Israel imesambaratisha mtandao wa kijasusi wa Iran?

Shirika la Usalama wa Taifa la Israel limemshutumu kamanda wa Iran aliyejitambulisha kwa jina la Namdar kwa kuwaajiri wanawake wa Israel kufanya ujasusi kupitia mtandao wa facebook.

Chanzo cha picha, facebook

Wakati mazungumzo ya kurejeshwa kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran yangali yanaendelea, tishio la vita kati ya Israel na Iran linaendelea, na vita vya kijasusi vinaendelea.

Mazungumzo ya Vienna kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran yalipoanza tena, moja ya mizozo mikuu katika Mashariki ya Kati, uhusiano kati ya Israeli na Iran, maadui wawili wa zamani, bado ulikuwa unasababisha wasiwasi na tishio la mapigano.

Israel imeeleza hadharani hofu yake kuwa mazungumzo ya mjini Vienna kuhusu kurejeshwa kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanaweza kuwa na matokeo mabaya kwa Israel, hivyo jeshi la Israel bado linaweza kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Katika vita hivyo vya giza, Israel hivi karibuni ilitangaza kuwa imeharibu mtandao wa kijasusi wa Iran.

Mnamo 2021, moto katika kituo cha nyuklia cha Natanz nchini Iran ulilemaza kituo hicho kwa miezi kadhaa. Vyombo vya habari vya Israel baadaye viliripoti kwamba idara ya ujasusi ya Israel ilikuwa imeajiri wanasayansi kadhaa wa Iran kabla ya shambulio hilo, kwa msaada wao kutekeleza shambulio hilo.

Mnamo Novemba 2021, Israel ilimshtaki mfanyakazi aliyeajiriwa katika makazi ya Waziri wa Ulinzi Benny Gantz kwa ujasusi na kumshutumu mtu huyo kwa kufanya kazi na "watu wanaohusishwa na Iran."

Lakini mnamo Januari 2019, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Israel ilitangaza kwamba waziri wa zamani wa Israel Gonen Segev alikiri kufanya ujasusi kwa Iran. Segev aliwahi kuwa waziri wa nishati wa Israel katika miaka ya 1990.

Mwanzoni mwa mwaka mpya wa 2022, wakati mazungumzo ya kuanza tena makubaliano ya nyuklia ya Iran yakiendelea, mashirika ya usalama ya ndani ya Israel yaliwakamata Waisraeli watano wanaotuhumiwa kuifanyia Iran ujasusi.

Kesi hiyo ilihusisha wanawake wanne wa Kiyahudi wenye asili ya Iran ambao waliajiriwa na mkufunzi wa kiume Myahudi aliyedai kuwa anaishi Iran, kwa mujibu wa Shirika la Usalama wa Taifa la Israel, Shin Bet.

Wanawake hao inadaiwa walipewa maelfu ya dola kupiga picha za tovuti nyeti, kufuatilia mipangilio ya usalama na kuanzisha uhusiano na wanasiasa.

Lakini mawakili wa wanawake hao walisema hawakujua mtu huyo alikuwa wakala wa Iran. Wanasheria pia wanasisitiza kuwa hawana nia ya kuhatarisha usalama wa Israel.

Lakini Shin Bet alisema ni kesi mbaya inayohusisha mpango wa kujenga mtandao wa kijasusi wa Iran ndani ya Israel na wanawake hao watakabiliwa na mashtaka mazito.

''Kuajiri kupitia mtandao wa Facebook''

Mkufunzi huyo raia wa Iran, aliyejitambulisha kwa jina la Rambod Namdar, anadaiwa kuwasiliana na wanawake hao kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na kisha kuendelea kuwasiliana nao kwa miaka kadhaa kupitia huduma ya utumaji ujumbe kwa njia ya kificho ya WhatsApp.

Shinbet anadai kuwa wakati wanawake hao wakimshuku mwanaume huyo kuwa afisa wa ujasusi wa Iran, baadhi yao waliendelea kuwasiliana naye, walikubali kufanya kazi mbalimbali alizowataka wafanye, na kupokea fedha kutoka kwake.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 40 kutoka kitongoji cha Tel Aviv cha Holon alikubali kupiga picha za ubalozi wa Marekani ukiwa bado mjini humo, pamoja na jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani na Masuala ya Kijamii ya Israel na kituo cha biashara. kwa mujibu wa shirika hilo.

Unaweza pia kusoma

Kamanda huyo pia alimtaka mwanamke huyo amruhusu mwanawe ajiunge na huduma ya kijasusi ya kijeshi ya Israeli wakati wa utumishi wa lazima wa kijeshi, ilisema taarifa hiyo.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 57 kutoka mji wa Israel wa Beit Shemesh anadaiwa kumhimiza mwanawe kujiunga na huduma ya kijasusi ya kijeshi na kupitisha nyaraka za siri za kijeshi.

Kulingana na Shin Bet, mwanamke huyo aliagizwa kuanzisha klabu kwa ajili ya Wairani-Waisraeli kukusanya taarifa zao za binafsi na kujaribu kuwa na urafiki wa karibu na mwanachama wa kike wa Bunge la Israel, Knesset.

Kurejeshwa kwa mazungumzo mjini Vienna kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran kunakuja huku Israel ikitishia kushambulia vituo vya Iran

Chanzo cha picha, EPA

''Mapambano yanayoendelea''

Pia inasemekana aliweka kamera iliyofichwa kwenye chumba cha kufanyia masaji nyumbani kwake, inaonekana katika jaribio la kukusanya picha zinazoweza kuwaaibisha wateja wake.

Waziri Mkuu wa Israel, Bennett alisema taifa la Israel liko katika mapambano yanayoendelea na Iran. Ni wazi: tunaona kwamba Wanajeshi wa Iran hawajawahi kuacha kuajiri raia wa Israel kwa shughuli za ujasusi.

Ameongeza kuwa, majaribio hayo ya Iran yamevuka mipaka ya usalama na kijasusi, na kwamba Wairani wanazidisha juhudi zao za kuwashawishi raia wa Israel na jamii ya Israel, na hivyo kupanda mbegu za mifarakano na migawanyiko, kudhoofisha uthabiti wa kisiasa wa Israel na kudhoofisha fikra za Umma kuhusu taifa hilo.