Jumuiya ya
kikanda ya Afrika Magharibi ECOWAS imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ilivyo
nchini Venezuela na kutoa wito wa kujizuia na kuheshimu sheria za kimataifa.
Katika
taarifa iliyotolewa jijini Abuja, Nigeria, ECOWAS inatambua haki ya mataifa kupambana na
uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi na biashara ya dawa za kulevya lakini
imeonya kwamba juhudi hizo "lazima zifanyike kulingana na kanuni
zilizowekwa za sheria za kimataifa."
Kambi hiyo imeikumbusha
jumuiya ya kimataifa kuhusu wajibu wake wa kuheshimu uhuru na mipaka ya chini katika Kifungu cha 2(4) cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
ECOWAS imesema
"inaunga mkono kikamilifu msimamo wa Umoja wa Afrika," na kuhimiza
mazungumzo jumuishi miongoni mwa Wavenezuela kama njia ya kutatua mgogoro huo.
ECOWAS imetoa
kauli hii kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na kukamatwa kwa Rais
Nicolás Maduro.
Umoja wa
Afrika umeonyesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu matukio hayo, ukisisitiza
kwamba hali hiyo inatishia amani na usalama wa kimataifa.
Umoja wa bara la Afrika, "umesisitiza umuhimu wa mazungumzo, utatuzi wa migogoro
kwa amani, na heshima kwa mifumo ya kikatiba na kitaasisi, katika roho ya
ujirani mwema, ushirikiano, na kuishi kwa amani miongoni mwa mataifa."
Umoja wa Afrika
umesema changamoto za ndani za Venezuela "zinaweza kushughulikiwa kupitia
mazungumzo ya kisiasa miongoni mwa Wavenezuela wenyewe."
Afrika
Kusini imehimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano haraka,
ikielezea mashambulizi ya Marekani na kumkamata Maduro kama "uvamizi wa
kijeshi."
Wizara ya
Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya nchi hiyo imesema vitendo vya Marekani
ni ukiukaji dhahiri wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unazitaka nchi zote
wanachama kujiepusha na matumizi ya nguvu dhidi ya uhuru wa eneo au uhuru wa
kisiasa wa taifa lolote.
Jirani wa
Afrika Kusini, Namibia pia amelaani vitendo vya Marekani, akielezea kukamatwa
kwa Maduro na mkewe kama ukiukaji wa uhuru wa Venezuela.
Wizara ya
Mahusiano na Biashara ya Kimataifa ya Namibia imesisitiza kwamba uadilifu wa
eneo na uhuru wa kisiasa wa mataifa yote lazima uheshimiwe kwa mujibu wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Venezuela, taifa la Amerika Kusini linakabiliwa na miaka mingi ya kutokuwa na utulivu wa
kisiasa, ugumu wa kiuchumi, na shinikizo la kimataifa, na kuacha mgawanyiko
mkubwa kuhusu njia bora ya kutatua mgogoro huo.