Virusi vya corona: Rwanda yabadili msimamo wa kuondoa kafyu baada ya mtu mmoja kufariki

Uamuzi wa saa sita usiku wa serikali kufutilia mbali hatua ya kupunguza masharti ya kukabiliana na virusi vya corona dakika chache kabla ya kuanza kutekelezwa, yanajiri baada ya Rwanda kurekodi kifo chake cha kwanza cha virusi vya corona mbali na kuongezeka kwa visa vipya.
Usafiri kutoka mikoa mengine hadi katika mji mkuu wa Kigali pamoja na uchukuzi wa teksi ulitarajiwa kurudi kuanzia tarehe mosi Juni baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi miwili.
Afisi ya waziri mkuu ilitangaza kwamba hilo limefutiliwa mbali , hatua iliowashangaza zaidi ya wahudumu 50,000 wa teksi hizo nchini Rwanda ambao familia zao ziliathiriwa vibaya na masharti hayo.
Katika tangazo lililowekwa katika mtandao wa twitter , wengi waliikosoa serikali kwa mabadiliko hayo ambayo yameweka maisha ya wahudumu wa pikipiki katika hali mbaya, huku wengine wakiwa tayari kuanza uchukuzi wao wa mkoa mmoja hadi mwengine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Afya aliambia chombo cha habari cha Rwanda kwamba mabadiliko hayo ya uamuzi yalitokana na wagonjwa wapya kupatikana katika wilaya ya Rusizi magharibi mwa Rwanda.
Katika tangazo lililochapishwa katika Twitter , serikali ilisema masharti zaidi yatatangazwa siku ya Jumanne tarehe 2 Juni.
Siku ya Jumapili Rwanda ilirekodi wagonjwa wapya 11 wa Covid-19 , ikiwemo wagonjwa wapya magharibi mwa taifa hilo, siku hiohio ambapo mgonjwa mmoja wa corona alizikwa kulingana na tamaduni za Kiislamu kandokando mwa mji wa Kigali.
Mwathiriwa aliejulikana kama Gisaka Hassan, 65 alikuwa dereva wa malori ambaye aliambukizwa ugonjwa huo Benako Tanzania na kurudi Rwanda mnamo tarehe 28 Mei akiwa katika hali mahututi vilisema vyombo vya habari.

Chanzo cha picha, Reuters
Vyama viwili vya upinzani nchini Rwanda, PS - Imberakuri na Dalfa-umurinzi , vimetoa taarifa vikiitaka serikali kuondoa masharti yote ya kukabiliana na virusi vya corona kwa kuwa yanawanyima raia wa Rwanda haki zao za kusafiri, kuabudu, kufanya kazi ili kuishi, kufanya harusi na kuburudika.
Kufikia Jumatatu, Rwanda ilikuwa imerekodi wagonjwa 370, huku 256 wakiwa wamepona na mtu mmoja kufariki.












