Omicron: Je, utajuaje kwamba umeambukizwa virusi vya Omicron

Chanzo cha picha, Getty Images
Visa vya kwanza vya virusi vya corona aina ya Omicron sasa vimegunduliwa kote ulimwenguni, baada ya kuangaziwa na wanasayansi nchini Afrika Kusini kama aina mpya inayoweza kutia wasiwasi.
Tayari imesambaa katika makumi ya nchi, baadhi zikiwa zimeweka marufuku ya usafiri kujaribu kujitenga
Ni vipimo gani vinavyotumika kugundua Omicron?
Vipimo vya PCR- hufanywa kupitia pua na mdomo, sana sana hutumika kubaini ikiwa watu wameambukizwa virusi vya Corona au la.
Kulingana na maabara ambayo vipimo vinapelekwa kwa uchunguzi, baadhi zinaweza kugundua aina fulani ya virusi kama, Delta au Omicron.
Ni baadhi ya maabara tu zinamiliki teknolojia inayohitjika kufanya vipimo hivi.
Marekani inaongoza duniani kwa vipimo vya PCR, ikifuatiwa na Uingereza, Urusi, Ujerumani na Korea Kusini kama nchi zilizo na viwango vya juu vya upimaji.
Nchini India, hata hivyo ni asilimia moja tu ya sampuli zinazotumwa kwenye maabara zinaweza kupimwa ili kugundua aina ya virusi vya Delta au Omicron.

Tunajuaje kwamba Omicron imeenea duniani kote?
Sampuli kutoka kwa vipimo vya PCR ambazo zimepatikana na maambukizi ya kile kinachoonekana kuwa kuwa Omicron zimetumwa kwenye maabara kufanyiwa uchambuzi kamili wa maumbile, kutumia mbinu inayojulikana kama genomic sequencing(mpangilio wa genomic).
Hii imethibitisha kuwa baadhi ya watu wameambukizwa aina hii mpya ya corona.
Uchambuzi huu wa kimaabara wa nyenzo za kijeni za virusi ni muhimu katika kugundua kirusi hiki kipya na kujua mienendo yake.
Visa vingi vya maambukizi ya Omicron havitambuliki kwa sababu inaweza kuchukua wiki kadhaa kabla mchakato huu kukamilika.
Watu 77 wamethibitishwa kuambukizwa corona aina ya Omicron katika Mkoa wa Gauteng nchini Afrika Kusini, ambayo inaweza kufikisha hadi asilimia 90 ya maambukizo yote mapya.
Inaonekana imeenea hasa Ulaya. Ureno na Uholanzi zimeripoti visa 13 (kila moja) vya maambukizi yaliyothibitishwa na Uingereza visa 14.
Hata hivyo, takwimu hizi huenda zisionyeshe ni nchi zipi zilizo na maambukizi mengi zaidi ya corona aina ya Omicron, lakini ni nchi zipi zimegundua hivi karibuni.
Dalili za Omicron ni zipi?
Shirika la Afya Duniani linasema hakuna habari inayoonyesha kuwa dalili za Omicron ni tofauti na zile za aina nyingine - kwa hivyo kikohozi kipya, homa na kupoteza ladha au harufu bado ni dalili za kuzingatia.
Watu waliopewa chanjo kamili nchini Afrika Kusini wameambukizwa Corona ya Omicron lakini dalili zao ni nyepesi.
Hospitali nchini Afrika Kusini zinapokea vijana wengi zaidi ambao wamelazwa wakiwa na dalili mbaya zaidi - lakini wengi hawajachanjwa au wamepewa dozi moja pekee.
Hii inaashiria kuwa kupata dozi mbili na dozi ya nyongeza ni njia nzuri ya kujilinda dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na aina mpya ya kirusi cha corona.
Kuna tofauti gani kati ya Omicron na aina zingine?
Omicron ina mabadiliko mengi tofauti ambayo hayajaonekana hapo awali, na mengine mengi ambayo yameonekana.
Katika majaribio ya kawaida, Omicron ina kile kinachojulikana kama "S-gene dropout" ambayo hurahisisha kufuatilia matukio chanya ambayo yanafanana na kirusi.
Lakini sio "S-gene dropout" zote zitakuwa Omicron - mpangilio kamili wa genomic unahitajika ili kuwa na uhakika.
Je, mpangilio wa genomic una jukumu gani?
Kuchambua muundo wa kijeni wa virusi ni sehemu muhimu ya kufanya kazi jinsi kirusi kinavyohusika.
Kwa kuangalia kwa karibu nyenzo za kijeni zinazotolewa, wanasayansi wanaweza kuthibitisha kama mtu ana kirusi cha Omicron au Delta ambacho tayari kinazunguka kwa wingi.
Mchakato huu hutoa tu habari kuhusu sampuli ambazo zinachambuliwa - lakini kwa kutumia matokeo hayo, wanasayansi wanaweza kukadiria ni sehemu gani ya kesi mpya inaweza kuwa aina mpya.
Wanasayansi nchini Uingereza na Afrika Kusini wako mstari wa mbele katika teknolojia hii, ndiyo maana anuwai nyingi mpya zimegunduliwa katika nchi hizi. Lakini hiyo haimaanishi kuwa walianzia hapo.
Tunajua nini kuhusu Omicron?
Kidogo sana kinachojulikana kuhusu jinsi kirusi hiki kinavyofanya kazi au ni kiasi gani cha tishio kinaweza kuwa.
Kwa mfano, haijulikani ikiwa kinasambaa kwa urahisi zaidi, ikiwa inawafanya watu wadhoofike zaidi kuliko virusi vingine au ikiwa ulinzi dhidi ya chanjo utakuwa mdogo kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.
Lakini kwenye karatasi inaonekana kuwa na wasiwasi na ndio maana serikali zinachukua hatua haraka, isije ikwa habari mbaya.













