Eunice Osayande: Kwanini barabara ya Brussels Ubelgiji ilipewa jina la kahaba huyu kutoka Nigeria?

Chanzo cha picha, Kevin Van den Panhuyzen/BRUZZ
Mji wa Brussels umesema kwamba utaipatia jina la kahaba wa Nigeria aliyeuawa barabara moja ya mji huo , kama kampeni kubwa ya kuwatambua wanawake nchini Ubelgiji.
Baraza la mji huo limesema kwamba barabara hiyo itapatiwa jina Eunice Osayande , ambaye alidungwa kisu hadi kufa na mteja mmoja aliyejawa na fedheha 2018.
Akivutiwa kwamba angepata kazi na kuwa na maisha bora barani Ulaya, bi Osayande aliwasili katika mji mkuu wa Ubelgiji 2016.
Bi Osayande alidhania kwamba wanaume waliomualika Ulaya walikuwa mawakala ambao wangemsaidia kuwa nyota mkubwa wa filamu.
Lakini ukweli ni kwamba walikuwa wakifanya biashara ya kulangua binadamu.
Alipowasili Brussels , bi Osayande alilazimishwa kuingilia Ukahaba . Aliambiwa kwamba anadaiwa $52,000 kama nauli ya usafiri, nyumba ya kuishi na ada ya ugawadi.
Wiki chache kabla ya kifo chake , aliwasiliana na shirika linalowasaidia mahakaba na kuliambia kwamba alikuwa akikabiliwa na unyanyasaji , kupigwa na kutishwa kazini.
Aliogopa kwenda polisi kwasababu alikuwa muhamiaji haramu. Mwezi Juni 2018, akiwa na umri wa miaka 23 , bi Osayande alidungwa kisu mara 17 na mteja wake katika wilaya ya Gare du Nord.
Maandamano yalioongozwa na jamii ya mahakaba yalizuka mji Brussels . Waandamanaji walitaka kupatiwa mazingira bora ya kufanya kazi na kutoa wito kwa utawala wa eneo hilo kuweka sheria mwafaka kuongoza sekta hiyo.
Ukahaba ni halali nchini Ubelgiji , lakini hakuna sharia zilizowekwa kitaifa.

Chanzo cha picha, Kevin Van den Panhuyzen/BRUZZ
Maxime Maes , mkurugenzi wa muungano wa makahaba mjini humo UTSOPI aliandaa maandamano hayo.
''Kifo cha Eunice kinaghadhabisha sana , miongoni mwa wahamiaji haramu katika eneo hilo ambalo alikuwa akifanya kazi'' , aliambia BBC.
Kumekuwa na ongezeko la ghasia na wanawake waliobaguliwa zaidi hulengwa.
Mtu mwenye umri wa miaka 17 alishtakiwa kwa mauaji ya bi Osayande na sasa anasubiri kuhukumiwa.
Wanachama wanne wa genge moja la ulanguzi wa binadamu walikamatwa mwezi Januari mwaka huu na wakahukumiwa jela vifungo vya miaka minne.
Kwa kuipatia barabara mpya jina la Bi Osayande , mji wa Brussels ulisema kwamba unataka kutoa hamasa kwa wanawake wote waliosahaulika ambao ni waathiriwa wa biashara ya ulanguzi wa binadamu , ghasia za kijinsia na mauaji ya wanawake.
Barabara hiyo itakuwa ya kwanza kupatiwa jina la kahaba nchini humo , kulingana na chombo cha habari nchini humo RTBF.
Barabara hiyo mpya , ambayo itakuwa kaskazini mwa mji huo , ni mojawapo ya mipango ya baraza la mji huo kuyapatia maeneo mengi majina ya wanawake.
Baraza hilo tayari limezipatia majina ya wanawake tajika baadhi ya barabara , ikiwemo Yvonne Nèvejean na Andrée De Jongh, na daraja moja kupewa jina la Suzan Daniel, Mwanaharakati wa kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja.
Lakini kwa mujibu wa Ans Persoons, mwanamke kutoka mji wa Brussels , alisema: "Kuwa mwanamke sio tu wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali.
'Kuwa mwanamke ni kuhusisha haki za wanawake na mapambano katika kila jamii'
Bi Persoons alisema asilimia 42 ya wanawake nchini Ubelgiji kati ya umri wa miaka 16 hadi 69 wana uzoefu wa kunyanyaswa kijinsia .
Asilimia hii ni ya juu miongoni mwa makahaba. Na hiyo ndio sababu bi Eunice Osayande anapatiwa barabara.
Barabara hiyo ambayo inaendelea kujengwa , itafunguliwa katika miezi michache ijayo.
Baraza la mji huo linasema kwamba makahaba na jamii za wahamiaji zitaalikwa kuzungumza katika hafla hiyo.












