Uchaguzi wa Marekani 2020: Biden na Trump wazuru majimbo muhimu

Chanzo cha picha, Reuters
Donald Trump na Joe Biden wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali kote Marekani wakati ambapo uchaguzi wa Marekani unakaribia.
Rais Trump alitembelea majimbo matano ambayo wagombea wote wawili wanapigania kunyakua kura za maeneo hayo huku mpinzani wake Bwana Biden akizungumza katika mkutano wa kampeni huko Pennsylvania.
Kulingana na kura za maoni bado mgombea wa Democratic anaongoza kabla ya uchaguzi utakaofanyika Jumanne.
Hata hivyo tofauti kati yao ni ndogo hasa katika majimbo muhimu ambayo huenda yakachangia pakubwa uamuzi wa matokeo ya uchaguzi huo.
Zaidi ya watu milioni 90 tayari wamepiga kura zao katika upigaji kura wa mapema ambako kunaweza kufanya idadi ya waliojitokeza ikawa ndio kubwa zaidi katika kipindi cha karne moja.
Uchaguzi huo unawadia huku janga la virusi vya corona likiendelea. Marekani imerekodi zaidi ya maambukizi na vifo vingi kuliko nchi nyingine yoyote duniani ikitangaza maambukizi zaidi ya 99,000 Jumamosi pekee.
Mtaalamu wa masuala ya virusi Anthony Fauci amekosoa vikali utawala wa Trump jinsi unavyoshughulikia janga la virusi vya corona, hatua ambayo Ikulu ya Marekani imeikemea Jumapili.
Je wagombea hao wametembelea majimbo gani?
Trump amezuru majimbo matano katika hatua ya mwisho ya kurai wapiga kura kumchagua.

Chanzo cha picha, EPA
Ratiba ya rais wa Republican ilikuwa na shughuli nyingi Jumapili akifanya mikutano ya siasa katika maeneo ya Iowa, Michigan, North Carolina na Georgia, na baadae akaelekea Florida - majimbo yote hayo inasemekana kwamba ushindani wa wapinzani hao wawili ni wa karibu mno kulingana na kura ya maoni.
Akizungumza huko Washington, mji wa Michigan kaskazini mwa Detroit, Bwana Trump aliwaambia wafuasi wake kwamba chini ya uongozi wake "sasa uchumi unakua kwa haraka kuliko wakati mwingine wowote ule".
Alitabiri atashinda tena kwenye jimbo hilo kama ilivyokuwa mwaka 2016, na kuongeza kuwa jimbo hilo linalofahamika kwa utengenezaji wa magari "miaka minne iliyopita wakati anachaguliwa, halikuwa na kiwanda chochote cha utengenezaji magari", na sasa amewatimizia moja ya mahitaji yao "Tuliwarejeshea kiwanda chenu cha magari," amesema.
Katika mkutano wa baadae huko Dubuque, Iowa - uliojumuisha wafuasi wa ngazi ya juu kama vile binti yake Ivanka na msaidizi wake Hope Hicks - Bwana Trump aliahidi usalama mipakani na kuongeza majaji wengi wenye msimamo mkali mahakamani.

Chanzo cha picha, Getty/EPA
Wakati huohuo, Bwana Biden alizuru eneo la Pennsylvania, alikozaliwa na jimbo muhimu.
Akiangazia janga la Covid-19, aliwaambia wafuasi wake kuwa wana nafasi ya kumchagua " Biden atakayewafungia" au "kupata chanjo salama kwa ungonjwa huo".
Matamshi yake yanawadia baada ya Dkt. Fauci, mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza, kuliambia gazeti la Washington Post kwamba Marekani "inakabiliwa na siku za majonzi " miezi ijayo.
Bwana Biden "alichukulia suala hili kwa uzito mkubwa katika mtazamo wa kiafya", huku Rais Trump akiwa na mtazamo tofauti akiangazia zaidi "uchumi na kufungua tena nchi", aliongeza.
Biden afanya kampeni yake Pennsylvania

Chanzo cha picha, Reuters
Mgombea wa Democratic na aliyekuwa makamu rais wakati huo huo alikuwa eneo la Pennsylvania, alikozaliwa na jimbo muhimu katika uchaguzi.
Bwana Trump alipata ushindi mdogo katika uchaguzi wa mwaka 2016 lakini kura za maoni sasa hivi zinaonesha Bwana Biden mwaka huu kidogo yuko mbele ya Trump.
Akiwa kwenye mkutano wa Philadelphia Bwana Biden alizungumza na jamii ya watu weusi na kuahidi kutatua "mfumo wa ubaguzi " nchini Marekani na kumshambulia rais vile alivyoshughulikia janga la corona.
"Vile alivyoshughulikia hilo inakaribia uhalifu," alisema. "Waliokufa na kujeruhiwa katika jamii ya watu weusi idadi yao ni kubwa na hilo lingeweza kuepukika."
Bwana Biden pia alizungumzia taarifa za tovuti moja ya habari ya Axio inayoosema kuwa rais atajitangaza mshindi Jumanne usiku ikiwa ataona anaelekea kuongoza kimatokeo.
"Rais hatatuibia uchaguzi huu," Biden aliwaambia wanahabari.
Mgombea huyo wa Democratic pia alimkosoa Bwana Trump kwa kuchochea wafuasi wake baada ya wengine kulazimisha basi la kampeni yake kusimama kwenye barabara kuu huko Texas, jambo ambalo Shirika la Ujasusi sasa hivi limethibitsha inalichunguza.












