Kuvamiwa kwa bunge: Democrats kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Trump

Nancy Pelosi speaks to reporters a day after supporters of US President Donald Trump occupied the Capitol

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wabunge wa Democrats wanatarajiwa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais Trump katika Bunge la Wawakilishi Jumatatu

Wabunge wa Democrats wanapanga kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Donald Trump kwa mchango wake katika vurugu za uvamizi wa bunge zilizotokea Jumatano katika bunge la Marekani.

Msemaji wa Bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema atawasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Bwana Trump ikiwa hatajiuzulu mara moja.

Jumatatu Democrats katika Bunge la Wawakilishi wanapanga kuwasilisha hoja kwasababu ya "kuchochea vurugu".

Wanamshutumu Bwana Trump kwa kuhamasisha kutokea kwa fujo bungeni ambako kulisababisha vifo vya watu watano.

Rais mteule Joe Biden alisema kura ya kutokuwa na imani ni maamuzi ya bunge, lakini akaongeza kwamba "kwa kipindi kirefu tu nimekuwa nikifikiria kuwa Rais Trump hakustahili katika kazi hii".

Hata hivyo Ikulu ya Marekani imetupilia mbali suala la hoja ya kutokuwa na imani na Trump ikisema kwamba "inachochewa kisiasa" hatua ambayo "itasababisha mgawanyiko zaidi katika nchi hiyo bora".

Karibu wabunge 160 wa Democrats katika bunge la Wawakilishi wametia saini hoja ambayo wabunge Ted Lieu wa California na David Cicilline wa Rhode Island walianza kuiandika wakiwa wamejificha wakati wa ghasia zilizotokea bungeni Jumatano.

Ikiwa mchakato huo utafanikiwa, hiyo itakuwa mara ya pili kwa Bunge la Wawakilishi kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais Trump.

Desemba mwaka 2019, bunge hilo lilipiga kura ya kutokuwa na imani na Trump kwa makosa ya utumiaji mbaya wa mamlaka na kukataa kutoa ushirikiano kwa bunge.

Lakini bunge la Seneti lilimuondolea mashitaka yote mawili Februari 2020.

Hakuna rais yeyote wa Marekani ambaye amewahi kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye mara mbili.

Hata hivyo, matarajio ya kupitishwa kwa kura hiyo bado ni finyu kwasababu Bwana Trump ana wabunge wengi wanaomuunga mkono katika bunge la Seneti.

Na hiyo inamaanisha kuwa kupigiwa kura hiyo katika Bunge la Wawakilishi kunaweza tu kuwa hatua iliyochukuliwa kuashiria kwamba Bwana Trump anastahili kuwajibishwa kwa uvamizi wa bunge.

Tazama:

Maelezo ya video, Uchaguzi wa Marekani 2020: Tazama jinsi waandamanaji walivyovamia bunge Marekani

Kulingana na kumbukumbu za ndani, siku ya karibu zaidi ambayo hoja ya kutokuwa na imani inaweza kutekelezwa ndani ya Bunge la Wawakilishi ni Januari 19, siku moja kabla ya muda wa Trump kuwa madarakani kumalizika na ikiwa kuna kesi yoyote basi inaweza kuanza baada ya yeye kuondoka madarakani.

Wataalamu wa katiba wamegawanyika katika suala la ikiwa kura ya kutokuwa na imani bado inaweza kuendelea katika Bunge la Seneti wakati huo.

Ikiwa Trump atapatikana na hatia, huenda akapoteza faida wanazopata marais waliomtangulia na pia maseneta huenda wakapiga kura ya kumpiga marufuku kabisa kushikilia wadhifa wowote ule katika ofisi ya umma.

Hatua hiyo inawadia wakati ambapo Bwana Trump amepigwa marufuku kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter alioupendelea sana katika mawasiliano.

Uvamizi wa bunge umefanya wanasiasa waaandamizi kuwa na wasiwasi kiasi cha hata Spika wa Bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi kufanya mazungumzo na afisa wa juu wa jeshi la nchi hiyo kuhusu namna za kumzuia Bwana Trump kufikia nambari za siri za silaha za nyuklia.

A still image taken from video provided on social media on January 8, 2021. Donald Trump via Twitter. US President Donald Trump gives an address, a day after his supporters stormed the US Capitol in Washington,

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Donald Trump

Je uamuzi wa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Trump unamaana gani?

Azimio la rasimu ambalo limeshirikishwa shirika la habari la CBS News, washirika wa BBC, linaangazia kosa moja: "uchochezi wa ghasia".

"Donald John Trump ilijihusisha na uhalifu mkubwa kwa kuchochea vurugu dhidi ya serikali ya Marekani," rasimu hiyo inasema.

Katika azimio hilo, wabunge wanamshutumu rais kwa kutoa matamshi ambayo yalichochea "matendo ya uvunjaji wa sheria bungeni"

Rasimu hiyo pia inasema hilo lilienda sambamba na juhudi zake za kuzuia na kuvuruga kikao cha "kuidhinisha ushindi wa Biden katika uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba.

"Hivyo basi alivunja uaminifu wake kama rais, kunakodhihirishwa na kujeruhiwa kwa raia wa Marekani," azimio hilo linasema.

Rais alihamasisha wafuasi wake kuandamana hadi bungeni siku ambayo wabunge walikuwa wanaidhinisha ushindi wa Biden wa kura za wawakilishi.

Kura ya kutokuwa na imani ni nini?

Kura ya kutokuwa na imani inaruhusu Bunge - sehemu ya serikali ya Marekani - kuandika na kuleta hoja - ya kumfungulia rais mashitaka.

Hoja ya kutokuwa na imani ni makosa ambayo yanawasilishwa na Bunge la Wawakilishi dhidi ya rais. Ikiwa Bunge hilo litayapitisha, mswada huo unawasilishwa katika Bunge la Seneti kuamua ikiwa ana au hana hatia.

Ni mchakato ambao ni nadra kutokea na ni wa kisiasa zaidi badala ya kiuhalifu.

Bwana Trump ni rais wa tatu kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Marais wengine wawili, Bill Clinton mwaka 1999 na Andrew Johnson mwaka 1868, walisalia madarakani baada ya bunge la Seneti kuwaondolea mashitaka.

Hata hivyo, Rais Richard Nixon alijiuzulu kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.