Afghanistan: Wanajeshi wastaafu wahuzunishwa na 'kuibuka' kwa Taliban na kushika hatamu

Jack Cummings kk

Chanzo cha picha, Jack Cummings

Maelezo ya picha, Jack Cummings alipoteza miguu akiwa katika shughuli za kijeshi Afghanistan.

Baada ya miaka 20 ya vita iliyogharimu maisha ya maelfu ya askari, kinachoendelea sasa nchini humo ni ngumu sana kwa askari wa zamani wa Uingereza na Marekani.

Wao na ndugu wa askari waliopoteza maisha wanahisi kwamba kila kitu kimeenda na 'maji' baada ya Taliban kushika hatamu ya nchi hiyo baada ya kuipigania kwa muda mrefu.

Kama ilivyo kwa Jack Cummings , mwanajeshi wa zamani wa Uingereza aliyekuwa Afghanistan ambaye alipoteza miguu yote miwili alipoenda kwa mara ya pili huko mashariki ya kati kwenye shughuli za kijeshi.

Kuona yanayotokea sasa, aliandika ujumbe ambao ulisambazwa na maelfu ya watu kwenye mtandao wa Twitter: "Tumepata chochote? Pengine hapana. Inaonekana nimepoteza miguu yangu bure tu. Marafiki zangu wamekufa bure tu."

"Nina hasira, nina huzuni, nahisi kama nimesalitiwa. Nimepoteza miguu kwa ajili ya nchi yetu, kuyaona haya yanayoendelea Afghanistan ni ya kutisha na yanavunja moyo," aliiambia haya baadae BBC.

"Imeniondoa kabisa na ninajua sio mimi peke yangu. Nimezungumza na wenzangu, wote wanahisi hivyo. Na wengine wanahangaika sasa hivi."

Jack Cummings

Chanzo cha picha, Jack Cummings

Maelezo ya picha, Karibu wanajeshi 450 wa Uingereza waliuawa katika mapigano nchini Afghanistan na maelfu wengine kujeruhiwa kama ilivyotokea kwa Jack Cummings.

Mike Jason, kanali mstaafu katika jeshi la Marekani, alikuwa katika operesheni kwa miaka 24 na amekuwa haamini kwa namna gani Taliban imeidhibiti Afghanistankwa mara nyingine tena kwa muda mfupi.

"Inasikitisha na inatia hasira. Kasi ya namna mambo yalivyoanza kuharibika ni ngumu kuingia akilini. Ni haraka sana kuliko uwezo wetu wa kuonyesha uzoefu wetu wa miaka 20 iliyopita," alisema.

"Nilivyokuja Afghanistan, lilikuwa somo kubwa, kufanya kazi katika mazingira mapya, na kushuhudia nchi nzuri yenye historia kubwa. Je nini tumepata? nilichokifanya kimeleta matunda? Kuna wakati nilifikiri nimefanya kazi nzuri, lakini sasa nahitaji muda wa kutathmini, "anasema kanali.

Marekani imepoteza zaidi ya wanajeshi wake 2,000 katika miaka 20 ya operesheni ya kijeshi nchini Afghanistan na wengine 20,000 walijeruhiwa, wakati Uingereza imeshuhudia zaidi ya askari wake 450.

Kilichotokea ni kama "kutwanga maji kwenye kinu"

Kilichotokea katika meneo kama Kabul haijawaathiri tu wanajeshi wastaafu lakini pia wote ambao walishuhudiwa ndugu zao wapendwa wakifariki kwenye ardhi ya Afghanistan.

Kwa upande wa Janette Binnie anasema kifo cha kijana wake wa miaka 22 Sean Binnie leo hii kinaonekana kama sadaka iliyokwenda bure, ambayo haijazaa matunda"

"Alijitoa kwa ajili ya kuleta mabadiliko," alisema. "mabadiliko hayo ni sawa na bure, hakuna."

Sean Binnie

Chanzo cha picha, Familia Binnie

Maelezo ya picha, Sean Binnie aliuawa mwezi Mei 2009 nchini Afghanistan, akiwa na umri wa miaka 22.

Sean Binnie alifariki mwezi 2009 akiwa anafanya doria akiwa na kikosi kilichokuwa kinafahamika kama "Black Guard" huko jimboni Helmand.

Mama yake anapatwa na mshtuko anavyoshuhudia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, ukidhibitiwa na Taliban huku rais wa nchi hiyo, Ashraf Ghani akitimkia ughaibuni.

"Ninajivunia mwanangu. Alitekeleza kile alichotakiwa kukifanya kama askari wa Uingereza. Lakini sasa nahisi kama kumbukumbu imeathiriwa na yanayotokea sasa. Ni kazi bure, "anasisitiza Janette Binnie.

Dylan Elchin

Chanzo cha picha, Familia Elchin

Maelezo ya picha, Sajenti Dylan Elchin wa Marekani aiuawa kwa bomu nchini Afghanistan.

Katika upande mwingine, Christian Easley anaamini kwamba mazingira ya sasa nchini Afghanistan hayajabadilisha mtazamo wake hata kidogo.

Easley alikuwa kwenye kikosi cha anga kama mkufunzi akisaidia kumfundisha mwanajeshi Dylan Elchin , ambaye aliuawa kwa bomu kando ya barabara nchini Afghanistan.

"Dylan alikuwa anapaswa kufuata malekezo yangu katika kutekeleza operesheni zake. Alifanya kila alichoambiwa na zaidi," alisema Easley.

"Haijalishi nini kimetokea katika wiki moja iiyopita, Nilijua fika, Dylan alifanya kila kitu sawa sawa."

Kuondolewa kwa wanajeshi nchini Afghanistan, lilikuwa kosa?

Marekani ilitumia dola $ 822 billion katika vita na operesheni na kuwafundisha wanajeshi wa Afghanistan, lakini sasa inashuhudia Taliban ikishinda kirahisi tena kwa haraka na kudhibiti nchi hiyo.

Zaidi ya wanajeshi 800,000 kutoka nchini humo walipelekwa Afghanistan katika vita ya muda mrefu kuwahi kushuhudiwa Marekani ikihusika.

Taliban kudhibiti nchi hiyo kwa kasi iliyoshuhudiwa inaonekana kama jambo la maana kwa mwanajeshi huyu mstaafu aliyezungumza na BBC.

"Nimesikitishwa", alisema Michelle Dunkley wa kikosi cha zamani cha anga kuhusu njia waliyotumia Marekani kujiondoa Afghanistan.

"Inahuzunisha. Nawaonea huruma waafghanistan," anasema.

"Je tulifanya tathmini ya uwezo wa jeshi la Afghanistan kabla ya kuondoka? Sidhani kama tulifanya, tuliwafundisha rubani wa ndege. Tulipaswa kuwafundisha na askari wao. Lakini hatukufanya vizuri kwenye hilo," anaongeza Dunkley, ambaye alikuwa Afghanistan mwaka 2016.

Kyle Hanson, aliyekuwa na kikosi cha Marekani kati ya mwaka 2006 na 2012, anazilaumu serikali za Donald Trump na Joe Biden kwa kusababisha kinachotokea sasa.

"Vita ni zaidi ya siasa. Jeshi letu limefanya kila linalowezekana ila wanasiasa wetu wametuangusha sisi na wamewaangusa waafghanistan, " anasema.

"Haijanishangaza imekuwa haraka hivyo - Taliban walipewa muda wa kutosha kujiandaa, ilifahamika mapema tu kwamba tukiondoka nini kitatokea."

Kanali mwingine mstaafu wa Marekani Mike Jason alinukuliwa akisema, "Tulitengeneza jeshi katika nchi ambayo haipo."

"Jeshi la Afghan halikuhisi kuwa watiifu kwa serikali waliyoiona haramu na iliyoonekana kukumbwa na rushwa. Sijui kama vikosi zaidi vya Marekani vingeweza kuzuia hilo. Sijui kama kuna yeyote aliyekuwa kwenye eneo la tukio anashangazwa na matokeo ya sasa," anasema.

Un

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bendera ya Taliban ikipeperushwa tena karibu maeneo yote ya Afghanistan.

Kilichotokea na athari zake kwa pade zote mbili

Kwa kuongezea anachosikitika na kujutia kuhusu juhudi za miongo miwili ikishuhudiwa Taliban wakishika hatamu, wanajeshi wastaafu wanahofu kuhusu kitakachowakuta wananchi wa Afghanistan.

"Nawaonea huruma raia wa Afghanistan, hasa wanawake ambao sasa watarudishwa kwenye zama za kati chini ya Taliban," anasema Michelle Dunkley.

Kwa upande wake Kanali Mike Jason, anasema"janga" ni kwamba wako rais wengi wa nchi hiyo ambao wanapambana kwa ajili ya "watoto wao ili wakue na wawe salama" na sasa wameachwa wasijue nini cha kufanya.

"Nimekuwa nikiwasiliana na maaafisa wa ngazi za juu wa Afghan wakiwa wamejificha. Familia yake pia imejificha. Hali ni mbaya huko," anaeleza.

"Kwa sisi wastaafu, jambo hili halitugusi, ila marafiki zetu wako hatarini. Bado mambo hayajakwisha. Sio muda wa kujifikiria sie kwa sasa," anaeleza Jason.

Kwa upande wake Matt Zeller, mwanajeshi mstaafu wa Marekani ambaye alipigana huko Afghanistan, anasema Marekani inapaswa kufanya kila linalowezekana kuokoa maisha ya waafghanistan.

Mwanajeshi mwingine wa Uingereza ambaye hakupenda kujitambulisha anasema "Kinachohuzunisha ni kwamba, familia huko zinahuzunika, sipati picha wanapitia mambo gani," alisema mwanajeshi huyo ambaye alihudumu kwa miaka 16.