Dapivirine Copper: Je kifaa hiki kinaweza kuwalinda wanawake dhidi ya maradhi ya HIV?

Dawa inayowalinda wanawake dhidi ya HIV , inaonekana na wengi kuwa habari njema, sivyo?.

Licha ya uboreshwaji wa tiba na kinga , maradhi ya HIV bado yanaendelea kusambaa katika maeneo ya bara hili.

Katika eneo la mashariki na kusini mwa Afrika, zaidi ya watu milioni 20 wanaishi na virusi vya ukimwi.

Wanawake walio katika umri mdogo ndio walio katika hatari zaidi, wao wapo hatarini kuambukizwa virusi hivyo zaidi ya wanaume.

Lakini kifaa kipya ambacho kimeidhinishwa na shirika la Afya duniani WHO huenda kikawapatia wanawake udhibiti zaidi kuhusu afya yao ya tendo la ngono.

Ni mpira wa mduara unaovaliwa ndani ya uke ambao hutoa dawa ya kukabiliana na virusi hivyo Dapivirine.

Lakini je mpira huo una uwezo kiasi gani na ni akina nani watakaoruhusiwa kuvaa?

Je kifaa hicho kina umuhimu gani ikilinganishwa na mbinu nyengine?

Doreen Morah Moracha, 28, ambaye anaishi jijini Nairobi , Kenya anaishi na virusi vya HIV , anasema kuimarisha kinga ndio njia pekee ya kukabiliana na virusi vya ukimwi.

Moracha amekuwa akitumia mbinu za kujikinga dhidi ya maradhi hayo kwa kipindi cha miaka 16 .

Kwake yeye utumizi wa dawa hizo kwa maisha yake yote sio kitu rahisi.

''Nataka kila mtu alindwe kutokana na Ukimwi, kwasababu watu wengine wanafikiria ni rahisi , lakini kula dawa kwa maisha yako yote sio rahisi hata kidogo'', alisema.

Baadhi ya mbinu zinazotumiwa kujikinga dhidi ya HIV ni matumizi ya mipira ya kondomu.

Bi Moracha anasema kwamba wanawake huona vigumu kutumia mipira ya kondomu ya kike kwa kuwa sio wao wanaofanya maamuzi.

Anasema wanaume ndio wanaotumia sana mipira ya kondomu kwasababu wao ndio wanaofanya uamuzi.

''Wakati mwanamke anapoulizia kuhusu kinga mwanamume asiyetaka kutumia humpuuza''.

Pia kuna tembe zinazotumiwa kabla ya ngono kwa mtu ambaye hajaambukizwa virusi hivyo kwa jina [PREP] lakini hizo sio rahisi kuzipata.

Mduara huo unaovaliwa ndani ya uke huvaliwa kwa kipindi cha siku 28 , na katika kipindi hicho chote hutoa dawa aina ya Dapivirine ambayo humfanya mtu kujilinda dhidi ya virusi vya Ukimwi.

Anna Kukundakwe ambaye husimamia mipango katika kituo cha afya na haki za binadamu nchini Uganda anasema kwamba kitu muhimu ni kwamba mkewe anaweza kuvaa mduara huo bila usaidizi wa daktari.

''Mara kwa mara iwapo mwanamke anataka kufanya tendo la ndoa bila kutumia kinga sio rahisi kumuuliza mpenzi wake kuvalia mpira wa kondomu. Lakini mduara huu unalinda kwa siri hivyobasi hana haja ya kumwambia mwanamume kuvalia kondomu''.

Uchunguzi wa mduara huo umebaini kwamba hatari ya kuambukizwa virusi ni chini ya asilimia 30 .