Mihadarati, silaha, na ugaidi: Mwanajeshi mtoro mkuu wa Korea Kaskazini ya Kim afichua siri

Tabia za zamani ya za usiri hazikumuacha Kim Kuk-song.
Imechukua wiki kadhaa za mazungumzo ili kuweza kupata mahojiano naye, lakini bado anahofu juu ya nani anayeza kuwa anasikiliza.
Huvaa miwani myeusi kwa ajili ya kupigwa picha ya kamera, na ni wawili tu kati ya wapiga picha wetu wanaofahamu ni nini tunachofikiria kuhusu jina lake halisi.
Bw Kim ameishi miaka 30 akitafuta kupata cheo cha juu zaidi cha mashirika ya ujasusi ya Korea Kaskazini.
Mashirika haya yalikuwa "macho, masikio na ubongo wa Kiongozi wa ngazi ya juu ", anasema.
Anadai alitunza siri zao, alitumwa kuwauwa wakosoaji wao, na hata kujenga maabara haramu ya mihadarati kusaidia kuchangisha pesa za ''mageuzi''
Sasa, afisa Kanali wa ngazi ya juu ameamua kuilezea BBC hadithi yake. Ni mara ya kwanza afisa wa aina hii wa kijeshi kutoka Pyongyang amefanya mahojiano na chombo kikuu cha habari.
Bw Kim alikuwa "mwekundu zaidi wa wekundu",anasema katika mahojiano ya kipekee. Mfanyakazi aliyejitolea kuwa mfuasi wa kikomunisti.
Lakini cheo na ufuasi haukupatii hakikisho la usalama wako katika Korea Kaskazini.
Alilazimika kutoroka kuyanusuru maisha yake katika mwaka 2014, tangu wakati huo amekuwa akiishi mjini Seoul na kulifanyia kazi shirika la ujasusi la Korea Kusini.
Anauonyesha uongozi wa Korea Kaskazini kama unaotaka kutengeneza pesa kwa njia zozote ziwezekanazo, kuanzia mikataba ya madawa ya kulevya, hadi mauzo ya silaha katika Mashariki ya Kati na Afrika.
Alituambia kuhusu mkakati uliokuwa nyuma ya maamuzi yaliyochukuliwa katika Pyongyang, mashambulio ya utawala dhidi ya Korea Kusini, na anadai kwamba huduma za siri za ujasisi za nchi hiyo na mitandao yake ya intaneti inaweza kufikia maeneo yote ya dunia.
BBC haiwezi kupata thibitisho huru la madai haya, lakini tumeweza kuthibitisha utambulisho wake na , pale inapowezekana, tumepata ushahidi wa vyanzo tofauti kwa madai yake.
Tuliwasiliana na ubalozi wa Korea Kaskazini mjini London na ubalozi mdogo wa New York kwa ajili ya kupata kauli, lakini hadi sasa hatujapata jibu.
'Kikosi kazi'
Miaka ya mwisho ya Bw Kim katika kikosi cha ngazi ya juu zaidi cha ujasusi ilimpatia picha ya maisha ya awali ya kiongozi wa sasa wa Korea Kaskazini , Kim Jong-un. Anamuelezea kama kijana aliyetaka kujithibitisha kama "mpiganaji".
Korea Kaskazini iliunda shirika jipya la ujasusi lililoitwa Reconnaissance General Bureau katika mwaka 2009, wakati Kim Jong-un alipokuwa akiandaliwa kumrithi baba yake, ambaye alikuwa ameugua kiharusi. Mkuu wa ofisi ya Kim Yong-chol, amabye amesalia kuwa mmoja wa washirika wanaoaminiwa zaidi na kiongozi wa Korea Kaskazini.
Kanali huyu alisema kuwa katika mwezi wa Mei 2009, amri ilishuka katika ngazi za mamlaka ya kuundwa kwa "kikosi kazi cha ugaidi" kumuua afisa wa zamani wa Korea Kaskazini ambaye alikuwa ametorokea Korea Kusini.
"Kwa Kim Jong-un, kilikuwa ni kitendo cha kumridhisha kiongozi wa ngazi ya juu zaidi (baba yake)," Bw Kim anasema.
" 'Kikosi cha ugaidi' kiliundwa kumuua Hwang Jang-yop kwa siri. Binafsi niliagizwa na kutekeleza kazi hiyo."

Chanzo cha picha, Reuters
Hwang Jang-yop wakati mmoja alikuwa ni mmojawapo wa maafisa waliokuwa na mamlaka zaidi nchini. Alikuwa muandaaji muhimu wa sera ya Korea Kaskazini.
Alitoroka kuelekea Korea Kusini katika mwaka 1997 na hajawahi kusamehewa.
Mara alipoingia Seo, alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala, na familia ya Kim ilitaka kulipiza kisasi.
Lakini jaribio la kumuua lilikosea. Mameja wawili katika jeshi la Korea Kaskazini wanatumikia kifungo cha miaka 10 mjini Seul kwa kufanya njama hiyo.
Pyongyang imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuwa ilihusika na ilidai Korea Kusini ilipanga jaribio bandia la kumuua.
Ushahidi wa Bw Kim unaelezea tofauti.
Kulikuwa na mengi ya kujitokeza. Mwaka mmoja baadaye, katika mwaka 2010, meli ya kijeshi ya Korea Kaskazini, Cheonan, ilizama baada ya kugongwa na topito. Watu arobaini na sita walipotea. Pyongyang imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika ajali hiyo.
Halafu, mwezi Novemba mwaka huo, makumi kadhaa ya makombora ya Korea Kaskazini yalipiga kisiwa cha Korea Kaskazini cha Yeongpyeong.
Wanajeshi wawili na raia wawili waliuawa.
Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu ni nani aliyetoa amri ya mashambulio hayo.
Bw Kim alisema kuwa "hakuhusika moja kwa moja [katika operesheni hizo dhidi ya Cheonan au kisiwa cha Yeonpyeong", lakini "hazikuwa ziri kwa maafisa wa ujasusi -RGB, zilifanywa kwa majivuno, kilikuwa ni kitu cha kujigamba".
Na mashambulio hayo hayangetokea bila amri kutoka juu, anasema.
"Katika Korea Kaskazini, hata wakati barabara inajengwa, haiwezi kufanyika bila idhini ya moja kwa moja ya Kiongozi wa ngazi ya juu zaidi.
'Jasusi katika nyumba ya bluu''
Bw Kim anasema mojawapo ya wajibu wake katika Korea Kaskazini ilikuwa ni kuandaa mikakati ya kukabiliana na Korea Kusini. Lengo lilikuwa "utii wa kisiasa".
Hiyo ilihusisha kuwa na macho na masikio wazi kuelewa kinachoendelea ndani ya nchi hiyo.
"Mara nyingi nilikuwa nikiwaagiza majasusi kwenda Korea Kusini na kuendesha shughuli ya ujasusi kupitia wao. Mara nyingi", anadai. Haelezei zaidi, lakini hatupatii mfano halisi wa jinsi alivyoendesha ujasusi.
"Ninaweza kukwambia kwamba shughuli za Korea Kaskazini za ujasusi zinaendelea katika mashirika mbali mbali ya kiraia pamoja na taasisi muhimu katika Korea Kusini." BBC haina njia ya kuthiobitisha dai hili.

Chanzo cha picha, Reuters
Korea Kaskazini inaweza kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani na nchi iliyotengwa zaidi, lakini mtoro wa zamani wa ngazi ya juu ametahadharisha kuwa Pyongyang imebuni jeshi lenye ujuzi wa kudukua la wanajeshi 6,000.
Kulingana na Bw Kim, kiongozi wa zamani wa Korea Kaskazini, Kim Jong-il, aliagiza kutolewa kwa mafunzo ya wanajeshi wapya katika miakaya 1980 ''kujiandaa kwa ajili ya vita vya mtandaoni ".
"Chuo kikuu cha Moranbong kilikuwa kikiwachukua wanafunzi wenye akili zaidi kutoka maeneo yote ya nchi na kuwaweka katika elimu maalumu ya miaka sita ,"anasema.
Maafisa wa usalama wa Uingereza wanaamini kuwa kikosi cha Korea Kaskazini kinachofahamika kama kikundi cha Lazarus kilikuwa nyuma ya shambulio la kimtandao lililoathiri utendaji wa huduma za afya za taifa hilo na mashirika mengine duniani katika mwaka 2017.
Bw Kim anasema ofisi ya kikosi hicho inafahamika kama - 414 Liaison Office.
Anadai kilikuwa na simu ya moja kwa moja kwa Kiongozi wa Korea Kaskazini.
"Watu wanasema mawakala wake wako katika Uchina, Urusi, katika nchi za Asia Kusini, lakini pia wanafanya kazi katika Korea Kaskazini yenyewe. Ofisi hiyo pia hulinda mawasiliano baina ya mawakala wa ujasusi wa Korea Kaskazini."
Mihadarati kwa ajili ya dola
Hivi karibuni Kim Jong-un alitangaza kwa mara nyingine tena kuwa inakabiliwa na "mzozo" na katika mwezi wa Aprili aliwatolea wito watu wake kujiandaa kwa "kipindi kingine cha maumivu" -kauli ambayo ilikuwa ikitumiwa kuelezea maafa ya njaa katika miaka ya 1990, chini ya utawala wa Kim Jong-il.
Wakati ule, Bw Kim alikuwa katika idara za utendaji na aliagizwa kuchangisha "pesa za mageuzi" kwa ajili ya kiongozi wa ngazi ya juu zaidi. Hilo anasema, lilimaanisha kupata pesa kutoka katika madawa haramu ya kulevya.
"Utengenezaji wa mihadarati katika Korea Kaskazini ya Kim Jong-il uliongezeka kwa kiwango cha juu wakati wa ''mzozo wa njaa''uliojulikana kama Arduous March," anasema. "Wakati mwingine, Idara ya utendaji ilikosa kabisa pesa za mageuzi kwa ajili ya Kiongozi wa ngazi ya juu zaidi.
Nilimuuliza Bw Mr Kim ni wapi pesa za mihadarati zilipokwenda. Je zilikusanywa kama pesa taslimu kwa ajili ya watu?
"Kukusaidia uelewe, pesa zote katika Korea Kaskazini ni mali ya Kiongozi ,"anasema. " Kwa kutumia fedha zile, alijenga majumba makubwa ya kifahari, alinunua magari, alinunua vyakula, alinunua nguo na kujifurahisha kwa anasa ."
Makadirio ya idadi ya vifo vilivyotokana na upungufu wa muda mrefu wa chakula katika Korea Kaskazini katika miaka ya 1990 yalikuwa kuanzia mamia ya maelfu hadi watu milioni moja.

Chanzo cha picha, Getty Images
Chanzo kingine cha mapato, kulingana na Bw Kim, kilitokana na mauzo ya silaha kwa Iran, yaliyosimamiwa na Idara ya utendaji.
" Kulikuwa na manuari ndogo, na manuari zinazoelea baharini zenye uwezo wa kuzama majini na kufika mahali zinapotakikana kwa haraka . Korea Kaskazini ilikuwa ilikuwa bora katika kutengeneza vifaa kama hivi ," anasema.
'Mhudumu mtiifu aliyesalitiwa'
Bw Kim aliishi maisha yenye fursa bora katika Korea Kaskazini. Anadai alipewa gari aina ya Mercedes-Benz na shangazi yake Kim Jong-un, na aliruhusiwa kusafiri nje ya nchi kuchangisha pesa kwa ajili ya kiongozi wa Korea Kaskazini.
Anasema aliuza vyuma vya thamani na makaa ya mawe ili kupata mamilioni ya pesa taslimu, ambazo alikuwa akizirejesha nchini katika kijisanduku cha -suitcase.
Uwezo wa Bw Kim wa kuchangamana kisiasa kupitia ndoa ulimuwezesha kuhama hama baina ya mashirika ya ujasusi, anasema. Lakini kufahamika kwake pia kuliiweka familia yake hatarini.
Kulingana na Bw Kim, jina la Jang Song-thaek lilikuwa limesambaa na kuwa maarufu kuliko lile la Kim Jong-un.
"Hapo ndipo nilipohisi Jang Song-thaek hatadumu kwa muda mrefu. Nilihisi kuwa angepelekwa mbali katika maeneo ya mashambani ,"anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini ilipofika Disemba mwaka 2013 vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vilitangaza kuwa Bw Jang ameuawa,
"Kuiacha nchi yangu, ambako kuna makaburi ya mababu zangu na familia, na kutorokea Korea Kusini, ambayo wakati fulani kwangu ilikuwa ni ardhi ya kigeni, ulikuwa ni uamuzi mbaya zaidi wa majonzi wa maumivu ya kihisia," anasema.
"Hii ndio kazi pekee ninayoweza kuifanya," anasema. "Nitafanya kazi zaidi kuanzia sasa kuendelea kuiweka huru Korea yangu ya Kaskazini iondokane na udikteta ili watu wafurahie uhuru wa kweli ."
Kuna zaidi ya watoro 30,000 wa Korea Kaskazini waliokimbilia Korea Kusini. Ni wachache wanaoamua kuongea na vyombo vya habari. Kadri unavyokuwa maarufu, ndivyo unavyokuwa na hatari zaidi kwako na kwa familia yako.
Bw Kim anaishi maisha yasiyo ya kawaida. Ushahidi wake unapaswa kusomwa kama sehemu ya hadithi ya Korea Kaskazini-sio yote. Lakini hadithi yake inatupatia mtizamo ndani ya utawala ambao ni wachache wanaweza kuukwepa, na kutuambia kitu fulani kuhusu jinsi utawala wa Korea Kaskazini unavyoendesha nchi












