Watoto wa Nepal wanavyotumikishwa kwenye mabaa na maeneo ya burudani

Wanaharakati wanasema mashirika mengi ambayo yanaajiri watoto ni sehemu za biashara ya ngono

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanaharakati wanasema mashirika mengi ambayo yanaajiri watoto ni sehemu za biashara ya ngono

Watoto wananyanyaswa katika baa za Kinepali na kumbi za muziki wa kitamaduni, ambazo baadhi ni sehemu za biashara ya ngono. Kulingana na makadirio mengine, maelfu ya watoto wanaathiriwa. Mwandishi wa BBC Geeta Pandey anaripoti kutoka Delhi.

Wakati Rita alipotoka kijijini kwao na kuhamia mji mkuu wa Nepal, Kathmandu, alidhani anakwepa umasikini.

Huko kijijini, Rita - ambaye jina lake limebadilishwa ili kumlinda -aliishi na mama yake aliyekuwa mraibu wa pombe na ndugu zake. Baba yake alikuwa amehamia Malaysia kufanya kazi japo alishia kuitelekeza familia.

"Awali alikuwa akitutumia pesa, lakini baadaye akaacha kufanya hivyo," Rita alisema. "Hatukuwa na ardhi ya kutosha, kwa hivyo ilinibidi nije Kathmandu nikiwa na umri wa miaka 12 au 13."

Kazi yake ya kwanza mjini Kathmandu ilikuwa ni pamoja na kufanya kazi katika kiwanda cha matofali, kufua na kuosha vyombo katika hoteli na kusaidia kuuza bidhaa dukani.

Malipo yalikwa kidogo ukilinganisha na kiwango cha kazi na wakati mwingine akikabiliwa na unyanyasaji kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa kiume waliojaribu kumshika na kumpapasa, alisema.

Akiwa na miaka 14, Rita alipata kazi katika mgahawa ambapo alitakiwa kukaa, kula na kunywa na wateja.

"Wateja walikuwa wakivuta sigara na kunywa pombe," anakumbuka. "Wangenishika mikono yangu, kusema maneno machafu, lakini sikuweza kupinga. Baadhi yao hata walitaka kunibusu. Nilikuwa natoroka nikisema nilitaka kwenda msalani."

Akisimulia hadithi yake na wanaharakati wa Mpango wa Utafiti wa Ajira kwa Watoto (Clarissa), unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza, Rita alitoa maelezo ya kina kuhusu matukio ambapo alilazimishwa kunywa pombe na ambapo wanaume walimpeleka kwenye nyumba za wageni zilizo karibu au vyumba vya kukodi na kumpa pesa kama malipo ya kufanya ngono naye.

Wanaharakati wanasema Rita ni mmoja wa mamia, ikiwezekana maelfu, ya watoto wa Nepali, wengine wakiwa na umri wa miaka 11, ambao wamenaswa katika sekta ya burudani ya watu wazima nchini humo, wanaojihusisha naaina mbaya ya ajira ya watoto.

Profesa Danny Burns, mkurugenzi wa Clarissa na profesa katika Taasisi ya Mafunzo ya Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Sussex, anasema tunapozungumzia ajira ya watoto, mijadala mingi inalenga makampuni makubwa na mitandao inayotoa huduma hiyo duniani.

"Lakini aina mbaya zaidi za ajira ya watoto inapatikana katika biashara ndogo ndogo na biashara zinazomilikiwa na familia - ambazp zinaajiri watoto kama Rita," Prof Burns aliambia BBC.

Baadhi ya wasichana na wanawake vijana wanaofanya kazi katika viungo hivi wanasema wamejikuta katika hali ya unyonyaji

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya wasichana na wanawake vijana wanaofanya kazi katika viungo hivi wanasema wamejikuta katika hali ya unyonyaji

Nepal ina watoto milioni 1.1 wenye umri wa kati ya miaka mitano na 17 wanaotumikishwa kwa watoto na watoto milioni 0.22 wanafanya kazi katika viwanda hatari, ingawa kuajiri watoto ni kinyume cha sheria nchini humo.

Kathmandu ameahidi kutokomeza utumikishwaji wa watoto ifikapo mwaka 2025 kuambatana na lengo la Umoja wa Mataifa la kukomesha utumikishwaji wa watoto kwa aina zote na pia kuweka lengo kabambe la kukomesha aina mbaya zaidi za utumikishwaji wa watoto ifikapo mwaka 2022.

Waziri wa Wanawake, Watoto na Wazee Uma Regmi alimwambia Binita Dahal wa idhaa ya BBC Kinepali kwamba "serikali imedhamiria kufikia lengo hilo".

"Tumesalia na muda mchache, lakini tutafanya jitihada zote kukomesha aina mbaya zaidi za utumikishwaji wa watoto ifikapo mwaka 2022," alisema.

Lakini wanaharakati wanasema ili kufikia lengo hilo, Nepal lazima izingatie biashara ndogo ndogo katika sekta isiyo rasmi, hasa sekta ya burudani ya watu wazima.

Pragya Lamsal, mtafiti katika shirika laClarissa huko Kathmandu, aliiambia BBC kwamba shirika la misaada limekusanya na kuchambua shuhuda za karibu watoto 400 walioajiriwa katika sekta hiyo.

"Katika visa vingi, watoto hao walikuwa wamehama kutoka vijijini na kwenda Kathmandu, waliajiriwa na wasuluhishi wasio rasmi kama vile marafiki, jamaa na majirani, na wengi wao waliishia kufanya kazi katika sehemu za kukanda watu, kumbi za burudani, nyumba za wageni na kadhalika," alisema..

Creative image of a young woman putting her hand out

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati wa Covid, watoto walilazimika kufanya chaguzi mbaya sana kwa sababu lilikuwa suala la riziki zao

Sudhir Malla, mkuu wa Clarissa nchini Nepal, alisema watoto wengi walitoka katika familia maskini au nyumba zilizovunjika na kuja katika jiji hilo, wanaajiriwa zaidi na "migahawa ya dohori" - taasisi zinazodai kukuza muziki wa asili.

"Kuna baadhi ya vituo vinavyofanya bishara halali , lakini sehemu zingine nyakat iza usiku zinageuka kuwa maeneo ya biashara ya ngono. Wanaajiri wasichana kufanya kazi ya kuuza pombe, kujumuika na wateja mezani," alisema.

Baadhi ya maeneo hayo yanaendesha biashara haramu, aliongeza - zinafanya kazi kwenye vyumba vya chini, vilivyo kando ya barabara na vyumba vya kibinafsi.

"Kisheria bisahara hizi zinatakiwa kisheria kusajili na kuhuisha hati zao mara kwa mara na kutoa maelezo ya wafanyakazi wao kwa mamlaka. Awali wamiliki wa hujiandikisha lakini baadaye wanabadili mkondo na hakuna wa kuwawajibisha wasipofanya hivyo. Kisha kuna wale ambao hawajajiandikisha kabisa."

Hakuna mikataba rasmi

Kwa hivyo, watoto hufanya kazi bila mikataba rasmi na hawapewi maelezo yoyote ya kazi au mishahara iliyowekwa.

Bi Lamsal alisema wengi wa wasichana na wanawake wachanga wanaofanya kazi katika maeneo haya wanasema wamejikuta katika hali za unyonyaji.

"Wasichana waliambiwa kwamba ikiwa wageni watatumia hela nyingi, bahashshi yao pia ingekuwa vya juu," alisema. "Wengi wao ni vijana na hawana elimu ya msingi, katika hali nyingi, hawana chaguo kwa sababu familia zao zinategemea pesa wanazopata. Wako hatarini sana na wengi wao huingia katika hali ambazo ni za kinyonyaji."

Wasichana pia walilazimika kukabiliana na unyanyapaa unaozunguka aina hii ya kazi," Bi Lamsal alisema. Wengi hata hawaambii wazazi wao, kwa hivyo hata wakinyanyaswa hawawezi kwenda kwa familia zao au polisi ili kupata msaada. pia hawawezi kuripoti unyanyasajidhidi yao kwa sababu ya kuogopa kupoteza kazi.

Na Covid-19 ilifanya hali yao kuwa mbaya zaidi, Bw Malla alisema.

"Wakati wa janga la corona serikali ililazimika kufunga sekta ya burudani, lakini baadhi ya bishara hizo ziliendelezwa kisiri," alisema. "Na watoto walilazimika kufanya maamuzi magumu. Ilikuwa ni suala la riziki zao, walipaswa kulipa kodi ya nyumba, walipaswa kupata chakula, na katika hali ambapo wao ndio walezi, walikuwa na familia zinazowategemea."

Kulingana na Prof Burns, Covid imerudisha nyuma maendeleo, na hakuna nchi iliyo na changamoto kubwa ya ajira ya watoto ambayo iko mbioni kukomesha ifikapo 2025.