Afghanistan: Taliban 'wafanya msako wa nyumba kwa nyumba' Umoja wa Mataifa umeeleza

Chanzo cha picha, EPA
Taliban wako kwenye operesheni ya kuwatafuta watu waliofanya kazi kwa vikosi vya Nato au serikali ya zamani ya Afghanistan, waraka wa Umoja wa Mataifa umeeleza.
Umesema wapiganaji hao wamekuwa wakienda nyumba kwa nyumba kuwatafuta wanaowalenga na kuzitishia familia zao.
Kundi hilo lenye msimamo mkali wa Kiislamu limejaribu kuwahakikishia Waafghan tangu kutwaa madaraka, na kuahidi hakutakuwa na "kisasi".
Lakini kuna hofu kwamba Taliban wamebadilika kidogo tangu miaka ya ukatili ya 1990.
Onyo ambalo limetolewa kuhusu kundi hilo linalowalenga "washirika" lililetwa katika hati ya siri na Kituo cha RHIPTO cha Norway cha Uchambuzi ambacho hutoa usaidizi wa masuala ya ujasusi kwa UN.
"Kuna idadi kubwa ya watu ambao kwa sasa wanalengwa na Taliban na tishio liko wazi," Christian Nellemann, ambaye anaongoza jopo la walioandaa ripoti hiyo, aliiambia BBC.
"Ik kwenye maandishi kuwa wasipojisalimisha Taliban watakawamata na kuwashtaki, na kuwaadhibu wanafamilia kwa niaba ya watu hao."
Alionya kuwa mtu yeyote kwenye orodha ya Taliban yuko katika hatari kubwa, na kwamba kunaweza kuwa na mauaji ya watu wengi.
Yanayojiri:
- Maandamano zaidi ya kupinga Taliban yamefanyika katika miji kadhaa. Katika mji mkuu Kabul, waandamanaji walipeperusha bendera ya kitaifa huku ikiripotiwa kuwepo kwa majeruhi kati miongoni mwa waandamanaji huko Asadabad
- Mmoja wa wale waliokufa akianguka kutoka kwa ndege ya Marekani iliyokuwa ikiondoka Kabul ametambuliwa kama Zaki Anwari wa miaka 19, ambaye alichezea timu ya kitaifa ya mpira wa miguu ya vijana ya Afghanistan
- Nchi za kigeni zinaendelea na juhudi zao za kuwatoa raia wao kutoka Afghanistan. Marekani inasema imewaokoa watu 7,000 tangu tarehe 14 Agosti
- Nje ya uwanja wa ndege wa Kabul hali bado hali tete. Taliban imekuwa ikizuia Waafghan wanaojaribu kukimbia, video moja ilionesha mtoto akikabidhiwa kwa mwanajeshi wa Marekani.
- Taliban sasa wanadhibiti maelfu ya magari ya kivita yaliyoundwa na Marekani, ndege 30-40 na idadi kubwa ya silaha ndogo ndogo, maafisa wa Marekani waliliambia Reuters
Taliban waliudhibiti mji wa Kabul siku ya Jumapili, baada ya kuidhibiti nchi nzima wakati vikosi vya kigeni vilipoondoka.
Ushindi wao unarudisha kikundi hicho madarakani baada ya miaka 20 wakati walipong'olewa katika operesheni iliyoongozwa na Marekani
Wakati wa utawala wa hapo awali wa kikundi hilo unyanyasaji ulioenea, pamoja na mauaji na kupiga marufuku wanawake kufanya kazi vilishuhudiwa.
Lakini katika mkutano wao wa kwanza wa waandishi wa habari tangu kuchukua tena udhibiti wa Afghanistan, kikundi hicho kiliahidi haki za wanawake zitaheshimiwa "katika mfumo wa sheria za Kiislamu".
Taliban wameripotiwa kuahidi kutowalazimisha wanawake kuvaa burka -vazi linalofunika uso na mwili. Badala yake, hijab - au kitambaa cha kichwa - kitakuwa cha lazima.

Chanzo cha picha, EPA
Walisema pia hawataki "maadui wowote wa ndani au wa nje" na kwamba kutakuwa na msamaha kwa washiriki wa zamani wa vikosi vya usalama na wale ambao walifanya kazi na mataifa ya kigeni.
Mamlaka ya kimataifa - na Waafghan wengi - wanabaki kuwa na wasiwasi.
Alipoulizwa katika mahojiano ikiwa alifikiri Taliban imebadilika, Rais wa Marekani Joe Biden alisema hapana, akiongeza kuwa kundi hilo lina uchaguzi kama wanataka kutambuliwa.














