Afghanistan: Ndege ya mwisho ya Marekani yaondoka, ikiashiria tamati ya operesheni yake

Wapiganaji wa Taliban kutoka kikosi cha Fateh Zwak,wakiwa na silaha za Marekani, vifaa na sare, wakiingia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kabul 31 Agosti 2021

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Ndege ya mwisho ya jeshi la Marekani imeondoka Kabul, ikiashiria mwisho wa uwepo wa nchi hiyo nchini Afghanistan.

Kamanda mkuu wa jeshi la Marekani katika eneo hilo, Jenerali Kenneth McKenzie, amesema ndege ya mwisho ya C17 iliondoka Kabul ikiwa na balozi wa Marekani baada ya saa sita usiku saa za eneo hilo.

Aliongeza kuwa ujumbe wa kidiplomasia kusaidia wale ambao hawakuweza kuondoka kabla ya tarehe ya mwisho utaendelea.

Milio ya risasi ya sherehe za Taliban ilisikika baada ya ndege ya mwisho kuondoka.

Kuondoka kwa ndege hiyo ya mwisho kunaashiria kumalizika kwa vita virefu kabisa vya Marekani, na juhudi kubwa ya uokoaji ambayo ilianza tarehe 14 Agosti mara tu baada ya Taliban kuchukua nchi.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Jenerali McKenzie alisema kuwa kwa jumla, ndege za Marekani na nato ziliwaondoa zaidi ya raia 123,000 - wastani wa zaidi ya raia 7,500 kwa siku wakati huo.

Akiongea baada ya tangazo hilo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alizungumza huko Washington, akiita uhamishaji huo "jukumu kubwa la kijeshi, kidiplomasia na kibinadamu" na moja wapo ya changamoto kubwa kwa kazi ambayo Marekani imewahi kutekeleza.

"Ukurasa mpya umeanza," alisema. "Ujumbe wa kijeshi umekwisha. Ujumbe mpya wa kidiplomasia umeanza."

Lakini alisema kuwa Taliban ilihitaji kupata uhalali wake na itahukumiwa kwa kiwango ambacho ilitimiza ahadi na majukumu yake ya kuruhusu raia kusafiri bure kwenda na kutoka nchini, ilinde haki za Waafghan wote wakiwemo wanawake, na ilizuia vikundi vya ugaidi kutokana na kupata nafasi nchini.

Aliongeza kuwa wakati Marekani ikisitisha uwepo wake wa kidiplomasia huko Kabul, na kuhamisha operesheni zake kwenda Doha, itaendelea na "juhudi zake" za kuwasaidia Wamarekani, na Waafghan na pasi za Marekani, kuondoka Afghanistan ikiwa wanataka.

Bwana Blinken alikuwa waziri wa kwanza wa baraza la mawaziri la Biden kuzungumza kuhusu kujitoa.

Rais Joe Biden alitoa taarifa fupi kuwashukuru wale wote waliohusika katika operesheni ya uokoaji kwa siku 17 zilizopita na kusema kuwa atalihutubia taifa baadaye Jumanne.

Wakati huo huo, Marekani bado haijaelezea ripoti kwamba shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya mtu anayeshukiwa kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga nchini Afghanistan liliwaua raia kadhaa, wakiwemo watoto sita na mtu ambaye alifanya kazi kama mtafsiri wa vikosi vya Marekani.

Jamaa wa watu hao walisema shambulio hilo, kwenye gari karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, lilitokana na taarifa isiyo sahihi. Pentagon ilisema ilikuwa ikitathmini na kuchunguza ripoti hizo.

line

Mustakabali wa mashaka kwa mamilioni ya Waafghan

Uchambuzi wa Lyse Doucet wa BBC

Hata baada ya miaka 40 ya vita, Waafghani wameishi kupitia kipindi cha mpito ambacho hakina uhakika, ambacho kimefunikwa sana na giza na umejaa hofu. Kuna kutokuwa na hakika kuhusu ya kile kilicho mbele.

Kuna kutokuwa na uhakika na hofu kwa maelfu ya Waafghan ambao wameondoka nchini katika siku chache zilizopita ambao watajiuliza ikiwa wataiona nchi yao tena.

Kwa Waafghan milioni 38 ambao wamebaki nchini, kuna kutokuwa na uhakika mkubwa juu ya aina gani ya sheria ambayo Taliban itatoa. Je! Watarudisha sheria kali na adhabu ambazo walionesha kipindi chao cha mwisho katika kuongoza nchi?

Waafghanistan wengi wanaangalia utawala wa Taliban katika maeneo ya vijijini na wanahofu kuwa hawajabadilika, lakini kwa namna fulani wamezidi kuwa wabaya.

Hii ni jamii ya jadi sana. Wanawake na wasichana walipata uhuru kidogo wakati vikosi vya muungano wa Magharibi vikihimiza elimu. Waliopoteza zaidi ni wasichana ambao walikuwa wakikua katika miaka 20 iliyopita ambao wanaamini sasa kwamba hawawezi kuishi maisha waliyoahidiwa,

Kesho itaanza sura mpya inayofuata ya vita hii ndefu. Vita virefu zaidi vya Marekani vimekwisha, lakini vita kwa Waafghan hakika bado havijaisha.