Wanafunzi ambao ni wapenzi wa jinsia moja Kenya kuzuiwa kwenda shule za mabweni-Waziri wa elimu

Chanzo cha picha, EduMinKenya/TWITTER
Waziri wa elimu nchini Kenya George Magoha anasema wanafunzi wote ambao ni wapenzi wa jinsia moja wanapaswa kuzuiwa kuhudhuria shule za bweni ili wasiwashawishi wanafunzi wengine.
Badala yake alisema wanapaswa kuhudhuria shule za kutwa karibu na makazi yao. Wale ambao tayari wako katika shule za bweni wanapaswa kuhamishwa aliongeza.
Aliwataka walimu wakuu kuchukua hatua kwa manufaa ya wengi kuliko watu wachache.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu tayari yamesema yatapinga mahakamani, utekelezaji wa agizo hilo ambalo wanasema linazuia haki za wanafunzi.
Mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya yanaweza kuadhibiwa kwa hadi miaka 14 jela - pingamizi kwa sheria hii ilikataliwa mwaka wa 2019.
Bw Magoha pia ameunga mkono wito wa kuwa na vipimo vya lazima vya dawa za kulevya kwa wanafunzi shule zitakapofunguliwa mwaka mpya akisema itasaidia kupunguza visa vya utumizi wa dawa za kulevya, ambao alitaja kuwa umekithiri kote nchini.
Kauli zake zinakuja kufuatia wimbi la hivi majuzi la uchomaji moto wa mabweni na madarasa ya shule mwezi uliopita ambapo taasisi kadhaa zilifungwa kwa muda kabla ya muhula kukamilika.
Maoni hayo yamezua hisia kali miongoni mwa Wakenya ambao wanamshutumu waziri kwa kutoa maoni ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wa LGBT.
Waziri huyo anayefahamika kwa kauli zake kali sio mgeni katika mabishano na ameleta mabadiliko kadhaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mtaala mpya wenye utata ambao ulibadilisha kabisa sekta ya elimu nchini Kenya












