Virusi vya corona: Ubalozi wa Marekani wawaonya watu wanaotaka kusafiri nchini Tanzania

Muda wa kusoma: Dakika 3

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umeonya wasafiri wanaotaka kutembelea taifa hilo kutofanya hivyo kutokana na uwepo wa maambukizi makubwa ya virusi vya corona na kwamba serikali haijatoa takwimu zozote tangu ilipofanya hivyo mwezi Aprili mwaka jana.

Taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani inasema taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kipindi chote cha mlipuko wa corona halijaweka marufuku ya kutoka nje kwa raia wake lakini pia halijachukua hatua nyingine kama kutoa miongozo ya namna bora za mikusanyiko kufanyika na matumizi ya usafiri wa umma.

Onyo hili la Marekani linakuja siku chache baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kusema kuwa serikali yake haijamzuia mtu yeyote kuvaa barakoa, japo anashauri matumizi ya barakoa zilizotengenezwa nchini akisema anaamini baadhi ya zile zinazoagizwa kutoka nje sio salama.

Kauli hiyo ya Bwana Magufuli aliyoitoa Jumapili katika kanisa moja jijini Dar es Salaam iliashiria kuwa amebadili msimamo wake kuhusu ugonjwa wa Covid 19. Kabla ya hapo, kiongozi huyo alisikika akibeza hadharani matumizi ya barakoa akisema nchi yake imefanikiwa kutokomeza maambukizi ya corona...Magufuli: 'Hatujazuia matumizi ya barakoa'

Hata hivyo kituo cha kupambana na magonjwa cha Marekani kinawaelekeza watu kutosafiri nchini Tanzani licha ya taifa hilo kusema liko salama kutokana na kutumia njia mbambali za asili ikiwemo kujifukiza na hata matumizi mimea na matunda.

Lakini shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeonya dhidi ya kutumia maji ya moto kwaajili ya kuoga kama sehemu ya kumaliza virusi, hii ni hatari sana unaweza kuungua... Je, kujifukiza ni tiba ya corona?

Mara kadhaa Rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli ameeleza kutokuwa na imani na chanjo ya corona inayotolewa kwingineko duniani na hata kuwalaumu baadhi ya watu waliokwenda ng'ambo na kupatiwa chanjo na ''kurejea na corona ya ajabu ajabu''

Rais Magufuli amekuwa akisisitizia kuwa vita ya uchumi ni kubwa na ni mbaya hivyo kuwataka raia wa Tanzania kusimama imara na kumtanguliza Mungu mbele kwani hakuna linaloshindikana kwake iwapo watamuomba kwa uaminifu.

Unaweza pia kusoma:

Hivi karibuni alitangaza siku tatu za maombi ambapo aliwataka waumini wa dini zote kufunga na kusali kuliombea taifa dhidi ya virusi vya corona hii ikiwa ni mara ya pili anawataka Watanzania kufanya hivyo.

Mwaka jana wakati maambukizi ya virusi hivyo yalipopamba moto kote duniani Rais Magufuli aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu na kusali na baadae kutangaza taifa hilo limeishinda corona kauli ambayo ameendelea kuishikilia na kuisisitiza ''kama mwaka jana tulishinda na mwaka huu tutashinda'', alisema wiki iliyopita.

Taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani inaonya kuwa huenda hospitali na vituo vya afya vikazidiwa na wagonjwa kutokana idadi kubwa ya watu kuambukizwa virusi vya corona, lakini upimaji wa virusi hivyo si wa uhakika kwani baadhi ya wale waliopimwa na kupatiwa vyeti vya kuonyesha hawana maambukizi hayo walipopimwa kwenye mataifa mengine walibainika kuwa na virusi hivyo.

Siku kadhaa zilizopita Oman nao walipiga marufuku wasafiri kutoka nchini Tanzania kuingia nchini humo, marufuku ambayo inatarajiwa kudumu kwa muda wa siku 15. Habari kutoka nchini Oman zinasema kuwa, hatua hiyo imetokana na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya udhitibi wa Corona nchini humo.

Kamati hiyo imewataka wananchi wa Oman kutosafiri nje ya nchi ili kuzuia maambukizi na ikibidi kusafiri basi kuwe na sababu maalum. Marufuku hiyo inatarajiwa kuathiri pakubwa wasafiri kutoka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwakwamba, kuna watu wengi wanaosafiri kila siku kuelekea Oman wakitokea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Unaweza pia kutazama:

Taarifa hiyo imekwenda mbali zadi na kuonya juu ya uwepo wa vitisho vya ugaidi kwenye maeneo ya kusini mwa Tanzania, Mkoa wa Mtwara ambao unapakana na nchi ya Msumbuji ambako kundi la dola la kiislamu IS lilatangaza uwepo wake mwaka jana.

Ubalozi wa Marekani unasema makundi ya kigaidi yanaweza kufanya mashambulizi kirahisi na kukiwa hakuna onyo kwa walengwa zikiwemo balozi, misikiti na maeneo yanayokaliwa na raia wa kigeni.

Katika kukabiliana na athari za mashambulio ya kigaidi, Tanzania imekuwa ikilinda eneo la mpaka wake. Mwezi Mei mwaka jana ilipeleka vikosi vyake kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na Msumbiji baada ya kuibuka kwa mashambulizi yaliyotekelezwa na wanamgambo kutoka kaskazini mwa Msumbiji, wanamgambo ambao wamekuwapo tangu mwaka 2017...Tanzania yapeleka wanajeshi wake mpakani na Msumbiji

Aidha taarifa hiyo umegusia juu ya haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kueleza kundi hilo limekuwa likibugudhiwa kwa namna mbali mbali nchini Tanzania na wakati mwingine hata kukamatwa na kutuhumiwa kwa tuhuma mbali mbali na wakati mwingine hata kufanyiwa vipimo kwa nguvu.

Licha ya kuwepo kwa taarifa za unyanyasaji dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ya Mambo ya nje mwaka 2018 ilitoa tangazo lake rasmi, kujitenga na hatua ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyekuwa ameanzisha kampeni ya kuwakamata na kuwashitaki ''mashoga''...Serikali ya Tanzania 'yamruka' Makonda

Taarifa hiyo ilisema kuwa kampeni hiyo ilikuwa ni mawazo binafsi ya Makonda na si msimamo rasmi wa serikali na kwamba serikali itaendelea kuheshimu miaktaba yote ya kimataifa ambayo imesaini na kuiridhia.