Mapinduzi Myanmar: Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya viongozi

Maandamano ya Yangon dhidi ya mapinduzi ya tarehe 10 mwezi Februari

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha agizo la watendaji kuweka vikwazo kwa viongozi wa mapinduzi ya Myanmar.

Hatua hizo zimechuliwa dhidi ya viongozi wa jeshi, familia zao na wafanyabiashara wanaohusishwa nao.

Hatua pia zinachukuliwa kuzuia jeshi kuzipata fedha kiasi cha dola bilioni 1 pesa za serikali zinazoshikiliwa Marekani.

Vikwazo hivyo vinakuja wakati ambao mwanamke aliyepigwa risasi kichwani wakati wa maandamano akipigania maisha yake hospitalini katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw.

Mya Thwe Thwe Khaing alijeruhiwa Jumanne wakati polisi walipojaribu kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia maji, risasi za mpira na risasi za moto.

Maelfu wamejitokeza katika maandamano ya barabarani kupinga mapinduzi ya wiki iliyopita, ambayo yalipindua serikali ya Aung San Suu Kyi iliyochaguliwa kidemokrasia licha ya marufuku ya hivi karibuni ya mikusanyiko mikubwa na amri ya kutotoka nje usiku.

Kumekuwa na ripoti za majeraha mengine mabaya kwani polisi wameongeza matumizi ya nguvu, lakini hakuna vifo hadi sasa.

Bw. Biden anahitaji nini?

Bwana Biden alitaka mapinduzi hayo yabatilishwe na kuachiliwa kwa viongozi wa raia akiwemo Bi Suu Kyi.

"Watu wa Burma wanapaza sauti zao na ulimwengu unaangalia," alisema, akiapa kuchukua hatua zaidi ikiwa itahitajika.

"Wakati maandamano yakishika kasi, vurugu dhidi ya wale wanaotumia haki zao za kidemokrasia haikubaliki na kupaza sauti ili vitendo hivyo vikome," ameongeza.

Wahudumu wa gari la kubeba wagonjwa walijiunga kwenye maandamano

Chanzo cha picha, EPA

Alisema utawala wake utabainisha awamu ya kwanza ya malengo ya vikwazo wiki hii, ingawa viongozi wengine wa jeshi la Myanmar tayari wameorodheshwa kutokana na ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

"Pia tutaweka udhibiti mkubwa wa mauzo ya nje. Tunazuia mali za Marekani ambazo zinafaidisha serikali ya Burma, wakati tunadumisha msaada wetu kwa huduma za afya, mashirika ya kijamii, na maeneo mengine ambayo yanawanufaisha watu wa Burma moja kwa moja," alisema. .

Hii ni hatu ya kwanza ya vikwazo kutangazwa na Bwana Biden tangu aingie madarakani mwezi uliopita.

Kinachojiri Myanmar

Wanajeshi wamekuwa wakifanya uvamizi na kufanya ukamataji zaidi wakati maandamano yakiendelea.

Kamatakamata ya hivi karibuni imefanyika dhidi ya maafisa wa serikali za mitaa na maafisa wanaofanya kazi kwenye tume ya uchaguzi, ambayo imekataa kuunga mkono madai ya jeshi ya udanganyifu mkubwa wa uchaguzi katika uchaguzi wa Novemba ambao ulifuta NLD ya Bi Suu Kyi.

Watu wakiwa na mishumaa na maua kwa ajili ya msichana aliyepigwa risasi siku ya Jumanne

Chanzo cha picha, AFP

Wakati huo huo, Mya Thwe Thwe Khaing bado yuko katika uangalizi mkubwa katika mji mkuu. Anatimiza miaka 20 leo.

Dada yake, Mya Tha Toe Nwe, ambaye pia alikuwa kwenye maandamano hayo, alisema uwezekano wa dada yake kunusurika ni mdogo.

"Inavunja moyo," alisema. "Tuna mama yetu tu, baba yetu tayari amefariki.

"Mimi ni mkubwa kati ya ndugu wanne, yeye ndiye wa mwisho. Siwezi kumfariji mama, hatuna maneno."

Maandamano ya hapo awali dhidi ya utawala wa kijeshi wa miaka mingi, mnamo mwaka 1988 na 2007, ulishuhudia idadi kubwa ya waandamanaji wakiuawa na vikosi vya usalama. Karibu waandamanaji 3,000 walikufa mwaka 1988 na watu wasiopungua 30 walipoteza maisha yao mnamo mwaka 2007. Maelfu walifungwa gerezani nyakati hizo.

Kwanini watu wanaandamana?

Wanajeshi walichukua udhibiti tarehe 1 Februari baada ya uchaguzi mkuu ambao Chama cha NLD kilishinda kwa kishindo.

Vikosi vya wanajeshi viliunga mkono upinzani, ambao walikuwa wakidai marudio ya zoezi la kura, wakidai kuwa kulikuwepo na udanganyifu

Mapinduzi yalifanywa wakati kikao kipya cha bunge kilipangwa kufunguliwa.

Bi Suu Kyi yuko chini ya kizuizi cha nyumbani na ameshtakiwa huku maafisa wengine wengi wa NLD pia wamewekwa kizuizini.