Kwanini Wasanii Afrika Mashariki wanakimbilia kutoa EP badala ya Albamu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania, Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz ,ameachia EP (Extended Playlist) yake ya kwanza usiku wa kuamkia leo inayoitwa First of All au FOA kwa kifupi.
Ni EP yenye nyimbo 10 ikishirikisha wasanii wengine wakali Afrika kama Adenkule Gold na Jaywillz kutoka Nigeria, Lethabo Sebetso 'Focalistic', Costa Titch na Pabi Cooper kutoka Afrika Kusini na wazawa wa lebo yake ya WBC Mbosso na Zuchu wa Tanzania.
Nyimbo hizo ni Melody aliyomshirikisha Jaywillz, Sona aliyomshirikisha Adenkule, Oka aliyowashirikisha Mboso na Fresh alioimba na wakali wa 'madiba' Focalistic, Costa Titch na Pabi Cooper . Nyimbo nyingine ni Nawaza, Fine, Loyal, Wonder, Somebody na mtasubiri aliomshirikisha Zuchu.
Hiyo ni EP ya kwanza katika maisha ya muziki ya Diamond tangu aanze muziki na kufahamika nchini Tanzania na Afrika miaka zaidi ya 10 iliyopita. Lakini Diamond sio msanii wa kwanza kutoa EP Afrika Mashariki, Nandy alitoa hivi karibunu EP zake Taste na Wanibariki, Lavalava alitoa Promise, New Chui 'Rayvanny, I am Zuchu ya Zuchu na LOL FIT ya Azawi wa Uganda. Swali kwanini sasa utoaji wa EP umeonekana kuwa ndio njia sahihi kwa wasanii wengi hasa wa Afrika Mashariki?
Tofauti ya EP na Albamu
Inawezekana kuwa na tofauti nyingi na kubwa, lakini tofauti rahisi na inayowezeka kueleweka inaweza kukupa ugumu wa kutofautisha EP na Albam, kama haujabobea sana kwenye masuala ya muziki. BBC inamuuliza Sir Tino, nini tofauti ya haya mawili, na kutaja maeneo matatu muhimu yanayotofautisha EP na Albamu; idadi ya nyimbo, muda wa nyimbo zote na ujumbe.
'EP huwa na nyimbo chache 4 mpaka 6, ingawa kwa sasa wapo wanaoweka mpaka 12, lakini nyimbo hizo zinapaswa kuwa chini ya dakika 30 na angalu zaidi ya dakika 9', anasema Sir Tino
Tofauti nyingine inayotajwa na wasanii wengi ni kwamba Albamu mbali na kujumisha nyimbo nyingi za msanii mmoja, inapaswa kuwa na 'theme' ama kauli mbiu ya kimuziki ambayo nyimbo nyingi zilizoko kwenye albamu husika zinaizungumzia ama kuigusa.
'Albamu ya kweli inawapa ugumu wasanii wengi kufikiria na kutunga nyimbo zinazokuwa na madhadhi na ujumbe ambao mwishowe unapasa kuakisi albamu yenyewe', lakini EP haikubani, una uhuru kutokana na (mzuka) ama namna unavyohisi wakati huo', alisema Sir Tino.

BBC inamuuliza Sir Tino ambayo yuko kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 10, kuhusu faida ya kutoa EP kwa msanii anasema; 'EP inakupa fursa ya kuweka ngoma kali chache zinazoweza kupendwa na kusikilizwa sana na kukutengeneza pesa, lakini Albamu utaweka nyimbo 30, lakini watu wakasikiliza moja tu, unakuwa umepoteza nguvu na fedha bure', anasema Sir Tino na kuhitimisha 'muziki ni biashara'.
Kwanini EP na sio Albamu kama zamani?
Ukiwauliza wasanii wa zamani kama Joseph Haule 'Profesa Jay', Juma Nature, Sugu, Lady Jay D, Fid Q au Mwana FA akili yao inaweza kukupeleka kwenye utoaji wa albam kwa sababu wakati huo kuanzia miaka 2000s mpaka 2010s albamu ilikuwa utambulisho wa msanii aliyekamilika.
Maendeleo ya kidijitali yamehamisha muziki kutoka kwenye albam zilizokuwa zinauzwa kwa mfumo wa mkanda au 'tape' na CD kwenda kwenye uuzaji wa usiohitaji mifumo hiyo. Mitandao ya muziki kama Spotify, Apple Music, Amazon Music, Tencent na You tube imekuwa sehemu kubwa inayotumiwa na wasanii wa muziki kupitisha nyimbo zao huko na kusikilizwa na mamilioni ya watu duniani.
Ipo mitandao mingine ya muziki kama Audiomark, Deezer, Netease na Yandex ambayo nayo inatumiwa na wasaniii mbalimbali duniani kuuza miziki yao huko.
Kwa mujibu wa takwimu za Midia kuna wateja wa muziki (wasilikizaji na watazamaji) zaidi ya nusu bilioni wanaofuatilia kupitia mitandao hii mbalimbali ya muziki duniani.
Pengine hilo linawafanya wasanii wa Afrika Mashariki kukimbilia hutoa EP na kuzipakia kwenye mitandao hii na kutoa fursa ya kutazamwa na kusikilizwa na watu wengi zaidi duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndio maana leo unasikia neno anatafuta 'views ama viewers', kwa sababu kila unapoitazaman kwa mfano video ya wimbo wowote wa Diamond, idadi kubwa zaidi ya watazamaji inamuongezea kipato zaidi msanii huyo.
''kibiashara albamu hazilipi kwa sasa hasa kwa mazingira yetu, mchongo upo kwenye mitandao, usimamizi wake ni wa uhakika lakini pia huitaji kuwa na nyimbo nyingi ambazo wakati mwingine zinatungwa ili kujazia albam tu', anasema Sir Tino, aliyezungumza kwa simu na BBC.
Sababu nyingine iliyowahi kutajwa mwanamuziki Banza Stone, muda mfupi kabla ya kifo chake ni usalama wa haki ya msanii.
'biashara ya muziki mtandao inakwenda sawa na jasho lako, walichotushinda vijana wa sasa (akiwarejea wasanii wa muziki wa kizazi kipya) ni kwamba wameweza kuupenyeza muziki wao mitandaoni kwa fujo, ni mifupi kulinganisha na dansi na ni rahisi kuidownload (pakua), kwa gharama nafuu ya bando tofauti na taarabu na dansi, alisema Banza.

Chanzo cha picha, WCB
Miaka hiyo anayoizungumzia Banza ni zaidi ya 7, wakati huo ndio kasi ya mitandao ya muziki inapamba moto, leo ni kama muziki umehamia huko zaidi.
Albamu hazijatupwa jalalani, zinaendelea kujenga heshima ya wasanii
Pamoja na wasanii wengi Afrika Mashariki, kujielekeza kwa kasi kwenye kutoa EP kati ya miaka ya 2000s na 2010s, utoaji wa albamu ulikuwa ni jambo linalotukuzwa na kujenga heshima ya msanii. Wapo wanaoamini kwamba heshima ya utoaji wa albamu kwa msanii itaendelea kuwepo.
Lakini bado mpaka sasa albamu hazijawekwa kando, wapo wasanii kutoka Afrika Mashariki wanaendelea kutoa albamu za muziki na kuziingiza sokoni, ikiwemo kupitia mitandao ya muziki.
Nchini Kenya kundi la Mbuzi Gang lilianza mwaka 2022 kwa mguu wa kulia kwa kutoa albamu yao yenye nyimbo 12 inayoitwa Three Wise Goats, ikiwashirkisha wasanii wakali Afrika kama Lavalava na Josee Chameleon, Wyre na Katapila.
Lady Jay Dee, malkia wa muziki wa kizazi kipya Tanzania na mkongwe wa muziki huo kwa zaidi ya miaka 20, ana albamu inayoitwa '20' kama ilivyo kwa wasanii wengi waliotoa albamu zao miaka ya hivi karibuni kama Ally Kiba 'Only One King, Afro Beat na 'High School' ya Harmonize, 'Sound from Africa' ya Rayvanny na Definition of Love ya Mbosso.
Azawi wa Uganda yeye ana albamu yake ya 'African Music' baada ya kutamba na EP yake ya LOL FIT iliyokuwa na nyimbo tano, anaonyesha kwanini kupitia albamu yake ni kwanini wasanii wakali kama Lydia Jazmine, Nina Roz, Eddy Kenzo walimtumia kwenye uandishi wa nyimbo zao.
Kutokana na tafsiri iliyopo huenda katika Albamu tajwa hapo juu, zipo zinazoweza kutafsirika kama EP na EP zikatafrisirika kama Albam kulingana na tafsiri inayotumiwa kwa wakati huo. Lakini hilo halikatazi wanaofuatilia muziki Afrika Mashariki kueleza kitu gani muhimu bila kujali kama ni EP ama Albam, heshima na muziki mzuri.
'msanii unaimba miaka 10 kama huna albam, wewe ni wa kuokotwa, iwe inalipa iwe hailipi ukomavu kisanii unahitaji utoe albam, kama ina nyimbo nzuri itauzika tu, watu watazitafuta kununua na kusikiliza', anasema Andrea Shija, mmoja wa wafuatiliaji wa kubwa wa muziki Tanzania.












