Nagaenthran Dharmalingam: Familia yaomba miujiza mwana wao mwenye akili punguani anapoelekea kunyongwa

Chanzo cha picha, Sarmila Dharmalingam
Sarmila Dharmalingam inaomba miujiza. Ndugu yake, Nagaenthran Dharmalingam, anatarajiwa kunyongwa katika gereza la Changi nchini Singapore. Ikiwa itafanyika, itakua hukumu ya kwanza ya kifo kutekelezwa tangu mwaka 2019.
"Nikiwa peke yangu namfikiria ndugu yangu, nahisi uchungu. Lakini [tunahitaji] kuwa na ujasiri na kuendelea kuomba - chochote kinaweza kutokea," aliambia BBC.
Nagaenthran atanyongwa Jumatano asubuhi, lakini alipewa muda wa dakika ya mwisho wa kusitisha kunyongwa kwa siku moja. Mahakama ya rufaa itaamua hatima yake siku ya Jumanne.
Mwaka 2009, Nagaenthran ambaye wakati huo alikua na miaka 21 alipatikana akijaribu kuingiza dawa ya kulevya aina ya heroin nchini Singapore kutoka Malaysia.
Raia huyo wa Malaysia alihukumiwa kifo licha ya uchunguzi wa kimatibabu uliofanywa na wataalamu kubaini kuwa kuwa ana IQ ya 69 - kiwango kinachoashiria kkuwa ulemavu wa akili.
Lakini serikali ya Singapore ilisema aligundulika kuwa "alielewa kwa uwazi asili ya vitendo vyake na hakupoteza hisia zake za uamuzi wa haki au ubaya wa kile alichokuwa akifanya".
Singapore ni moja ya nchi iliyo na sheria kali dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya duniani, na utumiaji wa hukumu ya kifo kwa kiwango kikubwa hauna utata. Lakini kesi hii imesababisha minung'uniko isiyo ya kawaida katika taifa hilo la kisiwani.
Mchanganyiko wa hasia
Zaidi ya watu 60,000 wametia Saini ombi la kutoa wito kwa rais wa Singapore kumsamehe Nagaenthran, zikisema kumuua mtu mwenye matatizo ya kunazuiliwa chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
"Inavunja moyo sana kuona mtu mwenye mlemavu wa akili anaadhibiwa kwa uhalifu usio na vurugu," alisema mtu mmoja aliyetia saini ombi hilo. "Si yeye wala familia yake wanastahili maumivu haya. Tafadhali muokoe."
Vuguvugu hilo pia limepata umaarufu kwenye mtandao wa kijamii, ambako kuna mmiminiko usio wa kawaida wa hasira na huruma.
Sarmila anasema anasema haeleweki kama Nagaenthran mwenyewe anaelewa jinsi hali yake ilivyo mbaya.
"Wakati mwingine ananipigia simu kuniambia kuwa atanyongwa na kwamba anahitaji kijiandaa," aliambia BBC.
"[Wakati mwingine] anasema kuwa anataka kuja nyumba kula chakula. Sijui kama anajua au hajui [kile kitakachotokea]."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mjadala wa ulemavu wa akili
Mwaka 2009, Nagaenthran alipatikana akivuka mpaka kuingia Singapore kutoka Malaysia akiwa na gramu 43 (1.5oz) za heroin iliyofungwa katika paja lake la kushoto.
Kwa mujibu wa sheria za Singapore, wale watakaopatikana na zaidi ya ghamu 15 za heroin watakabiliwa na adhabu ya kifo.
Wakati wa kesi yake, awali alisema alishurutishwa kubeba dawa za kulevya, lakini baadaye akasema alifanya kosa hilo kwa sababu alikuwa anahitaji pesa.
Mahakama ilisema utetezi wake wa awali ulikuwa "wa kubuni". Hatimaye alihukumiwa kifo kwa kunyongwa.
Mwishowe, mahakama iligundua kuwa hakuwa na ulemavu wa akili. Shinikizo la mwisho la kuachiliwa kwa rais pia lilikataliwa mwaka jana.

Chanzo cha picha, Sarmila Dharmalingam
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki kama vile Amnesty International na Human Rights Watch yamelaani hukumu hiyo.
"Kutoa watu uhai kwenyewe ni kitendo cha kikatili lakini kumnyonga mtu aliyepatikana na hatia ya kubeba dawa za kulevya, huku kukiwa na ushuhuda wa kutisha kwamba huenda haelewi kinachomkabili, ni jambo la kuchukiza," alisema Rachel Chhoa-Howard, mtafiti wa shirika la Amnesty International nchini Singapore. .
'Sikuweza kumtazama usoni'
Kesi hiyo pia imezua ghadhabu nchini Malaysia anakotokea Nagaenthran ambako maandamano yamefanywa kushinikiza kusitishwa kwa hukumu dhidi yake.
Waziri Mkuu wa Malaysia Ismail Sabri Yaakob pia ametoa wito binafsi kwa mwenzake wa Singapore.
Miaka 10 baada ya hukumu ya kifo, Sarmila alipokea barua kutoka kwa idara ya Magereza nchini Singapore ikisema kwamba hukumu ya Nagaenthran ilikuwa imepangwa kutekelezwa Novemba 10.
"Sikuweza kustahamili... Nilikua nikilia. Nililia siku nzima. Nilihofia kumwambia mama yangu kwa sababu anakabiliwa na changamoto kadhaa za kiafya. Singeliweza kumtazama usoni."
Familia ilipewa karibu wiki mbili kupanga safiri, karantini ya hoteli na kufanyiwa vipimo vya Covid walivyohitaji kabla ya kuruhusiwa kuingia Singapore. Wanaharakati waliangazia changamoto za ziada za kusafiri wakati wa janga la corona.
"[Familia inabidi] itoe maelezo ya afya, kupata bima ya usafiri, kutafuta makao yao wenyewe [miongoni mwa mengine]... [na] wanatarajiwa kusimamia gharama hizo zote," mwanaharakati Kirsten Han, ambaye alianzisha kampeni ya ufadhili wa kuchangisha pesa kwa ajili ya familia hiyo aliambia BBC.
"Hicho ni kiwango cha juu cha fedha kwa familia ya kawaida ya Malaysia, na bado kuna gharama [zingine] za kuzingatia, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa gharama ya mazishi."
Takriban dola 17,000 za kimarekani zilikusanywa kupitia kampeni ya mchango. Sarmila anasema familia haingeweza kusafiri Singapore bila msaada huo.
Familia iliwasili Singapore Ijumaa jioni. Sarmila hakuja Singapore na jamaa zake wengine, kwani anasema mtu alihitaika kusimamia shughuli zingine nyumbani.
Kwa kuwa hawezi kumuona ndugu yake kabla ya muda aliyopangiwa kunyongwa anasema kuwa anamuombea kila siku.














