Musta'ribeen: Kikosi Sugu cha Israel kinachowasaka Wapalestina wanaodaiwa kutishia usalama wa Israel

Jeshi la anga la Israel limesema kuwa limemuua Ali Qadhi, kamanda wa Hamas aliyeongoza shambulio la mpakani dhidi ya makaazi ya walowezi wa Israel Jumamosi iliyopita.
Jeshi la Israel limesema Ali Qadhi aliuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani kufuatia juhudi za kijasusi za shirika la usalama la Shin Bet na Kurugenzi ya Ujasusi ya Kijeshi. Israel ina vikosi mbali mbali maalum ambavyo vinahusika na oparesheni za kiusalama katika maeneo yake na kwenye sehemu zinazokaliwa za Ukanda wa Gaza na West bank .
Kati ya vikosi hivyo hakuna kinachoogopwa sana kuliko kikosi sugu kwa jina Musta'ribeen .
Kikosi hiki wakati mwingi huvalia kama Wapalestina na hata wanachama wake wanazungumza kama Wapalestina na kufanya mambo yote kuonekana kama Wapalestina .
Wakati wa maandamano , wanachama wa kikosi hiki huwa upande wa waandamanaji na hata kuwarushia mawe wanajeshi wa Israel na kutoa kauli za kuikashifu Israel .
Nyuso zao hufunikwa na keffiyehs au balaklava, lakini mbinu hiyo huwa ya kuwahadaa Wapalestina kujiunga na maandamano na pindi wanapokaribia wanajeshi wa Israel kundi hili ghafla linawageukia waandamanaji wengine wa Palestina, wakifyatua risasi hewani kutumia bunduki ambazo huwa zimefichwa chini ya mashati yao, na kuwakamata wale walio karibu nao.

Chanzo cha picha, EPA
Jeshi kisha hufika na kuendelea kuwakamata Wapalestina wanaohusika katika maandamano hayo. Wakati waandamanaji wengine wanapotawanyika, wao hupiga kelele na kutoa neno moja kama onyo kwa wengine: "Musta'ribeen!" Na hiyo huwa ishara kwamba kikosi hicho maalum cha Israel kipo ndani yao na tayari kinafanya oparesheni .
Wanafanya kila kitu kama Waarabu
Musta'ribeen, au mista'arvim kwa Kiebrania, ni neno ambalo limetokana na Kiarabu "musta'rib", au mtu anayejua lugha ya Kiarabu na utamaduni. Katika suala la usalama la Israeli, neno hilo linaashiria vikosi vya usalama vinavyojifanya kama Waarabu na kutekeleza misheni katikati ya jamii za Wapalestina au nchi nyingine za Kiarabu.
Majasusi hao wanapewa mafunzo mazito, na katika shughuli zinazohusu maeneo yanayokaliwa, wanafundishwa kufikiria na kutenda kama Mpalestina. Kazi yao kubwa , kulingana na mtaalam wa maswala ya Israeli Antoine Shalhat, ni pamoja na kukusanya habari za ujasusi, kuwakamata Wapalestina, na - machoni mwao - operesheni za za kupambana na ugaidi.
"Kitengo cha kwanza cha musta'ribeen kilianzishwa mnamo 1942 kabla ya taifa la Israeli kuanza hadi 1950," Shalhat alisema. "Kitengo hiki kilikuwa sehemu ya Palmach, kundi la wanamgambo wa Haganah, ambao baadaye waliunda sehemu kubwa ya jeshi la Israeli."
Mengi hayajulikani kuhusu kikosi hicho kwa sababu wanafanya kazi kwa siri, aliongeza. Jeshi la Israeli huvunja vitengo hivi mara tu kazi yao inapojulikana na kuunda vipya kuchukua nafasi zao.
" Maajenti lazima wazungumze Kiarabu kana kwamba ni lugha yao ya mama," Shalhat alisema. "Wanasoma kozi za lahaja za Palestina na lafudhi za Kiarabu kulingana na nchi gani ya Kiarabu wanayofanya kazi, kama vile Yemen au Tunisia."

Chanzo cha picha, AFP
Kozi hizi huchukua kati ya miezi minne hadi sita na zinajumuisha jinsi ya kutekeleza mila na mazoea ya kidini, kama vile kufunga na kuomba
Maajenti hutumia vipodozi na wigi ili kujificha lakini huchaguliwa kulingana na jinsi sura zao na maumbile yao zinavyofanana na nyuso za waarabu.
Kwa jumla, mafunzo yanaweza kuchukua hadi miezi 15, na inajumuisha mafunzo kuhusu mapigano na kazi kama kuendesha gari na kupiga picha, jinsi ya kuzunguka katika mazingira ya Wapalestina waliojaa, na mafunzo ya silaha.
"Moja ya vitengo vinavyojulikana zaidi ni Rimon, ambayo ilianzishwa mnamo 1978 na ikabaki hadi 2005," Shalhat alisema. "Kazi yao ilikuwa imejikita zaidi katika Ukanda wa Gaza. Kitengo kingine kilichofanya kazi huko Gaza kiliitwa Shimshon wakati wa miaka ya 80 na 90. "
"Kitengo maalum cha Duvdevan 217 bado kinafanya kazi ndani ya jeshi. kilianzishwa wakati wa miaka ya 1980 na [waziri mkuu wa zamani wa Israeli] Ehud Barak na kwa sasa kinafanya kazi katika Ukingo wa Magharibi na kina usiri mkubwa. "
Mauaji ya hivi karibuni
Mauaji ya hivi karibuni ya kikosi hicho yalitekelezwa siku ya jumanne katika eneo la West Bank katika mji wa Ramallah ambapo mwanamme mmoja Ahmad Jamil Fahd, kutoka kambi ya wakimbizi ya al-Amari aliuawa kwa kupigwa risasi mara kadhaa na maafisa wanaodaiwa kuwa wa Musta'ribeen. Mashahidi wanasema mwanamme huyo alipigwa risasi na akaachwa akivuja damu kwa muda kisha akafa kabla ya gari la ambulansi kuitwa .
Mauaji yake yalifanyika siku ambayo waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baadye alikutana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas .













