Aliko Dangote na Mohammed Dewji miongoni mwa mabilionea wa Afrika 2021

Barani Afrika na kwengineko duniani, watu matajiri wamepitia mlipuko wa virusi vya corona bila shaka.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes mwaka 2021, utajiri wa Mabilionea 18 kutoka bara hili uliongezeka kwa $4.1b, ikiwa ni asilimia 12 zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Kwa miaka kumi mfululizo Aliko Dangote kutoka Nigeria ndiye mtu tajiri zaidi barani Afrika akiwa na utajiri wenye thamani $12.1b.
Thamani hiyo imepanda kwa dola bilioni 2, ikilinganishwa na mwaka jana kutokana na kupanda kwa asilimia 30 ya bei za hisa za kampuni ya simiti ya Dangote kulingana na Forbes.
Mtu wa pili kwa utajiri ni Nassef Sawiris wa Misri ambaye mali yake kubwa ni asilimia sita ya hisa katika kampuni ya Addidas.
Katika nafasi ya tatu ni Nicky Oppeheimer wa Afrika Kusini ambaye alirithi hisa katika kampuni ya Almasi ya DeBeers na kusimamia kampuni hiyo hadi mwaka 2012 wakati alipouza asilimia 40 ya hisa za familia yake katika kampuni ya DeBeers kwa kampuni ya kuchimba madini ya AngloAmerican kwa $5.1 billioni.

Chanzo cha picha, Facebook/bbc
Mwengine aliyetajirika mwaka huu ni mfanyabiashara mwengine wa simiti, Abdulsamad Rabiu.
Hisa zake katika kampuni ya simiti ya BUA PLC ambayo iliorodheshwa katika soko la hisa la Nigeria mwezi Januari, zimepanda maradufu kwa thamani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hatua hiyo iliongeza thamani ya Rabiu kwa asilimia 77 hadi kufikia $5.5 billioni.
Kitu kimoja muhimu ni kwamba Rabiu na mwanawe wanamiliki asilimia 97 ya kampuni hiyo na kuifanya kupata umaarufu.
Soko la hisa la Nigeria linahitaji asilimia 20 ama zaidi ya hisa za kampuni kuuzwa kwa raia ama hisa hizo ziwe na thamani ya dola milioni 50 ili kuwa na hakika.
Msemaji wa soko la hisa la Nigeria aliambia Forbes kwamba kampuni ya simiti ya BUA inaafikia sharti la pili - Kwamba Forbes hutoa punguzo la thamani ya hisa wakati hisa hizo zilizouzwa kwa raia zipo chini ya asilimia 5.
Bilionea wa pekee kutoka Afrika mashariki aliyeorodheshwa katika orodha hiyo ya Forbes ni Mfanyabiashara wa Tanzania Mohammed Dewji aliyechukua nafasi ya 13. Dewji ana thamani ya dola bilioni 1.6 kulingana na ripoti hiyo ya jarida la Forbes.

Chanzo cha picha, AFP
Orodha ya watu matajiri zaidi duniani mwaka 2021:
1. Aliko Dangote ana thamani ya $12.1b
2. Nassef Sawiris ana thamani ya $8.5b
3. Nicky Openheimer thamani ya $8b
4. Johann Rupert ana thaman ya $7.2b
5. Mike Adenuga ana thamani ya $6.7b
6. Abdulsamad Rabiu ana thamani ya $ 5.5b
7. Issad Rebrad ana thamani ya $4.8b
8. Naguib Sawiris ana thamani ya $3.2b
9. Patrice Motsepe ana thamani ya $ 3b
10. Koos Bekker ana thamani ya $2.8b
Huku baadhi yao wakiongeza utajiri wao kwa mabilioni, mabilionea wawili kutoka katika orodha ya mwaka 2020 walishuka thamani na kuwa chini ya dola bilioni moja .
Wanawake wawili wa pekee walioorodheshwa mabilionea kutoka Afrika mwaka 2020 wameshuka katika orodha hiyo.
Kulingana na Forbes, thamani ya Folonrusho Alakija kutoka Nigeria , anayemiliki kampuni ya kuchimba mafuta ilishuka chini ya dola bilioni moja kutokana na bei ya chini ya mafuta.

Chanzo cha picha, Getty Images
Isabel dos Santos ambaye tangu 2013 amekuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika alishuka kwa thamani kutokana na maamuzi kadhaa ya mahakama ambayo yalipiga tanji mali yake nchini Angola na Portugal.
Mabilionea hao 10 kutoka Afrika wanatoka kutoka mataifa saba tofauti .
Afrika Kusini na Misri ina mabilionea watano, ikifuatiwa na Nigeria ilio na watatu na Morocco ilio na wawili.












