Mzozo wa Taiwan na China: Fahamu kwanini Marekani ilitaka kuishambulia China kwa bomu la nyuklia

Wanamikakati wa jeshi la Marekani walisisitiza kuishambulia China kwa kutumia bomu la nyuklia mwaka 1958 ili kuilinda Taiwan.

Mchambuzi wa zamani wa jeshi hilo Daniel Ellsberg , ambaye anajulikana kwa 'Pentagon papers' amedai tukio hilo kwa kuchapisha stakhabadhi za siri mtandaoni.

Pia imedaiwa kwamba wanamikakati wa jeshi la Marekani wakati huo pia waliamini kwamba muungano wa Usovieti ungewasaidia wandani wao China na silaha za kinyuklia ambazo zingewaua watu wengi zaidi.

Kulingana na ripoti hiyo iliochapishwa katika gazeti la Marekani la New York Times , wanamikakati wa Marekani walikuwa tayari kugharamikia shambulio hilo ili kuilinda Taiwan.

Baadhi ya ripoti za stakhabadhi hizo za siri ambayo imewekwa wazi na Danile Ellsberg , kwa mara ya kwanza zilichapishwa 1975.

Mchambuizi huyo mwenye umri wa miaka 90 aligonga vichwa vya habari 1971 wakati alipovujisha utafiti wa ngazi za juu uliohusiana na vita vya Vietnam kwa vyombo v ya habari vya Marekani katika kile kilichojulikana kuwa 'Pentagon papers

Aliambia The Times kwamba alikuwa amechukua nakala zenye siri kuu za utafiti huo kuhusu mzozo wa Taiwan mapema mwaka 70, lakini sasa ameanza kuzitoa kwasababu kuna wasiwasi mkubwa kati ya Marekani na China kuhusu Taiwan.

Kulingana na waadishi wa stakhabadhi hizo , kamanda wa jeshi jenerali Nathan Twining aliweka wazi kwamba iwapo kungekuwa na uvamizi, Marekani ingetumia silaha ya kinyuklia dhidi ya kambi za jeshi la angani la China ili kuzuia mashambulizi ya angani ya China.

Uamuzi

Stakhabadhi hizo zilimnukuu Twinning akisema , iwapo hilo halitazuia shambulio , basi kutakuwa hakuna njia mbadala ya kwenda Kaskazini mwa Shanghai ndani ya China ili kutekeleza shambulio la kinyuklia.

Lakini rais wa Marekani wakati huo DD Eisenhower aliamua kutegemea silaha za kawaida.

Mzozo wa 1958 ulikwisha wakati wanajeshi wa China walipositisha mashambulizi ya mabomu katika visiwa hivyo vinavyodhibitiwa na Taiwan , na kuacha eneo hilo chini ya udhibiti wa vikosi vya kitaifa chini ya Chiang Kai-shek.

China inaichukulia Taiwan kuwa chini ya udhibiti wake .

Marekani inaitambua China tangu 1979 lakini inachukulia Taiwan kama mshirika wake.

Kama mataifa mengine, Marekani haina uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan.

Lakini chini ya sheria yake, Marekani inaweza kuisaidia Taiwan kujilinda.

Hivi majuzi , Marekani ilionya kuhusu uchokozi wa China dhidi ya Taiwan.

China inaichukulia Taiwan kama ardhi yake china ya sera ya Umoja wa China, huku Taiwan ikijichukulia kuwa taifa huru.

China na Taiwan

Tangu mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini China 1949, kumekuwa na serikali tofauti zinazoongoza maeneo hayo.

China kwa muda mrefu imejaribu kupunguza vitendo vya Taiwan vya kimataifa . Zote zimetafuta kuzishawishi nchi za Pacific .

Kumekuwa na hali ya wasiwasi katika miaka ya hivi karibuni na China haijafuta utumiaji wa nguvu ili kuidhibiti Taiwan .

Ijapokuwa Taiwan inatambuliwa rasmi na baadhi ya mataifa, serikali yake iliochaguliwa kidemokrasia ina uhusiano mzuri wa kibiashara na mataifa mengi.

Kama mataifa mengi, Marekani haina uhusiano wa kidemokrasia na Taiwan , lakini sheria yake inatoa haki kwa taifa hilo kuisaidia Taiwan ijilinde.

Wasiwasi wa Marekani

Wataalamu wanasema kwamba China inaendelea kuwa na wasiwasi kuhusu ukweli kwamba serikali ya Taiwan inaelekea kujitangaza rasmi kuwa huru.

China inataka kuionya Taiwan kutochukua hatua hiyo.

Hatahivyo rais aliyepo madarakni wa Taiwan Sai ing Wen ameripoti kusema kwamba Taiwan ni taifa lililo huru.

Anasema kwamba hakuhitaji kuwepo kwa tangazo rasmi kufanya hivyo.

Taiwan ina katiba yake , jeshi lake na viongozi wake waliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Hathivyo China haijapinga uwezekano wa kutumia nguvu ili kuunganisha Taiwan.