazi karibu na Haifa kaskazini mwa Israel baada ya kupigwa na roketi. Hakujawa na ripoti zozote za vifo
Mapema Jumapili, Israeli ilifunga shule na kuzuia mikusanyiko ya watu katika maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi na Milima ya Golan inayokaliwa na Israeli.
Wakati huo huo, Israel ilisema ilifikia malengo ya Hezbollah siku ya Jumamosi, ikiwa ni pamoja na maelfu ya mapipa ya kurusha roketi.
Mashambulizi ya kuvuka mpaka kati ya Hezbollah na Israel yameanza tena. Hezbollah inasema imerusha makombora katika maeneo mawili ya kijeshi kaskazini mwa Israel, huku IDF ikisema inashambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon.
Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la Israel huko Beirut siku ya Ijumaa imeongezeka hadi 37, wizara ya afya ya Lebanon inasema, huku juhudi za utafutaji na uokoaji zikiendelea Dahieh.
Jeshi la Israel (IDF) limesema limewaua wanachama 16 wa Hezbollah katika shambulio hilo, wakiwemo makamanda wakuu 12.
Mkutano wa wanahabari wa wizara ya afya ya Lebanon umefichua asubuhi ya leo kwamba watu 152 bado wako katika hali mbaya baada ya vifaa vya mawasiliano kulipuka siku ya Jumanne na Jumatano. Pia ilisema idadi ya waliouawa katika siku mbili za milipuko imeongezeka kutoka 37 hadi 39
Mbali na Lebanon huko Gaza, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema takriban watu 22, "wengi" watoto na wanawake, wameuawa kufuatia shambulio la shule katika mji wa Gaza ambao ni makazi ya watu waliokimbia makazi yao.
Trump akataa mjadala wa pili wa TV akisema 'umechelewa sana'
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema hatashiriki katika mjadala wa pili wa televisheni kabla ya uchaguzi wa urais mwezi Novemba.
Wakati Makamu wa Rais Kamala Harris, mgombea wa Chama cha Democratic , alikubali mwaliko wa mdahalo wa CNN tarehe 23 Oktoba, mgombea mteule wa Republican Trump aliambia mkutano kuwa "umechelewa" kwani upigaji kura tayari umeanza.
Timu ya kampeni ya Harris ilisema kwamba kutokana na rais huyo wa zamani kudai kuwa alishinda mjadala wao wa awali huko Philadelphia mapema mwezi huu anapaswa kukubali.
Kura za maoni zilizopigwa baada ya mkutano huo zilipendekeza kuwa wengi wa watazamaji waliamini kuwa makamu wa rais alimshinda mpinzani wake.
Baada ya mjadala wa Septemba 10, Trump alisema hakutakuwa na mijadala zaidi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara huko Wilmington, North Carolina siku ya Jumamosi, alidai ushindi katika mdahalo huo wa awali na kusema "umechelewa sana" kwa mwingine.
"Upigaji kura tayari umeanza," alisema, akimshutumu Harris kwa kutafuta duru nyingine yapambano "kwa sababu anapoteza vibaya."
Katika taarifa siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa kambi ya kampeni ya Harris-Walz Jen O'Malley Dillon alisema kuwa Wamarekani "wanastahili fursa nyingine" ya kuona mjadala wa Harris na Trump kabla ya uchaguzi wa Novemba.
"Itakuwa jambo lisilokuwa la kawaida katika historia ya kisasa kwa kuwa na mjadala mmoja tu wa uchaguzi mkuu," alisema. "Mijadala inatoa fursa ya kipekee kwa wapiga kura kuona wagombea bega kwa bega na kutathmini maono yao ya ushindani kwa Marekani."
Kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, Harris alisema "amekubali mwaliko wa mjadala" kwa furaha na anatumai Trump pia atashiriki.
Israel yaamuru kufungwa kwa siku 45 kwa ofisi ya Al Jazeera Ukingo wa Magharibi
Chanzo cha picha, AlJAZEERA
Vikosi vya Israel vimevamia ofisi za shirika la utangazaji la Al Jazeera huko Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuamuru kufungwa kwa muda wa siku 45.
Wanajeshi wa Israel wenye silaha na waliojifunika nyuso zao waliingia ndani ya jengo hilo mapema Jumapili wakati wa matangazo ya moja kwa moja.
Watazamaji walitazama wanajeshi wakitoa agizo la kufungwa kwa mkuu wa ofisi hiyo katika Ukingo wa Magharibi Walid al-Omari ambaye aliisoma moja kwa moja ujumbe huo hewani.
Israel ilivamia ofisi za Al Jazeera huko Nazareth na Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu mwezi Mei baada ya kulielezea shirika hilo la utangazaji lenye makao yake Qatar kuwa tishio kwa usalama wa taifa.
"Kulenga waandishi wa habari kwa njia hii kila mara kunalenga kufuta ukweli na kuzuia watu kusikia ukweli," Omari alisema katika maoni yaliyoripotiwa na mwajiri wake.
Wanajeshi hao walichukua maikrofoni na kamera ya mwisho nje ya barabara ya ofisi hizo na kumlazimisha Omari kutoka nje ya ofisi, mwandishi wa habari wa Al Jazeera Mohammad Alsaafin alisema.
Akichapisha kuhusu uvamizi huo kwenye mitandao ya kijamii, Alsaafin alisema wanajeshi hao pia waling'oa bango la Shireen Abu Aqla - ripota wa Al Jazeera ambaye aliuawa wakati akiripoti uvamizi wa vikosi vya Israel katika Ukingo wa Magharibi.
Aljazeera na mashuhuda wa wakati huo walisema mwandishi huyo wa habari Mpalestina mwenye uraia wa Marekani alipigwa risasi na wanajeshi wa Israel. Hapo awali Israel ilidai kuwa alipigwa risasi na Mpalestina, hata hivyo miezi kadhaa baadaye ilihitimisha kuwa kulikuwa na "uwezekano mkubwa" kwamba mmoja wa askari wake alimuua.
Israel yazuia mikusanyiko kaskazini mwa nchi huku ikiendelea kushambulia Hezbollah
Chanzo cha picha, Reuters
Israel imeanzisha mashambulizi ya anga nchini Lebanon na inazuia mikusanyiko katika mji wa Haifa na maeneo mengine ya kaskazini huku ikiendelea kushambulia maeneo yanayohusishwa na Hezbollah.
Makumi ya ndege za kivita zilianza "kwa kiasi kikubwa" kushambulia kusini mwa Lebanon "kufuatia kugundulika kwa Hezbollah ikijiandaa kufyatua risasi kuelekea eneo la Israeli", msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Daniel Hagari alisema.
Mashambulizi ya hivi punde zaidi ya Israel yanakuja siku moja baada ya kufanya shambulio la anga huko Beirut, ambalo IDF ilisema liliua dazeni ya makamanda wakuu wa Hezbollah. Lebanon ilisema watu 37 - wakiwemo watoto watatu - waliuawa .
Serikali ya Marekani inawataka raia wake huko kuondoka "kupitia chaguzi za usafiri wa kibiashara wakati bado zinapatikana".
Siku ya Ijumaa, makabiliano ya mapigano mpakani yalianza tena kati ya Israel na Hezbollah.
Kabla ya mashambulio ya Waisraeli jioni kuanza, IDF ilisema hapo awali ilikuwa imeharibu "takriban maeneo 180 na maelfu ya mapipa ya kurusha roketi" kwa mashambulizi
IDF pia ilisema zaidi ya roketi 90 zilirushwa katika eneo la Israeli kutoka Lebanon. Hezbollah ilisema ililenga maeneo 11 ya kijeshi ya Israeli katika siku hiyo.
Siku ya Jumamosi usiku, Hezbollah ilisema kuwa ilirusha makumi ya roketi kuelekea kituo cha ndege cha Ramat David kilicho kaskazini mwa Israel ili kulipiza kisasi mashambulizi ya Israel.
Mapema wiki hii, watu 39 waliuawa na maelfu kujeruhiwa baada ya vifaa vya mawasiliano vilivyotumiwa na Hezbollah, wanamgambo na kundi la kisiasa linaloungwa mkono na Iran kulipuka kwa siku mbili kote Lebanon.
Siku ya Alhamisi, kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliilaumu Israel kwa mashambulizi hayo, akisema ilikuwa imevuka "mistari yote ya rangi nyekundu" na kuapa "adhabu kali".