Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Israel yakamata kundi la pili la wanaodaiwa kuwa majasusi wa Iran

Watu saba wamekamatwa katika eneo la Jerusalem Mashariki linalokaliwa kwa mabavu kwa tuhuma za kupanga mashambulizi kwa ajili ya Iran, idara za usalama za Israel zimesema.

Muhtasari

  • Rais Ruto: Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Gachagua
  • Blinken awasili Israel kushinikiza kusitishwa kwa mapigano Gaza
  • China imefanya mazoezi ya silaha karibu na Taiwan
  • Rais wa zamani wa Peru ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela
  • Harris anajaribu kushawishi Warepublican
  • Kenya: Mahakama kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa kwa Gachagua ofisini
  • Rais wa Cameroon hatimaye aonekana hadharani
  • Israel bado inazuia misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza - Unrwa
  • Umoja wa Mataifa 'unasikitishwa' kuwa Kenya iliwarudisha makwao kwa lazima wakimbizi kutoka Uturuki
  • Lebanon yasema watu wanne wameuawa katika shambulio la Israel karibu na hospitali iliyo kusini mwa Beirut

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Lebanon yasema watu 18 wameuawa katika shambulizi la Israel kusini mwa Beirut

    Takribani watu 18, wakiwemo watoto wanne, wameuawa katika shambulizi la anga la Israel karibu na hospitali kubwa ya umma ya Lebanon kusini mwa Beirut, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.

    Watu wengine 60 walijeruhiwa wakati takribani majengo matatu yapatayo umbali wa 50m (160ft) kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri yalipoharibiwa katika kitongoji cha Jnah Jumatatu usiku.

    Wizara ya afya ilisema shambulio hilo, moja kati ya 13 lililoripotiwa katika mji mkuu, lilisababisha "uharibifu mkubwa" kwa hospitali.

    Jeshi la Israel lilisema lilipiga "lengo la kigaidi la Hezbollah" karibu na hospitali hiyo, bila kutoa maelezo, na kusisitiza kuwa hospitali hiyo haikulengwa.

    Siku ya Jumanne asubuhi, waokoaji walipekua marundo ya saruji iliyovunjika na chuma kilichosokotwa, wengine wakiwa wamebeba majembe, wengine kwa mikono yao tu, kwenye eneo lilipotokea shambulizi.

    Mahali pazuri palikuwa kitongoji masikini na chenye watu wengi.

    Takribani majengo matatu ya ghorofa nyingi yaliporomoka na mengine kadhaa kuharibiwa vibaya.

    Mmoja wa waokoaji alisema hawakujua ni watu wangapi wanaweza kuwa chini ya vifusi.

    Timu ya BBC iliona mwili mmoja ukitolewa, huku mwingine ukipatikana walipokuwa wakiondoka.

    Mkazi mmoja alisema shambulio hilo lilitokea baada ya gari kuwasili katika eneo hilo, lakini akaongeza kuwa hawawezi kusema ni nani aliyekuwa ndani ya chombo hicho.

  2. Israel yakamata kundi la pili la wanaodaiwa kuwa majasusi wa Iran

    Watu saba wamekamatwa katika eneo la Jerusalem Mashariki linalokaliwa kwa mabavu kwa tuhuma za kupanga mashambulizi kwa Iran, idara za usalama za Israel zimesema, kesi hiyo ikiwa ni kesi ya pili katika siku nyingi.

    Wakala wa usalama wa ndani wa Shin Bet na polisi walisema katika taarifa ya pamoja kwamba washukiwa hao walikuwa wamepanga, "chini ya maelekezo ya Iran," kumuua mwanasayansi mkuu wa Israel na meya wa jiji.

    Pia walipewa jukumu la kulipua gari la polisi na kurusha guruneti kwenye nyumba, kwa malipo ya takribani shekeli 200,000 (£40,700; $53,000), mamlaka ilisema.

    Habari za kuzuiliwa huko zinakuja siku moja baada ya idara za usalama za Israel kutangaza kuwa Waisraeli saba wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa ajili ya Iran.

    Iran ni adui mkubwa wa Israel na mivutano kati ya nchi hizo mbili iko juu zaidi kwa miaka mingi. Israel imeahidi kulipiza kisasi dhidi ya shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israel tarehe 1 Oktoba.

    Taarifa hiyo ilisema kundi hilo lilikuwa linaongozwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 23, ambaye inadaiwa aliajiriwa kama mshirika wa Iran.

    Kiongozi huyo anasemekana kuwaajiri washukiwa wengine sita.

    Vyombo vya habari vya ndani vilisema mtu huyo alikiri kutekeleza "shughuli za kigaidi" kwa sababu za kitaifa.

    Taarifa ya Shin Bet na polisi ilisema: "Wanasayansi, mameya, maafisa wa usalama, na Waisraeli wengine mashuhuri wanalengwa na mawakala wa Iran.

    "Uchunguzi huu unasisitiza juhudi za Iran kuajiri raia wa Israeli kwa ugaidi. "Vyombo vya usalama vya Israel vitaendelea kushirikiana kuchunguza shughuli za Iran na kuwafungulia mashtaka wanaohusika."

    Unaweza kusoma

  3. Raia wa Urusi wahofiwa kufa baada ya ndege kudunguliwa nchini Sudan

    Ubalozi wa Urusi nchini Sudan umesema unachunguza ripoti kwamba ndege ya mizigo iliyokuwa na wafanyakazi wa Urusi ilidunguliwa huko Darfur, uwanja muhimu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

    Ndege hiyo, iliyotambuliwa kama lyushin Il-76 iliyotengenezwa nchini Urusi, ilikuwa kwenye misheni ya kupeleka vifaa na dawa katika mji unaoshikiliwa na jeshi wa el-Fasher, duru za kijeshi ziliambia vyombo vya habari vya Sudan.

    Siku ya Jumatatu, RSF ilisema iliiangusha ndege iliyotengenezwa Urusi iliyokuwa ikisafirishwa na jeshi la Misri ambayo ilishutumu kwa kuwalipua raia, ingawa ilitambuliwa kama Antonov.

    Misri inakanusha shutuma kwamba imekuwa ikitoa msaada wa kijeshi kwa jeshi la Sudan wakati wa mzozo uliodumu kwa miezi 18.

    Mapambano makali ya kugombea madaraka kati ya jeshi na RSF yalianza Aprili 2023, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita mojawapo ya machafuko mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.

    Baadhi ya makadirio yanaonesha hadi watu 150,000 wameuawa tangu vita vilipoanza mwaka jana, kulingana na maoni yaliyotolewa mwezi Mei na mjumbe maalumu wa Marekani kwa Sudan Tom Perriello.

    Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa pia umewalazimisha zaidi ya watu milioni 10, karibu theluthi moja ya watu kutoka kwenye makazi yao.

  4. Hezbollah yadai kuhusika na shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye nyumba Netanyahu

    Afisa wa habari wa Hezbollah amedai kuhusika kwa kundi hilo kwenye shambulio la wiki iliyopita la ndege isiyo na rubani kwenye nyumba ya mapumziko ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mji wa pwani wa Kaisaria.

    Ofisi ya Netanyahu ilisema ndege isiyo na rubani "ilirushwa kuelekea" makazi Jumamosi asubuhi.

    Si Netanyahu wala mke wake waliokuwepo wakati huo na hakuna aliyejeruhiwa.

    Netanyahu alihusisha shambulio hilo na Hezbollah katika chapisho kwenye X siku hiyo hiyo.

    Maoni ya Hezbollah yalikuja katika mkutano na waandishi wa habari uliotolewa na mkuu wa ofisi ya vyombo vya habari vya kundi hilo Mohammad Afif leo.

    Shirika la habari la Reuters linamnukuu Afif akisema: "Hezbollah imechukua jukumu la pekee la kulenga nyumba ya Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu."

    Unaweza kusoma;

  5. Rais apinga uwezo wa Mahakama ya Juu kusikiliza kesi za kumuondoa Gachagua madarakani

    Wakili wa Rais William Ruto ameanza kwa kusema kuwa anamwakilisha mteja wake na kwamba amesema Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi za kupinga kuondolewa kwa Rigathi Gachagua madarakani zilizowasilishwa.

    Jopo la majaji watu likiongozwa na Jaji Eric Ogola pia linajumuisha majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi lilichanguliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kusikiliza kesi zote zenye kuhusiana na kuondolewa madarakani kwa Rigathi Gachagua.

    Kupitia Wakili Adrian Kamotho, Ruto anadai kuwa Mahakama ya Juu Zaidi pekee ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

    Kulingana na Rais William Ruto, mahakama inafaa kutupilia mbali kesi hizo akidai kuwa zimewasilishwa kinyume cha sheria na ni utumiaji mbaya wa mchakato wa mahakama.

    Rais Ruto ameongeza kuwa kesi dhidi ya Rais au mtu anayetekeleza majukumu ya afisi ya Rais katika kipindi cha uongozi wake kuhusiana na jambo lolote lililofanywa au kutofanywa chini ya sheria ya Katiba ya Kenya 2010 haziwezi kufunguliwa katika mahakama yoyote tu.

    Kwa sasa mahakama imeahirisha kikao chake hadi mwendo wa saa nane mchana saa za Afrika Mashariki na kutoa uamuzi iwapo jopo hilo lina uwezo wa kusikiliza kesi hizo.

    Naibu Rais aliyeondolewa madarakani Rigathi Gachagua alikuwepo mahakamani.

    Soma zaidi:

  6. Blinken awasili Israel kushinikiza kusitishwa kwa mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewasili nchini Israel kwa mazungumzo na viongozi wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    Hiki ni kituo cha kwanza cha ziara pana zaidi katika Mashariki ya Kati - ikiwa ni ya 11 tangu vita vya Gaza kuanza - ambapo atajaribu kushinikiza mazungumzo ya kusitisha mapigano.

  7. China imefanya mazoezi ya kutumia silaha kwenye kisiwa kilicho karibu zaidi na Taiwan

    China imefanya mazoezi ya kutumia silaha kutoka eneo lake lililo karibu na Taiwan wiki moja baada ya kuzindua mazoezi makubwa ya kuzunguka kisiwa hicho.

    Mazoezi ya kijeshi ya China kwenye pwani ya Taiwan yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni huku madai yake juu ya kisiwa hicho kinachojitawala yakiongezeka.

    Beijing ilitangaza Jumatatu kwamba eneo karibu na Niushan - kisiwa kilicho kilomita 105 (maili 66) kutoka Taiwan - litafungwa kwa ajili ya mazoezi kwa saa nne kutoka 09:00 saa za eneo siku ya Jumanne.

    Waziri Mkuu wa Taiwan Cho Jung-tai alisema Jumanne kwamba China haipaswi kufanya mazoezi kama hayo kutokana na tishio lao la utulivu wa kikanda.

    Soma zaidi:

  8. Rais wa zamani wa Peru ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela

    Mahakama nchini Peru imemhukumu rais wa zamani Alejandro Toledo kifungo cha miaka 20 na miezi sita jela kwa kosa la rushwa na utakatishaji fedha.

    Waendesha mashtaka wanasema alichukua $35m (£27m) kama hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Brazil ambayo ilipewa kandarasi ya kujenga barabara kusini mwa Peru.

    Toledo, 78, alikuwa ofisini kati ya 2001 na 2006.

    Alikamatwa miaka mitano iliyopita huko California ambako alikuwa ameishi na kufanya kazi kwa miaka mingi, na kurejeshwa Peru mwaka jana.

    Kampuni ya Brazil ya Odebrecht ilikiri kulipa mamilioni ya dola kama rushwa kwa maafisa kote Amerika ya Kusini na Marekani ili kupata kandarasi za serikali.

  9. Harris anajaribu kushawishi Warepublican, huku Trump akisema 'mkono wa Mungu unaniongoza'

    Tunaendelea kukufahamisha kuhusu taarifa za kampeni za uchaguzi nchini Marekani.

    Zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya siku ya kupiga kura tarehe 5 Novemba, kampeni inakaribia kuingia katika kipindi chake cha lala salama:

    Yaliyojiri:

    Siku ya Jumatatu Kamala Harris alizuru majimbo muhimu na Liz Cheney, mbunge wa zamani wa Republican ambaye amekuwa akimkosoa vikali Donald Trump.

    Harris alijaribu kuomba kura kwa wapiga kura wa Republican ambao wamekatishwa tamaa na Trump, akiwaambia "hawako peke yao" katika jaribio la kuwashawishi kubadili chama.

    Kwingineko, Trump alihutubia hadhira ya Wakristo wa kiinjili huko North Carolina, jimbo lingine ambalo lina uwezekano wa kuchukuliwa na upande wowote katika uchaguzi huu

    Trump alisema "mkono wa kimuujiza" ulimwokoa kutokana na kuuawa mnamo mwezi Julai.

    Rais huyo wa zamani anashtakiwa kwa kumchafulia mtu jina katika maoni aliyotoa wakati wa mjadala wa televisheni mwezi uliopita

    Steve Bannon, mshirika mkuu wa Trump ambaye alimfanyia kazi katika Ikulu ya White House, ataachiliwa kutoka gerezani wiki ijayo

    Kambi ya Kampeni ya Harris ilitumia zaidi ya mara tatu ya kiasi kilichotumiwa naTrump mwezi uliopita, kulingana na takwimu mpya - na kura za maoni bado zinaonyesha kinyang’anyiro hicho kinakaribiana sana.

    Soma zaidi:

  10. Kenya: Mahakama kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa kwa Gachagua ofisini

    Jopo la majaji watatu leo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa ofisini kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais .

    Jopo hilo linaloongozwa na Jaji Eric Ogola pia lina majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi na liinatarajiwa kutoa uamuzi leo ikiwa litaondoa au kuongeza muda wa maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kuchukua wadhifa wa Naibu Rais baada ya uteuzi wake na Rais William Ruto na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa siku ya Ijumaa.

    Hii ni baada ya majaji Chacha Mwita kutoka Milimani na Richard Mwongo kutoka Kerugoya kutoa maagizo ya kusitisha utekelezwaji wa azimio lililopitishwa na Seneti kumwondoa Gachagua ofisini kupitia kura iliyopitisha mashtaka 5 kati ya 11 dhidi yake yaliyowasilishwa kwa seneti na bunge la Kitaifa na kumzuia Kithure kuchukua usukani katika Ofisi hiyo.

    Juhudi za Mwanasheria Mkuu wa serikali Dorcas Oduor kutaka maagizo hayo yaondolewe yalitupiliwa mbali na mahakama ya majaji watatu, ambayo badala yake iliamuru kusikilizwa kwa kesi baina ya pande zote Jumanne.

    Wakati huo huo Idara ya DCI nchini Kenya imemtaka Gachagua kufika katika makao yake ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai yake kwamba kulikuwa na majaribio mawili ya kumuua kutumia sumu .

    Idara hiyo imesema madai hayo yana uzito na hivyo basi Gachagua anafaa kuyatolea ufafanuzi.

    Soma zaidi:

  11. Paul Biya: Rais wa Cameroon hatimaye aonekana hadharani

    Rais wa Cameroon Paul Biya mwenye umri wa miaka 91 ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza ndani ya wiki sita huku kukiwa na uvumi kuhusu afya yake kudorora.

    Kutokuwepo kwake hadharani kulisababisha uvumi usio na msingi wa kifo chake.

    Lakini siku ya Jumatatu mchana televisheni ya taifa ilionyesha picha za kuwasili kwa rais katika uwanja wa ndege kwenye mji mkuu, Yaoundé, kwa ndege kutoka Uswizi.

    Serikali ilikuwa imepiga marufuku vyombo vya habari kujadili afya ya Biya – ambaye amekuwa madarakani tangu 1982 - ikiainisha kama suala la usalama wa taifa.

    Tetesi za kifo chake zimekuwa zikienea kila mara kwa miongo miwili iliyopita.

    Picha za Jumatatu zinaonyesha rais akiwa amevalia suti yake nadhifu ya kawaida na mwenye nguvu.

    Mara ya mwisho Biya kuonekana ilikuwa tarehe 8 Septemba akihudhuria mkutano wa kilele wa China na Afrika mjini Beijing.

    Tangu wakati huo, serikali imekuwa chini ya shinikizo kubwa kuthibitisha kwamba kiongozi huyo wa muda mrefu alikuwa hai.

    Maafisa wa serikali hatimaye walikanusha madai kwamba alifariki, wakisema kuwa Biya alikuwa bukheri wa afya na kwamba yuko katika ziara ya faragha huko Geneva.

    Anajulikana kwa ziara za mara kwa mara kwenye jiji la Uswizi.

    Baada ya kutua, Biya alikaribishwa na viongozi wa serikali na wanachama wa chama tawala.

    Ukusanyaji usio wa kawaida wa watu katika baadhi ya mitaa kwenye mji mkuu ulionyesha nia ya wazi ya serikali kukomesha uvumi kuhusu ustawi wake.

    Soma zaidi:

  12. Israel bado inazuia misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza - Unrwa

    Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa) amesema Israel inaendelea kuzuia misheni ya kibinadamu kufika kaskazini mwa Gaza ikiwa na vifaa muhimu kama chakula na dawa.

    "Hospitali zimeshambuliwa na kuachwa zimelemazwa huku watu waliojeruhiwa wakiachwa bila huduma," Philippe Lazzarini aliandika kwenye mtandao wa X.

    Pia alisema makazi yaliyosalia ya Unrwa yalikuwa yamejaa kupita kiasi hivi kwamba watu waliokimbia makazi "wanalazimika kuishi kwenye vyoo", na akataja ripoti kwamba watu wanaojaribu kukimbia walikuwa wakiuawa.

    Jeshi la Israel limekuwa likizidisha mashambulizi ya wiki moja katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza dhidi ya kile ilichosema ni wapiganaji wa Hamas waliojikita tena huko.

    Siku ya Jumatatu wakaazi na madaktari walisema vikosi vya Israel vilikuwa vinazingira hospitali na makazi ya watu waliokimbia makazi yao.

    Jeshi la Israel lilisema linarahisisha uhamishaji wa raia na kuhakikisha hospitali zinaendelea kufanya kazi huku likiendelea "kukabiliana na magaidi na miundombinu ya kigaidi".

    Soma zaidi:

  13. Umoja wa Mataifa 'unasikitishwa' kuwa Kenya iliwarudisha makwao kwa lazima wakimbizi kutoka Uturuki

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema "linasikitishwa" na habari kwamba wakimbizi wanne walirejeshwa Uturuki kutoka Kenya.

    Wakimbizi hao walirejeshwa makwao kwa ombi la serikali ya Uturuki, wizara ya mambo ya nje ya Kenya inasema.

    Kauli hiyo inajiri baada ya ripoti za watu kadhaa kutekwa nyara katika jiji kuu la Nairobi siku ya Ijumaa.

    Raia wa Uingereza aliambia BBC kuwa yeye na raia kadhaa wa Uturuki walikuwa wametekwa nyara na watu waliojifunika nyuso zao.

    Alisema alikuwa ameachiliwa baada ya saa nane alipowaonyesha watu wanaodaiwa kumteka nakala ya paspoti yake ya Uingereza.

    Katika taarifa yake, UNHCR ilisema: "UNHCR inaitaka Serikali ya Kenya kutii wajibu wao wa kisheria wa kimataifa, na hasa, kuheshimu kanuni ya kutorejesha wakimbizi [kwa lazima], ambayo inawalinda wanaotafuta hifadhi na wakimbizi dhidi ya aina yoyote ile ya hatua ambayo inaweza kusababisha kuondolewa kwao hadi mahali ambapo maisha au uhuru wao ungetishiwa."

    Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imesema imekubali ombi la Uturuki la kuwarejesha nyumbani watu hao wanne kwa sababu ya "uhusiano thabiti wa kihistoria na kimkakati" wa nchi hiyo na Uturuki, na kwamba imehakikishiwa wakimbizi "watatendewa utu".

    Wanne hao wanaaminika kuwa wafuasi wa vuguvugu la Gulen, jumuiya yenye nguvu ya Kiislamu yenye wafuasi nchini Uturuki na duniani kote, ambayo kiongozi wake amefariki dunia.

    Vuguvugu la Gulen linaendesha mtandao wa shule nchini Kenya na duniani kote.

  14. Lebanon yasema watu wanne wameuawa katika shambulio la Israel karibu na hospitali iliyo kusini mwa Beirut

    Watu wanne akiwemo mtoto wameuawa katika shambulizi la anga la Israel karibu na hospitali kuu ya serikali kusini mwa Beirut, wizara ya afya ya Lebanon inasema.

    Shambulizi hilo lilionekana kulenga maegesho ya magari ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri, chanzo cha hospitali kililiambia shirika la habari la Reuters.

    Wizara ya afya imesema watu 24 wamejeruhiwa.

    Ilikuwa ni miongoni mwa mashambulizi 13 ya anga yaliyokumba Beirut kusini Jumatatu jioni.

    Jeshi la Israel lilisema lilikuwa linashambulia vituo vinavyohusishwa na Hezbollah.

    Msemaji wa Israel hapo awali alikuwa amewaonya watu kuhama kutoka maeneo kadhaa kusini mwa Beirut, hata hivyo hospitali ya Rafik Hariri haikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotajwa.

    Video kutoka kitongoji cha Dahiyeh kusini mwa Beirut, ambapo maeneo saba yatakayolengwa yalitangazwa mapema, zilionyesha wenyeji wakikimbia kwa magari na kwa miguu huku mashambulizi hayo yakianza.

    Eneo moja lililotambuliwa kama shabaha ya jeshi la Israel lilikuwa takriban mita 400 kutoka uwanja wa ndege wa Beirut, ambao ndiyo pekee wa kimataifa unaohudumia Lebanon.

    Vyombo vya habari vya ndani vilishirikisha picha za baadhi ya madirisha katika jengo la uwanja wa ndege ambayo yalilipuliwa katika mlipuko huo.

    Israel haijatoa maoni yoyote tangu ilipotoa maonyo ya awali ya kuwahamisha.

    Awali, Jeshi la Israel lilikuwa limesema mapema Jumatatu kwamba liligundua ngome ya Hezbollah iliyojifichwa chini ya hospitali tofauti kusini mwa Beirut, ambayo tangu wakati huo imehamishwa.

    Msemaji wa IDF Admiral Daniel Hagari alisema bila kutoa ushahidi kwamba chumba cha kulala chini ya hospitali ya Sahel huko Haret Hreik kilikuwa na mamia ya mamilioni ya dola taslimu na dhahabu ambazo zilikuwa zikitumika kufadhili mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel.

    Hata hivyo, mkurugenzi wa hospitali ya Sahel alikanusha kuwa kulikuwa na chumba cha kulala chini yake na kutoa wito kwa jeshi la Lebanon kukagua eneo hilo.

    Israel inaonekana kupanua vita vyake dhidi ya Hezbollah zaidi ya miundombinu ya kijeshi na inasema inalenga mitandao ya kifedha ya kundi hilo.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 22/10/2024