Sharia ni nini na inamaanisha nini kwa wanawake wa Afghanistan?
Taliban wanasema wataongoza Afghanistan kulingana na muongozo thabiti wa mfumo wa sheria ya Kiislamu.
Katika mkutano wa kwanza na wanahabari baada ya kuchukua udhibiti wa Kabul, msemaji wa Taliban alisema masuala kama haki ya vyombo vya habari na wanawake yataheshimiwa kulingana na "misingi ya sheria ya Kiislamu",lakini kundi hilo halijatoa maelezo ya jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa kiuhalisia.
Mara ya mwisho walipokuwa madarakani, Taliban ilianzisha na kuunga mkono adhabu kama vile kuawa hadharani kwa watu waliopatikana na hatia ya kuua au kuzini.
Sharia ni nini?
Sharia ni mfumo wa kisheria wa dini ya Kiislamu. Inatokana na mafunzo ya kidini ya Koran na fatwa - uamuzi unaotolewa na wanazuoni wa Kiislamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maana halisi ya Sharia ni "njia iliyo wazi, sawa utakaso kwa kutumia maji".
Sharia ni muongozo wa kidini unaotakiwa kufuatwa na Waislamu wote, ikiwemo kusali, kufunga na kutoa msaada kwa wasiojiweza.
Inalenga kuwasaidia Waislamu kuelewa jinsi ya kuishi maisha yao ya kila siku kulingana na mapenzi ya Mungu.
Inamaanisha nini kiuhalisia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Sharia inaamua maisha ya kula siku ya Muislam.
Kwa mfano, ikiwa Muisilamu anashangaa afanye nini ikiwa wenzao kazini watawaalika kwenye baa baada ya kazi anaweza kutafuta ushauri kwa msomi wa Sharia ili kuhakikisha anafanya uamuzi kulingana na mfumo wa kisheria wa dini yake.
Masuala mengine ya maisha ya kila siku ambapo Waislamu wanaweza kugeukia Sharia kupata mwongozo ni pamoja na sheria za familia, fedha na biashara.
Je! Ni adhabu gani kali?
Sharia inagawanya makosa katika mafungu mawili makuu: "hadd", ambayo ni makosa yaliyo na adhabu maalum, na "tazir" makosa ambayo adhabu yake huamuliwa na jaji.
Makosa ya Hadd yanajumuisha wizi, ambayo adhabu yake ni kukatwa mkono na zinaa, ambayo adhabu yake ni kupigwa mawe hadi kufa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya mashirika ya Kiislamu yanasema kwamba kuna kinga nyingi na mzigo mkubwa wa uthibitisho katika matumizi ya adhabu ya hadd.
Umoja wa Mataifa umepinga adhabu ya kuuawa kwa kupigwa mawe, ukisema" ni ukatili,mwenendo ambao sio wa kibinadamu au ni adhabu ambayo ni ya kudhalilisha na imekatazwa".
Sio nchi zote za Kiislamu zinatekeleza adhabu kama hizo kwa makosa ya hadd, na utafiti unaashiria kuwa msimamo wa Waislamu huhusu adhabu hizo kali zinatofautiana.
Je Muislamu anaweza kuawa kwa kubadili dini?
Kuritadi au kuacha dini, ni suala tata sana katika ulimwengu wa Waislamu na wataalamu wanasema wanazuoni wengi wanaamini ni kosa ambalo adhabu yake ni kifo.
Lakini wanazuoni wenye misimamo ya kadri, hasa wale ambao wanajihusisha na jamii za Magharibi, wanahoji kwamba kiuhalisia katika dunia ya leo inamaanisha "adhabu" inastahili kuachiwa Mungu - na kwamba dini ya Kiislamu yenyewe haijatishiwa na uamuzi wa mtu kubadili dini.
Korani yenyewe inatangaza hakuna "kulazimishwa" katika dini.
Uamuzi unatolewa vipi?
Kama mfumo wowote wa kisheria, Sharia ni ngumu na utendaji wake unategemea ubora na mafunzo ya wataalam.
Majaji wa Kiislamu hutoa mwongozo na hukumu. Mwongozo ambao unachukuliwa kuwa uamuzi rasmi wa kisheria huitwa fatwa

Chanzo cha picha, Joshua Paul for the BBC
Kuna shule tano tofauti za mafunzo ya Sharia. Kuna mafundisho manne ya Kisunni: Hanbali, Maliki, Shafii na Hanafi, na fundisho moja la Shia, Shia Jaafari.
Mafundisho hayo matano yanatofautiana kwa jinsi maandishi yanavyotafsiri Sharia iliyotokana nayo.















