Kiongozi wa upinzani Msumbiji ataka maandamo yaendelee kwa miezi kadhaa

Venâncio Mondlane amekuwa akitoa wito kwa wafuasi wake kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Oktoba, ambapo alishika nafasi ya pili, nyuma ya mgombea kutoka chama tawala cha Frelimo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho.

  2. Trump amchagua mkwe mwingine kuwa mshauri

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Boulos alikuwa na jukumu kubwa lisilo rasmi katika kampeni ya Trump, akimsaidia kuwashawishi wapiga kura Waarabu na Waislamu

    Donald Trump amemteuwa baba mkwe wa bintiye Tiffany, Massad Boulos, kuwa mshauri wa masuala ya Kiarabu na Mashariki ya Kati.

    Mfanyabiashara huyo mwenye uraia wa Marekani na Lebanon ni mkwe wa pili kupewa nafasi katika utawala unaokuja, baada ya Trump kumchagua Charles Kushner, baba mkwe wa binti yake Ivanka, kuhudumu kama balozi nchini Ufaransa.

    Boulos alikuwa na jukumu lisilo rasmi katika kampeni ya Trump, akimsaidia kuwashawishi wapiga kura Waarabu na Waislamu – baada ya wengi wao wakichukizwa na utawala wa Biden kuhusu vita vya Israel na Gaza.

    Akitangaza uteuzi huo kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema Boulos "ni muhimu katika kujenga miungano mipya na jumuiya ya Waarabu Marekani."

    Kwenye kampeni, Boulos aliwaomba wapiga kura Waarabu na Waislamu kwa kuwaahidi kwamba Trump atarejesha amani Mashariki ya Kati.

    Mzaliwa wa Lebanon, anajulikana kuwa na uhusiano na vikundi kadhaa vya kisiasa katika nchi yake ya kuzaliwa.

    Boulos tayari amekuwa kama kiungo kisicho rasmi kati ya Trump na viongozi wa Mashariki ya Kati, gazeti la New York Times liliripoti.

    Pia anaripotiwa kukutana na Mahmoud Abbas, kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, kando ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba.

    Katika mkutano huo, Boulos aliripotiwa kuwasilisha nia ya Trump ya kumaliza vita vya Israel-Gaza na mizozo mingine kote ulimwenguni.

    Boulos alihamia Texas akiwa kijana, kulingana na wasifu wake katika tovuti ya New Arabu, alikwenda Chuo Kikuu cha Houston na kupata shahada ya sheria.

    Amefanya kazi katika biashara ya familia yake - kampuni ya mabilioni ya dola yenye makao yake makuu Nigeria ambayo inajishughulisha na usambazaji wa magari na vifaa kote Afrika Magharibi.

    Tofauti na uteuzi mwingine wa Trump, jukumu la ushauri la Boulos halihitaji kuthibitishwa na Seneti ya Marekani.

  3. Kiongozi wa upinzani Msumbiji ataka maandamo yaendelee kwa miezi mitatu

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Venâncio Mondlane, ambaye kwa sasa yuko mafichoni, anawasiliana na wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii

    Maandamano ambayo yamesababisha makabiliano ya wiki kadhaa na vikosi vya usalama vya Msumbiji yanapaswa kuendelea kwa "miezi miwili hadi mitatu," kiongozi wa upinzani nchini humo ameiambia BBC.

    Venâncio Mondlane amekuwa akitoa wito kwa wafuasi wake kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Oktoba, ambapo alishika nafasi ya pili, nyuma ya mgombea kutoka chama tawala cha Frelimo.

    Maandamano hayo ya wiki nzima yamesababisha makabiliano makali na polisi na watu wapatao 67 wameuawa, shirika la ufuatiliaji la Plataforma Decide limesema.

    Mondlane, ambaye sasa amejificha, aliiambia BBC anafikiri shinikizo kutoka maandamano hayo linaweza kuilazimisha Frelimo kuingia katika mazungumzo.

    Amesema hawezi kukubali matokeo ya uchaguzi, ambapo mgombea wa Frelimo, Daniel Chapo alishinda kwa asilimia 71 ya kura.

    Mondlane, mchungaji wa kanisa, aliyesimama kama mgombea huru baada ya kujitenga na chama kikuu cha upinzani cha Renamo, alipata 20% tu ya kura.

    Tume ya uchaguzi ilikanusha madai ya Mondlane kwamba kura ziliibiwa na kuipendelea Frelimo, ambacho kiko mamlakani tangu uhuru miaka 49 iliyopita.

    Lakini waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wamesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari, wakiashiria namba kubadilishwa na makosa mengine wakati wa mchakato wa kuhesabu kura.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Ubelgiji yatakiwa kuwalipa fidia waliotekwa wakiwa watoto DR Congo wakati wa ukoloni

    dfc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Simone Vandenbroeck (kulia) na La Mujinga Tavarese ni wawili kati ya wanawake watano ambao wameshinda kesi yao ya fidia.

    Mahakama ya Ubelgiji imeiamuru serikali ya nchi hiyo kuwalipa fidia wanawake watano waliochukuliwa kwa lazima kutoka katika familia zao katika enzi ya ukoloni wa Ubelgiji nchini DR Congo.

    Wanawake hao, ambao sasa wana umri wa miaka 70, walichukuliwa kutoka kwa mama zao walipokuwa watoto wadogo na kupelekwa katika vituo vya watoto yatima chini ya mpango wa serikali.

    Mahakama imesema serikali ilikuwa na "mpango maalumu wa kuwatafuta na kuwateka nyara watoto waliozaliwa na mama mweusi na baba mzungu."

    Siku ya Jumatatu majaji walisema, “ulikuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu” na utekaji nyara huo ni "kitendo cha kinyama cha mateso."

    Serikali ya Ubelgiji mwaka 2019 iliomba radhi rasmi kwa waathiriwa 20,000, waliotenganishwa kwa nguvu na familia zao nchini DR Congo, pamoja na Burundi na Rwanda.

    DR Congo ilitawaliwa na Ubelgiji kama koloni kutoka 1908 hadi 1960.

    Baba wengi wa kizungu walikataa kuwatambua watoto wao wa rangi mchanganyiko au kukiri kuwa ni watoto wao, na watoto hao pia hawakupokea utaifa wa Ubelgiji moja kwa moja.

    Kwa hivyo walichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa katika vituo vya watoto yatima vinavyosimamiwa na Kanisa Katoliki, ambapo mara nyingi walipitia unyanyasaji.

    2017, kanisa katoliki liliomba msamaha kwa waathiriwa. Na 2019, serikali ya Ubelgiji iliomba msamaha kwa kuhusika kwake.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Idadi ya waomba hifadhi Uingereza yaongezeka

    xc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Zaidi ya watu 30,000 wamevuka lango la baharini la kuingia Uingereza kwa boti ndogo mwaka 2024, kwa mujibu wa takwimu za serikali.

    Kwa upande mwingine, maombi jumla ya hifadhi kwa Uingereza, yameongezeka hadi watu 99,700, katika muda wa miezi 12 hadi Septemba.

    Kufikia 27 Novemba, watu 33,562 walikuwa wamevuka lango la baharini kwa boti ndogo ndani ya mwaka 2024.

    Idadi hiyo ni kubwa kuliko ya mwaka 2023, ambayo ilikuwa ni watu 29,437 katika mwaka mzima.

    Lakini, takwimu za juu zaidi zilizorekodiwa ni za 2022, watu 45,755 walivuka na kuingia Uingereza kupitia baharini.

    Tangu 2018, takwimu zilipoanza kurekodiwa kwa mara ya kwanza, zaidi ya watu 147,800 wamefika kwa boti ndogo kuingia Uingereza.

    Waziri Mkuu Sir Keir Starmer ameahidi kutumia mbinu za kukabiliana na ugaidi kukomesha magenge yanayosafirisha watu.

    Amesema kamandi mpya ya Usalama Mipakani ya Uingereza (BSC) itawatafuta washukiwa wa ulanguzi wa binadamu na kufunga akaunti zao za benki.

    Katika mwaka huu hadi Septemba 2024, karibu Waafghani 5,000 waliingia Uingereza. Wairani walikuwa kundi la pili kwa ukubwa, likifuatiwa na watu kutoka Syria, Vietnam na Eritrea.

    Imerekodiwa kuwa zaidi ya 80% ni wanaume. Karibu 40% ni kati ya miaka 25 na 39.

    Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), hufuatilia idadi ya watu wanaofariki wakivuka bahari hiyo, linasema zaidi ya watu 50 wamekufa mwaka 2024, idadi kubwa zaidi kwa mwaka wowote tangu ianze kurekodi takwimu mwaka 2014.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mwanamuziki wa Iran aachiliwa huru baada ya hukumu ya kifo kubatilishwa

    dcx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wanaharakati wanasema Salehi hakupaswa kufungwa

    Mwanamuziki wa kufoka wa Iran ambaye alihukumiwa kifo kwa kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali ameachiliwa kutoka jela baada ya miaka miwili.

    Toomaj Salehi alikamatwa Oktoba 2022 baada ya kuunga mkono hadharani maandamano yaliyozuka kote nchini Iran kufuatia kifo cha Mahsa Amini akiwa mikononi mwa polisi.

    Hukumu yake ya kifo ilibatilishwa mwezi Juni na akaachiliwa kutoka gerezani siku ya Jumapili "baada ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kwa propaganda dhidi ya serikali, shirika la habari la Iran linaloendeshwa na mahakama la Mizan liliripoti.

    Salehi, 34, aliwakosoa viongozi wa Iran katika muziki wake na alikuwa tayari amepigwa marufuku kutumbuiza kwenye tamasha kabla ya kukamatwa kwake.

    Alihukumiwa kifungo cha miaka sita na miezi mitatu jela mwezi Julai 2023, baada ya kukwepa hukumu ya kifo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu.

    Salehi aliachiliwa muda mfupi kwa dhamana kabla ya kukamatwa tena siku chache baadaye kwa tuhuma za kuchapisha "madai ya uwongo bila ushahidi." Baada ya kuchapisha video, akidai aliteswa na maafisa wa upelelezi.

    Alihukumiwa kifo Aprili 2024 kwa kosa la kusababisha uharibifu, ingawa hukumu hii ilibatilishwa baadaye. Pia rapa huyo alishtakiwa kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kueneza uwongo kwenye mitandao, kuvuruga utulivu wa umma na propaganda dhidi ya serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  7. BBC yashinikizwa kusitisha kipindi cha mapishi baada ya tuhuma za unyanyasaji wa kingono

    fc

    Chanzo cha picha, BBC/Shine TV

    Maelezo ya picha, Gregg Wallace, mtangazaji wa kipindi cha mapishi cha MasterChef

    Mbunge mmoja nchini Uingereza, amelitaka Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kufikiria kusitisha kipindi cha mashindano ya mapishi cha MasterChef, huku Gregg Wallace akichunguzwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa wa kingono.

    Rupa Huq, mbunge wa chama cha Labour na mjumbe wa Kamati ya Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo, amesema kuna pendekezo la kutaka kipindi hicho kusitishwa.

    Mtangazaji wa MasterChef, Gregg Wallace amekanusha tuhuma za unyanyasaji wa kingono, baada ya watu 13 kujitokeza wiki iliyopita wakimtuhumu kutoka kauli zisizofaa.

    Baada ya uchunguzi wa BBC News juu ya madai ya kauli zisizofaa za kingono na tabia zisizofaa dhidi yake, Wallace alijiondoa wiki iliyopita kuendesha kipindi hicho lakini tayari kuna vipindi vimesharikodiwa.

    Uchunguzi huo ni kutoka kwa watu 13 walio na umri tofauti, ambao walifanya kazi katika vipindi vitano tofauti.

    Uchunguzi wa BBC News pia uligundua kuwa Wallace alionywa na BBC baada ya malalamiko yaliyotolewa kuhusu yeye mwaka 2018, wakati akiendesha kipindi cha Impossible Celebrities.

  8. Watu watatu wafariki baada ya kula kasa

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kasa wa baharini huliwa kama kitoweo katika baadhi ya jamii nchini Ufilipino

    Watu watatu wamefariki na wengine 32 wamelazwa hospitalini nchini Ufilipino baada ya kula kasa wa baharini.

    Maafisa wanasema, makumi ya watu kutoka jamii ya Teduray waliripoti kuhara, kutapika na tumbo kuuma tangu kula kitoweo hicho wiki iliyopita katika mji wa pwani wa jimbo la Maguindanao del Norte.

    Ingawa ni kinyume cha sheria kuwinda au kula kasa wa baharini chini ya sheria za ulinzi wa mazingira za Ufilipino, viumbe hao bado wanaliwa katika baadhi ya jamii.

    Lakini kasa wa baharini ambao hula mwani mchafu, wanaweza kuwa na sumu wanapopikwa na kuliwa.

    Afisa wa eneo hilo Irene Dillo, aliiambia BBC, baadhi ya mbwa, paka na kuku waliolishwa kasa huyo pia walikufa. Aliongeza kuwa mamlaka inachunguza chanzo cha vifo hivyo.

    Wengi wa waliolazwa hospitalini tayari wameruhusiwa, vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti, huku watatu waliofariki wakizikwa mara moja - kulingana na mila za wenyeji.

    Mwaka wa 2013, watu 68 katika Mkoa wa Samar Mashariki mwa Ufilipino waliugua - na wanne kati yao walikufa - baada ya kula kasa wa baharini.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Watu 56 wamefariki katika mkanyagano kwenye uwanja wa mpira

    .

    Takribani watu 56 wamefariki katika mkanyagano kwenye mechi ya mpira wa miguu katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Guinea, Nzérékoré, serikali inasema.

    Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa vurugu zilitokea baada ya uamuzi wa refa, wa kuwatoa nje wachezaji wawili wa timu ngeni, Labé, na kutoa mkwaju wa penalti uliozua utata.

    Waziri Mkuu Mamadou Oury Bah amesema mkanyagano katika mechi hiyo ulisababisha watu 56 kupoteza maisha siku ya Jumapili na kutoa wito wa utulivu.

    Daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kuna miili kadhaa katika hospitali ya eneo hilo, na chumba cha kuhifadhia maiti kilikuwa kimejaa.

    Vyombo vya habari vya ndani vilisema polisi walitumia gesi ya kutoa machozi baada ya wafuasi wa timu iliyowatembelea, Labé, kurusha mawe kuelekea uwanjani kwa hasira dhidi ya mwamuzi.

    Hadi sasa hakuna takwimu rasmi za majeruhi ambazo zimetolewa.

    "Yote yalianza na uamuzi uliopingwa ulitolewa na mwamuzi. Kisha mashabiki wakavamia uwanja," shahidi mmoja aliambia AFP.

    Video na picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonekana kuonyesha matukio ya fujo nje ya uwanja, huku umati mkubwa wa watu ukijaribu kupanda juu ya kuta na miili mingi ikionekana chini.

    BBC haijaweza kuthibitisha video hizi kwa uhuru.

    Mamlaka za eneo zinajitahidi "kurudisha utulivu", Waziri Mkuu Bah alisema katika taarifa, na kuongeza kuwa hospitali zinawasaidia waliojeruhiwa.

  10. Uganda: Martha Karua anaongoza timu ya mawakili wanaomtetea Kizza Besigye

    .

    Chanzo cha picha, Martha Karua/facebook

    Waziri wa zamani wa sheria nchini Kenya Martha Karua, yuko nchini Uganda kuongoza timu ya mawakili wanaomtetea mwanaharakati wa kisiasa wa upinzani Dkt. Kizza Besigye na mshirika wake wa kisiasa, Hajj Obeid Lutale, katika mahakama ya kijeshi mjini Kampala hii leo Jumatatu.

    Besigye na Lutale walitekwa nyara na idara za usalama za Uganda mnamo Novemba 16 jijini Nairobi, ambapo walikuwa wamesafiri kuhudhuria uzinduzi wa kitabu na Martha Karua.

    Siku nne baadaye, wawili hao walifikishwa katika mahakama kuu ya kijeshi mjini Kampala, ambapo walishtakiwa kwa makosa manne yanayohusiana na usalama, kumiliki bastola mbili na risasi nane kinyume cha sheria.

    Wiki iliyopita siku ya Jumatatu, wakili kiongozi wa Besigye na Meya wa Kampala, Erias Lukwago, alitangaza kwamba Karua atachukua nafasi yake kama wakili mkuu.

    Na hapo jana Jumapili, Karua aliwasili Kampala kwa ajili ya kesi hiyo.

  11. Tebogo na Hassan waongoza katika Tuzo za Riadha za Dunia

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mabingwa wa Olimpiki Letsile Tebogo na Sifan Hassan walitawazwa kuwa mwanariadha bora wa kiume na wa kike katika Tuzo za Dunia za Riadha mjini Monaco.

    Tebogo, ambaye pia alitajwa kuwa mwanariadha bora wa mwaka wa mbio za kiume, alikua bingwa wa kwanza wa Olimpiki wa Botswana mjini Paris aliposhinda mbio za mita 200 katika muda wa sekunde 19.46.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 pia alisaidia kuweka rekodi mpya ya Afrika alipotwaa medali ya fedha katika mbio za kupokezana vijiti za mita 4x400 za wanaume.

    "Inafurahisha kujua kwamba mashabiki wako kila wakati kwa ajili yetu wanariadha," alisema Tebogo. "Ulikuwa mwaka mzuri sana. Hii ina maana kubwa."

    Hassan wa Uholanzi alishinda medali ya shaba katika mbio za mita 5,000 na 10,000 mjini Paris kabla ya kujinyakulia dhahabu katika mbio za marathon za wanawake na kuwa mwanariadha wa kwanza katika kipindi cha miaka 72 kushinda medali katika mashindano yote matatu kwenye mbio hizo.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 pia alitajwa kuwa mwanariadha bora wa mwaka nje ya uwanja, huku Tamirat Tola wa Ethopia, ambaye alishinda medali ya dhahabu ya mbio za marathon za wanaume huko Paris, akishinda tuzo ya mwanamume.

    "Sikuwahi kufikiria kuwa nitashinda hii," alisema Hassan. "Mwaka huu ulikuwa na ushindani mkubwa."

    Pia unaweza kusoma:

  12. 'Sikutarajia hilo Anfield' - Guardiola azungumzia nyimbo za 'kufutwa kazi asubuhi'

    .

    Chanzo cha picha, Rex Features

    Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amezungumzia kejeli za mashabiki wa Liverpool licha ya kushindwa na Manchester City kwenye uwanja wa Anfield.

    Mashabiki wa Liverpool walimlenga Guardiola huku wakiimba 'unafutwa kazi asubuhi' wakati wakielekea mwishoni mwa mechi hiyo.

    Nyimbo hizo zilianza wakati Liverpool walikuwa wanakaribia kupata ushindi ambao ungewafanya wafikishe pointi 11 mbele ya wapinzani wao Manchester City katika dakika ya 89.

    Nyimbo hizo zilikuwa zinaelekezwa kwa Pep Guardiola, ambaye ameongoza katika upatikanaji wa mataji sita ya Ligi ya Primia tangu aanze kuinoa City mwaka 2016.

    Kocha huyo wa City akiwa amesimama kwenye eneo lake, alijibu kwa tabasamu kisha akatoa mikono mfukoni na kuinua mkono mmoja juu huku mkono mwingine ukionyesha kidole kimoja kuashiria idadi ya mataji ambayo City imeshinda chini yake.

    "Sikutarajia hilo Anfield," Guardiola aliiambia Sky Sports baadaye alipoulizwa kuhusu nyimbo za "kufutwa kazi asubuhi".

    "Sikutarajia hilo kutoka kwa mashabiki wa Liverpool lakini ni sawa, ni sehemu ya mchezo, na ninaelewa kabisa.

    "Tumekuwa tukipambana pamoja. Na ninawaheshima."

    City, ambao wanamaliza wikendi wakiwa katika nafasi ya tano kwenye jedwali chini ya Liverpool, Arsenal, Chelsea na Brighton, wamepoteza mechi zao nne za mwisho za ligi kuu kwa mara ya kwanza tangu Agosti 2008.

    Isitoshe, hawajashinda katika mechi saba kwenye mechi zote – kitu ambacho hakijaonekana chini ya Guardiola ambaye ameleta furaha na mafanikio makubwa kwa City katika miaka minane iliyopita.

    "Viwanja vyote vinataka nifutwe kazi, ilianza Brighton [tarehe 9 Novemba]," aliongeza kocha huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye alitia saini mkataba mpya wa miaka miwili mwezi uliopita.

    "Labda wako sawa na matokeo ambayo tumekuwa tukiyapata."

    Pia unaweza kusoma:

  13. Joe Biden atoa msamaha usio na masharti kwa mwanawe Hunter

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Joe Biden ametoa msamaha rasmi kwa mtoto wake Hunter, ambaye alikuwa anakabiliwa na kesi mbili za uhalifu, licha ya kwamba awali, alikuwa ameondoa uwezekano wa hilo.

    Katika taarifa yake, alisema mwanawe "amelengwa" na kuzitaja kesi zake kuwa "ukosefu wa haki".

    Hunter Biden alikiri mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru mapema Septemba, na alipatikana na hatia ya kuwa mtumiaji haramu wa dawa za kulevya na kumiliki bunduki mnamo mwezi Juni - na kuwa mtoto wa kwanza wa rais aliyeko madarakani kuhukumiwa kwa uhalifu.

    Akijibu msamaha huo, Rais Mteule Donald Trump alisema: "Je, Msamaha uliotolewa na Joe kwa Hunter unajumuisha waliokamatwa [Januari 6], ambao sasa wamefungwa kwa miaka mingi? Unyanyasaji na ukosefu wa Haki!"

    Trump alikuwa akimaanisha wafuasi wake waliovamia Bunge la Marekani tarehe 6 Januari 2021 kwa nia ya kubatilisha kushindwa kwa Trump katika uchaguzi wa 2020.

    Msamaha kamili na usio na masharti wa Joe Biden kwa mtoto wake unawadia baada ya rais kusema hapo awali kuwa hatatoa msamaha kwa mtoto wake.

    Lakini Jumapili jioni, Rais Biden alisema ingawa anaamini katika mfumo wa haki, "siasa zimeingia katika mchakato huu na kusababisha kukosekana kwa haki".

    Soma zaidi:

  14. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT, Abdul Omar Nondo apatikana

    Abdul Nondo

    Chanzo cha picha, Abdul Nondo/Instagram

    Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, Abdul Nondo amepatikana usiku wa jana jumapili baada ya kutupwa jirani na makao makuu ya Chama hicho, yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam akiwa na majeraha.

    BBC imezungumza na Shangwe Ayo Naibu mwenezi taifa wa chama cha ACT Wazalendo, kutaka kufahamu taarifa za kupatikana kwa Abdul Nondo.

    Bi. Ayo amesema majira ya saa tano usiku jana walipatiwa taarifa kutoka kwa walinzi wa Chama katika makao makuu ya ofisi za ACT zilizopo eneo la Magomeni.

    ''Tuliambiwa Nondo ameletwa akiwa mahututi, amepigwa sana na hawezi kuongea. Kwa taarifa za awali viongozi wetu wa chama walifanya jitihada za kuhakikisha anakimbizwa hospitali, waliofanikiwa kumuona walimuhoji kidogo, akasema alitupwa maeneo aliyohisi ni Coco beach, akajivuta mpaka barabarani ambapo wasamaria wema walimuona'', Alisema.

    Amesema kwa mujibu wa madaktari hakuna maeneo ambayo amevunjika, ingawa ana majeraha makubwa na kuwa madaktari bingwa watakapomwangalia watatoa taarifa nini hasa kinachomsibu mwilini.

    Akizungumzia mazingira ya kutekwa kwake Bi. Ayo amesema; ''Mazingira aliyotekwa Abdul Nondo yalikuwa ni stendi ya Magufuli, kwenye purukushani za kumteka Nondo pingu ilidondoka, kwa hivyo wanaomiliki hivi vifaa kama pingu ni wazi ni jeshi la polisi, lakini tulifahamishwa kwamba yuko katika kituo cha polisi gogoni kibamba, viongozi wetu walilikuta lile gari ambalo shuhuda alilielezea ndilo lililomchukua Abdul Nondo''.

    Soma zaidi:

  15. Trump ayaonya mataifa ya Brics dhidi ya kutafuta mbadala wa dola

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais mteule wa Marekani Donald Trump ametishia kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa muungano wa mataifa tisa wa BRICS iwapo yataunda sarafu pinzani dhidi ya dola ya Marekani.

    "Wazo kwamba Nchi za BRICS zinajaribu kujiepusha na Dola huku sisi tukiwa tunatazama imefika MWISHO," Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii Jumamosi.

    Nchi zenye nguvu kubwa duniani China na Russia ni sehemu ya muungano wa Brics, pamoja na Brazil, India, Afrika Kusini, Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Wakati wa uchaguzi wa Marekani, Trump alifanya kampeni ya kutekeleza ushuru wa wigo mpana.

    Ametoa vitisho vya kutozwa ushuru mkubwa katika siku za hivi karibuni.

    Ujumbe huu kutoka kwa Trump, ambaye atachukua madaraka rasmi mwaka ujao tarehe 20 Januari, ulilenga Brics, muungano wa mataifa mengi yanayoinukia kiuchumi.

    Wanasiasa wakuu nchini Brazil na Urusi wamependekeza kuunda sarafu ya Brics ili kupunguza utawala wa dola ya Marekani katika biashara ya kimataifa.

    Lakini kutokubaliana ndani ya muungano huo kumepunguza maendeleo yoyote.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo ikiwa ni tarehe 02/12/2024