Air Tanzania kuwarejesha nyumba Watanzania waliokwama Dubai
Shirika la ndege la Tanzania, Air Tanzania limetangaza mpango wa kuwarejesha nyumbani raia wa nch hiyo walioathiriwa na hatua ya kusitishwa kwa safari za ndege kufuatia mgogoro uliozuka eneo la mashariki ya kati.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Machi 6, Air Tanzania imesema ndege hiyo maalum itasafiri kutoka Dar es Salam kuelekea Dubai na kurejea Dar es Salaam siku ya Jumapili.
Imesisitiza ndege hiyo sio ya kibiashara na kuongeza kwamba itawapatia kipaumbele wasafiri ambao walikuwa wamekata tiketi kabla ya safari kusitishwa.
Mashirika ya ndege ya kimataifa yamekuwa yakiahirisha safari za kuelekea Mashariki ya Kati tangu Marekani na Israel zilipoanza mashambulizi dhidi ya Iran Jumamosi iliyopita.
Safari za ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Tel Aviv, Dubai, Doha na vituo vingine vya kimataifa katika eneo hilo zimesitishwa.
Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza inawashauri raia wa Uingereza dhidi ya safari zote za kwenda Bahrain, Kuwait, Qatar na Falme za Kiarabu (UAE).
Wale ambao tayari wapo katika maeneo hayo wameshauriwa kuwa makini.
Iran imefanya mashambulizi katika mataifa ya Ghuba kama sehemu ya kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanza mapema Jumamosi.
Usafiri wa mbali umeathiriwa zaidi, huku Heathrow ikiwaomba wasafiri kuthibitisha safari zao na mashirika yao ya ndege.