SmartWater: Teknolojia inayowalinda wanawake dhidi ya unyanyasaji

Mtu wa kwanza nchini Uingereza amepatikana na hatia na kufungwa jela kwa unyanyasaji wa nyumbani baada ya kunyunyiziwa SmartWater - kioevu cha uchunguzi kinachoonekana chini ya mwanga wa ultraviolet. Teknolojia hiyo inajaribiwa na vikosi vya polisi kwa matumaini ya kuwaweka wanawake salama.
Dutu hii hukaa kwenye ngozi hadi wiki sita na kwenye nguo kwa muda mrefu zaidi na humhusisha mhalifu na kundi maalum la maji ambalo lilinyunyiziwa.
Mwathiriwa, huko West Yorkshire, ni mmoja wa wanawake zaidi ya 200 kote Uingereza ambao sasa wana vifurushi vya maji hayo katika nyumba zao. Vifurushi hivyo ni pamoja na mkebe unaoshikiliwa kwa mkono kwa ajili ya kunyunyuzia, jeli ya vishikizo vya mlango na lango, na mtego wa kiotomatiki unaonyunyiza maji hayo ikiwa mtu anakaribia nyumba.
Msimamizi wa Upelelezi wa Polisi wa West Yorkshire Lee Berry, ambaye alikuja na wazo hilo, aliiambia BBC: "Unyanyasaji wa nyumbani mara nyingi ni vigumu sana kufunguliwa mashtaka na matukio mengi ya uhalifu huu hutokea kwa siri.
"Ikiwa tutaweka alama kwa uchunguzi wa kitaalamu, basi tunaweza kufuatilia mtu mahali fulani. Tutajua mhusika ni nani, na tutajua mwathiriwa ni nani pia.

"Tunachosema kwa mhalifu ni kwamba, ukirudi kwenye eneo hilo na kukiuka masharti haya, utanaswa na alama za kiuchunguzi."
Vikosi vya Polisi vya West Yorkshire, South Yorkshire na Staffordshire vyote vinatumia vifaa hivyo, ambavyo hugharimu takribani pauin 150 kwa mwezi kwa kila mtu, kama sehemu ya mkakati wao wa kupambana na unyanyasaji wa nyumbani.
Kwa wastani inagharimu polisi kama pauni 640 kushughulikia tukio la unyanyasaji wa nyumbani, kulingana na uchunguzi wa uhalifu wa Uingereza na Wales. DS Berry alisema kikosi hicho kitaokoa takriban pauni 500 kwa kila kikosi ikiwa kitatumia alama za uchunguzi kama kizuizi.
Unyanyasaji wa nyumbani huathiri wanaume na wanawake.
Waathiriwa wengi wanaotumia teknolojia hiyo wamewaambia polisi wanahisi kuwa salama zaidi, na 94% ambao walihojiwa walisema wangependekeza na wengine watumie.
Takriban vikosi 20 kati ya 43 vya polisi nchini Uingereza vinakutana na kushirikishana kile wanachofanya ili kukabiliana na unyanyasaji wa nyumbani kama sehemu ya mkakati wa Uingereza wa Unyanyasaji dhidi ya Wanawake na Wasichana. DS Berry anatumai vikosi vingine vitaamua kutekeleza teknolojia hiyo pia.
DS Berry alisema: "Ninatumai sana vikosi vingine vya polisi vitaona kile tunachofanya hapa West Yorkshire. Kadiri tunavyoweza kuwalinda kuwalinda waathiriwa na kuwafanya wajisikie salama katika nyumba zao, ndivyo wanavyokuwa bora zaidi. Hiyo ndiyo hadithi ya mafanikio ya kweli hapa."

Kwa miaka mingi, SmartWater imekuwa ikitumika kulinda mali na kuzuia wezi kwa kuwekwa kwenye vitu vya thamani ya juu. Wakati vikiwa vikavu majimaji hayo hayaonekani kwa macho , lakini hung'aa rangi ya manjano ikiwa itamulikwa na taa za ultra violet na kurunzi ambazo hutumiwa na polisi.
Ikiwa vitu vya thamani vitaibiwa na baadaye kurejeshwa, mmiliki wake wa asili anaweza kupatikana baada ya uchunguzi wa maabara wa sampuli.
Teknolojia hiyo tayari imepewa sifa ya kupunguza nusu ya wizi wa kubadilisha fedha, kulingana na Baraza la Wakuu wa Kitaifa wa Polisi.
Lakini matumizi ya teknolojia ya kusaidia kukabiliana na unyanyasaji wa nyumbani ni mpya.
Mwanaume huyo kutoka Wakefield, West Yorkshire, alikuwa akimsumbua mpenzi wake wa zamani na kukiuka amri ya kutomnyanyasa ambayo ilitamka kwamba lazima amwache peke yake. Alipojitokeza na kujaribu kuingia ndani ya nyumba, alinyunyiza majimaji hayo kutoka kwenye mkebe kwenye dirisha lake.
SmartWater ilisaidia maafisa kumkamata mtu huyo, kwani ilimweka kwenye eneo la uhalifu.
Alifungwa kwa wiki 24 na kupewa amri ya zuio la miaka miwili.

Rachael Oakley, mkurugenzi wa kitengo cha kijasusi cha SmartWater, anasema kwamba hakuna jambo la shaka linapokuja suala la kutumia alama za kiuchunguzi, tofauti na vizuizi vingine, kama vile CCTV.
"SmartWater inaundwa na mchanganyiko wa viambata adimu ambavyo haviwezi kupatikana kwa asili popote pengine duniani. Kila chupa ina kiasi tofauti cha chembe hizo ndani yake na kila bachi ni ya kipekee.














