Balozi wa Ubelgiji Korea Kusini aomba msamaha baada ya mke wake kumpiga kofi mfanyakazi wa dukani

Maelezo ya video, Xiang Xueqiu anaonekana kwenye CCTV akimsukuma na kumpiga kofi mfanyakazi mmoja wa dukani

Balozi wa Ubelgiji nchini Korea Kusini ameomba msamaha baada ya mke wake kufanya kitedo kisichokubalika wakati akiwa anakabiliana kwa maneno na mfanyakazi wa duka moja mjini Seoul.

Kupitia CCTV iliyooneshwa kwa umma, inamuonesha mke wake Peter Lescouhier, Xiang Xueqiu, akimpiga kofi msaidizi wa duka la kuuza nguo.

Mfanyakazi huyo alikuwa akitaka kuangalia nguo alizokuwa anaondoka nazo ikiwa ni zake kukiwa na wasiwasi kwamba huenda ameiba.

Ubalozi wa Ubelgiji huko Seoul umesema kuwa Bi. Xiang, 63, sasa hivi anaendelea kupata matibabu hospitali baada ya kupata kiharusi.

Atashirikiana na polisi katika uchunguzi unaoendelea kuhusu tukio hilo punde atakapoweza kufanya hivyo, taarifa hiyo imesema.

Tukio hilo lilifanyika Aprili 9 katika duka la kuuza nguo huko Yongsan-gu, Seoul.

Bi. Xiang alikuwa kwenye duka hilo akijaribu nguo kwa karibu saa moja kabla ya kuondoka, vyombo vya habari vya Korea Kusini vimesema.

Na akafuawa na mfanyakazi mmoja wa duka hilo ambaye alitaka kuangalia nguo ambazo amevaa kwa ndani kama ni zake.

Mke huyo wa balozi inasemekana kuwa alimfuata mfanyakazi huyo hadi kwenye duka hilo na katika makabiliano kama inavyoonekana kwenye CCTV, alionekana kumsukuma na kumpiga kofi mfanyakazi mwingine ambaye alijaribu kuingilia makabiliano yao.

Blurred image of shop worker with swollen red face

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mfanyakazi wa dukani aliyepigwa kofi amelalamika kuwa shavu lake limefura

"Sikumjua mwanamke huyo ni nani wakati ninashambuliwa, lakini alionekana kujiamini kweli na wala hakuonekana kuwa tayari kuomba msamaha," Amesema mfanyakazi wa pili, ambaye alilalamika kuwa shavu lake limefura baada ya kupigwa kofi, kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari vya Korea Kusi

Taarifa kutoka ubalozini inaonesha Bwana Lescouhier amesema "anajutia tukio hilo" na "anaomba msamaha" kwa niaba ya mke wake.

"Haijalishi hali ilivyokuwa, alivyofanya haikubaliki," aliongeza.

Bi. Xiang hajaweza "kufika kwenye kituo cha polisi kwasababu anapata matibabu baada ya kuuguwa kiharusi mwanzoni mwa wiki iliyopita.

"Ni matumaini yetu kuwa afya yake itaimarika haraka, ili aweze kusaidia polisi kwa uchunguzi wao, sote tuweze kusahau tukio hili la kusikitisha."

Tukio hilo limesababisha hasira nchini Korea Kusini huku kukiwa na madai ya kwamba Bi. Xiang atapata kinga ya msamaha na kuepuka kufunguliwa mashitaka.