Wanawake ambao mimba zao zitaharibika au kuzaa mtoto aliyefariki wanaruhusiwa kuchukua likizo New Zealand

Muda wa kusoma: Dakika 1

Wanandoa nchini New Zealand ambao mimba ya mke imeharibika au mtoto amefariki dunia kabla ya kuzaliwa wanaruhusiwa kuchukua likizo ya kulipwa chini ya sheria mpya iliyopitishwa na bunge.

Mbunge Ginny Andersen, aliyewasilisha mswada huo, alisema kwamba sheria hiyo itaruhusu kina mama na wenzi wao kupata nafasi ya kujifariji na "kukubali yaliyowatokea" bila kuchukua liziko ya kuugua.

Mswada huo pia unajumuisha wale ambao watapoteza watoto waliokuwa watawapata kwa njia ya kuasili au kupitia mama anayekubali kumzalia mwanamke mwingine mtoto.

New Zealand inasemekana kuwa nchi ya pili tu kote duniani kuanzisha sheria hiyo baada ya India.

Sheria hiyo ambayo ilipitishwa kwa kauli moja na bunge, inatoa siku tatu za maombolezi.

Bwana Anderson alisema kuwa mwanamke mmoja kati ya wanne nchini New Zealand mimba yake imewahi kuharibika na ana imani kwamba sheria mpya iliyopitishwa, itawapa "muda wa kukubali yaliyotokea bila ya wao kutumia likizo ya kuugua".

"Wakati huo wa kuomboleza sio kwamba mtu ni mgonjwa, lakini amempoteza mtu wake wa karibu. Na kukubali kufiwa inachukua muda," alisema.

Mwaka mmoja uliopita, bunge lilipitisha mswada wa marekebisho uliohalalisha utoaji mimba na kuwaruhusu wanawake kuwa na uwezo wa kuavya mimba ya hadi wiki 20.