Kwaheri hadi kesho
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho panapo majaliwa.
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Putin amesema Moscow itatumia "njia zote za uharibifu,” iwapo Ukraine itataka kumiliki silaha za nyuklia, kulingana na shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA Novosti.
Na Lizzy Masinga & Rashid Abdallah
Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho panapo majaliwa.
Akiwa katika mkutano na wanahabari nchini Kazakhstan, Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema nchi yake haitairuhusu Ukraine kumiliki silaha za nyuklia.
Anasema Moscow itatumia "njia zote za uharibifu,” iwapo Ukraine itataka kumiliki silaha za nyuklia, kulingana na shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA Novosti.
"Hatutaruhusu hilo," rais wa Urusi amesema.
Matamshi yake yanafuatia ripoti ya gazeti la Marekani la New York Times, wiki iliyopita, ambayo ilisema maafisa wa nchi za Magharibi walijadili njia mbalimbali ambazo Rais wa Marekani Joe Biden anaweza kuzifanya kuisaidia Ukraine kabla ya kuondoka madarakani mwezi Januari.
Kulingana na gazeti la Times, maafisa ambao hawakutajwa majina walijadili njia za kuizuia Urusi, na wengine walipendekeza kurejeshwa kwa silaha za nyuklia ambazo ziliondoshwa kutoka Ukraine mwishoni mwa Vita Baridi.
Lakini hatua kama hiyo itakuwa ngumu na ya hatari kubwa.
Nchi ya Australia itapiga marufuku watoto walio chini ya miaka 16 kutumia mitandao ya kijamii, baada ya baraza la Seneti kuidhinisha sheria hiyo.
Marufuku hiyo - ambayo itatekelezwa baada ya miezi 12 - inaweza kusababisha kampuni za mitandao ya kijamii kutozwa faini ya hadi dola za Kimarekani milioni 32.5 ikiwa hazitatii.
Waziri Mkuu Anthony Albanese anasema sheria hiyo inahitajika ili kuwalinda vijana dhidi ya "madhara" ya mitandao ya kijamii, huku makundi mengi ya wazazi yakiiunga mkono.
Lakini wadadisi wanasema maswali kuhusu jinsi marufuku hiyo itakavyo fanya kazi na athari zake kwa uhusiano wa kijamii bado hayajajibiwa.
"Hili ni tatizo la kimataifa," Albanese alisema wakati akiwasilisha mswada huo kwenye baraza la mawaziri wiki iliyopita. "Tunataka wazazi wawe na amani ya akili."
Baada ya kupita Seneti kwa kura 34 dhidi ya 19 mwishoni mwa Alhamisi, mswada huo utarejea katika Baraza la Wawakilishi - ambapo serikali ina wingi wa kura, ikimaanisha ina uhakika wa kupita, kabla ya kuwa sheria.
Sheria haijabainisha ni majukwaa gani yatapigwa marufuku. Maamuzi hayo yatafanywa baadaye na waziri wa mawasiliano wa Australia, ambaye atatafuta ushauri kutoka kwa kamisheni ya usalama wa mtandaoni ambayo itasimamia sheria hiyo.
Majukwaa ya michezo ya gemu na kutuma ujumbe hayataguswa, na tovuti zinazoweza kufikiwa bila kuuda akaunti, mfano YouTube.
Serikali inasema inategemea kutakuwa na aina fulani ya teknolojia ya uthibitishaji wa umri kutekeleza marufuku hii na jukumu litakuwa kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii kuweka teknolojia hiyo.
Hata hivyo watafiti wa kidijitali wameonya kuwa hakuna hakikisho kwamba teknolojia ambayo haijabainishwa - itafanya kazi.
Pia wameonya kuwa vizuizi vinaweza kuepukwa kwa urahisi kupitia program kama VPN - ambayo inaweza kuficha eneo la mtumiaji na kumfanya aonekane yuko nchi nyingine.
Lakini watoto ambao watavunja sheria hiyo hawatakabiliwa na adhabu.
Kura za maoni juu ya sheria hii, zinaonyesha inaungwa mkono na wazazi na walezi wengi wa Australia.
Pia unaweza kusoma:
Mwanajeshi wa zamani wa jeshi la Uingereza Daniel Khalife amepatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa ajili ya Iran.
Khalife, ambaye alitoroka jela wakati akisubiri kesi yake, alikusanya taarifa na kuzifikisha Tehran na imebainika kuwa amekusanya majina ya askari wa kikosi maalumu.
Aliondolewa shtaka la kutekeleza udanganyifu wa bomu la uongo kwenye kambi yake ya jeshi.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alikiri kutoroka gereza la Wandsworth huko London mwezi Septemba 2023, kwa kujifucha chini ya lori la kupeleka chakula wakati wa kesi yake katika Mahakama ya Woolwich.
Jaji Bobbie Cheema-Grubb amesema katika Mahakama ya Woolwich Corwn kwamba Khalife anaweza kukabiliwa na "hukumu ya kifungo cha muda mrefu" atakapohukumiwa mapema mwaka ujao.
Vitendo vyake vilikiuka sheria kuhusu siri na sheria ya Ugaidi na hakuonesha kujuta wakati akipatikana na hatia.
Waendesha mashtaka wanasema Khalife aliwasiliana na mtu anayehusishwa na ujasusi wa Iran mara tu baada ya kujiunga na jeshi Septemba 2018, kabla ya kuwaambia MI6 kuwa alitaka kuwa jasusi wa nchi mbili.
Mahakama ilielezwa kuwa, alikusanya taarifa nyeti na kuzipeleka kwa watu wasiofaa na hilo lilileta hatari kubwa katika mikono isiyofaa.
Khalife aliwasiliana na mwanaume anayehusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kwenye Facebook.
Alijenga uhusiano na maafisa wa Iran – na wakati mmoja alitumiwa dola za Kimarekani 2,000 – na kutakiwa kuzichua katika mfuko katika bustani ya London kaskazini.
Wakati akihudumu jeshini, Khalife alikusanya majina ya wanajeshi 15 - wakiwemo baadhi kutoka katika kikosi maalumu.
Waendesha mashtaka wanaamini alituma orodha hiyo kwenda Iran kabla ya kufuta ushahidi wowote.
Alikanusha kutuma taarifa hizo na kudai kuwa taarifa alizotoa zilikuwa za uwongo. Lakini, inaonekana alituma hati mbili - moja kwenye kuhusu ndege zisizo na rubani na nyingine kuhusu "habari za kijasusi, Ufuatiliaji na taarifa za kijeshi."
Uingereza kujua taarifa nyingine nyeti ambazo Khalife alizipeleka - kwani jumbe nyingi alizotumia na waasiliani kwenye programu ya mawasiliano ya njia fiche ya Telegram zilifutwa.
Khalife alisakwa baada ya kutoroka gerezani , kabla ya kukamatwa saa 75 baadaye alipoonekana akiendesha baiskeli karibu na mto. Alifanya jaribio la kuwasiliana na Wairani kabla ya kupatikana, na kutuma ujumbe wa Telegram ambao ulisema: "Nasubiri."
Kutoroka kwa Khalife kutoka gereza la Wandsworth kulizua maswali mazito kuhusu usalama na wafanyakazi katika gereza hilo, na kupelekea wafungwa 40 kuhamishwa kwa muda kupisha uchunguzi wa tukio hilo ukifanyika .
Pia unaweza kusoma:
Wateule kadhaa wa baraza la mawaziri la Donald Trump na wateule wa timu yake ya White House wamekuwa wakilengwa kwa vitisho vya mabomu.
FBI inasema, inafahamu kuhusu "vitisho vya mabomu, kupitia simu za uwongo." Vitisho hivyo vilitolewa kwa takribani watu tisa waliochaguliwa na Trump kuongoza Idara za Ulinzi, Makazi, Kilimo na Kazi, pamoja na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, miongoni mwa wengine.
Polisi wanachunguza matukio hayo yaliyotokea Jumanne usiku na Jumatano.
Karoline Leavitt, msemaji wa timu ya mpito ya Trump, anasema walioteuliwa na Trump "walilengwa kwa vitisho vya vurugu, juu ya maisha yao na wale wanaoishi nao."
Si Leavitt wala FBI waliowatambua wahusika kwa majina hadi sasa.
Vyombo vya usalama vinasema, Trump, ambaye alinusurika majaribio mawili ya kuuawa wakati wa kampeni yake, hakuwa miongoni mwa waliopokea simu hizo za uongo.
Pia unaweza kusoma:
Aliyekuwa mbabe wa kivita wa Liberia na Seneta Prince Johnson amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72.
Chanzo kamili cha kifo chake bado hakijajulikana, lakini inasemekana alifariki katika kituo kimoja cha afya mapema leo.
Prince Johnson alikuwa muhimu katika vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1989 na 2003.
Mbabe huyo wa vita aliogopwa sana. Video ikimuonyesha akinywa bia huku wapiganaji wake wakimtesa Rais wa zamani Samuel Doe hadi kufa mnamo 1990, ilifichua kiwango cha ushiriki wake katika vita vya kwanza vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia.
Baada ya kuishi uhamishoni nchini Nigeria kwa miaka kadhaa, Johnson alirejea Liberia mwaka 2004 kufuata malengo yake ya kisiasa.
Baadaye alikua seneta mwenye ushawishi mkubwa katika kaunti yake ya Nimba iyenye kura nyingi, akichukua jukumu kubwa katika uchaguzi wa Rais aliye madarakani Joseph Boakai.
Wakati nchi bado inapambana na mauaji ya takriban watu 250,000 wakati wa vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe, kifo cha Johnson kinaweza kuibua mijadala kuhusu urithi alioacha nyuma.
Takriban watu 13 wameuawa katika maporomoko ya udongo mashariki mwa Uganda, lakini maafisa wanahofia kwamba idadi halisi ya waliokufa ni kubwa zaidi kwani takriban nyumba 40 zilisombwa na maji.
Maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa yaliathiri vijiji vingi katika wilaya ya Bulambuli, takriban kilomita 280 kutoka mji mkuu Kampala.
Shirika la Msalaba Mwekundu cha Uganda kimesema takriban watu 13 wamefariki, lakini AFP imeripoti kuwa idadi ya waliofariki inaweza kufikia watu 30.
Operesheni ya uokoaji inaendelea, Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda lilisema kwenye X.
Miili mingi iliyopatikana ni ya watoto, kulingana na gazeti la ndani la Daily Monitor. Makumi ya watu bado hawajulikani waliko.
Mvua kubwa imenyesha katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa siku chache zilizopita.
Siku ya Jumatano, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa onyo la maafa kupitia X.
Kingo za mito zimepasuka, shule na makanisa zimefurika na kuharibu madaraja, na kuwatenga watu wengi . Wanajeshi wametumwa kusaidia katika juhudi za utafutaji na uokoaji.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, ametishia kuyashambulia majengo ya kufanyia maamuzi ya Kyiv baada ya msururu wa mashambulizi makubwa jana usiku.
Amezungumza kwa mara ya kwanza akiwa katika mkutano wa kilele nchini Kazakhstan na kusema majengo ya kufanyia maamuzi yanaweza kulengwa kwa kombora jipya la balestiki ambalo Urusi ililitumia kushambulia mji wa Dnipro wa Ukraine wiki iliyopita.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi imeshambulia Ukraine kwa makombora 90 na ndege zisizo na rubani 100 usiku kucha kujibu mashambulizi ya Ukraine kwa kutumia silaha za Uingereza na Marekani wiki iliyopita.
"Tumefanya mashambulizi makubwa," amesema, na kuongeza kuwa vituo 17 vya kijeshi katika eneo la Ukraine vimepigwa.
Amesema Urusi imerusha makombora 100 na ndege zisizo na rubani 466 kwenda Ukraine katika siku mbili zilizopita.
Zaidi ya watu milioni moja nchini Ukraine hawana umeme baada ya Urusi kushambulia mitambo ya umeme ya nchi hiyo katika maeneo kadhaa.
Pia unaweza kusoma:
Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum anaonekana kupingana na madai ya Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump kwamba wawili hao wamefikia makubaliano ya kuzuia wahamiaji kwenda kwenye mpaka wa Marekani.
Baada ya mazungumzo ya simu siku ya Jumatano, Trump alichapisha taarifa katika mtandao wa kijamii, akisema: "Amekubali kusitisha uhamiaji kupitia Mexico, kuingia Marekani, na kufunga mpaka wetu wa Kusini."
Sheinbaum alijibu haraka kwamba msimamo wa Mexico sio kufunga mipaka, bali kushughulikia suala la uhamiaji huku ikiheshimu haki za binadamu.
Siku ya Jumatatu, Trump aliwashtua washirika wa kibiashara wa Marekani, kwamba atakapochukua madaraka Januari 2025, ataongeza ushuru wa 25% kwa bidhaa zinazotoka Mexico na Canada, na ushuru wa 10% kwa bidhaa kutoka China.
Alisema ushuru huo kwa Mexico na Canada utaondolewa mara tu uhamiaji haramu na usafirishaji wa dawa za kulevya kwenda Marekani utakapokoma.
Kuhusu China alisema ushuru huo utabaki, hadi itakapokabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya fentanyl.
Sheinbaum aliapa siku ya Jumatano kulipiza kisasi iwapo Marekani itaanzisha vita vya kibiashara.
Pia unaweza kusoma:
Makampuni makubwa ya utengenezaji wa taulo za kike (pedi) nchini China, yamelazimika kuomba radhi baada ya kushutumiwa kuuza taulo za kike ambazo ni fupi kuliko zilivyo tangazwa.
Hilo linakuja huku kukiwa na dhoruba ya hasira baada ya video za mitandao ya kijamii kuwaonyesha wanawake wa China wakipima urefu wa pedi, kuonyesha kwamba wamekosa kile kilichoelezwa kwenye vifungashio hivyo.
Katika mojawapo ya video, iliyochapishwa tarehe 3 Novemba, mtumiaji kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii la China, Xiaohongshu, alikagua pakiti tisa za pedi na kuzipima kwa utepe wa kupimia, na kuonyesha kuwa zote zina pungukiwa na urefu uliotajwa kwenye vifungashio vyao.
Ufichuzi huo wa hivi karibuni umezua ukosoaji mkubwa, na watumiaji wakiwashutumu watengeneza pedi kwa udanganyifu.
Uchunguzi wa zaidi ya pedi 20 tofauti uliofanywa na chombo cha habari cha China, The Paper uligundua kuwa karibu 90% ya bidhaa hizo ni fupi kwa angalau milimita 10 tofauti na inavyoelezwa kwenye vifungashio vyake.
Kufuatia wimbi la malalamiko, viongozi wa serikali wamesema wanarekebisha urefu pedi, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Pedi ndio bidhaa inayotumika zaidi kati ya bidhaa za usafi kwa wanawake nchini China, ambapo soko la bidhaa hizo lina thamani ya dola za kimarekani bilioni 13.
Pia unaweza kusoma:
Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti anaamini kuwa mshambuliaji wake Mfaransa Kylian Mbappe anahitaji "upendo na usaidizi" baada ya kutofunga bao kwa klabu yake ya Uhispania kwenye Ligi ya Mabingwa ya UEFA.
Mchezaji wa zamani wa Paris Saint-Germain Mbappe alitarajia uhamisho wake kwenda Real Madrid hatimaye ungemaliza kusubiri kwake kushinda Ligi ya Mabingwa lakini siku ya Jumatano ilikuwa mbali sana baada ya kichapo cha 2-0 kutoka kwa Liverpool kilichowaacha mabingwa hao watetezi katika hatari ya kuondolewa kutoka kwa mashindano makubwa ya klabu za Uropa katika hatua ya kwanza.
Iwapo Madrid watatoka mapema, Mbappe atautaza usiku wa Jumatano huko Anfield kuwa usiku wa mashaka ambapo alikosa mkwaju wa penalti ambao ungesawazisha bao la liverpool.
Ancelotti alisema baadaye nyota huyo alikuwa akipitia "wakati mgumu" miezi michache tu baada ya kujiunga na mabingwa hao mara 15 wa Uropa.
"Tunapaswa kumpa sapoti na upendo wetu na hivi karibuni atakuwa sawa," Ancelotti alisema alipokuwa akikabiliwa na maswali mengi kutoka kwa waandishi wa Uhispania kuhusu mchezo wa Mbappe.
Urusi imefanya mashambulizi makubwa dhidi ya miundombinu ya nishati ya umeme ya Ukraine, Waziri wa nishati wa nchi hiyo amesema, huku milipuko ikiripotiwa katika miji kadhaa.
Herman Halushchenko amesema kwenye ukurasa wa Facebook kwamba mashambulizi dhidi ya vituo vya nishati ya umeme "yamefanyika kote Ukraine na kukatika kwa umeme, na kuwataka watu kujificha.”
Mapema siku ya Alhamisi, jeshi la anga la Ukraine lilitoa onyo juu la mashambulizi ya anga ya nchi nzima "kutokana na tishio la makombora."
Jeshi la anga lilitoa tahadhari juu ya makombora na ndege zisizo na rubani zinazoelekea katika mikoa ya nchini humo, ikiwa ni pamoja na Kyiv, Rivne, Vinnytsia, Kropyvnytskyi, Balta, na Mykolaiv.
Meya wa Kharkiv, Igor Terekhov, amesema kulikuwa na makombora katika eneo la kiraia katika jiji hilo, na Meya wa Lutsk, Ihor Polishchuk, amesema milipuko mingi imesikika na umeme umekatika katika sehemu ya jiji.
Chombo cha habari cha Zerkalo Tyzhnya kiliripoti kwamba milipuko imesikika katika jiji la Odesa, huku gavana wa mkoa Oleg Kiper akiwataka wakazi kusalia mahali salama.
Mamlaka katika maeneo ya Sumy na Volyn pia wameripoti mashambulizi.
Mashambulizi ya Urusi yameongezeka siku ya hivi karibuni, imefanya mashambulizi ya anga zaidi ya 1,500 nchini Ukraine, na kupiga karibu nusu ya mikoa ya nchi hiyo katika kipindi cha siku chache zilizopita, kulingana na serikali ya Ukraine.
Unaweza kusoma;
Michael Sullivan alitumikia zaidi ya miaka 27 katika gereza la Massachusetts kwa mauaji ambayo alisisitiza kwa miaka kwamba hakufanya. Aliachiliwa mnamo 2013 baada ya jaribio jipya na teknolojia mpya ya DNA kuthibitisha kuwa hana hatia.
Mapema mwezi huu, Sullivan alitunukiwa $13m (£10m) kutoka kwa jimbo hilo, ingawa kanuni za Massachusetts hutoa tuzo ya $1m. kwa kuhukumiwa kimakosa
Sullivan, ambaye alifiwa na mama yake na kaka zake wanne alipokuwa jela, anasema pesa hizo "haziwezi kumaliza miaka" aliyopoteza.
Sean “Diddy” Combs amenyimwa dhamana kwa mara ya tatu na hakimu katika jiji la New York.
Majaji wawili hapo awali walikataa kuachiliwa kwa Bw.Combs kutoka kizuizini, haswa kwa sababu ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuchezea mashahidi, wakiona kuwa ni hatari kubwa ikiwa ataachiliwa kabla ya kesi, ambayo imepangwa Mei 2025.
Bwana Combs anazuiliwa katika Kituo cha Kizuizi cha Metropolitan huko Brooklyn, New York, akishtakiwa kwa kula njama, biashara ya ngono na usafirishaji kwa shughli za ukahaba.
Amedai kutokuwa na hatia na pia amekanusha zaidi ya dazeni mbili za tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia zilizowasilishwa katika msururu wa kesi za madai.
Hakimu alitoa ushahidi katika kesi hiyo unaoonesha madai ya Bw Combs kuingilia ushahidi, ukiukaji wake wa kanuni za gereza akiwa gerezani na madai kwamba aliendesha "biashara ya uhalifu" ikiwa ni pamoja na kazi ya kulazimishwa na utekaji nyara.
Jaji wa Wilaya ya Marekani Arun Subramanian alihitimisha mahakama haiwezi kumwamini Bw Combs ikiwa angeachiliwa kwa dhamana.
"Mahakama inaona kwamba serikali imeonesha kwa ushahidi wa wazi na wa kuridhisha kwamba hakuna masharti au mchanganyiko wa masharti yatahakikisha usalama wa jamii," jaji aliandika katika uamuzi wa Jumatano.
Waendesha mashtaka walikuwa wamepinga kumpa Bw Combs dhamana, wakitaja utovu wa nidhamu wake akiwa kizuizini.
Katika kesi iliyowasilishwa mahakamani hivi karibuni, waendesha mashtaka walimshutumu mwanamuziki huyo wa rap kwa kutumia vibaya mawasiliano ya jela kushawishi mashahidi katika kesi yake.
Lakini mawakili wa utetezi wa Bw Combs walisema anapaswa kuachiliwa kwa hivyo ana muda wa kutosha kujiandaa kwa kesi yake mwaka ujao.
Unaweza kusoma;
Wamarekani watatu waliokamatwa nchini China waliachiliwa baada ya utawala wa Biden kufanya mazungumzo ya kubadilishana wafungwa.
Mark Swidan, Kai Li, na John Leung wako njiani kurejea Marekani, msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa (NSC) alisema katika taarifa Jumatano.
“Hivi karibuni watarejea na kuunganishwa na familia zao kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi,” ilisema taarifa hiyo.
Mabadilishano hayo yaliripotiwa kuwa yamefanyika kwa miezi kadhaa, na ni pamoja na kuachiliwa kwa raia mmoja wa China chini ya kizuizi cha Marekani.
Rais Biden alizungumzia suala la Wamarekani waliozuiliwa kimakosa nchini China moja kwa moja na Rais Xi Jinping mapema mwezi huu wakati wawili hao walipokutana wakati wa mkutano wa Apec nchini Peru, kulingana na afisa wa Marekani anayefahamu mazungumzo hayo.
Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan pia aliwataka warejee wakati wa ziara yake nchini China mnamo Agosti.
"Shukrani kwa juhudi za Utawala huu na diplomasia na PRC, Wamarekani wote waliozuiliwa kimakosa katika PRC wako nyumbani," msemaji wa NSC alisema.
Bw.Swidan, 48, alikuwa amezuiliwa tangu 2012 na alikuwa anakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya kukutwa na hatia ya ulanguzi wa mihadarati.
Swidan alikanusha mashtaka na Wizara ya Mambo ya Nje ilimtaja kuwa alizuiliwa kimakosa, na hapo awali kuibua wasiwasi kuhusu afya yake.
Mark Li, 60, alikuwa akishikiliwa nchini China tangu Septemba 2016 kwa kile wanaharakati wanasema ni mashtaka ya uwongo ya ujasusi.
John Leung, 78, ameongoza makundi kadhaa yanayoIunga mkono Beijing nchini Marekani. Alikamatwa mwaka wa 2021 na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ujasusi miaka miwili baadaye.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, maafisa wengi wa Marekani walisema walijadili kumwachilia raia wa China Xu Yanjun, 42, ambaye alipatikana na hatia nchini Marekani kwa makosa ya ujasusi miaka miwili iliyopita na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Xu alikuwa afisa wa kwanza wa ujasusi wa serikali ya China kuwahi kurejeshwa Marekani ili kujibu mashtaka, Wizara ya Sheria ilisema.
Kufikia Jumatano asubuhi, Xu aliorodheshwa katika mfumo wa Ofisi ya Magereza kama "hayuko chini ya ulinzi wa BOP". Mkataba huo unaashiria ushindi wa kidiplomasia kwa Biden katika miezi ya mwisho ya urais wake.
Hatua hii inafuatia kuachiliwa kwa Mmarekani mwingine anayeelezwa kuwa amezuiliwa kimakosa: David Lin, mchungaji ambaye alikuwa amefungwa nchini China kutoka 2006 hadi kuachiliwa kwake mnamo Septemba.
Katika miaka yake minne katika Ikulu ya White House, Biden alisimamia kuachiliwa kwa Wamarekani zaidi ya 70, wakiwemo kutoka Urusi, Venezuela na Iran.
Unaweza kusoma;
Israel itakata rufaa kupinga hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant.
Majaji wiki iliyopita walitoa vibali kwa watu hao wawili pamoja na kamanda wa kijeshi wa Hamas Mohammed Deif, wakisema kuna sababu za kuridhisha za kuamini kuwa watu hao watatu waliwajibika kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Serikali ya Israel, pamoja na Netanyahu na Gallant, walikanusha vikali shutuma hizo.
Siku ya Jumatano, ofisi ya waziri mkuu ilisema ilikuwa imefahamisha ICC kuhusu "nia yake ya kukata rufaa mahakamani pamoja na kutaka kuzuia utekelezaji wa hati za kukamatwa".
Ofisi ya Netanyahu pia ilisema Seneta wa Marekani Lindsey Graham amemjulisha Netanyahu "juhudi anazoendeleza katika Bunge la Marekani dhidi ya ICC na nchi ambazo zimeshirikiana nayo".
Rais wa Marekani Joe Biden alitaja hati hizo kuwa za "chukizo" wiki iliyopita. "Chochote ICC inaweza kumaanisha, hakuna usawa kati ya Israel na Hamas. Daima tutasimama na Israel dhidi ya vitisho kwa usalama wake," alisema.
Nchi wanachama wa ICC, ambazo hazijumuishi Israel au Marekani , zinalazimika kuchukua hatua katika kumzuia mshtakiwa anayesakwa iwapo atapatikana kuwa katika mamlaka yao.
Baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zimedokeza kuwa zitaheshimu uamuzi wa ICC, huku nyingine zikikataa kusema zitafanya nini iwapo Netanyahu ataingia katika eneo lao.
Serikali ya Uingereza imedokeza kuwa Netanyahu atakamatwa iwapo atasafiri kwenda Uingereza.
Unaweza kusoma;