Uchunguzi wabaini mabilionea wa Marekani wanalipa 'kodi ya chini mno'

Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa za madai yaliyoibuka zinazoonesha kuwa mabilionea wa Marekani wanalipa kiwango cha chini cha kodi na zimevuja katika tovuti za habari.
Tovuti ya habari ya ProPublica imesema kuwa imeona kiwango cha ushuru kinacholipwa na baadhi ya watu matajiri duniani akiwemo Jeff Bezos, Elon Musk na Warren Buffett.
Tovuti hiyo ya habari inadai kuwa Bwana Bezos wa kampuni ya Amazon hakulipa kodi yoyote mwaka 2007 na mwaka 2011 huku Bwana Tesla Musk akiwa hakulipa chochote mwaka 2018.
Msemaji wa Ikulu ametaja uvujaji wa taarifa hizo kuwa "kinyume cha sheria", na kwamba shirika la FBI na mamlaka ya ukusanyaji ushuru zinafanya uchunguzi.
Tovuti ya ProPublica imesema kwamba ilikuwa inafanya kile ilichokiita "uchunguzi wake kuhusu takwimu za ndani ya ulipaji ushuru" kwa mabilionea na kuwa itatoa taarifa zaidi wiki chache zijazo.
Huku BBC ikiwa haijafanikiwa kuthibitisha madai hayo, taarifa zilizovuja zinawadia wakati ambapo kuna mjadala mkubwa kuhusu kiwango cha kodi wanachotakiwa kulipa na kuchangia kuongeza pengo kati ya matajiri na maskini.
Tovuti ya ProPublica ilisema kuwa watu 25 tajiri zaidi duniani wanalipa kiwango cha chini cha kodi - wastani wa asilimia 15.8 cha mapato yao ya jumla - ikilinganishwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wa Marekani.
Jesse Eisinger, mwanahabari mwandamizi na mhariri wa ProPublica, ameelezea kipindi cha Today kuwa: "Tulishangaa sana kujua kwamba kodi yako inaweza kwa sifuri kabisa ikiwa wewe ni bilionea. Kutolipa chochote ndiko kuliko tushangaza zaidi. Matajiri wanaweza kukwepa mfumo huo kwa njia halali kabisa."
"Wana uwezo mkubwa wa kupunguziwa kodi na kutumia vibaya mianya iliyopo," alisema.
Kwa hiyo, wakati utajiri wao unaongezeka pakubwa kupitia umiliki wa hisa katika kampuni zao, hilo halirekodiwi kama mapato.
Lakini pia kuna zaidi ya hilo, alisema: "Pia wanapunguziwa pakubwa kodi mara nyingi kwasababu wameomba mikopo kuwezesha miradi yao."
Alisema kuwa mabilionea wa Marekani wanaweza kununua mali, wakajenga utajiri wao au kurithi utajiri na kisha wakaomba mikopo licha ya utajiri walio nao.
Kwasababu hawapati faida yoyote au kuuza chochote, inachukuliwa kwamba hawaingizi mapato ambayo yanaweza kukatwa kodi.
"Kisha wanakopa benki kwa riba ya chini, na kutumia kiwango hicho kama chanzo cha pesa zao na pia wanaweza kutumia gharama za riba kama njia ya kupunguziwa kodi katika mapato yao," ameelezea.
Mipango ya Biden
Tovuti hiyo imesema kuwa "kwa kutumia mikakati kabambe ya kodi kisheria, matajiri wengi wameweza kupunguza kodi zao hadi kufikia sifuri au karibu na kuwa hakuna chochote wanacholipa "hata wakati ambapo utajiri wao unaongezeka katika kipindi cha miaka michache iliyopita.
Matajiri hao wamefankiwa kupunguza gharama za kodi katika mapato yao kupitia mambo kama vile utoaji misaada na kupata pesa kutokana na mapato ya uwekezaji badala ya mapato ya mshahara.
Tovuti ya ProPublica, kwa kutumia data ya jarida la Forbes, imesema kuwa matajiri 25 wa Marekani utajiri wao uliongezeka hadi dola bilioni 401 kutoka mwaka 2014 hadi 2018 - lakini walilipa kodi ya dola bilioni 13.6 kama ushuru katika kipindi hicho.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Joe Biden ameahidi kuongeza kodi kwa Wamarekani matajiri kama sehemu ya mpango wake wa kuimarisha usawa na kupata pesa za mradi wake wa uwekezaji katika miundo mbinu.
Anataka kuongeza kiwango cha kodi , kuongeza mara dufu kile wanachopata matajiri kutokana na uwekezaji na kubadilisha kodi ya urithi.
Hata hivyo, utafiti wa tovuti ya ProPublica umehitimisha kuwa: "Wakati baadhi ya matajiri Marekani watakuwa wanalipa kodi zaidi chini ya pendekezo la utawala wa Biden, idadi kubwa kati ya matajiri 25 watashuhudiwa mabadiliko kidogo tu."
Mmoja wa mabilionea ambaye amekuwa mtoaji mkubwa wa misaada George Soros, pia naye anadaiwa kulipa kiwango cha chini cha kodi. Hata hivyo, ofisi yake haikujibu ombi la BBC la kutaka kutoa maoni yake kuhusiana na suala hilo lakini ikasema katika taarifa yake kwa tovuti ya ProPublica kwamba Bwana Soros hakutakiwa kulipa kodi kwa miaka kadhaa kwasababu ya hasara aliyokuwa anapata katika uwekezaji wake.
Uvujaji wa taarifa hizo ni 'kinyume cha sheria'
Kulingana na ripoti za Marekani, Michael Bloomberg, aliyekuwa meya wa New York ambaye taarifa zake za kodi zilikuwa miongoni mwa zilizochunguzwa, amesema kuwa uchapishaji wa taarifa hizo kumezua wasiwasi kuhusu faragha ya mtu na huenda akatumia "njia halali" kugundua chanzo cha uvujaji wa taarifa hizo.
ProPublica, tovuti ya taarifa za uchunguzi, imeandika makala kadhaa kuhusu vile kupunguzwa kwa pesa za matumizi katika mamlaka ya utozaji ushuru kumeathiri uwezo wake wa kutekeleza kikamilifu sheria za kodi kwa matajiri na mashirika makubwa.
Shirika hilo la habari limesema kuwa lilipata nyaraka zilizovuja kama majibu ya makala ambayo imekuwa ikitayarisha.
Katibu wa habari Ikulu Jen Psaki amesema kuwa "utoaji wa taarifa zozote zile za serikali bila idhini" ni kinyume cha sheria.
Afisa wa mamlaka inayoshughulikia mapato ya ndani Marekani, Charles Rettig amesema: "Siwezi kusema lolote kuhusu walipa kodi. Ninachoweza kuthibitisha ni kwamba uchunguzi unaendelea kuhusiana na madai kwamba chanzo cha taarifa hizo katika makala iliyoandikwa ni afisa wa mamlaka ya utozaji ushuru."














