Mashambulio ya mabomu ya 1998: Mbinu za kupambana na ugaidi Kenya zilivyoongeza makurutu wa kigaidi

Chanzo cha picha, AFP
Miaka 23 iliyopita mwezi kama huu tarehe saba ,mashambulizi mawili ya kigaidi yaliotekelezwa kwa wakati mmoja yaliikumba miji ya Nairobi, Kenya na Dar Es Salaam Tanzania.
Mashambulizi hayo ya Agosti mwaka wa 1998, yalibadilisha kabisa hali ya usalama wa kanda hii na kuzitosa nchi hizo katika kampeni iliyojulikana kama 'vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi'.
Wiki hii tunakuletea Makala maalum kuhusu mashambulizi hayo ,wahusika wakuu na matokeo ya kampeni ya vita dhidi ya ugaidi na athari zake kwa nchi za Kenya, Tanzania , Uganda na kanda nzima.
Leo tunaangazia jinsi jinsi mbinu na mikakati ya kenya kupambana na ugaidi ilivyozua makovu kwa familia nyingi na kupelekea hata baadhi ya vijana kuamua kujiunga na makundi ya kigaidi.
Mauaji ya kiholela na kupotea kwa mashehe na vijana ni baadhi ya vilivyotumiwa na magaidi kuwashawishi wengi kujiunga nayo katika 'jihadi'

Wakati wanajeshi wa Kenya wakipambana na wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia, chini ya vikosi vya Amisom mashine ya propaganda ya kundi hilo lenye msimamo mkali iliendelea kuwalenga vijana waliokatishwa tamaa nyumbani kwao katika vitongoji masikini vya Kenya.
Katika mahojiano ambayo kijana mmoja alifanya na BBC mwaka wa 2014 wakati vita vilikuwa vimepamba moto nchini Somalia alisema alisajiliwa na al-Shabab lakini ikiwa ungemwona amevaa shati lake la mpira wa miguu la Uhispania na kofia ya baseball iliyoandikwa "New York", angeonekana kama Mkenya mwingine yeyote.
Jambo lisilo la kushangaza pia juu ya kijana huyu ni kwamba anasema alijiunga tu na kikundi cha wanamgambo wa Kiislam huko Somalia, ambapo alikuwa akiishi kwa miaka miwili, kwa sababu walimpa pesa.
Kisa chake ni ishara ya jinsi serikali ilivyoshindwa kukabiliana na tatizo la vijana kujiunga na kundi hilo .Mkakati wa serikali ulikuwa kutumia nguvu za polisi kuwakamata washukiwa na wakati mwingine ilishtumiwa kwa kuwauwa waliodhaniwa kuwa wanachama ama wafuasi wa kundi hilo .
Njia hiyo ilionekana kuzidisha tatizo la kiini kikubwa cha ukosefu wa kazi ama njia ya kujipatia kipato ilipuuzwa kama mojawapo ya sababu zilizokuwa zikiwavutia wengi kujiunga na makundi ya kigaidi .
Wanawake watatu tuliokutana nao wakati huo ambao jamaa zao wote walikwenda kupigania al-Shabab huko Somalia walituambia jamaa zao walikuwa wameenda kupigana huko Somalia kwa sababu hiyo hiyo.
Kurutu huyo wa zamani wa miaka 24 tuliyekutana naye, ambaye hatutamtambua ili kumlinda , anasema alilipwa zaidi ya $ 1,000 (Pauni 640) kujiunga na kikundi hicho.

Chanzo cha picha, MAINA/AFP/GETTY
Alipokuwa na umri wa miaka 18 alisajiliwa na al-Shabab wakati alikuwa akiishi katika makazi duni ya Majengo mjini Nairobi.
Hali ya makaazi katika mtaa huo ni duni . Mabanda ya mabati katika sehemu hiyo ndio yanayotumiwa na watu kama nyumba .
Watoto hucheza karibu na majaa ya taka na pembeni kuna mitaro ya kinyesi na maji taka
Sehemu kama hizo ndio sasa eneo mwafaka kwa watu wanaosajili vijana katika makundi ya kigaidi .
Kijana ambaye tulikutana naye alielezea al-Shabab kama "biashara".
Anasema alifundishwa katika shule za dini nchini Somalia na malipo ya mara moja aliyopokea yalikuwa sawa na "mshahara".
Anasisitiza kuwa hakuenda Somalia kwa sababu ya imani ya kiitikadi au jihadi lakini kwa sababu tu ya pesa.
"Kama ningekuwa na kazi, nisingeenda huko," anasema.
Kijana ambaye tulikutana naye anadai kwamba hakuwahi kumuua mtu yeyote na alipogundua kuwa atatarajiwa kuua alitaka kuondoka al-Shabab.
Amri za kuua
Wakati akiwa na kundi hilo anasema alisaidia kusafirisha silaha kupita mpaka wa Somalia hadi Kenya.
Anasema walihonga polisi mpakani na kuficha maguruneti katikati ya chakula.
Kurutu huyo wa zamani wa al-Shabab alisema hakuwahi kukutana na wapiganaji wa kigeni lakini alikuwa akifahamu kulikuwa na Waarabu watatu na mzungu mmoja ambao walipeleka silaha kwa kitengo chake.
Anasisitiza kuwa hafanyi kazi tena, au hana uhusiano wowote na, al-Shabab.

Chanzo cha picha, Reuters
Na anasema aliweza kuondoka kwenye kikundi hicho kwa sababu waliamini alikuwa anarudi Kenya kufanya mashambulio.
Anasema wanachama wa al-Shabab walimwamuru kulipua bomu katika soko la Nairobi mnamo Mei. Mwaka wa 2014
Walakini, aliwaambia kuwa hakuweza kufanya hivyo kwa sababu alikuwa anajulikana katika eneo hilo.
Soko la Gikomba la Nairobi lililipuliwa kwa bomu mnamo 16 Mei 2014, na watu 12 waliuawa.
Sasa kurutu huyo wa zamani wa al-Shabab anasema alihofia maisha yake ikiwa atakataa kushiriki katika mashambulio yajayo.
Kuachwa nyuma
Katika mtaa wa mabanda, kwenye barabara yenye matope, yenye harufu mbaya kati ya safu za mabanda, tunazungumza na wanawake watatu.
Mnamo Mei 5, 2012, mume wa Amina mwenye umri wa miaka 29 aliondoka nyumbani na hakurudi tena.
Kaka wa Halima aliondoka tarehe 27 Januari 2011.
Na mtoto wa Mwanaisha wa miaka 14 aliondoka mnamo Agosti 2009.
Wanawake wote watatu wana hakika jamaa zao waliondoka Kenya kwenda Somalia kupigana na al-Shabab.
Kwa kweli Mwanaisha alipokea simu kutoka kwa mtoto wake miezi miwili baada ya kuondoka, akithibitisha alikuwa akilipigania kundi hilo huko Somalia.
"Sijui kama amekufa au yuko hai," anasema "Nimekata tamaa."
Amina hajavunjika matumaini kwamba mumewe, siku moja atarudi.
Lakini ana uhakika kuwa aliondoka ili kutoroka umaskini katika mtaa wao wa mabanda.
"Alikuwa hana njia ya kupata pesa hapa," anasema. "waliomsajili katika kundi hilo walimpa pesa ."
Kuwakomesha wanaowasajili vijana katika makundi ya kigaidi
Amina, Halima na Mwanaisha wote waliniambia hapakuwa na uaminifu kabisa kati ya watu wanaoishi kwenye makazi duni na polisi.
Lakini tishio linalosababishwa na vijana wa Kenya wanaopigania al-Shabab nchini Somalia na kisha kurudi nyumbani kutekeleza mashambulio, ni kweli.
Lakini kwa sababu ya ukosefu wa uaminifu kati ya polisi na jamii ya wenyeji, na haswa Waislamu wanaoishi katika maeneo kama makazi duni ya Majengo, hakuna habari zinazotolewa kwa mamlaka na hali hiyo inajirudia kote nchini katika maeneo ya jamii za Waislamu na wasio Waislamu ambako umaskini na ukosefu wa fursa unawaweka maelfu ya vijana katika hatari ya kujipata katika mikono inayokaribisha makundi kama al shabaab .
Serikali ya Kenya hata hivyo ilianzisha mikakati ya kushughulikia tatizo hilo la mafunzo ya itikadi kali kwa kuangalia shina la tatizo .
Iwapo itatoa fursa na kuangalia vichocheo vinavyowafanya vijana kuvutiwa na makundi ya kigaidi , basi itakuwa na uhakika wa kuepuka kuwazawadi magaidi makurutu ambao wanaendeleza vitendo vya kigaidi na kutishia usalama na amani ya nchi .














