Waomba hifadhi wafanya mgomo wa kutokula huku Uingereza ikijiandaa kuwafurusha hadi Rwanda

Rouge by Desir Hotel in Rwanda

Wanaotafuta hifadhi katika kituo cha uhamiaji wanapozuiliwa cha Uingereza walisema wameanza mgomo wa kutokula baada ya kuambiwa kuwa watasafirishwa na kupelekwa Rwanda.

Watu kumi na saba wanaotafuta hifadhi katika kituo cha Brookhouse karibu na uwanja wa ndege wa Gatwick mjini Sussex, waliiambia BBC kuhusu shida hiyo na waliokamatwa kuonyesha kukata tamaa.

Mwezi Aprili, serikali ya Uingereza ilitangaza mipango ya kurejesha waotafuta hifadhi nchini humo, huko Rwanda.

Lakini ofisi ya mambo ya ndani ya Uingereza ilisema kuwa ustawi wa wafungwa ulikuwa "muhimu".

Wanaotafuta hifadhi walishirikisha mawazo yao BBC na kutoa taarifa za ilani dhidi yao zilizotolewa.

Hati moja ya tarehe Juni mosi, inaorodhesha wanaotafuta hifadhi huko Brookhouse kuwa wanakaribia kusafirishwa kwenda mji mkuu wa Rwanda Kigali.

Pia, inasema hawawezi kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Priti Patel tayari amesema ndege ya kwanza ya kuwaondoa watu walioingia bila kibali nchini Uingereza itaondoka Juni 14 - wiki moja baadaye kuliko ilivyotangazwa awali.

Baada ya kuanzishwa kwa sheria ya 'Uraia na Mipaka mwezi Aprili, serikali ya Uingereza itachukua jukumu la kutoa hifadhi kwa "nchi nyengine salama", Rwanda, kwa wale wanaowasili Uingereza kupitia njia zisizo halali, kama vile mtu anayevuka bahari kwa boti kutoka Ufaransa.

Hatua ya kuwasafirisha watu hao wanaotafuta hifadhi maili 4,500 (kilomita 7,240) hadi Rwanda, ni sehemu ya mkataba wa pauni milioni 120 ($151m) kati ya Uingereza na nchi ya Afrika ya kati.

Priti Patel looks on as Foreign Minister Vincent Biruta addresses a news conference

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Makubaliano ya kuwatuma waomba hifadhi nchini Rwanda yamekosolewa na viongozi wa upinzani, mashirika ya misaada na viongozi wa kidini

Muomba hifadhi aliyezungumza na BBC alisema kuwa alikuwa mmoja wa watu 17 waliomaliza mgomo wa kutokula wa siku tano Jumatano usiku wakati walinzi walipoacha kuwapa sukari ya kuchanganya na maji yao kwa wale waliokataa kula.

Mtu huyo, Ali, aliiambia BBC kuwa alikuwa na familia nchini Uingereza na mkutano wake wa mwisho na maafisa wa uhamiaji ulikuwa ni wa kumaliza mgomo wa kukataa kula. "Jambo la mwisho ambalo waliniambia ni 'Kula ili uweze kupanda ndege ukiwa na afya njema'."

Miongoni mwa waliokuwa kwenye mgomo wa kukataa kula ni Wamisri wanaotafuta hifadhi, na karibu watu 100 waliokuwa wamewasili Uingereza waliambiwa na Ofisi ya Mambo ya Ndani watapelekwa Rwanda. Kundi moja lilijulishwa Jumatano kuhusu ndege yao kuondoka nchini Juni 14.

Room

Waliozuiliwa walisema kuwa serikali ya Brookhouse iliwapiga marufuku kutumia simu za rununu zenye kamera, na kuwapokonya simu zao za kisasa, na kuwapa simu ambazo hazitumii mtandao wa intaneti.

BBC iliweza kupata nakala kamili ya taarifa za ilani ya kuondolewa kwao iliyoelezea kuhusu hali yao. Barua hiyo ambayo ina zaidi ya kurasa 20, imechapishwa kwa lugha ya Kiingereza tu. Lakini moja ya sura inasema kuwa kulikuwa na wafasiri kuelezea maudhui yake kwa wanaotafuta hifadhi. Hati hiyo ilipotosha jina la mtu huyo mara kadhaa.

Watafuta hifadhi wawili kila mmoja aliwauliza waandishi wetu kuhusu yaliyomo kwenye nyaraka hizo kwa sababu hawakuweza kufahamu kwa undani maneno hayo kwa lugha ya Kiingereza, lakini walitakiwa kuyaweka sahihi.

Ofisi ya Mambo ya Ndani haikuthibitisha ni watu wangapi wamepokea ilani ya kuhamishwa kwao. Hata hivyo, shirika la msaada la Care4Calais inakadiria kuwa karibu watu 100 wanaotafuta hifadhi waliowasili Uingereza mwezi uliopita wameonywa kuwa watapelekwa nje ya Uingereza.

Shirika la Care4Calais limebaini na linatoa msaada kwa zaidi ya watu 60.

Mtu mmoja kutoka Syria ambaye anahitajika nchini mwake kwa ajili ya kuorodheshwa jeshini, aliiambia BBC kwamba "amejiandaa kufa, lakini hayuko tayari kupelekwa Rwanda".

"Niliposikia kwamba tutasafirishwa kwenda Rwanda na kwamba tutaenda kupata kibali cha kuishi huko kwa miaka mitano, nilianza kujipiga", alisema.

Akijibu swali kuhusu mgomo wa kula katika kituo cha Brookhouse, afisa wa makao makuu alisema: "Afya na ustawi wa watu waliozuiliwa katika kituo cha uhamiaji ni vyenye umuhimu mkubwa".

"Tutafanya kila kitu kwa uwezo wetu ili kuzuia watu wasijidhuru wenyewe au kujiua, ikiwa ni pamoja na kuwa na timu zilizojitolea kwenye kila kituo cha uhamiaji ambazo zina jukumu la kuwatambua watu wanaoishi katika mazingira magumu na kutoa usaidizi kama inavyohitajika".

Raia mmoja wa Misri aliiambia BBC kwamba alikuwa miongoni mwa watu 17 ambao walishiriki katika mgomo wa kutokula. "Niliendelea na mgomo wa kula mara mbili kabla sijapata nafasi ya kukutana na Ofisi ya Mambo ya Ndani", alisema.

"Ilibidi niondoke nchini mwangu ili kutatua mgogoro wa kifamilia. Kile nilichokiona nchini Libya njiani nikija hapa kilinisababishia matatizo ya afya ya akili ".

Picha: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel alisafiri hadi Rwanda kutia saini mkataba huo

Katika kutangaza taarifa kuhusu safari hizo kuanzia katikati ya mwezi Juni siku ya Jumanne (Mei 31), Katibu Mkuu wa Wizara Patel alisema: "Tunajua kutakuwa na majaribio ya kuzuia mchakato huo na kuchelewa kuwarejesha makwao; Sitatishika na nitafanya kila linalowezekana kukamilisha kinachotarajiwa na umma wa Uingereza ".

Hata hivyo, Steven Galardo-Andrew, mwanasheria aliyebobea katika masuala ya sheria ya uhamiaji, aliiambia BBC kuwa hafikirii serikali itatimiza kuanza kwa usafirishaji huo mnamo Juni 14 kwa ndege ya kwanza kama ilivyopangwa.

"Inaonekana kwamba sheria inayoruhusu serikali kufanya hivyo haitatekelezwa hadi Juni 28, mwaka huu", alisema.

"Kile wanachokifanya kinaweza na kitapingwa. Wanajua na wanategemea hilo".