Rwanda: Hatuhusiki na mashambulizi ya M23 DRC

Jeshi la nchi hiyo limesema taarifa zozote zinazodai kuwa kundi hilo lilianzia Rwanda ni propaganda za kudhoofisha mahusiano mazuri kati ya Rwanda na DRC.

Moja kwa moja

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. Mwanaume anayegombea kiti cha uongozi cha wanawake

    BBC

    Chanzo cha picha, BBC Hausa

    Bw Ameer Sarkee, mwenye umri wa miaka 26, ambaye anagombea kiti maalum cha wanawake katika chama tawala cha Nigeria UPC, ameiambia BBC kuwa anagombea kiti hicho kwasababu yeye ni mwanaume ambaye anapaswa kusimamia mausla ya wanawake wakati wote.

    Mwaka 2019 Bw Ameer aligombea kiti cha wanawake kupitia chama cha PDP tawi la la Kano lakini hakuweza kuchaguliwa. Laini ansema mara hii hatakubali kushindwa kwasababu lazima ashugulikie masuala ya wanawake.

    "Tangu nilipokuwa mtoto nilikuwa nikiwaona wanawake wanaohitaji msaada na kuwasaidia-kama vile kubeba nguo au kuwanunulia kitu fulani-na ndio maana ninataka kuwa kiongozi wa wanawake katika chama chetu ," alisema.

    "Baadhi ya watu huniuliza kwanini unagombea uenyekiti wa wanawake na jibu langu ni ‘Mungu aliumba mwanaume awapende wanawake ,'" alisema Ameer.

  3. Mbwa wa familia ageuka mbweha Peru

    Mbwa

    Chanzo cha picha, bb

    Familia moja nchini Peru iliyofikiri kuwa imenunua mbwa iligundua punde kwamba walikuwa na mbweha mikononi mwao baada ya kuwashambulia wanyama wengine walio jirani zao.

    Familia ya Sotelo walimnunua mbwa huyo kwa $13 (£9.50) kutoka kwenye duka dogo katika mji mkuu, Lima.

    Lakini baada ya muda, walipata malalamiko kutoka kwa majirani kuhusu mbwa wao aliyeitwa Run Run. Muuzaji huyo wa mbwa tangu wakati huo amekamatwa na maafisa wa wanyamapori.

    Ilibainika kuwa kulikuwa na kisa cha utambulisho kimakosa mpaka pale Run Run ilipoanza kuwafukuza nguruwe, kuku na bata ili kuwaua au kuwala, na hivyo kusababisha hasira za majirani.

    "Takriban mwezi mmoja uliopita, mwanamke mmoja hapa alisema kwamba alikula nguruwe zake watatu. Na kisha siku mbili au tatu zilizopita, bibi wa eneo hilo alikuja na kusema kwamba mbwa huyo aliua nguruwe," mmiliki Maribel Sotelo aliliambia shirika la habari la Reuters.

    Run Run aligeuka kuwa mbweha wa Andean, ambaye ana miguu nyembamba, mkia wa manyoya. Huduma ya Kitaifa ya Misitu na Wanyamapori nchini Peru inasema wanyama pori mara nyingi hununuliwa na walanguzi kutoka maeneo ya Amazonia na huuzwa kinyume cha sheria huko Lima.

  4. Rwanda: Hatuhusiki na mashambulizi ya M23 DRC

    Watu elfu tano walikimbia mapigano siku ya Jumatatu

    Chanzo cha picha, social Media

    Jeshi la Ulinzi la Rwanda limesema halihusiki wala kuunga mkono kundi la zamani la M-23.

    Imeripotiwa kuwa kundi la watu wenye silaha linaloaminika kuwa waasi wa M-23, siku ya Jumapili jioni , walivuka DRC kutoka Uganda ambako ndiko yaliko makazi yao na kushambulia na kudhibiti Tshanzu na Runyoni.

    Waasi wa zamani wa M23 wanaoelezwa hawakuomba hifadhi ya ukimbizi Rwanda wakati walipoondolewa DRC mwaka 2013, lakini wamekuwa nchini Uganda, ambako ndiko shambulizi lilikoanzia, na ambako kundi hilo lenye silaha lilipoondoshwa.

    Jeshi la nchi hiyo limesema taarifa zozote zinazodai kuwa kundi hilo lilianzia Rwanda ni propaganda za kudhoofisha mahusiano mazuri kati ya Rwanda na DRC.

  5. Ethiopia hatarini kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe - UN,

    Pande zote mbili katika mgogoro wa Ethiopia zinakubali kwamba mzozo huo ni wa kisiasa

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Ethiopia iko katika hatari ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoongezeka ikiwa mapigano katika eneo la kaskazini la Tigray hayatakoma.

    Mkuu wa masuala ya kisiasa na ujenzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo, alisema hakuna malori ya misaada yaliyofika mji mkuu wa Tigray Mekelle tangu katikati ya Oktoba, licha ya watu milioni saba kuhitaji msaada wa haraka wa chakula.

    Umoja wa Mataifa unasema watu 400,000 kati ya wale wenye uhitaji wanaishi katika hali ya njaa.

    Akihutubia baraza hilo, mjumbe wa Umoja wa Afrika katika Pembe ya Afrika, Olusegun Obasanjo, alisema amekutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na kiongozi wa eneo la Tigray, Debretsion Gebremichael.

    Alisema wote wawili walikubaliana kuwa mzozo huo ulikuwa wa kisiasa ingawa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

    Baraza la Usalama linataka wanajeshi na wanamgambo kuondoka katika eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa chakula na dawa zinazohitajika sana.

  6. Tutaingia hadi Addis Ababa - TPLF

    Msemaji wa TPLF Getachew Reda

    Msemaji wa waasi wa Tigray amesema vikosi vyao vitaendelea kusonga mbele hadi mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa hadi serikali iondoe vikwazo vyake katika eneo la kaskazini.

    Getachew Reda alikiambia kipindi cha redio cha BBC Focus on Africa kwamba kikwazo pekee ambacho kilikuwa kikizuia njia ya amani ya Ethiopia ni "takwa la Waziri Mkuu Abiy Ahmed na suluhisho la kijeshi kwa kile ambacho kimsingi ni shida ya kisiasa".

    Waasi wanasonga mbele kuelekea mji mkuu, na serikali imewataka wakazi wa Addis Ababa kuhamasisha na kulinda vitongoji vyao.

    Bw Getachew alisema kuendelea na maandamano yao "sio Addis Ababa lakini nia yetu ni kumshinikiza [Bw Abiy] ili kuondoa kizuizi kwa watu wetu".

    "Ni uamuzi wa Abiy kusema ndiyo kwa madai yetu…na kukomesha mzozo," msemaji wa chama cha Tigray People Liberation Front (TPLF) alisema.

    Msemaji huyo alisema rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ambaye yuko Ethiopia akijaribu kufanya mazungumzo ya kusitisha vita, alikuwa na mazungumzo yenye manufaa na kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael. Alisema kiongozi wa TPLF "ameeleza tunachosimamia".

  7. Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amewaambia raia waache kuomba kwa wanasiasa

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amewataka raia kila mmoja kuwajibika katika kuleta maendeleo ya nchi hiyo badala ya kuyadai kutoka kwa wanasiasa.

    Amesema alikua na nia ya ujumbe kwenye simu yake watu wakimtaka "kuziendesha familia zao" kwasababu tu yeye ni rais-akiongeza kuwa Wabunge walipata ujumbe wa namna hiyo hiyo kutoka kwenye majimbo yao.

    "Lazima tujitibu tabia ya kuomba kwa wanasiasa kuliko tunachokitaka kutoka kwetu wenyewe..nchi yetu haitaendelea kwa tabia ya namna hii," alisema.

    Rais wa Malawi amewataka raia kutekeleza mipango katika ngazi ya familia ambayo inakwenda sambamba na mpango wa maendeleo wa taifa ambao alikua akiuzindua.

    Alitoa mfano mpango wa kuimarisha uzalishaji,kilimo cha biashara ambao amesema hautafanikiwa kama "hakutakuwa na mabadiliko katika ngazi ya familia".

    Hotuba ya rais huyo iliwekwa kwenye mtandao wa Facebook.

  8. Kuna nafasi ndogo ya kumaliza mzozo wa Ethiopia-Au na Marekani

    rthiopia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Umoja wa Afrika(AU) wamesema wanaamini kuwa kuna nafasi ndogo ya kutatua mgogoro Ethiopia Ujumbe maalumu Jaffrey Feltman amerejea Adis Ababa kukutana na maafisa wa AU.

    Alikua nchini Ethiopia juma lililopita ambapo alikutana na maafisa wa serikali ya shirikisho na wa serikali.

    Mjumbe wa AU Obasanjo aliniambia baraza la Usalama la Umoja wa Maraifa kuwa muda wake unamalizika na kuwa kutakuwa na athari kubwa ikiwa mgogoro hautashughulikiwa.

    Mzozo nchini Ethiopia ulianza mwaka mmmoja uliopita wakati vikosi vilivyopambana kaskazini mwa nchi hiyo. Waasi wanatishia kuingia mji mkuu Addis Ababa.

  9. Vipindi vya joto kali kuendelea kujitokeza mwezi Novemba Tanzania

    TMA inatabiri kuwa maeneo mengi ya Tanzania yatapata joto la hali ya juu mwezi wote wa Novemba.

    Chanzo cha picha, EyeWire, Inc.

    Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania, TMA hapo jana ilitoa tahadhari kuhusu ongezeko la joto nchini, linalosababishwa na kuongezeka kwa jua na ukame unaoendelea katika maeneo mengi nchini.

    Meneja wa kituo kikuu cha utabiri wa hali ya hewa TMA Samwel Mbuya alisema kwa kawaida, jua la utosi hufikia kilele chake mwezi Novemba wakati jua linahamia kusini - na hali hiyo hutokea Februari wakati jua la utosi linapoelekea kaskazini.

    "Jua la utosi uhusishwa na halijoto kali kwa sababu mnururisho wa jua husogezwa karibu na uso wa dunia katika eneo fulani. Aliieleza The Citizen.

    "Vile vile, hali ya joto kali hujitokeza zaidi kunapokuwa na ukandamizaji wa mvua - kama ilivyoshuhudiwa katika kipindi hiki," alisema.

    TMA inatabiri kuwa maeneo mengi ya Tanzania yatapata joto la hali ya juu mwezi wote wa Novemba.

    Katika kipindi hiki, viwango vya juu vya joto vilivyorekodiwa vinaonekana katika maeneo mbalimbali, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukiripoti joto la 36.4C.

  10. Pogba apata jeraha baya la nyonga

    Pogba

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Pogba

    Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba hatoshiriki katika mechi ya michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia baada ya kupata jeraha la nyonga.

    Mshindi huyo wa Kombe la Dunia , mwenye umri wa miaka 28alipata jeraha wakati wa mazoezi siku ya Jumatatu , Shirikisho la soka nchini Ufaransa FFF limesema.

    Pogba hatoshiriki katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Kazakhstan ama mechi ya ugenini dhidi ya Finland Novemba 16.

    Tayari alitarajiwa kukosa mechi ya United ugenini dhidi ya Watford katika ligi ya Premia tarehe 20 Novemba , huku akikamilisha marafuku yake ya mechi tatu .

    Pogba alipokea marufuku hiyo kabla ya kutolewa nje wakati wamechi ya kichapo cha 5-0 dhidi ya Liverpool tarehe 24 mwezi Oktoba.

  11. Watoto wachanga wafariki baada ya moto kuzuka kwenye wodi India

    Moto kuzuka kwenye hospitali si jambo la kushangaza India

    Chanzo cha picha, ABHISHEK SHARMA

    Takribani watoto wachanga wanne wamefariki wakati moto ulipozuka katika wodi ya watoto wachanga ya hospitali katika jimbo la kati la India la Madhya Pradesh.

    Wafanyakazi wa zima moto waliweza kuwaokoa watoto 36 kutoka Hospitali ya Watoto ya Kamla Nehru huko Bhopal Jumatatu usiku.

    Picha za kutatanisha zinaonesha wazazi wakijaribu kukimbilia katika hospitali iliyojaa moshi.

    Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana lakini maafisa walisema kuwa saketi ya umeme inaweza kuwa sababu.

    Waziri Mkuu Shivraj Singh Chouhan alisema tukio hilo lilikuwa la uchungu. Aliamuru uchunguzi ufanyike na akatangaza kulipa rupia 400,000 (£4000; $5400) kwa familia za waathiriwa.

    Moto huo ulizuka mwendo wa saa 3:00 kwa saa za huko, na kusababisha hospitali hiyo kuwa gizani.

    Picha zinaonesha wazazi wenye hasira wakijaribu kuingia ili kuwaokoa watoto wao huku vyombo vya usalama vya hospitali hiyo vikijitahidi kuwazuia.

    Zima moto walichukua saa tatu kuuzima moto huo.

    Moto wa hospitali nchini India si jambo la ajabu kwani viwango vya usalama havifuatwi kikamilifu kila wakati.

    Siku ya Jumapili, wagonjwa 11 walikufa katika chumba cha ICU cha wagonjwa wa Covid katika jimbo la Maharashtra wakati moto ulipozuka. Uchunguzi umeamriwa kufanywa kujua chanzo cha moto huo.

  12. Marekani yawakamata raia wa DRC kwa ulanguzi wa pembe za ndovu

    Sehemu za wanyama hao zilikatwa vipande vidogo vidogo

    Chanzo cha picha, US Embassy Kinshasa/Twitter

    Raia wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekamatwa nchini Marekani kwa tuhuma za kusafirisha meno ya tembo na pembe za faru kutoka nchini mwao.

    "Herdade Lokua, 23, na Jospin Mujangi, 31, wa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walikamatwa tarehe 3 Novemba nje ya Seattle," Idara ya Sheria ya Marekani ilisema katika taarifa yake.

    Ilisema wawili hao walikuwa wamefunguliwa mashtaka ya "njama, utakatishaji fedha, ulanguzi na ukiukaji wa kisheria wa biashara hiyo".

    Shauri la mashtaka 11 linadai kuwa wawili hao walifanya kazi na mtu wa kati kusafirisha kwa njia ya magendo vifurushi vinne vya pembe za ndovu na pembe za faru hadi Marekani.

    Linasema walikata sehemu za wanyama hao katika vipande vidogo ambavyo vilipakwa rangi nyeusi na kuchanganywa na mti wa buluu ili kuepuka kugunduliwa. Washukiwa hao wanadaiwa kutoa hongo ili wasafirishwe.

    Wanunuzi hao walilipa $14,500 (£10,600) kwa pembe ya ndovu na $18,000 kwa pembe za faru, kulingana na mashtaka.

    Pia inasemekana waliuza mizani ya pangolini kwa mnunuzi wa Marekani lakini hatimaye hawakuisafirisha.

    Wanaweza kukabiliwa na kifungo cha zaidi ya miaka 20 ikiwa watapatikana na hatia, wizara ya sheria imeeleza.

  13. Sierra Leone yawazikwa kwa pamoja waliokufa katika mlipuko

    m

    Watu 115 walifariki katika mlipuko wa tenki la mafuta siku ya Ijumaa, nchini Sierra Leone wanazikwa kwa pamoja katika mji mkuu wa Freetown.

    Wengi waliungua sana hata ikawa vigumu kuwatambua.

    Mamlaka imetoa wito wa watu kujitolea damu kwa haraka ili kuweztibu wahanga walioungua na moto ambao ni zaidi ya 100 wamelazwa hospitalini.

    Maofisa wanasema wasambazaji wa damu wanaweza kuishiwa ndani ya saa 72.

    Mazishi hayo yamefanyika katika eneo ambalo watu wapatao 1000 walizikwa mwaka 2017 baada ya kuuawa kutokana na mmomonyyoko wa udongo, anasema mwandishi wa nchini humo Umaru Fofana.

    Msemaji wa waziri wa afya amethibitisha kuwa idadi ya vifo vilivyotokea katika ajali ya Ijumaa ni 115.

    Rais Julius Maada Bio ametangaza siku tatu za maombolezo kitaifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kufuatia janga lililotokea Ijumaa.

    • Mlipuko Sierra Leone: Takribani watu 99 wapoteza maisha baada ya lori la mafuta kugongana na gari jingine
  14. Muuza duka muislamu atishiwa kwa kuuza biryani siku ya Diwali

    PROMICROSTOCKRAW

    Chanzo cha picha, PROMICROSTOCKRAW

    Video inayomuonesha mwanaume akimtishia muuza duka wa imani ya Kiislamu ambaye anamiliki duka la biryani katika eneo la Sant Nagar huko Burari huko Delhi imezua gumzo mtandaoni.

    Kwa mujibu wa gazeti la kiingereza la Times of India, limeandika kuwa katika video hiyo mtu huyo anamtishia muuza duka kwa sababu alifungua duka lake siku ya Diwali.Polisi wa Delhi wameandikisha tukio hilo.

    Katika video hii, mtu anayetoa vitisho anasema jina lake ni Naresh Kumar Suryavanshi na kujiita kuwa yeye ni mwanachama wa Bajrang Dal.

    Katika video hii ameonekana akiwatishia wauza maduka kufungua maduka wakati wa tamasha.

    Baada ya kutishiwa, mmiliki wa duka na wafanyakazi wake walifunga duka hilo haraka. Video hiyo ilirekodiwa saa tisa alasiri siku ya Alhamisi na kuanza kuenea katika mitandao ya kijamii.

  15. China yatengeza mfano wa meli ya kivita ya Marekani katika jangwa

    m

    Chanzo cha picha, Satelite Image

    China inaonekana kuwa imetengeneza mfano wa meli za kivita za Marekani katika jangwa lake lililoko eneo la kaskazini-magharibi la Xinjiang nchini humo, picha za satelaiti zinaonyesha.

    Moja ya picha, iliyonaswa na kampuni ya Marekani inayoangazia teknolojia ya anga -Maxar, imeonesha muundo wenye umbo la kubeba ndege za kijeshi uliowekwa kwenye njia za reli.

    Taarifa kutoka USNI News, tovuti maalumu kwa Jeshi la Wanamaji la Marekani, ilisema miundo hiyo inaonekana kuwa kuwalenga na iliyojengwa na wanajeshi.

    Beijing imekuwa ikitengeneza na kufanya majaribio ya makombora ya kuzuia meli kwa miaka.

    Marekani imeonya kwamba katika miezi ya hivi karibuni China imekuwa ikiongeza ukubwa wa jeshi lake kwa kasi, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa nyuklia, huku hali ya wasiwasi ukiongezeka katika Bahari ya China Kusini.

    Siku ya Jumapili, USNI News ilisema miundo iliyopigwa picha kwenye Jangwa la Taklamakan ilionekana kujumuisha muhtasari wa meli za kijeshi za Marekani bila silaha au maelezo mengine.

    • Picha za satellite zinaashiria kuwa Korea Kaskazini inajiandaa 'kurusha' kombora
  16. Wapenzi waishitaki kliniki kwa madai ya kumpandikiza mtu mwingine mimba yao

    m

    Wapenzi waishio California wamepata mtoto wa mtu wasiyemfahamu baada ya kutumia mbinu ya maabara kupata mtoto(IVF) na kupewa kiinitete kisicho sahihi ambacho kilirutubishwa kliniki, inasema mahakama.

    Daphna na Alexander Cardinale wanasema walijifungua mtoto wa kike Septemba 2019 ambaye alikuwa hafanani kabisa na wao.

    Baada ya kufanya vipimo vya vina saba DNA , walifanikiwa kuwapata wapenzi waliochukua mtoto wao na kubadilishana.

    Hii sio kesi ya kwanza kwa mchakato wa IVF kuchanganywa.

    IVF ni mbinu ya uzazi ambapo mayai ya mwanamke urutubishwa na mbegu za mwanamume katika maabara kabla ya viinitete kupandikizwa kwa mwanamke.

    • Mwanamke aliyang’ang’ania mayai yake ya ziada ya uzazi
    • Athari za mpango wa uzazi wa IVF
  17. Watoto wapatao 25 wamefariki baada ya darasa lao kuungua moto Niger

    niger

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watoto wapatao 25 wenye umri kati ya miaka mitano na sita wamefariki baada ya darasa lao kuungua moto.

    Wengine kadhaa walijeruiwa wakati wa ajali hiyo ya moto ambayo ilitokea Jumatatu asubuhi wakati watoto wakiwa darasani wakisoma katika shule iliyopo eneo la Maradi.

    Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika bado.

    Nchini Niger, madarasa huwa yanajaa na mara nyingi hujengwa kwa kutumia mbao na majani wakati miundo mikuu ya matofali haiwezi kujenga shule zote.

    Moto uliotokea Jumatati umeteketeza madarasa matatu , meya wa mji Maradi, Chaibou Aboubacar, ameviambia vyombo vya habari.

    Shuhuda mmoja ameiambia BBC kuwa ameona watoto kadhaa wakitolewa eneo la tukio na kupelekwa hospitali wakiwa katika hali ya mahututi.

    Masomo yamesitishwa katika shule hiyo kwa muda.

    Si kawaida kwa shule za Niger kuungua na kusababisha idadi kubwa ya vifo.

    Ingawa mwanzoni mwa mwaka huu katika mji mkuu wa nchi hiyo shule iliungua na kuua watoto 20 .

  18. Habari na karibu katika matangazo ya moja kwa moja katika kurasa yetu ya BBC Swahili leo ikiwa Jumanne 09/11/2021.