Waridi wa BBC: Kwanini namzungumzia mwanangu aliyejitoa uhai

Chanzo cha picha, Namuye
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kabla ya mwezi Agosti, 2019 maisha ya Jaqueline Namuye Mutere yalikuwa ya kawaida na yaliyojaa matumaini tele. Lakini bila kutarajia, mambo yalibadilika.
Kabla ya hapo, alikuwa na watoto watano lakini tangu wakati huo akabaki na wanne.
Mwanae wa kiume alikuwa amejitoa uhai wake tarehe 4 Agosti. Ni tukio lililobadilisha maisha yake.
Anasema amejikuta akiwa kwenye huzuni ya ndani kwa ndani mara kwa mara.
Sababu kuu ni kwamba wakati mwingine huhisi kana kwamba alikuwa na uwezo wa kuzuia yaliyotokea.
"Nimejikuta nikiwa njia panda ya kujilaumu kama mama wa mtoto wangu wa kiume kwamba nilikosea wapi hadi mtoto wangu akafikia kujitia kitanzi?" anasema.
"Mbona sikufahamu yaliyokuwa yanaendelea kwenye dhamira yake? Nilikuwa wapi nisomuokoe mwanangu?" Amejiuliza maswali haya mara kwa mara bila majibu.

Chanzo cha picha, Namuye
Maisha ya mwanawe Vernon
Jerry Vernon Ogolla almaarufu Chichi alizaliwa tarehe 30 Juni mwaka wa 1999 katika hospitali ya Masaba jijini Nairobi, akiwa mtoto wa tatu kwenye familia.
Kwake Namuye, Chichi alikuwa wa kipekee kwa kuwa alikuwa mtoto wake wa kwanza wa kiume, baada ya binti wawili kutangulia.
Mama yake Chichi anasema kuwa Chichi kama watoto wengine wa kiume alipitia vituko vya wavulana wanapo baleghe, japo hakuwahi kuingia kwenye hatari yoyote.
" Niligundua kuwa kulea mtoto wa kike na kiume ni vitu viwili tofauti sana, kwani mambo ambayo Chichi aliyapenda yalikuwa tofauti sana na dada zake, pia ari, maumbile na nguvu zake zilikuwa tofauti mno," Anakumbuka Bi Namuye
Haipatikani tena
Tazama zaidi katika FacebookBBC haihusiki na taarifa za kutoka mitandao ya nje.Mwisho wa Facebook ujumbe
Mama huyu anasema kuwa mwanae alikuwa sio mchokozi, alikuwa hapendi vita.
Kwa hivyo, kabla hajafahamu mikakati ya kujiwekea vizuizi vya migongano ya kawaida kati ya wavulana, alikwaruzwa hapa na pale.
Japo mama yake Chichi anasema kuwa mwanawe alikuwa mwenye tahadhari lakini mwerevu.

Chanzo cha picha, Namuye
Siri kuu shuleni
Chichi alifurahia na kupenda soka, alipenda sana michezo na alikuwa kijana chipukizi aliyekuwa na ndoto nyingi kati ya umri wa kuzaliwa hadi alipohitimu kuingia shule ya sekondari kidato cha kwanza .
Mama yake Chichi anasema Mwanae alifuzu vyema kuingia shule nzuri ya bweni nchini Kenya. Na hapo ndipo masaibu ya Chichi yalianzia, kwa mujbiu wa mama yake.
"Wakati wa kurejea shuleni Chichi kutoka likizo, akawa hataki kurudi. Alianza kuwa na sababu baada ya sababu kwanini asirejee shuleni. Kilichofwatia ni kuwa alama zake shuleni zilianza kushuka mno. Alianza kuwa na tabia ya kutowajibikia masomo kabisa," Bi Namuye anakumbuka.
Mama yake Chichi anasema kuwa tabia na mienendo ya mwanawe ilibadilika mno baada ya kuingia shule ya sekondari na kila mwaka hali ilizidi kila mbaya .
"Alikuwa anapenda michezo, lakini ghafla ikamchukiza. Tabia yake ikageuka kuwa hasira, hisia zake zikawa zinabadilika kama kinyonga anavyobadilisha rangi, pia alianza kuwa na tabia ya kufoka kila mara bila sababu za kimsingi, kuitisha vitu vengine ambavyo kumnunulia ilikuwa haiwezekani,"Mama Namuye anakumbuka.
Kama mama Namuye alidhani ni msimu aliokuwa anapitia mwanawe kwani alikuwa anabalehe, pia alidhania ni umri wake na pengine msukumo wa vijana kupenda vitu vingi na vya anasa.
Mama Chichi anasema kuwa Chichi alibadilisha shule mara kadhaa katika kipindi cha miaka miwili tu na kuongeza utundu maradufu.

Chanzo cha picha, Namuye
" Mwaka wa mwisho wa kidato cha nne, ghafla alionekana mchangamfu ghafla na hata kuomba masomo ya ziada kuhakikisha kuwa anaupita mtihani ila nilimkumbusha kuwa alipoteza muda mwingi kwa kusudi lake juu ya tabia zake na nikamweleza alikuwa amepoteza nafasi hiyo," Bi Namuye anakumbuka .
Hasira za mkizi
Matokeo ya mtihani wake wa mwisho yalipotolewa hakuwa amefanya vyema. Tena akabadilisha tabia.
Hasira za mkizi. Wakati mmoja anakula zaidi, wakati mwengine hali kabisa. Aliongeza marafiki kwa kasi na kuwapoteza kwa kasi hiyo hiyo.
Pia mama Chichi anasema wakati mwengine hakuwa anazingatia usafi hata kidogo.
Mara akaonekana kurejesha fahamu zake kwa hali halisia ya maisha, akasema anatamani kurejea kucheza soka.
Mama yake alihakikisha amenunua sare za soka, ila ziliishia kutupwa uvunguni mwa kitanda .
"Alianza kukaa gizani akiwa mpweke, alimchapa mbwa aliyekuwa swahiba wake hakutoka chumbani mwake hadi kila mtu atoke nyumbani , ugomvi wa kila siku haukukosa," Bi Namuye anakumbuka.
Mama yake Chichi anasema kuwa marehemu mwanawe aliishi bila kuvaa nguo wakati mwengine kutembea na chupi ya ndani bila aibu yoyote nyumbani.
Mama anakiri kijana aliyekuwa mstaarabu aligeuka na kuwa tofauti mno.
Kabla ya Chichi kujitoa uhai ugomvi ulisheheni pale nyumbani kwao, kati ya mama, na dada zake.
Alivunja gilasi zote zilizokuwa jikoni. Alikuwa na hasira zilizoogofya mno .
Usiku mmoja, alikoroga sumu na kuinywa ila aliitapika ghafla. Mama anakiri kuwa alikosa kuona kuwa zilikuwa dalili za tukio mbaya zaidi.
Chichi alitapika ile sumu huku mama akimpa maziwa kumtuliza.
Mwanamke huyu anakiri kuwa dalili za mahangaiko ya mwanawe Chichi yzilikuweko lakini hakufahamu kilichokuwa kinamfanyikia.

Chanzo cha picha, Namuye
Siku ya mauti
Jumapili ya Agosti 4 usiku, walikuwa wanajitayarisha kulala , ghafla wale dada na ndugu wadogo walikimbia chumbani kwamama na kusema kuwa Chichi alikuwa anacheza mchezo hatari.
"Haukuwa mchezo. Mwanangu alikuwa amejitia kitanzi...nilipanda juu na kumuondoa pale huku nikipiga mayowe," anakumbuka Bi Namuye
Ni mayowe ya mwanamke huya yaliyowaita majirani. Anasema ni kana kwamba saa zilisimama ghafla! Kiza kikuu kikaghubika maisha yake asijue la kufanya.
Walimkimbiza Chichi hospitali, lakini tayari alikuwa amekata roho.
"Tulipofika hospitalini nilikuwa nashangaa mbona madaktari hawamshughulikii? Walikuwa wanamtazama tu bila kufanya chochote, na ndipo nikakubali kuwa kila kitu kilikuwa kimekwisha," anakumbuka Bi Namuye.
Chichi alizikwa wiki mmoja baada ya kifo chake. Maisha yalibadilika kabisa kulingana na mama huyu.
Anaporejesha macho nyuma mwanamke huyu anasema kuwa kulikuweko na dalili nyingi kuashiria kuwa mwanawe alikuwa anapitia magumu ila hakuna aliyekuwa na habari kuwa angejitoa uhai wake.
Mama huyu anasema kuwa hudhani kuwa marehemu Chichi alikuwa amedhulumiwa kimwili shuleni alipojiunga na bweni ila hakumweleza yoyote .
" Mara kadhaa akiwa shuleni nilikuwa naamuliza ni kwanini hataki kurudi shuleni, lakini alikuwa anapuuza maswali yangu na kusema kuwa alikuwa hapendi mazingira ya huko," anasema.
" Nilimuuliza ikiwa amechapwa shuleni akakuna kichwa, ikiwa alidhulumiwa kimwili akanyanyuka na kuondoka kwa hasira , kwa hio nadhani kuna jambo lilimpata shuleni, akakosa ujasiri wa kusema."
Njia tofauti za kuomboleza
Haijakuwa rahisi kusonga mbele kwake mama huyu na wanawe wanne waliohai, anasema kuwa kwa muda mrefu walilala sebuleni baada ya kifo cha Chichi.
Kila mtu alikuwa na njia zake tofauti za kuomboleza.
Kwa mfano chumba cha Chichi na nguo zake havikuguswa kwa muda mrefu. Wametafuta njia mbalimbali za kuzungumza kuhusu alichokifanya Chichi
Mama Chichi anasema kuwa kukubali kuzungumza hadharani kuhusu alichokifanya mwanawe ni kumbukumbu yake na pia kuhamasisha vijana kuzungumza wanapopitia magumu yeyote.
Anasema kuwa hakuna kitu ambacho hakiwezi kusemwa.
Anashauri wazazi kuwa karibu na watoto wao na wanapotambua dalili zozote ambazo ni kinyume cha mienendo yao ya kawaida basi wachukue hatua ya kuchunguza zaidi.
Bi Namuye amekuwa mstari wa mbele kuzungumzia tukio la mwanawe kujitoa uhai, alitumai kuwa itasaidia kuwazuiwa vijana wengine kukata tamaa na kujitoa uhai.












