Ngozi Okonjo awa Mwafrika na mwanamke wa kwanza kuongoza Shirika la biashara la dunia

Mwanamama Ngozi Okonjo-Iweala kutoka Nigeria ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara duniani (WTO)

Dkt . Okonjo -Iweala ameweka historia kuwa mwanamke wa kwanza, na Mwafrika wa kwanza kuongoza WTO.

Muhula wake utaanza tarehe 1 mwezi Machi mwaka 2021.

Mkutano wa baraza kuu la shirika hilo limefikia hatua hiyo baada ya kupitia mchakato wa mchujo uliowahusisha wagombea wanane kutoka duniani kote.

Licha ya kwamba hivi karibuni alipata uraia wa Marekani, alisema kwamba yeye ni raia wa Nigeria na kujivunia kuwa mzalendo - mwafrika aliyekuwa amevaa nguo yenye utambulisho wa Afrika maarufu kama kitenge.

Akizungumza na BBC mwaka 2012, alisema kwamba yeye kama mama anayefany akazi mwenye watoto wanne, anapenda sana nguo za aina hiyo, ni nzuri na pia gharama yake ni ya chini.

Akiwa amehitimu katika chuo kikuu cha Havard, mwanamke huyo mwanauchumi anaonekana kuwa mnyenyekevu na mchapa kazi, akizungumza na kipindi cha HardTalk cha BBC mnamo mwezi Julai, alielezea kuwa kile kinachohitajika katika Shirika la Biashara Duniani ni mabadiliko.

"Wanahitaji kitu tofauti, haiwezekani mambo yakawa yanachukuliwa kama kawaida tu kwa WTO - [wanahitaji] mtu ambaye yuko tayari kufanya mabadiliko na kuongoza."

Wasifu wake

Alizaliwa mwaka 1954 nchini Nigeria

Alisomea Harvard 1973-76 na kupata PhD yake katika Chuo cha Teknolojia cha Massachusetts (MIT) mwaka 1981

Alifanya kazi katika Benki ya Dunia kwa miaka 25 na kupanda ngazi hadi wadhifa ambao ni wa pili kiuongozi kama mkurugenzi (2007-11)

Alikuwa waziri wa fedha nchini Nigeria mara mbili - 2003-2006 na 2011-2015 - na mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo

Alikuwa waziri wa mambo ya nje kwa kipindi kifupi mwaka 2006 na pia mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo

Pia ni mwanachama wa bodi za Twitter, Benki ya Standard Chartered na Shirika la Kimataifa la ushirikiano wa Chanjo Duniani (GAVI)

Aliteuliwa na rais Mohammadu Buhari kuwa mgombea wa wadhifa wa WTO Juni 2020.