Baraza la Usalama la UN ni nini na Kenya itafaidika vipi na wadhifa huu?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baada ya panda shuka zo joto la kisiasa, Kenya imeiangusha Djibouti na kunyakua kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).

Kenya sasa itakaa katika baraza hilo linalopitisha maazimio muhimu duniani kwa muhula wa miaka miwili.

Lakini, urefu wa kampeni na sarakasi za kutafuta ushawishi zinaweza kukufanya ukajiuliza, nafasi hiyo ina umuhimu gani?

Baraza hilo lina wanachama 15, nchi tano, Uchina, Marekani, Ufaransa, Urusi na Uingereza ni wanachama wa kudumu.

Nchi 10 zilizosalia hugombea kwa kupigiwa kura na kuingia kwenye baraza kwa kipindi cha miaka miwili.

Kenya itaungana na Norway, Ireland, India na Mexico ambao walichaguliwa Jumatano. Nchi hizo zitahudumu kwa mwaka 2021 mpaka 2023 katika baraza. Mchuano baina ya Kenya na Djibouti ilibidi uamuliwe Alhamisi jioni kwa saa za Marekani ili kumpata mshindi ambaye atachukua nafasi ya Afrika Kusini.

Baraza hilo ndilo ambalo hupitisha maazimio yote ya muhimu ya UN kama kuwekwa kwa vikwazo na kutumika kwa nguvu za kijeshi.

Nchi wanachama hupata vitu vitatu kushiriki kwenye baraza hilo, profesa Adam Chapnick wa Chuo cha Kijeshi cha Canada, ameiambia BBC.

Vitu hivyo ni, ushawishi, umuhimu na kufikia nyenzo za maamuzi.

"Kwa miaka miwili, kila siku, nchi ambayo si dola yenye nguvu inakuwa karibu na nchi kubwa na nyenzo za muhumi za kufanyia maamuzi," Profesa Chapnick anaeleza.

"Ukaribu huo unafanya mataifa hayo kuwa na umuhimu na ushawishi."

Ili kupata nafasi hiyo nchi zinazogombea hufanya kampeni ya muda mrefu, Kenya ilifanikiwa kupata uungwaji mkono na Umoja wa Afrika.

Baadhi ya nchi huandaa mpaka matamasha ya muziki. Canada ambayo imeangushwa kwenye kinyang'anyiro cha Jumatano ilikuwa inagawa chokoleti kwa wajumbe wa wa kupiga kura.

Kenya imepokea vipi ushindi?

Rais Uhuru Kenyatta ametaja ushindi wa Kenya kama kukua kwa wasifu wa nchi hiyo na ushawishi wake miongoni mwa mataifa kama hatua isiyoyumbishwa na lolote na kwamba ni mshirika muhimu wa maendeleo.

Kiongozi wa nchi ameshukuru washindani wake katika uchaguzi huo, nchi ya Djibouti kwa kuwa mpinzani kuhimu na Umoja wa Afrika kwa idhinisho lao kama mpeperusha bendera wa bara la Afrika kwenye kinyanganyiro hicho.

Rais huyo wa Kenya, amesema, nchi hiyo itajitahidi kadiri ya uwezo wake kuunganisha Afrika na kusimamia msimamo wa bara hili katika Baraza la Usalama na itaendeleza ajenda zake 10 kama zilivyoonyeshwa wakati wa kipindi cha kampeni.

Kenya imeshinda kiti katika Baraza ka Usalama la Umoja wa mataifa baada ya kushinda Djibouti katika duru ya pili ya uchaguzi Alhamisi.

Kinyanganyiro hicho kati ya Kenya na Djibouti kiliingia katika duru ya pili baada ya matokeo ya duru ya kwanza kuonesha kwamba kwamba Kenya haijapata kura za kutosha kuiwezesha kushinda nafasi hiyo ya Umoja wa Mataifa moja kwa moja.

Huku nchi 191 zikipiga kura kati ya 193, Kenya ilipata kura 129 na kuipiku Djibouti kwa kura 62.

Hii ina maanisha nini kwa Kenya?

Kunzia Januari 2021, nchi hiyo inakuwa kiungo muhimu na yenye nguvu katika Umoja wa Mataifa baada ya miaka 23 ambapo itahusika katika meza ya maamuzi muhimu duniani katika masuala ya amani na usalama.

Baadhi ya maamuzi hayo, Kenya inaweza kuhusika ni pamoja vikwazo, uidhinishaji wa utumiaji nguvu ili kuhakikisha Amani inadumu pamoja na kuchagua majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Kushirikiana pamoja na wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo, zenye uwezo wa kupiga kura ya turufu ( Urusi, Uingereza, marekani, China na Ufaransa), Kenya itaungana na nchi zingine tisa wanachama wa baraza hilo wasio wa kudumu na huenda ikapata fursa ya kuwa mwenyekiti kwenye vikao vya baraza hilo, fursa muhimu ya kushinikiza ajenda.

Lakini kwa kuwa iliungwa mkono na AU, Kenya itakuwa na uhalali wa kulisemea bara la Afrika katika baraza hilo.