Mahakama ya ICC yaanza uchunguzi wa 'uhalifu wa kivita' maeneo ya Palestina

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya the Hague Fatou Bensouda

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 1

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa amefungua uchunguzi rasmi wa madai ya uhalifu wa kivita katika maeneo ya Palestina.

Fatou Bensouda alisema uchunguzi huo utahusu matukio katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli, Mashariki mwa YerusalemU na Ukanda wa Gaza tangu 13 Juni 2014.

Mwezi uliopita, Mahakama ya Hague iliamua kwamba inaweza kutumia mamlaka yake juu ya maeneo hayo.

Israeli ilipinga uamuzi wa Bi Bensouda, wakati maafisa wa Palestina wakiusifu

ICC ina mamlaka ya kuwashtaki wale wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika eneo la nchi zinazohusika na Mkataba wa Roma, mkataba wake wa msingi.

Israeli haijawahi kuridhia Mkataba wa Roma, lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikubali kutawazwa kwa Wapalestina mnamo 2015.

Bi Bensouda alisema alikuwa amefanya "uchunguzi wa awali" ambao ulidumu kwa karibu miaka mitano na akaahidi kuwa uchunguzi huo utafanywa kwa uhuru, bila upendeleo na kwa malengo, bila woga au upendeleo.

ICC iliahidi kufanya uchunguzi kwenye eneo la Palestina

Chanzo cha picha, Anadolu Agency

"Hatuna ajenda nyingine isipokuwa tu kukidhi majukumu yetu ya kisheria chini ya Sheria ya Roma kwa uadilifu wa kitaaluma,"

"Katika hali ya sasa, hata hivyo, kuna msingi mzuri wa kuendelea na kuna kesi zinazoweza kukubalika," ameongeza.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema uamuzi wa kufungua uchunguzi ni "kielelezo cha chuki dhidi ya Wayahudi na unafiki".

"Taifa la Israeli linashambuliwa usiku wa leo," alionya.

"Korti iliyoundwa kuzuia kutokea tena kwa ukatili unaofanywa na Wanazi dhidi ya watu wa Kiyahudi sasa inageuka dhidi ya Wayahudi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad al-Maliki alisema: "Uhalifu uliofanywa na viongozi wa uvamizi wa Israeli dhidi ya watu wa Palestina - ambao unaendelea, unafanya uchunguzi huu kuwa muhimu na wa haraka."

Kundi la waangalizi wa Haki za Binadamu la Marekani limesema uamuzi huo "unawasogeza waathirika wa Israeli na Wapalestina wa uhalifu mkubwa hatua moja karibu kupata haki ambayo waliitafuta kwa muda mrefu.