Wadukuzi wa Urusi walenga mashirika ya misaada, yasema Microsoft

Picha ya mdukuzi akitumia Kompyuta

Chanzo cha picha, AFP via GETTY

Microsoft imesema wimbi jingine la shambulio la kimtandao la Urusi limelenga mashirika ya serikali na vikundi vya haki za binadamu katika nchi 24,mengi ya nchini Marekani.

Ilisema karibu akaunti 3,000 za barua pepe katika mashirika zaidi ya 150 zilishambuliwa wiki hii.

Kundi lililohusika lilikuwa lile lile lililofanya mashambulio ya SolarWinds ya mwaka jana, ambayo Huduma ya Upelelezi wa Mambo ya nje ya Urusi (SVR) inatuhumiwa kwa kuratibu , Microsoft ilisema.

Urusi imekataa mashambulizi yote ya kimtandao.

Kremlin Ijumaa ilisema haina ufahamu wa matukio ya udukuzi ya hivi karibuni, na ikaitaka kampuni kubwa ya teknolojia ya Marekani kujibu maswali zaidi, pamoja na jinsi matukio hayo yalivyohusishwa na Urusi.

Ni kwa namna gani udukuzi ulifanyika?

Katika chapisho la blogu lililochapishwa Alhamisi, Microsoft ilisema mashambulio hayo mapya yalilenga mashirika ya serikali yaliyohusika katika sera za kigeni kama sehemu ya "juhudi za kukusanya taarifa za kiintilejensia".

Imesema karibu robo ya mashirika yaliyolengwa yalishiriki katika maendeleo ya kimataifa, kazi za kibinadamu na haki za binadamu.

Wakati mashirika mengi ni yaliyoko Marekani, waliolengwa wanatoka nchi takribani 24.

Kwa mujibu wa Microsoft, Nobelium, kundi lililoundwa Urusi, lilitekeleza mashambulizi ya wiki hii kwa kupata akaunti ya uuzaji za barua pepe zinazotumiwa na shirika la misaada la Marekani USAID.

Microsoft ilisema akaunti 3,000 za barua pepe zilidukuliwa

Chanzo cha picha, Reuters

Wadukuzi walituma barua pepe ambazo zilionekana kuwa za kweli lakini zilijumuisha tovuti ambayo mtu anapobofya data huibiwa na kuathiri mtandao wa kompyuta nyingine.

Msemaji wa Wakala wa Usalama wa Kimtandao na Usalama wa Miundombinu (Cisa) aliiambia Mamlaka ya Shirika la Habari za CBS kuwa walikuwa wanajua juu ya shambulio hilo na walikuwa wakijaribu "kuelewa zaidi kiwango cha athari zilizojitokeza na waathirika''.

Microsoft ilisema mashambulizi mengi yanayowalenga wateja wake yalizuiliwa moja kwa moja. Haikufahamika mara moja ni majaribio mangapi yalifanikiwa.

Mwaka jana, wadukuzi walitumia jukwaa la kampuni ya Marekani ya SolarWinds 'Orion kulenga idara za serikali za Marekani, karibu kampuni binafsi 100 na idadi ndogo ya mashirika ya Uingereza. Mwishowe, karibu wateja 18,000 waliweka programu hiyo ya udanganyifu.

SVR ilishutumiwa na Uingereza na Marekani kwa udukuzi huo. Lakini ilikana shutuma hizo.

Mkuu wa SVR aliiambia BBC kuwa haihusiki na kampeni hiyo ya mwisho, hata akidokeza Marekani ingeweza kujidukua yenyewe. Na sasa Microsoft imegundua kampeni mpya na kikundi hicho hicho.

Itaongeza swali tena - katika mkutano kati ya Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin katika wiki chache - kuhusu kama kuna jambo lolote linaloweza kufanywa kudhibiti tishio hili.