Mzozo wa Rwanda na DRC: Waasi wa M23 waondoka maeneo walioteka huku Kagame na Tshisekedi wakizungumza

Chanzo cha picha, FLICKR.COM/PAULKAGAME
Waasi wa M23 wamejiondoa katika maeneo waliyokuwa wameyateka katika mapigano ya hivi majuzi na jeshi la serikali katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo.
Msemaji wa waasi hao, Meja Willy Ngoma, ameambia BBC kwamba "tumeondoka katika maeneo hayo ili kufanya amani".
Haijabainika ni wapi waasi hao wamekimbilia, lakini Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa inasema walienda katika maeneo yaliyo karibu na mpaka na Rwanda.
Zaidi ya watu laki moja walikuwa wamekimbia kwa sababu ya uhasama. Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba wengi sasa wanarejea katika makazi yao katika maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo.

Chanzo cha picha, Thinkstock
'Hakuna mazungumzo na magaidi'
Katika kikao na wanahabari siku ya Jumatatu, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Patrick Muyaya, amefutilia mbali uwezekano wowote wa mazungumzo na "magaidi wa M23".
"Ni nini kingekuwa kiini cha mazungumzo na kundi la kigaidi?... Hakuna nafasi tena ya mazungumzo [na M23]", Bw Muyaya aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kwamba nguvu inapaswa kutumika dhidi ya kundi hilo.

Chanzo cha picha, AFP
Bw Ngoma wa M23 alisema hawakuwa kundi la kigaidi. "Kutuita hivyo haina maana, ni vile tu [serikali] wanafikiria", aliiambia BBC Gahuza .
M23 ilitengwa na serikali katika mazungumzo ya Nairobi na makumi ya makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Aprili wakishutumu kundi hilo kwa kuanzisha uhasama kabla ya mazungumzo hayo.
Mazungumzo ambayo bado hayajafikia maamuzi, yanatazamiwa kurejelewa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Marais wakutana
Awali rais wa Rwanda Paul Kagame alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi pamoja na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sall huku kukiwa na mvutano wa mpaka.
Serikali ya Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 katika mapigano mapya mashariki mwa DR Congo - jambo ambalo serikali mjini Kigali inakanusha.
Maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao huku jeshi la Kongo likipambana na waasi katika jimbo la Kivu Kaskazini.
"Nawashukuru Marais Felix Tshisekedi na Paul Kagame kwa mazungumzo yetu ya simu jana na leo [Jumatatu] katika kutafuta suluhu la amani la mzozo kati ya DR Congo na Rwanda," Bw Sall, ambaye pia ni rais wa Senegal, alisema kwenye Twitter .
Alimhimiza Rais wa Angola João Lourenço kuendelea kupatanisha suala hilo chini ya Mkutano wa Kimataifa wa Kikanda wa Kanda ya Maziwa Makuu.Bwana Sall hapo awali alielezea "wasiwasi mkubwa" kutokana na kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Alitoa wito wa mazungumzo kusuluhisha mzozo huo.
Wiki iliyopita, DR Congo ilisitisha safari za ndege kuelekea Rwanda na kumwita balozi wa Kigali kuhusu suala hilo.
M23 ni nani? Wanataka nini?
Ukizungumzia M23, inawakumbusha wengi kuwahusu watu kama Sultani Makenga na wengine kama Bosco Ntaganda, huku wengine wakirudi nyuma na kumkumbuka Laurent Nkunda.
Tangu mwaka 2004, Jenerali Nkunda amejiondoa katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na wanajeshi wake katika vilima vya Rutshuru na kuunda CNDP, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali na mji wa Goma.
Sababu za vita vyake ni kulinda watu wa kabila lake na aliendeleza mapambano dhidi ya makundi mengine ya waasi ambayo pia yanatokana mapigano ya kikabila na ni miongoni mwa sababu zilizotolewa na Nkunda na wapiganaji wake wakiwemo Makenga na Ntaganda.
Wote watatu walikuwa wanachama wa waasi wa zamani wa APR waliochukua mamlaka nchini Rwanda mwaka 1994, kabla ya kuendeleza vita vyao nchini DR Congo mwishoni mwa miaka ya 1990.
Nkunda alikamatwa nchini Rwanda mapema mwaka 2009 na kufungwa, huku CNDP ikiongozwa na Ntaganda ikijadiliana na serikali ya Kabila katika makubaliano ya Machi 23, 2009.
Miaka minne baada ya kusitishwa kwa mapigano, kundi la watu wanaojiita wapiganaji wa M23 lilizaliwa mwaka 2012, likiongozwa na Ntaganda na Makenga, ambao wanasema makubaliano ya serikali na CNDP Machi 23 hayajafuatwa.
Serikali za Rwanda na Uganda zimeshutumiwa na wataalam wa UN kwa kuwa nyuma ya makundi ya waasi, lakini wameendelea kukanusha.













