Waridi wa BBC: 'Kwanini Lucy Mwikali alificha siri ya kubakwa zaidi ya mara 30'

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, 'Kwanini Lucy Mwikali alificha siri ya kubakwa zaidi ya mara 30
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Lucy Mwikali ni mwanamke ambaye alilazimishwa kufahamu mambo yaliozidi umri wake wa miaka 12 kwa kupotoshwa kwenye masuala ya ngono ya lazima.

Na alipofikisha umri wa miaka kumi na mbili, alibakwa na mtu aliyemtambua na kumuona kama baba yake .

"Mara yangu ya kwanza nilibakwa na mtu ambaye nilimuona kama baba, mimi na ndugu zangu tulillelewa na mama peke yake , kwa hivyo huyu mtu nilimpenda na kumuheshimu kama baba yangu mzazi . Nilisoma na binti wa mzee huyo na kwa hivyo kila mara nilijikuta tukiwa pamoja hata katika mazingira ya kwao nyumbani" anakumbuka Lucy Mwikali.

Lucy Mwikali mwenye umri wa miaka 43 bado anakumbuka siku ya kwanza alipoingiliwa kimwili kwa lazima .

Anasimulia kwa simanzi jinsi safari yake ya kurejea nyumbani baada ya kusaga unga wa mahindi ilivyomtumbukiza kwenye matata makubwa , ambayo yaliendeleza msururu wa kubakwa mara kwa mara katika maisha yake ya utotoni hadi alipotimiza umri wa mtu mzima .

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Lucy Mwikali mwenye umri wa miaka 43 bado anakumbuka siku ya kwanza alipoingiliwa kimwili kwa lazima

"Ilikuwa majira ya jioni na ilibidi nipitie barabara ambayo ilikuwa na vichaka vichaka , kutoka sokoni hadi kufika kwetu kuna mto na nilipokuwa nikivuka mto huo nilikutana na yule mzee ambaye nilikuwa namuona kama baba - alinishurutisha nitembee naye hadi shambani kwake kwa kisingizio cha kunipa mihogo na maembe nipeleke nyumbani kwetu .

Mara ghafla alinikaba koo kwa nguvu huku akiniambia kuwa iwapo ningejaribu kupiga mayowe au kusema chochote angeniuwa papo hapo alianza kunibaka " anakumbu ka Mwikali .

Mwikali anasema kuwa ni uchungu ambao ulimuumiza sana ikiwa mara yake ya kwanza kufanya tendo hilo ovu , lililpomuwacha na kumbukumbu nyingi.

Kuanzia hapo maisha yake yalichukua mkondo mpya na baada ya tendo hilo alifika nyumbani kwao akiwa amechelewa .

Anakumbuka kwamba unga aliokuwa ameenda kuusaga ulikuwa umemwagika na kwa kuwa ilikuwa muda wa usiku hakuna mtu aliyeshughulika kujua ni kipi ambacho kilisababisha yeye kuchelewa kurudi nyumbani.

Kwa kipindi cha wiki mmoja msichana huyo aliamua kutotoka ya chumba chake . Alimueleza mamake kuwa alikuwa anaumwa na kichwa.

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Kwa kipindi cha wiki mmoja msichana huyo aliamua kutotoka ya chumba chake . Alimueleza mama yake kuwa alikuwa anaumwa na kichwa.

Mama yake alikuwa anafanya biashara ya kuuza sokoni hivyo basi alikuwa akirudi nyumbani kuchelewa .

Mwikali alifika nyumbani na majeraha katika sehemu zake za siri pamoja na maumivu moyoni mwake . Bila kuzungumza na mtu yeyote alielekea kulala, jamii yake isijue mabaya yaliomkabilia mtoto wao .

Kwa kipindi cha wiki mmoja msichana huyo aliamua kutotoka ya chumba chake . Alimueleza mama yake kuwa alikuwa anaumwa na kichwa.

"Nilikuwa naogopa kusema chochote , kila wakati nilikumbuka tishio kutoka kwa mzee aliyenibaka la kuniuwa na nikaamua ninyamaze , tangu wakati huo nilianza kuwa msichana muoga ambaye hakuwa anajiamini hata kidogo" anakumbuka Mwikali "

Akiwa na kati ya miaka 14-15 alisafiri na kwenda kuishi na shangazi yake , akiwa kama kijakazi .

Kisa cha pili cha kubakwa kilifanywa na mume wa shangazi yake.

"Shangazi yangu alikuwa anaondoka kuelekea kazini alfajiri , mimi nilikuwa nabaki nyumbani na mtoto wao mdogo , naye mume wake alikuwa anaondoka baadaye , siku moja nadhani alimfinya mtoto wake wakiwa chumbani na aliniita ili nimchukue .

''Katika pilikapilka za kujaribu kumpakata mtoto , yule bwana alinishika kwa nguvu na papo hapo kunibaka "anasimulia.

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Ni kisa kilichomuacha na machungu mengi , kiasi cha yeye kujaribu kujitoa uhai wake .

Ni kisa kilichomuacha na machungu mengi , kiasi cha yeye kujaribu kujitoa uhai wake .

Mwanadada huyu anasema kuwa alipojaribu kumweleza shangazi yake kilichojiri alinyamazishwa. Mwikali anasema kuwa mtukio ya ubakaji katika maisha yake yaliendelea .

Kati ya miaka 12-17 , Mwikali anasema kuwa wanaume kati ya 7-9 waliwahi kumbaka baadhi yao walimfanyia kitendo hicho mara kwa mara.

Mwikali anaamini kuwa katika maisha yake ya utotoni alibakwa zaidi ya mara 30 .

Akiwa na miaka 17 alipokuwa akiishi katika kitongoji kimoja mjini Nairobi , yeye na rafiki yake wa kike walikuwa wanarejea nyumbani baada ya harakati za siku .

Walikutana na wanaume watatu ambao waliwaandama .

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Akiwa na miaka 17 alipokuwa akiishi katika kitongoji kimoja mjini Nairobi , yeye na rafiki yake wa kike walikuwa wanarejea nyumbani baada ya harakati za siku .

Tukio hili Mwikali anasema liilimtia uoga mno kwani wanaume hawa waliwatishia kwa visu , waliwaelekeza kwenye sehemu moja iliokuwa na kichaka ambapo wanaume hao walimbaka kwa zamu .

Anasema baada ya tukio hilo alijaribu kila njia kujitoa uhai wake kwa kukosa dhamana ya maisha yake lakini bado ilishindikana na aliokolewa na wasamaria wema akiwa kwenye harakati za kutekeleza tendo hilo.

Mara kwa mara alikuwa akijiuliza ni kwanini yeye amekuwa muathiriwa wa ubakaji wa kila mara ?

Ndio swali lililojiriudia katika fikra zake mara kwa mara . Ila hakuwa na ujasiri wa kujitokeza kuzungumzia matukio hayo . Ni siri alioiweka kwa miaka mingi na anasema kuwa hadi kipindi ambacho mama yake mzazi aliaga dunia hakufahamu kuwa binti yake alikuwa amebakwa zaidi ya mara 30.

Kimya hiki Mwikali anasema kilisababishwa na hali ya aibu uoga na hali ya kujidunisha .

Alianza kupata matibabu yaliomshirikisha mwanasaikolojia na pia kupewa ushauri nasaha kwasababu ya machungu mengi aliokuwa ameyabeba tangu akiwa na umri wa miaka 12 .

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Mwanadada huyu anasema kuwa watu wa jamii yake hawakuwa wanafahamu kuwa alikuwa amebakwa mara kwa mara.

Mwanadada huyu anasema kuwa watu wa jamii yake hawakuwa wanafahamu kuwa alikuwa amebakwa mara kwa mara.

Anasema kwamba mama yake marehemu aliaga dunia kabla ya kumfahamishwa kwamba binti yake alikuwa muathiriwa wa ubakaji .

"Sikuwa nimewahi kuzungumzia siri ya kubakwa na ni jambo ambalo lilinifanya kujawa na hasira pamoja na uchungu mwingi wa ndani"anaongezea

Kwa mwanadada huyu imekuwa ni safari ndefu mno ya kujikubali na vilevile kuwaamini wanaume, na kutofautisha hulka za wanaume ambao ni wabakaji na wanaume ambao ni wazuri

Lucy Mwikali

Chanzo cha picha, Lucy Mwikali

Maelezo ya picha, Kwasasa Lucy Mwikali kando na kuwa mtoa nasaha na mwanaharakati anayepigania haki za wasichana haswa kuhusu sheria dhidi ya ubakaji yeye pia ni muimbaji ya nyimbo za injili .

Kwasasa Lucy Mwikali kando na kuwa mtoa nasaha na mwanaharakati anayepigania haki za wasichana haswa kuhusu sheria dhidi ya ubakaji, yeye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili .