Waridi wa BBC: Sikuweza kula wala kunywachochote katika siku tatu nilizobakwa

Cecilia

Chanzo cha picha, Cecilia

Maelezo ya picha, Masaibu aliyoyapitia Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba, yamemhamasisha kuwasaidia wanawake wenzake waliopitia matatizo aliyopitia
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Kubakwa ni tukio ambalo Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba, hatawahi kulisahau maishani mwake. Lakini tukio hili ambalo alilipitia utotoni limeacha kovu moyoni mwake, lakini bila shaka halikumkatisha tamaa ya kusonga mbele na maisha na kuwasaidia wengine waliopitia masaibu kama yake.

Akiwa na umri wa miaka 17, usiku mmoja kama ilivyokuwa kawaida, mama yake Cecilia alimtuma kwenda dukani kununua sukari na bidhaa nyingine za matumizi ya nyumbani.

Cecilia anasema duka hilo la 'Kioski'' halikuwa mbali sana na nyumbani kwao, kwa hiyo ilikuwa rahisi kwake kwenda na kurudi nyumbani mara moja.

Hatahivyo kadri alivyokuwa akisonga mbele kuelekea dukani aligundua nyuma yake kulikuwa na wanaume wawili wanaomfuata nyuma.

Cecilia

Chanzo cha picha, Cecilia

"Nilipokuwa natembea niligundua kwamba kuna watu waliokuwa wananifuata, lakini sikujali… Nilipofika dukani na kununua bidhaa nilizotumwa, ghafla nilimuona mwanamume mmoja aliyekuwa jirani yetu wakati huo , aliniuliza, wewe!, ni wapi unapeleka hiyo sukari?... na kabla sijamjibu ghafla aliniziba mdomo na kunielekeza kwa nguvu hadi nyumbani kwake,karibu kabisa na nyumbani kwetu, " anakumbuka Cecilia.

Kulingana naye mtu aliyemteka nyara alikuwa kijana aliyemfahamu vyema, kwani walikuwa majirani.

Baada ya kumuingiza ndani ya nyumba yake kilichofuata ni machungu na masaibu ambayo kamwe hatawahi kuyasahau, aliniambia Cecilia.

"Ghafla yule mtu alianza kunibaka… wakati huo mimi nilikuwa bikra, hilo halikumbabaisha licha ya kelele na kilio nilichokuwa nacho. Aliendelea na unyama huo kwa siku tatu, huku maumivu yakiendelea kunizonga. Sikuweza kula wala kunywa chochote katika siku tatu nilizobakwa.Yule mwanamume alikuwa ananifungia ndani ya nyumba kuondoka na kurudi kila wakati na kuendeleza machafu hayo", anakumbuka Cecilia.

Kuokolewa ndani ya nyumba ya mbakaji

Bi Cecilia anasema siku ya nne ndani ya nyumba ya mbakaji, ndipo alipoweza kuokolewa dhidi ya adha ya kubakwa.

Cecilia

Chanzo cha picha, Cecilia

''Niliwasikia watu wakiongea nje ya nyumba niliyokuwa nimefungiwa, na kwa bahati aliyekuwa ameniteka hakuwepo…nilipiga mayowe ambayo yaliwafanya watu waliokuwa nje ya nyumba kusogelea nyumba ile, na wakanisaidia kuniondoa mle ndani'', anasema Bi Cecilia na kuongeza kuwa:

"Wale akinamama walikuwa wanapalilia nje ya nyumba nilimokuwa nimefungiwa walisikia mayowe yangu, wakakimbia na kumuita mama yake na kijana aliyenibaka na ambaye alikuwa ndiye mwenye nyumba ili anifungulie mlango, kwa kuwa mwanae alikuwa ameondoka na ufunguo…Alikuja na aliponifungulia nilimueleza kile kilichojiri kwa siku tatu. Alinishauri nirudi nyumbani kwani ilikuwa masaa ya jioni, na kwamba angewajibika katika kuhakikisha kuwa nimepata matibabu kwani nilikuwa nahisi nimeumizwa sehemu zangu za siri", anasema Cecilia.

Masaibu hayakuishia hapo

Ndoto ya kufika nyumbani kwao baada ya kutekwa na kubakwa na jirahi yake haikutimia kwa Cecilia usiku ule. Alipokuwa akielekea kwao huku akiwa ameshikiliwa kutokana na maumivu aliyokuwa nayo, njiani alikutana na polisi waliokuwa wanafanya doria ambao walimkamata kwa madai ya uzururaji ovyo usiku, ili hali yeye ni mwanafunzi ."anakumbuka Cecilia.

Tetesi za kuwa Cecilia alilala kituo cha polisi baada ya kupotea kwa siku kadhaa zilimfikia baba yake mzazi, na ndipo alipoamua kwenda katika kituo cha polisi. Cecilia anasema hapo ndipo ilikuwa mara ya kwanza baba yake kufahamishwa kwamba mwanae alikuwa amebakwa.

Juhudi za kupatanisha familia

Mama yake kijana aliyembaka na kumteka nyara alikubali kugharamia garama za matibabu hospitalini na garama nyingine. Wakati huo Cecilia anasema alikuwa mdogo sana kwahivyo hakuelewa chochote kuhusu kutafuta haki kama msichana aliyebakwa.

Siku aliyotoka kituo cha polisi, na kuwasili nyumbani kwao, Cecilia na baba yaka walimkuta mama yake akiwa na ghadhabu: ''Ni kana kwamba mama hakuamini ''nilikuwa nimetekwa na kubakwa na jirani yetu…hakuamini kwamba nilitekwa nyara aliponituma dukani kununua sukari… alidhani nilitoroka mwenyewe kama kawaida ya wasichana wa rika langu, ila aliamini alipoziona nguo nilizokuwa nimevaa zina madoa ya damu ", Cecilia anakumbuka.

Cecilia alipelekwa hospitalini kupata matibabu ambapo alifanyiwa uchunguzi wa damu na magonjwa mengine, lakini anasema kwamba uchunguzi wa iwapo alikuwa amepata ujauzito au la haukufanywa.

"Nilifanyiwa uchunguzi na vipimo mbali mbali, na kupewa madawa ya kuzuia maambukizi ya HIV, hii ilikuwa kama njia ya kuziba pengo la uwezekano wa kupata virusi hivyo iwapo aliyenifanyia kitendo kile alikuwa na ugonjwa, na vile vile madawa ya kuzuia maumivu makubwa niliyokuwa nayo sehemu ya chini ya tumbo langu", anaeleza Bi Cecilia.

Baada ya matibabu, familia ilikubaliana kwamba Cecilia asirejeshwe shuleni kwanza, na badala yake apelekwe kwa bibi (nyanya) yake, katika hali ya kumtuliza kimawazo na kiakili. Alipelekwa na huko alianza maisha ya kuishi na bibi huku akiendelea kutokwa damu: ''Bibi yangu alikuwa anadhani kuwa nilikuwa na hedhi ya kawaida, kwa hiyo hakufikiria kwamba kuna uwezekano wowote wa mimi kuwa na ujauzito'', anakumbuka Bi Cecilia.

"Baada ya ubakaji, sikuwa najielewa kwani hisia zangu zilikuwa ni mchanganyiko, hakuna mtu aliyeniketisha chini angalau kunipa nasaha au pole , baba yangu alijaribu sana kusimama na mimi katika kipindi kile , alikuwa kila wakati ananisihi kwamba hayo yote yatapita , na kunipa nguvu , kando na yeye wengi walionizunguka waliniangalia tu "anakumbuka Cecilia.

Mzozo wa mimba ndani ya familia

Baada ya mwezi mmoja wazazi wa Cecilia walikubaliana kwamba arejeshwe shuleni, huku baba yake akitilia msisitizo umuhimu wa yeye kurudi shuleni. Lakini mama yake alikuwa na maoni kwamba Cecilia aozwe kwa kijana aliyembaka, kwani familia ya kijana huyo walikuwa tayari aolewe na mtoto wao.

"Baba yangu alikataa kupokea mahari kutoka jamii mtu aliyenibaka , alisisitiza kwamba nirejeshwe shuleni. Kweli nilirejeshwa shuleni , lakini haikuchukua muda… ikagundulika kwamba nina ujauzito, nilikaa shuleni kwa kipindi cha miezi miwili pekee na kufukuzwa.Niliporudi nyumbani nilihisi kana kwamba mama yangu alikuwa na aibu ya mimba yangu, kwani nilikuwa bado nina umri wa miaka 17. Nilijaribu kumuelewa lakini pia nilikuwa najiuliza mbona baba ananielewa na mama hanielewi?" Cecilia anakumbuka akijiuliza.

Mvutano kati ya wazazi uliibuka ndani ya familia anasema Cecilia, na kuongeza kuwa '' Mama yangu na mama yake kijana aliyenibaka walisisitiza niolewe na kijana yule na tayari kijana mwenyewe aliyehusika na hali hii tangu aliponibaka alikuwa anashinikiza kwamba mtoto azaliwe kwao. Lakini baba yangu alisistiza kwamba siwezi kuolewa, kwanza kijana muhusika alikuwa haonekani alikuwa amekwepa , ni mama yake tu aliyekuwa anashugulika na mimi , kwa hiyo baba aliuliza ….sasa unataka kumchukia binti yangu kwa kijana ambaye hapatikani? sasa ataishi pekee yake huko ?" Cecilia anakumbuka hali hiyo anayosema ilimchanganya kimawazo zaidi.

Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba sasa ni mhungaji wa Kanisani nchini Uganda

Chanzo cha picha, Cecilia

Maelezo ya picha, Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba aliamua kuingia katika fani ya kuhubiri na kujishugulisha na masuala mengine ya kidini.

Kufuatia malumbano hayo ya kifamilia, baba yake Cecilia alimua kwamba ataendelea kuishi nyumbani kwao, ajifungue na akamuahidi kuwa baada ya kujifungua atamrejesha shuleni kuendelea na masomo. Baada ya muda wa miezi 9 hatimaye nalijifungua mtoto wa kike na baada ya hapo baba yake alianza kuugua. ''Hapo ndipo ndoto yagu ya kureshea shuleni ilipofifia'', anasema Cecilia

'Njama iliyobadili maisha'

Mtoto wa Cecilia alipofika umri wa miezi 7, maamuzi yaliyobadilisha mkondo wa maisha yake yalichukulia kumhusu bila yeye kujua.

Njama ilipangwa na kutekelezwa ya kumuoza kwa mzee mmoja aliyekuwa anaishi mbali na kwao, ambaye hakuwa kwenye ndoa ila alikuwa na watoto.

Njama hii ilipagwa na watu wa karibu wa familia kwa ushirikiano na jirani mwanamke aliyemsafirisha hadi nyumbani kwa mzee huyo. Alipowasili alipokelewa vizuri, lakini aligundua kwamba boma lile alikopelekwa halikuwa na mama mwenye nyumba au mke , pia watoto wa yule mzee walikuwa wanamuita mama, na hapo hapondipo alipogundua kwamba yeye ndiye alikuwa awe mama wa nyuma.

Cecilia anasema kuwa yeye na mwanaume aliyemuoa walipishana miaka takriban 17 kwa umri.

Majukumu ya ndoa ya mapema hayakuwa rahisi kutokana na tofauti ya umri wake na pia malezi yake ndoa ilikuwa na changamoto nyingi.

Hatahivyo anasema aliamua kupiga moyo konde na kukubali kwamba ameanza maisha ya ndoa japo alikuwa bado mdogo sana.

"Japo nilikuwa tayari mzazi , sikuwa na maarifa yeyote ya ndoa , sikuwa na ufahamu wowote wa jinsi ya kumtunza mume hasa mwanamume kama yule ambaye alikuwa ni mtu mzima. Nakumbuka akinifokea kana kwamba alihisi sikuwa na hekima ya kutosha ya kuwa mke ."anasema Cecilia.

Licha ya hayo alijizatiti kuwalea watoto wa mume wake aliowapata katika nyumba ile pamoja na wale aliojaaliwa akiwa kwenye ndoa ile.

Cecilia anasema maisha hayakuwa mepesi kwake, kwani mwaka mmoja baada ya mwengine alikuwa haoni mwanga katika ndoa ile, hasa kwa kuwa hakuwa na uhusiano wa karibu na baba wa watoto wake wakati huo.Maisha yake yalizungukia tu kuwa mama nyumbani na hakuwa na fursa ya kujieleza kwa uhuru.

Cecilia

Chanzo cha picha, Cecilia

Mwanadada huyu anasema kuwa aliishi kwenye ndoa hiyo kwa takriban miaka 17, na baada ya hapo alianza kuhisi kuwa amevumilia vya kutosha kuishi katika ndoa ambayo hakuielewa vyema.

Malumbano ya joni mmoja kati yake na mumewe yalimfanya ajipate ametupwa nje ya nyumba ile bila chochote na kuanzia hapo alianza maisha mapya bila ndoa tena.

"Nakumbuka kwamba kilichonitenganisha mimi na yule mtu , ni kwamba aliingia nyumbani akiwa na hasira…alikuwa ananitishia , kilikuwa kisa kilichonitetemesha sana…binti yangu aliposikia kelele kutoka chumbani alikuja kwa haraka na kunisaidia kutoka mikononi mwa aliyekuwa mume wangu ambaye alikuwa akinipiga. Nilitoroka na sikurejea tena katika nyumba ile ."anasema Cecilia.

Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba akiwa na mume wake wa sasa Mganda, Ssewagaba katika siku yao ya harusi

Chanzo cha picha, Cecilia

Maelezo ya picha, Mchungaji Cecilia Muthoni Ssewagaba akiwa na mume wake wa sasa Mganda, Ssewagaba katika siku yao ya harusi

Baada ya ndoa hiyo la lazima, Cecilia alianza maisha taratibu kwa kufanya biashara ndogo ndogo na kufanikiwa kujikimu kimaisha. Baadaye aliingia katika fani ya kuhubiri na kujishugulisha na masuala mengine ya kidini.

''Ndoa ya pili''

Katika pilikapilika za kufanya biashara kati ya Kenya na Uganda, siku moja akiwa mjini Kampala Cecilia alikutana na mwanamume mmoja ambaye walianza urafiki ambao ulikua na kufikia kiwango cha mapenzi na hatimaye baada ya mwaka mmoja wawili hao wakaamua walifunga ndoa na mumewe mwenye asili ya Uganda -Bwana Ssewagaba.

Mume wake huyu wa pili alikubali kumuoa na pia kuwaasili watoto wa Cecilia watatu.

"Mimi ni shahidi kwamba kuna mapenzi ya dhati , tangu wakati ninapitia ubakaji na pia kukaa kwenye ndoa ambayo sikupendwa, ndani yangu nilihisi kana kwamba bado mume wangu angali ananisubiri. Matukio ya kukutana na barafu wangu wa moyo ni matukio ya ajabu ambayo ninaweza sema ni ya kiMungu tu", anasisitiza Cecilia, huku akitabasamu.

Kwa sasa Cecilia anashughulika sana katika kufanikisha shirika lake kwa jina Empowerment of traumatized women in Africa, linalohusika zaidi na akinamama ambao wamejipata katika unyanyasaji mbali mbali kama alioupitia Bi Cecilia.

Bi Cecilia pia hutumia shirika hilo kuwahamasisha wanawake kuhusiana na unyanyasaji mbali mbali unaowakumba wasichana na wanawake waliomo katika ndoa. Vile vile husaidia katika utoaji wa ushauri nasaha kwa waathiriwa wa ubakaji, unajisi, sonona na unyanyasaji wa kisaikolojia.