Mashindano ya Riadha ya Dunia: Omanyala mwenye uchu wa dhahabu anayolenga kuishindia Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa wa Michezo ya Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala amelinganisha "ushindani" wa mbio za mita 100 na ndondi huku akilenga dhahabu kwenye Mashindano ya Riadha ya Dunia mwezi huu huko Budapest.
Mkenya huyo ataingia katika mji mkuu wa Hungary baada ya kujipatia ushindi wake wa kwanza wa mbio a Diamond League mwezi Julai.
Omanyala, 27, aliibuka mshindi katika mashindano ya Monaco mbele ya Letsile Tebogo wa Botswana, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 100 miongoni mwa vijjana, huku Wajamaika Ackeem Blake na Yohan Blake wakiwa wa tatu na wa nne mtawalia.
Sasa mwanariadha huyo wa Afrika Mashariki anasema yuko tayari kutinga kwenye jukwaa la kimataifa katika riadha anayosema inavutia watu wengi zaidi kutokana na kufanana kwake na ndondi.
"Mita 100 ni maarufu zaidi kwa sababu ya kelele zake - naiona kama mechi ya ndondi," aliiambia BBC Sport Africa.
"Katika mechi ya ndondi, kuna mbwembwe za kila aina ikiwemo vyombo vingi vya habari na (mbio za mita 100) ni kama sekunde tisa za ushindani.
"Kwa wanariadha wa 100m, naweza kusema ni wa hali ya juu sana - wenye bidii kupita kiasi - ndio maana tunaufanya mchezo kuwa wa kuvutia."

Afrika iko tayari kunguruma
Akiwa mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika, baada ya kukimbia sekunde 9.77 mwaka wa 2021, Omanyala alitwaa dhahabu kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2022 mjini Birmingham alipokimbia sekunde 10.02.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya kuweka rekodi bora zaidi ya mita 100 mwaka huu - 9.84s nyumbani Nairobi wakati wa Mashindano ya Kip Keino Classic mnamo mwezi `Mei - Omanyala sasa analenga kumaliza wa kwanza katika mbio za mita 100 katika mashindano ya dunia.
Bara la Afrika limeshinda medali katika mbio za mita 200 kwa wanaume (kupitia Frankie Fredericks wa Namibia, kisha Mnigeria Francis Obikwelu na Wanariadha wa Afrika Kusini Anaso Jobodwana na Wayde van Niekerk) na katika mbio za mita 100 kwa wanawake (Wana Ivory Coast Murielle Ahoure na Marie-Josee Ta Lou) lakini sio kwenye mashindano hayo.
"Afrika haijawahi kupata medali katika mbio hizi na hilo ndilo jambo ninalotaka kuvunja. Nataka kubadilisha hilo, kwa hivyo nataka kushinda medali - nataka kushinda dhahabu," Omanyala aliendelea.
"Kuingia kwenye mashindano ya dunia kama mmoja wa wanariadha bora, watu wanakutazama na kukutegemea - watu wanakuhesabu kwenye mabano ya medali.
"Mimi naenda kushinda dhahabu."
Matarajio ni makubwa kwa Mkenya wa kwanza kushinda mbio za mita 100 za Diamond League, huku mwanariadha wa mita 400 pekee Nicholas Bett akiwahi kjushinda mbio za Diamond League za wanaume kwa nchi hiyo hapo awali.
Omanyala anasema kuweka historia si jambo litakalomshinda.
"Kila mara kuna mbwembwe nyingi mashindano yakikaribia, watu wanaotabiri hapa na pale, na watu hutuma maoni ya aina tofauti.
"Hiyo ndiyo mara kwa mara huleta mvutano lakini unapoingia kwenye kujiandaa na kisha kuingia uwanjani, huwa ni hadithi tofauti - kwa sababu hakuna kurudi nyuma, uko peke yako katika hili.
"Wakati ninapoingia uwanjani, na kuona umati wa watu na jinsi uwanja unavyoonekana na kuelewa kuwa huu ndio ukweli ulivyo, wasiwasi wangu wote hupotea tu.
"Halafu unapoenda kwenye eneo la kuanzia na kuweka alama, unaamua kuweka historia au ushindwe, halafu watu watazungumza kwa njia yoyote.
"Lazima tu uhakikishe kuwa unakimbia mbio hizi na kuzifanya bora zaidi ya maisha yako."
Mbio za Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Sio tu mbio za Omanyala na Kenya hata hivyo, kwani pia ni mbio za Afrika.
Mwanariadha wa Liberia Joseph Fahnbulleh - ambaye alimaliza wa 5 katika fainali ya Olimpiki ya mita 200 kabla ya kushika nafasi ya 4 katika mashindano hayo hayo mwaka jana - anaamini kuwa Afrika sasa iko tayari kupinga ubabe wa Marekani wa mbio za mita 100.
"Kwa muda, imekuwa Wamarekani. Kuna mabadiliko sasa kwa upande wa Afrika - napenda hivyo," Fahnbulleh aliiambia BBC. "Tunaikabili dhoruba, lakini polepole."
Akimuunga mkono Fahnbulleh, Omanyala anasema bara la Afrika hatimaye liko tayari kuchukua nafasi katika jedwali la mbio fupi duniani na licha ya matarajio yake mwenyewe, anajua kwamba ushindi wowote unaweza kufungua milango kwa Waafrika zaidi.
"Wacha dhahabu," alihitimisha. “Medali yoyote katika Mashindano ya Dunia itakuwa na maana kubwa kwangu.
"Moja: kuimarisha hali ya kifedha. Mbili: kuingia katika hadhi hiyo, ambapo unaweza kukimbia mbio zozote duniani na kupata utambuzi unaostahili na ambao tunastahili kama Waafrika.
"Tukienda katika mashindano ya riadha ya Ligi ya Almasi wanasema Wamarekani hawapo - vitu kama hivyo. Kwa hivyo ni kitu ambacho ninashikilia sana moyoni mwangu, kwa sababu najua hii itakuwa na athari kubwa kwa Afrika, kwa Kenya, na kwa kizazi cha wanariadha wanaokuja baada yangu na urithi ambao ninaenda kuweka.
"Siyo kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya nchi yangu, kwa vizazi, kwa watu - wanariadha wajao barani Afrika - kuonyesha kuwa inawezekana na kuonyesha Afrika kwamba hakuna lisilowezekana katika dunia hii."
Mashindano ya mbio za mita 100 kwa wanaume yataanza Jumamosi tarehe 19 Agosti, siku ya kwanza ya mchezo huko Budapest, na fainali itafanyika tarehe 20 Agosti.
Mashindano ya Riadha ya Dunia, ambayo Hungary inaandaa kwa mara ya kwanza, yatamalizika Jumapili tarehe 27 Agosti.












