Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kafala ni nini, mfumo tata wa ajira ya udhamini ambao 'huwafanya' watu kuwa watumwa
Alidhani amepata ajira ya ndoto yake , lakini aliishia kuwa mhanga wa kufanyishwa kazi bila malipo.
Athenkosi Dyonta, muuza kahawa mwenye miaka 30, alifanya kazi katika mgahawa mmoja mjini George Town, sehemu maarufu inayopendwa na watalii nchini mwake Afrika kusini.
Kijana huyo alikuwa akipenda sana kushirikisha kwenye Facebook "sanaa yake ya latte,"uchoraji unaofanywa kwa kutumia maziwa juu ya kahawa ambao pia hufanywa na wauzaji kahawa wenzake katika kundi lao Facebook.
Ni katika ukumbi huo ambapo mwanamke mmoja aliwasilaina naye na kumpatia nafasi ya ajira nchini Oman.
Mbali na mshahara mzuri, pia walimpatia makazi ya bure, chakula na usafiri.
Mwanamke huyo pia alisema atashughulikia hati yake ya usafiri. Kile Athenkosi alihitajika kufanya ni kulipia nauli ya ndege, ukaguzi wa kimatibabu, na vipimo vya covid-19.
"Nilifikiria atakaporudi baada ya mwaka mmoja tutanunua nyumba na kuwapeleka watoto wetu katika shule nzuri,"anakumbuka mpenzi wake Pheliswa Feni, 28, ambaye alikuwa amezaa naye watoto wawili.
Wapenzi hao walikopa pesa za kumwezesha Athenkosi, kusafiri kwenda Oman.
Alipowasili katika nchi hiyo ya uarabuni, muandaaji kahawa huyo alipelekwa hadi mji mkuu, Muscat, na baadaye kusafirishwa hadi mji unaoitwa Ibra, ambako alioneshwa makazi yake mapya.
"Palikua mahali pachafu, chumba kidogo, kilichokua na godora na masanduku," Athenkosi aliambia BBC.
Huo ulikuwa mwanzo wa masaibu yaliyomkumba mtu huyo ambaye baada ya muda mfupi aligundua ''ajira ya ndoto yake'' haikuwepo.
Athenkozi alienda kufanya kazi ya kuosha vyombo kwenye mgahawa kwa kati ya saa 12-14 kwa siku.
Wakati hayupo kazini alilazimishwa kujifungia ndani ya chumba chake. Chakula kilikua kibaya na walikua hawamlipi.
"Alikula mkate na maziwa,wakati mwingine keki na yai moja. Hakupokea mshahara bali alikuwa anafanya kazi tu."
Kile ambacho mtu huyo hakujua ni kwamba alitia saini makubaliano ya udhamini unaofahamika kama Kafala, unatumiwa katika baadhi ya nchi za mashariki ya kati, ambao unawapatia raia na makampuni udhibiti wa ajira na hadhi ya makazi kwa wafanyakazi uhamiaji.
Kwa huruma ya mwajiri
"Kafala au mfumo wa udhamini unaowaunganisha wafanyakazi wa kigeni na waajiri wao," May Romanos, mtafiti katika shirika la kutetea haki la Amnesty International (AI) anayejihusisha na masuala ya kutetea haki ya wahamiaji katika eneo la Ghuba aliambia BBC Mundo.
Romanos ni mmoja wa waandishi wa ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2019 kuhusu mfumo wa kafala nchini Lebanon.
Kafala ni neno la Kiarabu linalomaanisha udhamini.
Katika mfumo huu "wafanyakazi hawawezi kuingia nchini au kupata visa hadi wawe na wadhamini."
"Na mwajiri anaweza kufuta kibali cha makazi wakati wowote na kumwacha mfanyakazi kama mhamiaji haramu aliye katika hatari ya kufukuzwa nchi," anaelezea Romanos.
"Mfanyakazi hawezi kubadilisha kazi au kuondoka nchini bila ruhusa kutoka kwa mwajiri wake, kwa hivyo anaishia kunaswa katika mzunguko wa dhuluma."
Mfumo huo uliundwa ili kuhakikisha upatikanaji wa wafanyikazi kwa gharama ya chini rahisi wakati waenzi ya ukuaji wa uchumi.
Waungaji mkono mfumo huo wanadai kuwa unawafaidi wafanyabiashara wa ndani na ni kichocheo cha maendeleo, ijapokuwa mfumo huo umeendelea kukumbwa na utata kutokana na ripoti ya visa vya dhulma.
Licha ya uwezekano wa kutumikishwa vibaya wafanyakazi wanakubali ajira kupitia mfumo wa kafala kwa sababu malipo wanayoahidiwa ni bora kuliko kile wangelipata katika nchi zao, linasema Baraza la Uhusiano wa KigenI (CFR). lililo na makao yake mjini New York, Marekani.
Wafanyakazi wengi wanatuma hela nyumbani, hatua ambayo Benki ya Dunia inasema inaweza kusaidia kumaliza umasikini miongoni mwa nchi zilizo na kipato cha chini na zile zenye kipato cha wastani.
Mwaka 2019, Kuwait, Saudi Arabia na Muungano wa Miliki za Kiarabu zilikuwa kati ya nchi 10 ambazo wafanyakazi walituma hela kwa wingi.
Wanaounga mkono mfumo huo wanasema kuwa kuwezesha uingiaji nchini kisheria kwa wafanyikazi katika nchi hizo kunawepusha wafanyakazi dhidi ya hatari ya biashara ya ulanguzi wa binadamu.
Mfumo wa kafala hutumiwa kwa njia tofauti katika nchi zote za Ghuba, zikiwemo Jordan na Lebanon.
"Nchini Lebanon, kwa mfano, wafanyakazi wahamiaji hawawezi kubadilisha ajira bila idhini ya waajiri wao lakini wanaweza kuondoka nchi humo," Romanos anasema.
"Ijapokuwa kiuhalisia ni vigumu sana kufanya hivyo endapo mwajiri atakataa kulipia nauli ya ndege, kwa kuwa wafanyakazi hawa wanalipwa mshahara mdogo sana. Wakati mwingine mwajiri hushikilia pasipoti zao."
Utafiti wa shirika la kutetea haki la Human Rights Watch mwaka 2008 ulibaini kuwa wafanyikazi wa kigeni wanaofanya kazi za ndani walikuwa wakifariki nchini Lebanon kwa kiwango kikubwa kila wiki, kutokana na visa vya kujitoa uhai baada ya kutibuka kwa jaribio lao la kutoroka.
Bahrain, Qatar na Saudi Arabia
Mnamo mwaka 2009 Bahrain ilitangaza kwamba itavunja mfumo wa kafala na kuanzisha shirika la umma,Mamlaka ya Udhibiti wa Soko la Ajira, kudhibiti hadhi ya wahamiaji badala ya waajiri.
Hata hivyo , Shirika la Kimataifa la Kazi, ILO, iligusia kuwa Mamlaka hiyo inatumika kama njia ya kuwaleta wafanyakazi "lakini haijaanza kutekeleza jukumu la udhamini, kwa hivyo mfumo wa kafala umesalia na vikwazo."
Lakini ILO ilionya kuwa uhuru huo ulidhibitiwa baadaye na sheria nyingine ya mwka 2011 ''ambayo inazuia wafanyikazi kubadilisha kazi ndani ya mwaka mmoja."
Qatar pia ilifanyia marekebisho mfumo wake wa kafala "kufuatia shinikizo za kimataifa hasa inapojianda kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022," Romanos anasema.
Nchi hiyo ina karibu wafanyakazi wa kigeni milioni mbili, wanaochangia asilimia 95 ya ajira,kulingana na Amnesty International..
ILO, imetaja marekebisho yaliyofanywa na Qatarkatika mfumo wake wa kafala "kama mabadiliko ya kihistoria".
"Qatar imeondoa masharti yanayowalazimu wahamiaji kuomba ruhusa kutoka kwa waajiri wao .
Saudi Arabia, kwa upande wake, "ina zaidi ya wafanyakazi wahamiaji milioni 10," Romanos anasema.
Nchi hiyo pia ilifanya mabadiliko, "lakini zaidi yako kwenye vitabu lakini kiuhalisia hali ni tofauti," kulingana na uchunguzi wa Amnesty International.