Polisi Nigeria wamnusuru mwanaume aliyefungiwa katika gereji ya wazazi wake

Mwanamume mmoja nchini Nigeria ameokolewa na polisi kutoka kwenye eneo la kuegesha magari ya wazazi wake, ambako alikuwa kwa muda mrefu, wanasema polisi.

Hamidu mwenye umri wa miaka 30 alipatikana katika gereji ya nyumba ya wazazi wake iliyopo katika mji wa kaslazini mwa Nigeria wa Kano ambako alikua amefungiwa kwa miaka mitatu bila kutoka nje.

Ahmed Aminu, alipatikana baada ya polisi kuivamia nyumba ya familia yao.

Majirani wa familia hiyo walilifahamisha shirika moja lisilo la kiserikali juu ya masaibu aliyokuwa akipitia mwanaume huyu, kisha likawaita polisi

Baba yake mzani Bwana Aminu pamoja na mama yake wa kambo wamekamatwa na polisi wanasema uchunguzi zaidi unaendelea kubaini ni kwanini Amidu alifungiwa kwenye gereji hilo kwa miaka mitatu.

Katika video ya kutisha iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Amidu alionekana akiwa mchovu, dhaifu na hakuweza hata kutembelea, huku akisaidiwa kupanda gari alipokuwa akipelekwa hospitalini baada ya kutolewa kwenye eneo la gereji na polisi.

Ngozi ya magoti yale ilionekana imenyauka na mifupa yake ya miguu ilikua inaonekana kana kwamba haina nyama za mwili.

"Tulimpata Aminu akiwa katika hali mbaya sana, akijisaidia haja zote kubwa na ndogo pale pale na alikua hapewi chakula chochote na alikuwa anaonekana kama mtu ambaye angekufa wakati wowote ," Haruna Ayagi, Shirika lisilo la kiserikali la Mtandao wa Haki za binadamu aliiambia BBC.

Polisi ilisema kuwa mwanaume huyo amekuwa akifungiwa na wazazi wake ambao walikuwa wakimshuku kuwa anatumia madawa ya kulevya na wakamyima chakula na huduma ya afya.

Baadhi ya taarifa zilisema kuwa amekuwa akifungiwa kwa hadi miaka saba.

Huyu ni mtu wa pili kupatikana akiwa na hali mbaya na kunusuriwa katika nyummba ya wazazi wiki hii nchini Nigeria.

Jumatano polsi katika jimbo la Kaskazini -magharibi mwa Nigeria walimuokoa mvulana mwenye umri wa miaka 10 kutoka kwenye zizi la wanyama ambako amekuwa akifungiwa kwa miaka miwili na wazazi wake.

Mwandishi wa BBC Nduka Orjinmo aliyeko mjini Abuja anasema kwamba katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria kuna tatizo la uraibu wa madawa ya kulevya lakini maeno machache yanayodhaminiwa na taifa , kwahiyo baadhi ya wazazi wanaamua kujichukulia hatua za kuwasaidia watoto wao wenye matatizo.

Baadhi ya wazazi wamewapeleka watoto wao wenye matatizo ya mihadarati katika vituo vya kibinafsi vya kidini vya kurekebisha tabia, lakini baadhi ya vituo hivyo vimekuwa vikivamiwa na maafisa wanaovielezea vituo hivyo kama ''nyumba za mateso''.

Uchunguzi wa BBC wa mwaka 2018 ulifichua hali za kutisha katika kituo kilichopo katika jimbo la Kano, ambako wagonjwa wenye matatizo ya kiakili walikuwa wamefungwa kwa minyororo chini.